Isaya 54

Utukufu Wa Baadaye Wa Sayuni

1 “Imba, Ewe mwanamke tasa,

wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto;

paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha,

ninyi ambao kamwe

hamkupata utungu wa kuzaa;

kwa sababu watoto wa mwanamke

aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume,”

asemaBwana.

2 “Panua mahali pa hema lako,

tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali,

wala usiyazuie;

ongeza urefu wa kamba zako,

imarisha vigingi vyako.

3 Kwa maana utaenea upande wa kuume

na upande wa kushoto;

wazao wako watayamiliki mataifa

na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa.

4 “Usiogope, wewe hutaaibika.

Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa.

Wewe utasahau aibu ya ujana wako,

wala hutakumbuka tena

mashutumu ya ujane wako.

5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

6 Bwanaatakuita urudi

kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa

na kuhuzunishwa rohoni;

kama mke aliyeolewa bado angali kijana

na kukataliwa,” asema Mungu wako.

7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

8 Katika ukali wa hasira

nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

lakini kwa fadhili za milele

nitakuwa na huruma juu yako,”

asemaBwanaMkombozi wako.

9 “Kwangu mimi hili ni kama siku za Noa,

nilipoapa kuwa maji ya Noa

kamwe hayatafunika tena dunia.

Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi,

kamwe sitawakemea tena.

10 Ijapotikisika milima na vilima viondolewe,

hata hivyo upendo wangu

usiokoma kwenu hautatikisika,

wala Agano langu la amani halitaondolewa,”

asemaBwana, mwenye huruma juu yenu.

11 “Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba

na usiyetulizwa,

nitakujenga kwa almasi,

nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.

12 Nitafanya minara yako ya akiki,

malango yako kwa vito ving’aavyo,

nazo kuta zako zote za mawe ya thamani.

13 Watoto wako wote watafundishwa naBwana,

nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.

14 Kwa haki utathibitika:

Kuonewa kutakuwa mbali nawe;

hutaogopa cho chote.

Hofu itakuwa mbali nawe;

haitakukaribia wewe.

15 Kama mtu ye yote akikushambulia,

haitakuwa kwa ruhusa yangu;

ye yote akushambuliaye

atajisalimisha kwako.

16 “Tazama, ni mimi niliyemwumba mhunzi

yeye afukutaye makaa kuwa moto,

na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake.

Tena ni mimi niliyemwambia mharabu

kufanya uharibifu mwingi;

17 hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

itakayofanikiwa,

nawe utauthibitisha kuwa mwongo

kila ulimi utakaokushitaki.

Huu ndio urithi wa watumishi waBwana

na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,”

asemaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/54-8a15f0a458827af4e4b879f5f7f872ed.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nine + sixteen =