Ahadi Ya Kuishi Kwa Uadilifu Na Kwa Haki
(Zaburi Ya Daudi)
1 Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako;
kwako wewe, EeBwana,
nitaimba sifa.
2 Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama:
utakuja kwangu lini?
Nitatembea nyumbani mwangu
kwa moyo usio na lawama.
3 Sitaweka mbele ya macho yangu
kitu kiovu.
Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani;
hawatashikamana nami.
4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami;
nitajitenga na kila ubaya.
5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri,
huyo nitamnyamazisha;
mwenye macho ya dharau
na moyo wa kiburi sitamvumilia.
6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,
ili waweze kuishi pamoja nami;
yeye ambaye moyo wake
hauna lawama atanitumikia.
7 Mdanganyifu hatakaa
nyumbani mwangu,
yeye asemaye kwa uongo
hatasimama mbele yangu.
8 Kila asubuhi nitawanyamazisha
waovu wote katika nchi;
nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya
kutoka katika mji waBwana.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/101-94c837dab923fee4400aad2840d4c3c4.mp3?version_id=1627—