Yeremia 51

1 Hili ndilo asemaloBwana:

“Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi

# dhidi ya Babeli na watu wakaao Leb-Kamai.

2 Nitawatuma wageni Babeli

kumpepeta na kuiharibu nchi yake;

watampinga kila upande

katika siku ya maafa yake.

3 Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake,

wala usimwache avae silaha zake.

Usiwaonee huruma vijana wake;

angamiza jeshi lake kabisa.

4 Wataanguka waliouawa katika Babeli,

wakiwa na majeraha ya kutisha

katika barabara zake.

5 Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa

na Mungu wao,BwanaMwenye Nguvu Zote,

ingawa nchi yao imejaa uovu

mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

6 “Kimbieni kutoka Babeli!

Okoeni maisha yenu!

Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake.

Ni wakati wa kisasi chaBwana,

atamlipa kile anachostahili.

7 Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono waBwana;

aliufanya ulimwengu wote ulewe.

Mataifa walikunywa mvinyo wake;

kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.

8 Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika.

Mwombolezeeni!

Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake,

labda anaweza kupona.

9 “ ‘Tungemponya Babeli,

lakini hawezi kuponyeka;

tumwache na kila mmoja aende kwenye nchi yake mwenyewe,

kwa kuwa hukumu yake inafika angani,

inapanda juu mpaka mawinguni.’

10 “ ‘Bwanaamethibitisha haki yetu;

njoni, tutangaze katika Sayuni

kitu ambachoBwanaMungu wetu amefanya.’

11 “Noeni mishale,

chukueni ngao!

Bwanaamewaamsha wafalme wa Wamedi,

kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli.

Bwanaatalipiza kisasi,

kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

12 Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli!

Imarisheni ulinzi,

wekeni walinzi,

andaeni waviziao!

Bwanaatatimiza kusudi lake,

amri yake juu ya watu wa Babeli.

13 Wewe uishiye kando ya maji mengi

na uliye na wingi wa hazina,

mwisho wako umekuja,

wakati wako wa kukatiliwa mbali.

14 BwanaMwenye Nguvu Zote

ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:

‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige,

nao watapiga kelele za ushindi juu yako.’

15 “Aliifanya dunia kwa uweza wake;

ameweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake

na kuzitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

16 Apigapo radi, maji katika mbingu hunguruma,

huyafanya mawingu yainuke

kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua

Na huuleta upepo kutoka kwenye ghala zake.

17 “Kila mtu hana ufahamu na hana maarifa;

kila sonara ameaibika kwa sanamu zake.

Vinyago vyake ni vya udanganyifu,

havina pumzi ndani yake.

18 Hazifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha,

hukumu yao itawadia, zitaangamia.

19 Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,

kwa maana yeye ni Muumba wa vitu vyote,

pamoja na kabila la urithi wake:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo ni jina lake.

20 “Wewe ndiwe rungu langu la vita,

silaha yangu ya vita

kwa wewe navunjavunja mataifa,

kwa wewe naangamiza falme,

21 kwa wewe navunjavunja

farasi na mpanda farasi,

kwa wewe navunjavunja

gari la vita na mwendeshaji wake,

22 kwa wewe napondaponda

mwanaume na mwanamke,

kwa wewe napondaponda

mzee na kijana,

kwa wewe napondaponda

kijana wa kiume na mwanamwali,

23 kwa wewe nampondaponda

mchungaji na kundi,

kwa wewe nampondaponda

mkulima na maksai,

kwa wewe nawapondaponda

watawala na maafisa.

24 “Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote waishio Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asemaBwana.

25 “Mimi niko kinyume nawe, Ee mlima unaoharibu,

wewe uangamizaye dunia yote,”

asemaBwana.

“Nitanyosha mkono wangu dhidi yako,

nikuvingirishe kutoka kwenye kilele cha mwamba,

na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.

26 Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako

kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni,

wala jiwe lo lote kwa ajili ya msingi,

kwa maana utakuwa ukiwa milele,”

asemaBwana.

27 “Twekeni bendera katika nchi!

Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa!

Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

iteni falme hizi dhidi yake:

Ararati, Mini na Ashkenazi.

Wekeni jemadari dhidi yake,

pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.

28 Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

wafalme wa Wamedi,

watawala wao na maafisa wao wote,

pamoja na nchi zote wanazotawala.

29 Nchi inatetemeka na kugagaa,

kwa kuwa makusudi yaBwana

dhidi ya Babeli yanasimama:

yaani, kuangamiza nchi ya Babeli

ili kwamba pasiwe na ye yote atakayeishi humo.

30 Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana,

wamebaki katika ngome zao.

Nguvu zao zimekwisha,

wamekuwa kama wanawake.

Makazi yake yameteketezwa kwa moto,

makomeo ya malango yake yamevunjika.

31 Tarishi mmoja humfuata mwingine

na mjumbe humfuata mjumbe

kumtangazia mfalme wa Babeli

kwamba mji wake wote umetekwa,

32 Vivuko vya mito vimekamatwa,

# mabwawa yenye mafunjoyametiwa moto,

nao askari wameingiwa na hofu kuu.”

