Isaya 32

Ufalme Wa Haki

1 Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu

na watawala watatawala kwa haki.

2 Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo

na kimbilio kutokana na dhoruba,

kama vijito vya maji jangwani

na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu.

3 Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena,

nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza.

4 Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa,

nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha.

5 Mpumbavu hataitwa tena muungwana

wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu.

6 Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu,

moyo wake hushughulika na uovu:

Hutenda mambo yasiyo ya uchaji Mungu,

na hueneza habari za makosa kuhusuBwana;

yeye huwaacha wenye njaa bila kitu

na wenye kiu huwanyima maji.

7 Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu,

hufanya mipango miovu

ili kumwangamiza maskini kwa uongo,

hata wakati ambapo hoja za mhitaji ni za haki.

8 Lakini mtu mwungwana hufanya mipango ya kiungwana

na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa.

Wanawake Wa Yerusalemu

9 Enyi wanawake wenye kuridhika sana,

amkeni na mnisikilize,

enyi binti mnaojisikia kuwa salama,

Sikieni lile ninalotaka kuwaambia!

10 Kwa zaidi kidogo ya mwaka

ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka,

mavuno ya zabibu yatakoma

na mavuno ya matunda hayatakuwepo.

11 Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika,

tetemekeni, kwa hofu enyi binti mnaojisikia salama!

Vueni nguo zenu,

vaeni nguo ya gunia viunoni mwenu.

12 Pigeni matiti yenu kwa ajili ya mashamba mazuri,

kwa ajili ya mizabibu iliyozaa vizuri

13 na kwa ajili ya nchi ya watu wangu,

nchi ambayo miiba na michongoma imemea:

naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha

na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe.

14 Ngome itaachwa,

mji wenye kelele nyingi utahamwa,

ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele,

mahali pazuri pa punda na malisho ya makundi ya kondoo,

15 mpaka Roho amwagwe juu yetu kutoka juu,

nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba

na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu.

16 Haki itakaa katika jangwa

na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba.

17 Matunda ya haki yatakuwa amani,

matokeo ya haki yatakuwa utulivu

na matumaini milele.

18 Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani,

katika nyumba zilizo salama,

katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu.

19 Hata mvua ya mawe iangushe msitu

na mji ubomolewe kabisa,

20 tazama jinsi utakavyobarikiwa,

ukipanda mbegu yako katika kila kijito,

na kuwaacha ng’ombe wako

na punda wajilishe kwa uhuru.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/32-3621b8ccce0d1fe34d61cabc87da26c8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 − 9 =