Mithali 6

Maonyo Dhidi Ya Upumbavu

1 Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako,

ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi

kwa ajili ya mwingine,

2 kama umetegwa na ulichosema,

umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,

3 basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru,

kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako:

Nenda ukajinyenyekeshe kwake,

msihi jirani yako!

4 Usiruhusu usingizi machoni pako,

usiruhusu kope zako zisinzie.

5 Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji,

kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji.

6 Ewe mvivu, mwendee mchwa,

zitafakari njia zake ukapate hekima!

7 Kwa maana yeye hana msimamizi,

wala mwangalizi, au mtawala,

8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi

na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.

9 Ewe mvivu, utalala hata lini?

Utaamka lini kutoka katika usingizi wako?

10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

bado kukunja mikono upate usingizi!

11 Hivyo umaskini wako huja kama mnyang’anyi

na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

12 Mtu mbaya sana na mlaghai,

ambaye huzungukazunguka

na maneno ya upotovu,

13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,

anayetoa ishara kwa miguu yake

na kuashiria kwa vidole vyake,

14 ambaye hupanga ubaya

kwa udanganyifu moyoni mwake:

daima huchochea fitina.

15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;

ataangamizwa mara, pasipo msaada.

16 Kuna vitu sita anavyovichukiaBwana,

naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

17 macho ya kiburi,

ulimi udanganyao,

mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

18 moyo ule uwazao mipango miovu,

miguu ile iliyo myepesi kukimbilia uovu,

19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo

na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

Onyo Dhidi Ya Uasherati

20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

21 Yafunge katika moyo wako daima,

yakaze kuizunguka shingo yako.

22 Wakati utembeapo, yatakuongoza,

wakati ulalapo, yatakulinda,

wakati uamkapo, yatazungumza nawe.

23 Kwa maana amri hizi ni taa,

mafundisho haya ni mwanga

na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,

24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka,

kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.

25 Moyo wako usitamani uzuri wake

wala macho yake yasikuteke,

26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini

hata ukose kipande cha mkate

naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.

27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake

bila nguo zake kuungua?

28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka

bila miguu yake kuungua?

29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine;

hakuna ye yote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.

30 Watu hawamdharau mwizi kama akiiba

kukidhi njaa yake wakati ana njaa.

31 Pamoja na hayo, kama akikamatwa,

lazima alipe mara saba,

ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.

32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa;

ye yote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.

33 Mapigo na aibu ni fungu lake

na aibu yake haitafutika kamwe;

34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume,

naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi.

35 Hatakubali fidia yo yote;

atakataa malipo hata yakiwa makubwa kiasi gani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/6-a4b3c022120d52ef14e70a88c5e20644.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 3 =