Zaburi 107

Kumsifu Mungu Kwa Wema Wake

1 MshukuruniBwana, kwa kuwa yeye ni mwema,

upendo wake wadumu milele.

2 Waliokombolewa waBwanana waseme hivi,

wale aliowaokoa kutoka katika mkono wa adui,

3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,

kutoka mashariki na magharibi,

kutoka kaskazini na kusini.

4 Baadhi yao walitangatanga jangwani,

hawakuona njia ya kuwafikisha katika mji

ambao wangeweza kuishi.

5 Walikuwa na njaa na kiu,

nafsi zao zikadhoofika.

6 Ndipo walipomliliaBwanakatika shida zao,

naye akawaokoa kutoka katika taabu zao.

7 Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi kwenye mji

ambao wangeweza kuishi.

8 Basi na wamshukuruBwana

kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu

kwa wanadamu,

9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu

na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu,

wafungwa wakiteseka katika minyororo,

11 kwa sababu walikuwa wameasi

dhidi ya maneno ya Mungu

na kudharau shauri

la Aliye Juu Sana.

12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu;

walijikwaa na hapakuwepo

na ye yote wa kuwasaidia.

13 Ndipo walipomliliaBwanakatika shida yao,

naye akawaokoa kutoka kwenye taabu yao.

14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu

na akavunja minyororo yao.

15 Basi na wamshukuruBwana

kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu

kwa wanadamu,

16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba

na kukata mapingo ya chuma.

17 Wengine wakawa wajinga kutokana na uasi wao,

wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.

18 Wakachukia kabisa vyakula vyote,

wakakaribia malango ya mauti.

19 Ndipo walipomliliaBwanakatika shida yao,

naye akawaokoa kutoka kwenye taabu yao.

20 Akalituma neno lake na kuwaponya,

akawaokoa kutoka maangamizo.

21 Basi na wamshukuruBwana

kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu

kwa wanadamu,

22 Na watoe dhabihu za kushukuru,

na wasimulie matendo yake

kwa nyimbo za furaha.

23 Wengine walisafiri baharini kwa meli,

walikuwa wafanya biashara kwenye maji makuu.

24 Waliziona kazi zaBwana,

matendo yake ya ajabu katika kilindi.

25 Kwa maana alisema

na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu.

26 Yakainuka juu mbinguni yakashuka chini hadi vilindini,

katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.

27 Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi,

ujanja wao ukafikia ukomo.

28 Ndipo walipomliliaBwanakatika shida yao,

naye akawatoa kutoka kwenye taabu yao.

29 Akatuliza dhoruba kwa mnong’ono,

mawimbi ya bahari yakatulia.

30 Walifurahi ilipokuwa shwari,

naye akawaongoza hadi kwenye bandari waliyoitamani.

31 Basi na wamshukuruBwana

kwa upendo wake usiokoma,

na kwa matendo yake ya ajabu

kwa wanadamu,

32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu,

na wamsifu katika baraza la wazee.

33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa,

chemchemi za maji zitiririkazo

kuwa ardhi yenye kiu,

34 nchi izaayo ikawa ya chumvi na isiyofaa,

kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.

35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji,

nayo ardhi kame

kuwa chemchemi za maji zitiririkazo;

36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo,

nao wakajenga mji wakaishi humo.

37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu,

nayo ikazaa matunda mengi,

38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana,

wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.

39 Kisha hesabu yao ilipungua,

walinyenyekeshwa kwa kuonewa,

maafa na huzuni,

40 yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu,

aliwafanya watangetange

kwenye nyika isiyo na njia.

41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao,

na kuongeza jamaa zao

kama makundi ya kondoo.

42 Wanyofu wataona na kufurahi,

lakini waovu wote

watafunga vinywa vyao.

43 Ye yote aliye na hekima, ayasikie mambo haya

na atafakari upendo mkuu waBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/107-26377a1b5677ac9f51893a4d49503e03.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen + 2 =