Zaburi 51

Kuomba Msamaha

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Baada Ya Kukemewa Na Nabii Nathani Kwa Kuzini Na Bathsheba)

1 Ee Mungu, unihurumie,

kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

kwa kadiri ya huruma yako kuu

uyafute makosa yangu.

2 Unioshe na uovu wangu wote

na unitakase dhambi yangu.

3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

ili uthibitike kuwa mkweli unenapo

na kuwa na haki utoapo hukumu.

5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,

mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba

kwa mama yangu.

6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,

ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.

7 Unioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,

unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

8 Unipe kusikia furaha na shangwe,

mifupa uliyoiponda na ifurahi.

9 Uufiche uso wako usiitazame dhambi yangu

na uufute uovu wangu wote.

10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

11 Usinitupe kutoka mbele zako

wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.

12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,

unipe roho ya utii, ili initegemeze.

13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,

na wenye dhambi watakugeukia wewe.

14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye,

niokoe na hatia ya kumwaga damu,

ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.

15 EeBwana, fungua midomo yangu,

na kinywa changu kitatangaza sifa zako.

16 Wewe hupendezwi na dhabihu,

au ningaliileta,

hufurahii sadaka za kuteketezwa.

17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,

moyo uliovunjika wenye toba,

Ee Mungu, hutaudharau.

18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,

ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.

19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,

sadaka nzima za kuteketezwa

za kukupendeza sana,

pia mafahali watatolewa

madhabahuni mwako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/51-d7e86911e361376b39ce500423ad55e4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

9 + eight =