Zaburi 59

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Usiharibu. Utenzi Wa Daudi Wakati Sauli Alipotuma Wapelelezi Wamwue)

1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,

unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.

2 Uniponye na watu watendao mabaya,

uniokoe kutokana na wamwagao damu.

3 Tazama wanavyonivizia!

Watu wakali wanajiunga pamoja

kwa ubaya dhidi yangu,

EeBwana, mimi sijakosea

wala kutenda dhambi.

4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.

Inuka unisaidie,

uone hali yangu mbaya!

5 EeBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!

Zinduka uyaadhibu mataifa yote,

usionyeshe huruma kwa wasaliti.

6 Hurudi wakati wa jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzungukazunguka mji.

7 Tazama yale wanayotema kutoka katika vinywa vyao,

hutema upanga kutoka katika midomo yao,

nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”

8 Lakini wewe,Bwana, uwacheke;

unayadharau mataifa hayo yote.

9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,

wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

10 Mungu wangu unipendaye.

Mungu atanitangulia,

naye atanifanya niwatazame kwa furaha

wale wanaonisingizia.

11 EeBwana, ngao yetu, usiwaue,

au sivyo watu wangu watasahau.

Katika uwezo wako wafanye watangetange

na uwashushe chini.

12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,

kwa ajili ya maneno ya midomo yao,

waache wanaswe katika kiburi chao.

Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,

13 wateketeze katika ghadhabu,

wateketeze hadi wasiwepo tena.

Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia

kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.

14 Hurudi jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzunguka zunguka mji.

15 Wanatangatanga wakitafuta chakula

wasipotosheka hubweka kama mbwa.

16 Lakini mimi nitaimba juu ya nguvu zako,

wakati wa asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

na kimbilio langu wakati wa shida.

17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa,

wewe, Ee Mungu ndiwe ngome yangu,

Mungu unipendaye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/59-00e3ed39a1437da771044d392663d592.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

8 + 11 =