Hukumu Ya Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Utenzi Wa Daudi Baada Ya Doegi, Mwedomu, Kumwendea Sauli Na Kumjulisha Kuwa Daudi Amekwenda Nyumbani Kwa Abimeleki)
1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?
Kwa nini unajivuna mchana kutwa,
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi,
ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.
3 Unapenda mabaya kuliko mema,
uongo kuliko kusema kweli.
4 Unapenda kila neno lenye kudhuru,
ewe ulimi wenye hila!
5 Hakika Mungu atakushusha chini
kwa maangamizi ya milele:
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu
kutoka katika hema yako,
atakung’oa kutoka nchi ya walio hai.
6 Wenye haki wataona na kuogopa,
watamcheka, wakisema,
7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,
bali alitumainia wingi wa utajiri wake
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”
Neema Ya Mungu
8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni
unaostawi katika nyumba ya Mungu,
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma
milele na milele.
9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/52-866b48522de5e9ba80791781fd94b645.mp3?version_id=1627—