Waefeso 5

Kuenenda Nuruni

1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao,

2 Mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.

3 Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yo yote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu.

4 Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu.

5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Mwasherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu.

6 Mtu ye yote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii.

7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.

8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru

9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli),

10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana.

11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni.

12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.

13 Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana,

14 kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:

“Amka, wewe uliyelala,

ufufuke kutoka katika wafu,

naye Kristo atakuangazia.”

15 Kwa hiyo iweni waangalifu jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima,

16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu.

17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini yaliyo mapenzi ya Bwana.

18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho.

19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu,

20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

Mafundisho Kuhusu Wake Na Waume

22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana.

23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake.

24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.

25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake

26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake,

27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lo lote, bali takatifu lisilo na hatia.

28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake.

30 Sisi tu viungo vya mwili wake.

31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.”

32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa.

33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/5-fbf0b82424bfee2a26b8eef58e24dfc6.mp3?version_id=1627—

Waefeso 6

Mafundisho Kuhusu Watoto Na Wazazi

1 Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema.

2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi,

3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

Mafundisho Kuhusu Watumwa Na Mabwana

5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo.

6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo.

7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu.

8 Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lo lote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.

9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

Silaha Za Mungu

10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.

14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani.

16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu.

18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri,

20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

Salamu Za Mwisho

21 Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya sasa.

22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali zetu, na awatie moyo.

23 Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo.

24 Neema iwe na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo wa dhati. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EPH/6-ad13160cfa1b084b4fb41d5b64bc2c04.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 1

Salamu

1 Paulo mtume: si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo na Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu;

2 na ndugu wote walio pamoja nami:

Kwa makanisa ya Galatia:

3 Neema iwe nanyi na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo,

4 aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa kutoka katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu.

5 Utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Hakuna Injili Nyingine

6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata injili nyingine,

7 ambayo kwa kweli si injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo.

8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele!

9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu ye yote atawahubiria injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

Paulo Ameitwa Na Mungu

11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu.

12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.

13 Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa Kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza.

14 Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilikuwa na bidii kubwa katika desturi za baba zangu.

15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake,

16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu ye yote,

17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.

18 Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefana nilikaa naye siku kumi na tano.

19 Lakini sikumwona mtume mwingine ye yote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana.

20 Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo.

21 Baadaye nilikwenda sehemu za Syriana Kilikia.

22 Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo.

23 Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.”

24 Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/1-649c2f7f95ab2e700f543da9f9e1b989.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 2

Paulo Akubaliwa Na Mitume

1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami.

2 Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure.

3 Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa.

4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani,

5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.

6 Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea cho chote.

7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi.

8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu Mataifa.

9 Basi, Yakobo, Kefana Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi tuende kwa watu Mataifa na wao waende kwa Wayahudi.

10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.

Paulo Ampinga Petro Huko Antiokia

11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi.

12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara.

13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.

14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?

Wayahudi Na Watu Mataifa Wanaokolewa Kwa Imani

15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu Mataifa,

16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mmoja atakae hesabiwa haki.

17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi, je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!

18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji.

19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu.

20 Nimesulibiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/2-7872fb98b94c1694841c8c00bf7bd0f6.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 3

Imani Au Kushika Sheria?

1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaloga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulibiwa.

2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia?

3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili?

4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure!

5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

6 Kama vile Abrahamu, alivyomwamini Mungu ikahesabiwa kwake kuwa haki.

7 Fahamuni basi kwamba wale walio na imani hao ndio watoto wa Abrahamu.

8 Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.”

9 Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

Sheria Na Laana

10 Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria, wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Amelaaniwa mtu yule asiyeshika na kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.”

11 Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu ye yote anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

12 Lakini sheria haitegemei imani, kinyume chake, “Ye yote atendaye matendo ya sheria ataishi kwa sheria.”

13 Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.”

14 Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

Sheria Na Ahadi

15 Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka katika maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii.

16 Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo.

17 Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kulibatilisha.

18 Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kusudi La Sheria

19 Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamuriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.

20 Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21 Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria.

22 Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe.

24 Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani.

25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

Watoto Wa Mungu

26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani.

27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo.

28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu.

29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/3-c03f3a49d19911af5d993d60ec187ce0.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 4

1 Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi akiwa bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote.

2 Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake.

3 Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu.

4 Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,

5 kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu.

6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.”

7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

Paulo Awashawishi Wagalatia

8 Zamani, mlipokuwa hamumjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu.

9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu ambazo mnataka ziwafanye tena watumwa?

10 Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka!

11 Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.

12 Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lo lote baya.

13 Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria injili,

14 ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu.

15 Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imekwenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngeng’oa macho yenu na kunipa mimi.

16 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia kweli?

17 Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku.

18 Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu.

19 Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea utungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu.

