Zaburi 106

Wema Wa Bwana Kwa Watu Wake

1 MsifuniBwana.

MshukuruniBwana, kwa kuwa ni mwema;

upendo wake wadumu milele.

2 Ni nani awezaye kusimulia

matendo makuu yaBwana

au kutangaza kikamilifu sifa zake?

3 Heri wale wanaodumisha haki,

ambao daima wanafanya yaliyo mema.

4 EeBwana, unikumbuke unapowatendea mema watu wako,

uwe msaada wangu unapowaokoa,

5 ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako,

niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako,

na kuungana na urithi wako katika kukusifu.

6 Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda,

tumekosa na tumetenda kwa uovu.

7 Wakati baba zetu walipokuwa Misri,

hawakuzingatia maajabu yako,

wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako,

bali waliasi kando ya bahari,

Bahari ya Shamu.

8 Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake,

ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.

9 Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka,

akawaongoza katika vilindi vyake

kama vile jangwani.

10 Aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui;

kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.

11 Maji yaliwafunika adui zao,

hakunusurika hata mmoja.

12 Ndipo walipoamini ahadi zake,

nao wakaimba sifa zake.

13 Lakini mara walisahau aliyowatendea,

wala hawakungojea shauri lake.

14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao,

walimjaribu Mungu nyikani.

15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba,

lakini akatuma juu yao

ugonjwa wa kudhoofisha.

16 Kambini waliwaonea wivu Mose na Aroni,

ambaye alikuwa amewekwa wakfu kwaBwana.

17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani,

ikawazika Abiramu na kundi lake.

18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao,

mwali wa moto uliwateketeza waovu.

19 Huko Horebu walitengeneza ndama

na kuabudu sanamu ya kusubu

kutoka kwenye dhahabu.

20 Waliubadilisha Utukufu wa Mungu

na kuipa sanamu ya fahali,

ambaye hula majani.

21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa,

ambaye alikuwa ametenda

mambo makuu huko Misri,

22 miujiza katika nchi ya Hamu

na mambo ya kutisha

huko Bahari ya Shamu.

23 Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza:

kama Mose mteule wake,

asingesimama kati yao na Mungu

kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.

24 Kisha waliidharau ile nchi nzuri,

hawakuiamini ahadi yake.

25 Walinung’unika ndani ya mahema yao,

wala hawakumtiiBwana.

26 Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa

kwamba atawafanya waanguke jangwani,

27 kuwatawanya wazao wao waanguke

miongoni mwa mataifa

na kuwatawanya katika nchi zote.

28 Walijifunga nira na Baali wa Peori,

wakala dhabihu zilizotolewa

kwa miungu isiyo na uhai,

29 waliichochea hasira yaBwana,

wakamkasirisha kwa matendo yao maovu,

tauni ikazuka katikati yao.

30 Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati,

nayo tauni ikazuiliwa.

31 Hili likahesabiwa kwake haki,

kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.

32 Kwenye maji ya Meriba, walimkasirishaBwana,

janga likampata Mose kwa sababu yao;

33 kwa maana walimwasi Roho wa Mungu

na maneno yakatoka midomoni kwa Mose bila kufikiri.

34 Hawakuyaangamiza yale mataifa

kamaBwanaalivyowaagiza,

35 bali walijichanganya na mataifa

na wakazikubali desturi zao.

36 Waliabudu sanamu zao,

zikawa mtego kwao.

37 Wakawatoa wana wao

na binti zao dhabihu kwa mashetani.

38 Walimwaga damu isiyo na hatia,

damu za wana wao na binti zao,

ambao waliwatoa dhabihu

kwa sanamu za Kanaani,

nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.

39 Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda;

kwa matendo yao wenyewe

wakajifanyia ukahaba.

40 Kwa hiyoBwanaakawakasirikia watu wake

na akauchukia sana urithi wake.

41 Akawakabidhi kwa mataifa

na adui zao wakawatawala.

42 Adui zao wakawaonea

na kuwatia chini ya mamlaka yao.

43 Mara nyingi aliwaokoa

lakini wao walikuwa wamezama kwenye uasi,

nao wakajiharibu katika dhambi zao.

44 Lakini akaangalia mateso yao

wakati aliposikia kilio chao;

45 kwa ajili yao akakumbuka Agano lake

na kutokana na upendo wake mkuu

akapooza hasira yake.

46 Akawafanya wahurumiwe

na wote waliowashikilia mateka.

47 EeBwanaMungu wetu, utuokoe,

utukusanye tena kutoka kwa mataifa,

ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu

na kujisifu katika sifa zako.

48 AtukuzweBwana, Mungu wa Israeli,

tangu milele na hata milele.

Watu wote na waseme, “Amen!”

MsifuniBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/106-e75590dd685bd20a7f4923c70dfa3630.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 − 6 =