Miungu Ya Babeli
1 Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama;
sanamu zao hubebwa na wanyama wa mizigo.
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,
mzigo kwa waliochoka.
2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,
wote wanakwenda utumwani pamoja.
3 “Nisikilizeni mimi, Ee nyumba ya Yakobo,
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.
4 Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi Mimi ndiye,
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.
Nimewahuluku nami nitawabeba,
nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.
5 “Mtanilinganisha na nani
au mtanihesabu kuwa sawa na nani?
Ni nani mtakayenifananisha naye
ili tuweze kulinganishwa?
6 Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao
na kupima fedha kwenye mizani;
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,
kisha huisujudia na kuiabudu.
7 Huiinua kuiweka mabegani na kuichukua;
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo,
wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.
Ingawa mtu huililia, haijibu;
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.
8 “Kumbukeni hili, mkajionyesha kuwa waume,
litieni akilini, liwekeni moyoni, enyi waasi.
9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;
mimi ndimi Mungu,
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.
10 Ni mimi tangazaye mwisho tangu mwanzo,
naam, tangu zamani za kale,
mambo ambayo hayajatendeka.
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;
kutoka nchi ya mbali,
mtu atakayetimiza kusudi langu.
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;
lile nililolipanga, hilo ndilo nitakalolitenda.
12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,
ninyi mlio mbali na haki.
13 Ninaleta haki yangu karibu,
haiko mbali;
wala wokovu wangu hautachelewa.
Nitawapa Sayuni wokovu,
Israeli utukufu wangu.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/46-eac1d24dd960b072cef119ad4ac2543f.mp3?version_id=1627—