Isaya 59

Dhambi, Toba Na Ukombozi

1 Hakika mkono waBwanasi mfupi hata usiweze kuokoa,

wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.

2 Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi

na Mungu wenu,

dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake,

ili asisikie.

3 Kwa maana mikono yenu imetiwa mawaa kwa damu

na vidole vyenu kwa hatia.

Midomo yenu imenena uongo,

nazo ndimi zenu zimenong’ona mambo maovu.

4 Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki;

hakuna hata mmoja

anayetetea shauri lake kwa haki.

Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo,

huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.

5 Huangua mayai ya nyoka wenye sumu kali

na kutanda wavu wa buibui.

Ye yote alaye mayai yao atakufa,

na wakati moja lianguliwapo,

nyoka mwenye sumu kali hutoka humo.

6 Utando wao wa buibui haufai kwa nguo;

hawawezi kujifunika

kwa kile walichokitengeneza.

Matendo yao ni matendo maovu,

vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao.

7 Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,

ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia.

Mawazo yao ni mawazo mabaya;

uharibifu na maangamizi

huweka alama njia zao.

8 Hawajui njia ya amani,

hakuna haki katika mapito yao.

Wamezigeuza kuwa njia za upotovu,

hakuna ye yote apitaye katika njia hizo

atakayeifahamu amani.

9 Hivyo uadilifu uko mbali nasi,

nayo haki haitufikii.

Tunatazamia nuru, kumbe! yote ni giza,

tunatazamia mwanga,

lakini tunatembea katika giza kuu.

10 Tunapapasa ukuta kama kipofu,

tunapapasa katika njia zetu

kama watu wasio na macho.

Adhuhuri tunajikwaa kama wakati wa gizagiza,

katikati ya wenye nguvu, tuko kama wafu.

11 Wote tunanguruma kama dubu;

tunalia kwa uchungu

kwa maombolezo kama hua.

Tunatafuta haki, kumbe hakuna kabisa;

tunatafuta wokovu, lakini uko mbali.

12 Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako,

na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu.

Makosa yetu yako pamoja nasi daima,

nasi tunayatambua maovu yetu:

13 Uasi na udanganyifu dhidi yaBwana,

kumgeuzia Mungu wetu kisogo,

tukichochea udhalimu na maasi,

tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi.

14 Hivyo uadilifu umerudishwa nyuma,

nayo haki inasimama mbali,

kweli imejikwaa njiani,

uaminifu hauwezi kuingia.

15 Kweli haipatikani po pote,

na ye yote aepukaye uovu huwa mawindo.

Bwanaalitazama naye akachukizwa

kwamba hapakuwepo haki.

16 Aliona kuwa hakuwepo hata mtu mmoja,

akashangaa kwamba hakuwepo

hata mmoja wa kuingilia kati;

hivyo mkono wake mwenyewe

ndio uliomfanyia wokovu,

nayo haki yake mwenyewe

ndiyo iliyomtegemeza.

17 Alivaa haki kama dirii kifuani mwake,

na chapeo ya wokovu kichwani mwake,

alivaa mavazi ya kisasi

naye akajifunga wivu kama joho.

18 Kulingana na kile walichokuwa wametenda,

ndivyo atakavyolipa

ghadhabu kwa watesi wake

na kisasi kwa adui zake,

atavilipa tena visiwa sawa na wanavyostahili.

19 Kuanzia magharibi, watu wataliogopa jina laBwana

na kuanzia maawio ya jua,

watauheshimu utukufu wake.

Wakati adui atakapokuja kama mafuriko,

Roho waBwanaatainua kiwango dhidi yake

na kumshinda kumfukuza.

20 “Mkombozi atakuja Sayuni,

kwa wale wa uzao wa Yakobo

wanaozitubia dhambi zao,”

asemaBwana.

21 “Kwa habari yangu mimi, hili ni Agano langu nao,” asemaBwana. “Roho wangu, aliyeko juu yenu na maneno yangu ambayo nimeyaweka katika vinywa vyenu hayataondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao kuanzia sasa na hata milele,” asemaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/59-ecfce4b395d865a4f791bddcefdd149a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × 4 =