Zaburi 79

Maombi Kwa Ajili Ya Wokovu Wa Taifa

(Zaburi Ya Asafu)

1 Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako,

wamelinajisi Hekalu lako takatifu,

wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.

2 Wametoa maiti za watumishi

kuwa chakula cha ndege wa angani

na nyama ya watakatifu wako

kwa wanyama wa nchi.

3 Wamemwaga damu kama maji

kuzunguka Yerusalemu yote,

wala hakuna ye yote wa kuwazika.

4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu,

cha dharau na mzaha

kwa wale wanaotuzunguka.

5 Hata lini, EeBwana?

Je, wewe utakasirika milele?

Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?

6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali,

juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,

7 kwa maana wamemrarua Yakobo

na kuharibu nchi ya makao yake.

8 Usituhesabie dhambi za baba zetu,

huruma yako na itujie hima,

kwa maana tu wahitaji mno.

9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie,

kwa ajili ya utukufu wa jina lako;

tuokoe na kutusamehe dhambi zetu

kwa ajili ya jina lako.

10 Kwa nini mataifa waseme,

“Yuko wapi Mungu wenu?”

Mbele ya macho yetu,

dhihirisha kati ya mataifa

kwamba unalipiza kisasi

cha damu iliyomwagwa

ya watumishi wako.

11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako;

kwa nguvu za mkono wako

hifadhi wale waliohukumiwa kufa.

12 Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao

aibu walizovurumisha juu yako, EeBwana.

13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako,

tutakusifu milele;

toka kizazi hadi kizazi

tutasimulia sifa zako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/79-be3042ef5e97803f3fb6e99253d7d312.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 + seventeen =