Uovu Wa Wanadamu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Mahalathi. Utenzi Wa Daudi)
1 Mpumbavu anasema moyoni mwake,
“Hakuna Mungu.”
Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa,
hakuna hata mmoja atendaye mema.
2 Mungu huwachungulia wanadamu chini
kutoka mbinguni
aone kama wako wenye akili,
wo wote wanaomtafuta Mungu.
3 Kila mmoja amegeukia mbali,
wameharibika wote pamoja,
hakuna hata mmoja atendaye mema,
naam! Hata mmoja.
4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza,
wale ambao huwala watu wangu
kama watu walavyo mkate,
na ambao hawamwiti Mungu?
5 Hapo watatetemeka kwa hofu kuu,
ambapo hakuna cha kutetemesha.
Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia;
umewaaibisha, kwa sababu Mungu amewadharau.
6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni!
Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake,
Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/53-b53885ea57ed4462561650e8e252af99.mp3?version_id=1627—