Zaburi 69

Kilio Cha Kuomba Msaada Wakati Wa Dhiki

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi)

1 Ee Mungu, uniokoe, kwa maana maji

yamenifika shingoni.

2 Ninazama kwenye vilindi vya matope,

pasipo mahali pa kukanyaga;

nimefika kwenye maji makuu,

mafuriko yamenigharikisha.

3 Nimechoka kwa kuomba msaada,

koo langu limekauka.

Macho yangu yanafifia,

nikimtafuta Mungu wangu.

4 Wale wanaonichukia bila sababu

ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;

wengi ni adui bila sababu,

wale wanaotafuta kuniangamiza.

Ninalazimishwa kurudisha

kitu ambacho sikuiba.

5 Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,

wala maovu yangu hayakufichika kwako.

6 Ee Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

wakutumainio wasiaibishwe

kwa ajili yangu;

wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu,

Ee Mungu wa Israeli.

7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,

aibu imefunika uso wangu.

8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,

mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe,

9 kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,

matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.

10 Ninapolia na kufunga,

wao hunitukana kwa kufanya hivyo.

11 Nilipovaa nguo ya gunia,

nilikuwa kitu cha kudharauliwa na watu.

12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,

nimekuwa wimbo wa walevi.

13 Lakini EeBwana, ninakuomba,

kwa wakati ukupendezao,

katika upendo wako mkuu;

Ee Mungu, unijibu

kwa wokovu wako wa hakika.

14 Uniokoe katika matope,

usiniache nizame;

niokoe na hao wanichukiao,

kutoka kwenye vilindi vya maji.

15 Usiache mafuriko yanigharikishe

au vilindi vinimeze,

au shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

16 EeBwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako;

kwa huruma zako nyingi unigeukie.

17 Usimfiche mtumishi wako uso wako,

uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.

18 Njoo karibu na uniokoe,

nikomboe kwa sababu ya adui zangu.

19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa,

kufedheheshwa na kuaibishwa,

adui zangu wote unawajua.

20 Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa,

nimetafuta wa kunihurumia,

lakini sikumpata ye yote,

wa kunituliza, lakini sikumpata ye yote.

21 Waliweka nyongo katika chakula changu

na walinipa siki nilipokuwa na kiu.

22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,

nayo iwe upatilizo na tanzi.

23 Macho yao yatiwe giza ili wasione,

migongo yao na ipinde milele.

24 Uwamwagie ghadhabu yako,

hasira yako kali na iwapate.

25 Mahali pao na pawe mahame,

asiwepo ye yote atakayeishi katika mahema yao.

26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,

na kuzungumza juu ya maumivu

ya wale uliowaumiza.

27 Walipize uovu juu ya uovu,

usiwaache washiriki katika wokovu wako.

28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima

na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.

29 Mimi niko katika maumivu na dhiki;

Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.

30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

31 Hili litampendezaBwanakuliko ng’ombe dume,

zaidi ya fahali akiwa

na pembe na kwato zake.

32 Maskini wataona na kufurahi,

ninyi mnaomtafuta Mungu,

mioyo yenu na iishi!

33 Bwanahuwasikia wahitaji

na wala hadharau watu wake waliotekwa.

34 Mbingu na dunia na vimsifu,

bahari na vyote viendavyo ndani yake,

35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni

na kuijenga tena miji ya Yuda.

Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki.

36 Watoto wa watumishi wake watairithi

na wale wote walipendao jina lake

wataishi humo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/69-14c7d602a9ec7a028a4fa2d12acf7a7d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × 4 =