Zaburi 139

Mungu Asiyeweza Kukwepwa

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

1 EeBwana, umenichunguza

na kunijua.

2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka;

unatambua mawazo yangu tokea mbali.

3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;

unaelewa njia zangu zote.

4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,

wewe walijua kikamilifu, EeBwana.

5 Umenizunguka nyuma na mbele;

umeweka mkono wako juu yangu.

6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,

ni ya juu sana kwangu kuyafikia.

7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako?

Niende wapi niukimbie uso wako?

8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;

# nikifanya vilindikuwa kitanda changu,

wewe uko huko.

9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,

kama nikikaa pande za mbali za bahari,

10 hata huko mkono wako utaniongoza,

mkono wako wa kuume

utanishika kwa uthabiti.

11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha

na nuru inayonizunguka iwe usiku,”

12 hata giza halitakuwa giza kwako,

usiku utang’aa kama mchana,

kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.

13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba

utu wangu wa ndani;

uliniunga pamoja tumboni

mwa mama yangu.

14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

kazi zako ni za ajabu,

ninajua hayo kikamilifu.

15 Umbile langu halikufichika kwako,

nilipoumbwa mahali pa siri.

Nilipoungwa pamoja kwa ustadi

katika vilindi vya nchi,

16 macho yako yaliniona

kabla mwili wangu haujakamilika.

Siku zangu zote ulizonipangia

ziliandikwa katika kitabu chako

kabla haijakuwapo hata moja.

17 Tazama jinsi gani yalivyo ya thamani

mawazo yako kwangu, Ee Mungu!

Jinsi gani jumla yake ilivyo kubwa!

18 Kama ningezihesabu,

zingekuwa nyingi kuliko mchanga.

Niamkapo,

bado niko pamoja nawe.

19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!

Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!

20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,

adui zako wanatumia vibaya jina lako.

21 EeBwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia?

Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?

22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,

ninawahesabu ni adui zangu.

23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,

nijaribu na ujue mawazo yangu.

24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,

uniongoze katika njia ya milele.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/139-a92dc228fd3bdfb24c069e45c20f4d67.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen − 16 =