Zaburi 49

Upumbavu Wa Kutegemea Mali

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Wana Wa Kora)

1 Sikieni haya, enyi mataifa yote,

sikilizeni, ninyi wote mkaao dunia hii.

2 Wakubwa kwa wadogo,

matajiri na maskini pamoja:

3 Kinywa changu kitasema maneno ya hekima,

usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu.

4 Nitatega sikio langu nisikilize mithali,

nitafafanua kitendawili kwa zeze:

5 Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja,

wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,

6 wale wanaotegemea mali zao

na kujivunia utajiri wao mwingi?

7 Hakuna mwanadamu awaye yote

awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,

au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.

8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa,

hakuna malipo yo yote yanayotosha,

9 ili kwamba aishi milele

na asione uharibifu.

10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa;

wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia

na kuwaachia wengine mali zao.

11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele,

makao yao vizazi vyote;

ingawa walikuwa na mashamba

na kuyaita kwa majina yao.

12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu;

anafanana na mnyama aangamiaye.

13 Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe,

pia wa wafuasi wao,

waliothibitisha misemo yao.

14 Kama kondoo wamewekewa kwenda kaburini

na kifo kitawala.

Wanyofu watawatawala asubuhi,

maumbile yao yataozea kaburini,

mbali na majumba yao makubwa ya fahari.

15 Lakini Mungu atakomboa uhaiwangu na kaburi,

hakika atanichukua kwake.

16 Usitishwe mtu anapotajirika,

fahari ya nyumba yake inapoongezeka,

17 kwa maana hatachukua cho chote atakapokufa,

fahari yake haitashuka pamoja naye.

18 Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri,

na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa,

19 atajiunga na kizazi cha baba zake,

ambao hawataona kamwe nuru ya uzima.

20 Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu

ni kama wanyama waangamiao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PSA/49-4c002caae8dd81754a149ad4bb43413d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen − eight =