Ayubu 38

SEHEMU YA NNE: MUNGU ANAZUNGUMZA

Bwana Anamjibu Ayubu

1 KishaBwanaakamjibu Ayubu kutoka katika upepo wa kisulisuli. Akasema:

2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza

kwa maneno yasiyo na maarifa?

3 Jikaze kama mwanaume,

nami nitakuuliza swali,

nawe unijibu.

4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?

Niambie, kama unafahamu.

5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?

Hakika wewe unajua!

Ni nani aliyenyosha kamba ya kupimia juu yake?

6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,

au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,

7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja

na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango

ilipopasuka kutoka katika tumbo,

9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake

na kuyafungia katika giza nene,

10 Nilipoamuru mipaka yake

na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,

11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi,

hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?

12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,

au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,

13 yapate kushika miisho ya dunia

na kuwakung’uta waovu waliomo?

14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;

sura yake hukaa kama ile ya vazi.

15 Waovu huzuiliwa nuru yao,

nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.

16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?

Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?

17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?

Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?

18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?

Niambie kama unajua haya yote.

19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?

Nako masikani mwagiza ni wapi?

20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?

Unajua njia za kufika maskani mwake?

21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!

Kwani umeishi miaka mingi!

22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji

au kuona ghala za mvua ya mawe,

23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,

na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?

24 Ipi ni njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,

au mahali upepo wa mashariki

unaposambaziwa juu ya dunia?

25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi

na njia ya umeme wa radi,

26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,

jangwa lisilo na ye yote ndani yake,

27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa

na majani yaanze kumea ndani yake?

28 Je, mvua ina baba?

Ni nani baba azaaye matone ya umande?

29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani?

Ni nani aliyezaa ukungu kutoka mbinguni

30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,

wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?

31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?

Waweza kulegeza kamba za Orioni?

32 Waweza kuliongoza kundi la nyota kwa majira yake

au kuongoza Dubu na watoto wake?

33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?

Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?

34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni

na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?

35 Wewe je, hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?

Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?

36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima

au kuzipa akili ufahamu?

37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?

Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni

38 wakati mavumbi yawapo magumu

na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?

39 “Je, utamwindia simba jike mawindo

na kuwashibisha simba wenye njaa

40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao

au wakivizia kichakani?

41 Ni nani ampaye kunguru chakula

wakati makinda yake yanapomlilia Mungu

yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/38-7c604a5e83e01c6fdafe8560184cbdb2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen + 5 =