Zaburi 66

Kusifu Mungu Kwa Ajili Ya Wema Wake

(Kwa Mwimbishaji: Wimbo. Zaburi)

1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!

2 Imbeni utukufu wa jina lake;

mpeni sifa zake kwa utukufu!

3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!

Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba

adui wananyenyekea mbele zako.

4 Dunia yote yakusujudia,

wanakuimbia wewe sifa,

wanaliimbia sifa jina lako.”

5 Njoni mwone yale Mungu aliyoyatenda,

mambo ya kutisha aliyoyatenda

miongoni mwa wanadamu!

6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu,

wakapita kati ya maji kwa miguu,

njoni, tumshangilie.

7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,

macho yake huangalia mataifa yote,

waasi na wasithubutu kujiinua dhidi yake.

8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,

sauti ya sifa yake na isikike,

9 ameyahifadhi maisha yetu

na kuizuia miguu yetu kuteleza.

10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu,

ukatusafisha kama fedha.

11 Umetuingiza kwenye nyavu

na umetubebesha mizigo mizito

migongoni mwetu.

12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,

tulipita kwenye moto na kwenye maji,

lakini ulituleta kwenye nchi

iliyojaa utajiri tele.

13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa

na kukutimizia nadhiri zangu:

14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi

na nilizotamka kwa kinywa changu

nilipokuwa katika shida.

15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono

na sadaka za kondoo waume,

nitakutolea mafahali na mbuzi.

16 Njoni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,

nami niwaambie aliyonitendea.

17 Nilimlilia kwa kinywa changu,

sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.

18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,

Bwana asingekuwa amenisikiliza;

19 lakini hakika Mungu amenisikiliza

na amesikia sauti yangu katika maombi.

20 Sifa apewe Mungu,

ambaye hakulikataa ombi langu

wala kunizuilia upendo wake!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/66-70ae261997c556379da49c61557244d9.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × two =