33 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria

wakati inapokanyagwa;

wakati wa kumvuna utakuja upesi.”

34 “Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula,

ametufanya tuchangayikiwe,

ametufanya tuwe gudulia tupu.

Kama nyoka ametumeza

na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri,

kisha akatutapika.

35 Jeuri iliyofanyiwa miili yetuna iwe juu ya Babeli,”

ndivyo wasemavyo wakaao Sayuni.

“Damu yetu na iwe juu ya wale waishio Babeli,”

asema Yerusalemu.

36 Kwa hiyo, hili ndiloBwanaasemalo:

“Tazama, nitatetea shauri lako

na kulipiza kisasi kwa ajili yako;

nitaikausha bahari yake

na kuzikausha chemchemi zake.

37 Babeli utakuwa lundo la magofu

na makao ya mbweha,

kitu cha kutisha na kudharauliwa,

mahali asipoishi mtu.

38 Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo,

wanakoroma kama wana simba.

39 Lakini wakati wakiwa wameamshwa,

nitawaandalia karamu

na kuwafanya walewe,

ili wapige kelele kwa kicheko,

kisha walale milele na wasiamke,”

asemaBwana.

40 “Nitawatelemsha kama wana-kondoo

waendao machinjoni,

kama kondoo dume na mbuzi.

41 “Tazama Sheshakiatakamatwa,

majivuno ya dunia yote

yatakuwa yamefikia mwisho.

Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani

kati ya mataifa!

42 Bahari itainuka juu ya Babeli;

mawimbi yake yenye kunguruma yatamfunika.

43 Miji yake itakuwa ukiwa,

kame na jangwa,

nchi ambayo hakuna ye yote anayeishi ndani yake,

ambayo hakuna mtu anayepita humo.

44 Nitamwadhibu Beli katika Babeli

na kumfanya atapike kile alichokimeza.

Mataifa hayatamiminika tena kwake.

Nao ukuta wa Babeli utaanguka.

45 “Tokeni ndani yake, enyi watu wangu!

Okoeni maisha yenu!

Ikimbieni hasira kali yaBwana.

46 Msikate tamaa wala msiogope tetesi

zitakaposikika katika nchi;

tetesi moja inasikika mwaka huu,

nyingine mwaka unaofuata;

tetesi juu ya jeuri katika nchi

na ya mtawala dhidi ya mtawala.

47 Kwa kuwa hakika wakati utawadia

nitakapoziadhibu sanamu za Babeli;

nchi yake yote itatiwa aibu

na watu wake wote waliouawa

wataangukia ndani yake.

48 Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo ndani yake

vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli,

kwa kuwa kutoka kaskazini

waharabu watamshambulia,”

asemaBwana.

49 “Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli,

kama vile waliouawa duniani kote

walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.

50 Wewe uliyepona upanga,

ondoka wala usikawie!

MkumbukeBwanaukiwa katika nchi ya mbali,

na utafakari juu ya Yerusalemu.”

51 “Tumetahayari, kwa maana tumetukanwa

na aibu imefunika nyuso zetu,

kwa sababu wageni wameingia

mahali patakatifu pa nyumba yaBwana.”

52 “Lakini siku zinakuja,” asemaBwana,

“nitakapoadhibu sanamu zake,

na katika nchi yake yote

waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.

53 Hata kama Babeli ikifika angani

na kuziimarisha ngome zake ndefu,

nitatuma waharabu dhidi yake,”

asemaBwana.

54 “Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli,

sauti ya uharibifu mkuu

kutoka nchi ya Wakaldayo.

55 Bwanaataiangamiza Babeli,

atanyamazisha makelele ya kishindo chake.

Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu,

ngurumo ya sauti zao itavuma.

56 Mharabu atakuja dhidi ya Babeli,

mashujaa wake watakamatwa,

nazo pinde zao zitavunjwa.

Kwa kuwaBwanani Mungu wa kisasi,

yeye atalipiza kikamilifu.

57 Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe,

watawala wao, maafisa,

pamoja na wapiganaji wao;

watalala milele na hawataamka,”

asema Mfalme, ambaye jina lake

niBwanaMwenye Nguvu Zote.

58 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa,

na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto;

mataifa yanajichosha bure,

taabu ya mataifa ni nishati tu

kwa ajili ya miali ya moto.”

59 Huu ndio ujumbe Yeremia aliompa afisa Seraya mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake.

60 Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli.

61 Akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa.

62 Kisha sema, ‘EeBwana, umesema utaangamiza mahali hapa ili kwamba mtu wala mnyama asiishi ndani yake, itakuwa ukiwa milele.’

63 Utakapomaliza kusoma hiki kitabu lifungie jiwe kisha ulitupe ndani ya Mto Eufrati.

64 Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ”

Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/51-4d833f0116381e8ad748c9778b3ebe9b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten + ten =