Kuomba Ulinzi
(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Nyuzi Za Uimbaji. Zaburi Ya Daudi)
1 Ee Mungu, sikia kilio changu,
usikilize maombi yangu.
2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,
ninaita huku moyo wangu unadhoofika;
uniongoze kwenye mwamba
ule ulio juu kuliko mimi.
3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,
ngome imara dhidi ya adui.
4 Natamani kukaa hemani mwako milele
na kupata kimbilio chini ya uvuli wa mbawa zako.
5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,
umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.
6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake,
miaka yake kwa vizazi vingi.
7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi
mbele za Mungu milele;
amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.
8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako
na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/61-3ac274c7c3493b29ad55324abf7cd5cb.mp3?version_id=1627—