Zaburi 65

Kusifu Na Kushukuru

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi. Wimbo)

1 Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni;

kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.

2 Ee wewe usikiaye maombi,

kwako wewe watu wote watakuja.

3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi,

wewe ulisamehe makosa yetu.

4 Heri wale uliowachagua

na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako!

Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako,

mema ya Hekalu lako takatifu.

5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki,

Ee Mungu Mwokozi wetu,

tumaini la miisho yote ya duniani

na la bahari zilizo mbali sana,

6 uliyeumba milima kwa uwezo wako,

ukiwa umejivika nguvu,

7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari,

ngurumo za mawimbi yake,

na ghasia za mataifa.

8 Wale wanaoishi mbali sana

wanaogopa maajabu yako,

kule asubuhi ipambazukiapo

na kule jioni inakofifilia

umeziita nyimbo za furaha.

9 Waitunza nchi na kuinyeshea,

waitajirisha kwa wingi.

Vijito vya Mungu vimejaa maji

ili kuwapa watu nafaka,

kwa maana wewe umeviamuru.

10 Umeilowesha mifereji yake

na kusawazisha kingo zake;

umeilainisha kwa manyunyu

na kuibariki mimea yake.

11 Umeuvika mwaka taji ya baraka,

magari yako yanafurika kwa wingi.

12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha;

vilima vimevikwa furaha.

13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama,

na mabonde yamepambwa kwa mavuno;

vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/65-f12412d24536665e5d22b9fcfae35ba2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen − 15 =