Zaburi 83

Maombi Kwa Ajili Ya Kushindwa Kwa Adui Wa Israeli

(Zaburi Ya Asafu. Wimbo)

1 Ee Mungu, usinyamaze kimya,

usinyamaze, Ee Mungu usitulie.

2 Tazama watesi wako wanafanya fujo,

jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao.

3 Kwa hila wanafanya shauri dhidi ya watu wako,

wanafanya shauri baya dhidi ya wale unaowapenda.

4 Wanasema, “Njoni,

tuwaangamize kama taifa,

ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.”

5 Kwa nia moja wanapanga pamoja mashauri mabaya,

wanafanya muungano dhidi yako,

6 mahema ya Edomu na Waishmaeli,

ya Wamoabu na Wahagari,

7 Gebali, Amoni na Ameleki,

Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro.

8 Pia Ashuru wameungana nao

kuwapa nguvu wazao wa Loti.

9 Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani,

na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini

penye kijito cha Kishoni,

10 ambao waliangamia huko Endori

na wakawa kama takataka juu ya nchi.

11 Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zebu,

watawala wao kama Zeba na Zalmuna,

12 ambao walisema, “Na tumiliki nchi

ya malisho ya Mungu.”

13 Ee Mungu wangu, wapeperushe

kama mavumbi ya kisulisuli,

kama makapi yapeperushwayo na upepo.

14 Kama vile moto uteketezavyo msitu

au mwali wa moto unavyounguza milima,

15 kwa hiyo wafuatilie kwa tufani yako

na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.

16 Funika nyuso zao kwa aibu

ili watu walitafute jina lako, EeBwana.

17 Wao na waaibishwe na kufadhaishwa,

wao na waangamie kwa aibu.

18 Na wajue kwamba wewe,

ambaye jina lako niBwana,

kwamba wewe peke yako

ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/83-34518efc42844b96fe74402423a0cd6a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × five =