Kuomba Ulinzi Dhidi Ya Maadui
(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)
1 Ee Mungu, unisikie, ninapoeleza lalamiko langu,
uyahifadhi maisha yangu kutokana
na vitisho vya adui.
2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu,
kutokana na zile kelele
za kundi la watenda mabaya.
3 Wanaonoa ndimi zao kama panga
na kuelekeza maneno yao
kama mishale ya kufisha.
4 Hutupa mishale kutoka kwenye mavizio
kwa mtu asiye na hatia,
humrushia ghafula bila woga.
5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake
katika mipango mibaya;
huzungumza juu ya kuficha mitego yao,
nao husema, “Ni nani ataiona?”
6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema,
“Tumebuni mpango mkamilifu!”
Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.
7 Bali Mungu atawapiga wao kwa mshale,
nao utawapata ghafula na kuanguka.
8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao
na kuwaleta kwenye maangamizi;
wote wawaonao watatikisa vichwa vyao
kwa dharau.
9 Wanadamu wote wataogopa,
watatangaza kazi za Mungu
na kutafakari yale aliyoyatenda.
10 Wenye haki na wafurahi katikaBwana,
na wakimbilie kwake;
wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/64-0954e5e1243e91350d7b817e5d554bc1.mp3?version_id=1627—