Mwokozi Pekee Wa Israeli
1 Lakini sasa hili ndilo asemaloBwana,
yeye aliyekuumba, Ee Yakobo,
yeye aliyekuhuluku, Ee Israeli:
“Usiogope kwa maana nimekukomboa,
nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
2 Unapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
3 Kwa kuwa Mimi ndimiBwana, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako,
ninaitoa Misri kuwa fidia yako,
Kushi na Seba badala yako.
4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,
nami kwa kuwa ninakupenda,
nitatoa watu badala yako
na mataifa badala ya maisha yako.
5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,
nitawaleta watoto wako kutoka mashariki
na kukukusanya kutoka magharibi.
6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’
nayo kusini, ‘Usiwazuie.’
Walete wana wangu kutoka mbali
na binti zangu kutoka miisho ya dunia:
7 kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,
niliyemwumba kwa utukufu wangu,
niliyemhuluku na kumfanya.”
8 Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni,
wenye masikio lakini hawasikii.
9 Mataifa yote yanakutanika pamoja
na mataifa wanakusanyika.
Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya
na kututangazia mambo yaliyopita?
Walete mashahidi wao ili kuthibitisha kuwa walikuwa sahihi,
ili kwamba wengine waweza kusikia na kusema, “Ni kweli.”
10 “Ninyi ni mashahidi wangu,” asemaBwana,
“na mtumishi wangu niliyemchagua,
ili mpate kunijua na kuniamini
na kutambua kwamba Mimi ndiye.
Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa,
wala hatakuwepo mwingine baada yangu.
11 Mimi, naam mimi, ndimiBwana,
zaidi yangu hakuna mwokozi.
12 Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza:
Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu.
Ninyi ni mashahidi wangu,” asemaBwana,
“kwamba Mimi ndimi Mungu.
13 Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye.
Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa
kutoka katika mkono wangu.
Mimi ninapotenda,
ni nani awezaye kutangua?”
Huruma Za Mungu Na Kukosa Uaminifu Kwa Israeli
14 Hili ndiloBwanaasemalo,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Kwa ajili yenu nitatumana Babeli
na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi,
katika meli walizozionea fahari.
15 Mimi ndimiBwana, yeye Aliye Mtakatifu wako,
Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”
16 Hili ndilo asemaloBwana,
yeye aliyefanya njia baharini,
mahali pa kupita kwenye maji mengi,
17 aliyeyakokota magari ya vita na farasi,
jeshi pamoja na askari wa msaada,
nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe,
wamekomeshwa, wakazimika kama utambi:
18 “Msiyakumbuke mambo yaliyopita,
wala msiyatafakari mambo ya zamani.
19 Tazama, nitafanya jambo jipya!
Sasa litachipuka, je, hamtalitambua?
Nitafanya njia jangwani
na vijito vya maji katika nchi kame.
20 Wanyama wa mwituni wataniheshimu,
mbweha na bundi,
kwa sababu ninawapatia maji jangwani,
na vijito katika nchi kame,
ili kuwapa watu wale maji, ambao ni chaguo langu.
21 Watu wale niliowaumba kwa ajili yangu,
ili wapate kutangaza sifa zangu.
22 “Hata hivyo hukuniita mimi, Ee Yakobo,
hujajitaabisha kwa ajili yangu, Ee Israeli.
23 Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa,
wala kuniheshimu kwa dhabihu zako.
Sikukulemea kwa sadaka za nafaka
wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.
24 Hukuninunulia uvumba wo wote wenye manukato,
wala hukunipa kwa ukarimu
mafuta ya wanyama wa dhabihu zako.
Lakini umenilemea kwa dhambi zako
na kunitaabisha kwa makosa yako.
25 “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,
kwa ajili yangu mwenyewe,
wala sizikumbuki dhambi zako tena.
26 Tafakari mambo yaliyopita,
njoo na tuhojiane,
leta shauri lako, uweze kupewa haki yako.
27 Baba yako wa kwanza, alitenda dhambi,
wasemaji wako wameasi dhidi yangu.
28 Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako,
nami nitamtoa Yakobo aangamizwe
na Israeli adhihakiwe.
—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/43-9fe976cb0192986d267c1965feb29cf4.mp3?version_id=1627—