20 Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.

Mfano Wa Hagari Na Sara

21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema?

22 Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru.

23 Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

24 Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza, ni lile lililofanyika katika mlima wa Sinai, lizaalo watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hagari.

25 Basi Hagari anawakilisha mlima Sinai ulioko Arabuni na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake.

26 Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu.

27 Kwa maana imeandikwa:

“Furahi, wewe uliye tasa

wewe usiyezaa;

paza sauti, imba kwa furaha,

wewe usiyepatwa na utungu;

kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ni wengi

kuliko watoto wa yule aliye na mume.”

28 Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaki, tu watoto wa ahadi.

29 Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa.

30 Lakini maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.”

31 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/4-84e7bdaec3a31f486347619ea2b12d16.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 5

Uhuru Ndani Ya Kristo

1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia cho chote.

3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote.

4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.

5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

6 Kwa maana ndani ya Kristo, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri, ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita.

9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.”

10 Nina hakika katika Bwana kwa habari yenu kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu awaye yote anayewachanganya anastahili adhabu.

11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini basi bado niteswe na Wayahudi? Ukweli kwamba bado wananitesa, ni ushahidi kwamba bado ninahubiri wokovu kupitia msalaba wa Kristo peke yake.

12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.

14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

Maisha Ya Kiroho

16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, nayo Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.

18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,

20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.

25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.

26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/5-0a09bd629b94c9a5d7636f4632568b9f.mp3?version_id=1627—

Wagalatia 6

Chukulianeni Mizigo

1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejezeni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.

2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

3 Kama mtu ye yote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.

4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.

5 Kwa maana, kila mtu atauchukuwa mzigo wake mwenyewe.

6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.

8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake, atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.

10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Si Kutahiriwa Bali Kuwa Kiumbe Kipya

11 Angalieni ni herufi gani kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanaotaka wawalazimishe kutahiriwa, sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo.

13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu.

14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu cho chote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu.

15 Kwa maana katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!

16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii na juu ya Israeli wa Mungu.

17 Hatimaye, tangu sasa mtu ye yote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae pamoja na roho zenu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/6-d9677d634dbb0670988eeccdee00c81a.mp3?version_id=1627—

2 Wakorintho 1

Salamu

1 Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu na Timotheo ndugu yetu,

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko Akaya yote:

2 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Mungu Wa Faraja Yote

3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote.

4 Yeye atufarijiye katika taabu zetu zote, ili tuweze kuwafariji wale walio katika taabu yo yote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu.

5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyotiririka ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.

6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu, kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata.

7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.

8 Ndugu wapendwa, hatutaki msijue kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi.

9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu.

10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo ataendelea kutuokoa. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba atatuokoa tena.

11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka tulizopata kwa maombi ya wengi.

Paulo Aahirisha Ziara

12 Basi haya ndiyo majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeenenda katika ulimwengu na hasa katika uhusiano wetu na ninyi, katika utakatifu na uaminifu utokao kwa Mungu. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu.

13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba,

14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu.

15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili.

16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Uyahudi.

17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kidunia, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?

18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajawa “Ndiyo na Siyo.”

19 Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye tulimhubiri kwenu: Mimi, Silvanona Timotheo, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo,” bali katika yeye siku zote ni “Ndiyo.”

20 Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni “Ndiyo.” Kwa sababu hii ni katika yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu.

21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Ametutia mafuta

22 kwa kututia muhuri wake na kutupa Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia kile kijacho.

23 Mungu ni shahidi wangu kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kuwahurumia ninyi sikurudi Korintho.

24 Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CO/1-50c1c677c34a85ad1c599ed14c5e7ed2.mp3?version_id=1627—

2 Wakorintho 2

1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi.

2 Kwa kuwa kama nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha?

3 Niliandika hivyo kama nilivyofanya, ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao wangenifanya nifurahi. Nina uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu.

4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana kwa moyo wangu tena kwa machozi mengi, shabaha yangu si ili niwasababishe mhuzunike bali kuwaonyesha kina cha upendo wangu kwenu.

Msamaha Kwa Mwenye Dhambi

5 Lakini ikiwa mtu ye yote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi.

6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha.

7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi.

8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake.

9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo.

10 Kama ninyi mkimsamehe mtu ye yote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu cho chote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.

Wasiwasi Wa Paulo Huko Troa

12 Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango,

13 bado nilikuwa sina utulivu akilini mwangu kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao nikaenda Makedonia.

14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kwa kupitia sisi hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.

15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea,

16 sisi kwa wale wanaopotea ni harufu ya mauti iletayo mauti, lakini kwa wale wanaookolewa sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?

17 Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CO/2-4b7999417f41f999a86db19e88a21f84.mp3?version_id=1627—