Isaya 58

Mfungo Wa Kweli

1 “Piga kelele, usizuie.

Paza sauti yako kama tarumbeta.

Watangazieni watu wangu uasi wao

na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.

2 Kwa maana kila siku hunitafuta,

wanaonekana kutaka kujua njia zangu,

kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lile lililo sawa

na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake.

Hutaka kwangu maamuzi ya haki,

nao hutamani Mungu awakaribie.

3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?

Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’

“Lakini katika siku ya kufunga kwenu,

mnafanya mnavyotaka

na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.

4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,

na kupigana ninyi kwa ninyi

kwa ngumi za uovu.

Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo

na kutazamia sauti zenu

kusikiwa huko juu.

5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,

siku moja tu kwa ajili ya mtu kujinyenyekeza?

Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama unyasi

Na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?

Je, huo ndio mnaouita mfungo,

siku iliyokubalika kwaBwana?

6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

kufungua minyororo ya udhalimu

na kufungua kamba za nira,

kuwaweka huru walioonewa

na kuvunja kila nira?

7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

na kuwapatia maskini

wasiokuwa na makao hifadhi,

unapomwona aliye uchi, umvike,

wala si kumkimbia mtu

wa nyama na damu yako mwenyewe?

8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

na uponyaji wako utatokea upesi;

ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

na utukufu waBwana

utakuwa mlinzi nyuma yako.

9 Ndipo utaita, nayeBwanaatajibu,

utalia kuomba msaada,

naye atasema: Mimi hapa.

“Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

kutokunyosha kidole na kuzungumza maovu,

10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

ndipo nuru yenu itakapong’aa gizani,

nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

11 Bwanaatakuongoza siku zote,

atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

naye ataitia nguvu mifupa yako.

Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

kama chemchemi ambayo maji yake

hayakauki kamwe.

12 Watu wako watajenga tena magofu ya zamani

na kuinua misingi ya kale;

utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,

Mwenye Kufanya upya Barabara zenye Makazi.

13 “Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato

na kutokufanya kama vile upendavyo

katika siku yangu takatifu,

kama ukiita Sabato siku ya furaha

na siku takatifu yaBwanaya kuheshimiwa,

kama utaiheshimu kwa kutoenenda

katika njia zako mwenyewe

na kutokufanya yakupendezayo

au kusema maneno ya upuzi,

14 ndipo utakapojipatia furaha yako katikaBwana,

nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi

na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”

Kinywa chaBwanakimenena haya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/58-c7382a8cff973714fa434a93b7cf7d85.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 + seven =