Yoshua 23

Yoshua Anawaaga Viongozi

1 Baada ya muda mrefu kupita, nayeBwanaalikuwa amewapa Israeli raha mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo alikuwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana,

2 akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa wao, na kuwaambia: “Mimi ni mzee na umri umeendelea sana.

3 Ninyi wenyewe mmeona kila kituBwanaMungu wenu, alichowatendea makabila haya yote kwa ajili yenu, ilikuwa niBwanaMungu wenu aliyewapigania.

4 Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa ajili ya makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari ile kuu upande wa magharibi.

5 BwanaMungu wenu mwenyewe, atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vileBwanaMungu wenu alivyowaahidi.

6 “Iweni hodari sana, iweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto.

7 Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia.

8 Bali mtashikamana kwa uthabiti na Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.

9 “Bwanaamewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna ye yote aliyeweza kusimama mbele yenu.

10 Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu, kwa kuwaBwanaMungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi.

11 Kwa hiyo iweni waangalifu sana kumpendaBwanaMungu wenu.

12 “Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao,

13 basi mwe na hakika kuwaBwanaMungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu na miiba machoni penu, mpaka mwangamie kutoka katika nchi hii nzuri, ambayoBwanaMungu wenu amewapa.

14 “Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zo zote njemaBwanaMungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia.

15 Bali kama vile ambavyo kila ahadi njema yaBwanaMungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyoBwanaataleta maovu yote aliyosema, mpaka awe amewaangamiza kutoka katika nchi hii nzuri aliyowapa.

16 Kama mkilivunja Agano laBwanaMungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira yaBwanaitawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia mara kutoka katika nchi nzuri aliyowapa ninyi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/23-66bad3d200ae96492b40ac9253ae7665.mp3?version_id=1627—

Yoshua 24

Agano Lafanywa Upya Huko Shekemu

1 Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.

2 Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Abrahamu na Nahori, waliishi ng’ambo ya Mto Eufrati nao waliiabudu miungu mingine.

3 Lakini nilimwondoa baba yenu Abrahamu kutoka nchi hiyo ng’ambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaki,

4 naye Isaki nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.

5 “ ‘Kisha nikawatuma Mose na Aroni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa huko.

6 Nilipowatoa baba zenu katika nchi ya Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka kwenye Bahari ya Shamu.

7 Lakini wakamliliaBwanawakitaka msaada, Mungu akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.

8 “ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki ya Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao.

9 Wakati Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani.

10 Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.

11 “ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raia wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu.

12 Nikatuma manyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi.

13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga, mkaishi ndani yake na kula mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’

14 “Sasa basi mcheniBwanana kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ng’ambo ya Mto Eufrati na huko Misri, nanyi mtumikieniBwana.

15 Lakini msipoona vyema kumtumikiaBwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo Eufrati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikiaBwana.”

16 Ndipo hao watu wakajibu, “Hili liwe mbali nasi la kumsahauBwanana kuitumikia miungu mingine!

17 Ilikuwa niBwanaMungu wetu mwenyewe aliyetutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao.

18 Bwanaakawafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikiaBwana, kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”

19 Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikiaBwana. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu.

20 Ikiwa mkimwachaBwanana kuitumikia miungu migeni, yeye atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”

21 Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikiaBwana.”

22 Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikiaBwana.”

Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”

23 Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni iliyo katikati yenu, nanyi mtoleeniBwana, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”

24 Nao watu wakamwambia Yoshua, “TutamtumikiaBwanaMungu wetu na kumtii yeye.”

25 Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria.

26 Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa akalisimamisha huko, chini ya mwaloni huko karibu na mahali patakatifu paBwana.

27 Akawaambia watu wote, “Angalieni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yoteBwanaaliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”

Kuzikwa Katika Nchi Ya Ahadi

28 Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.

29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi waBwanaakafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi.

30 Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Serakatika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima wa Gashi.

31 Israeli wakamtumikiaBwanawakati wote wa kipindi cha Yoshua, na kipindi cha hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa na ambao waliona wenyewe kila kituBwanaalichowatendea Israeli.

32 Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu.

33 Naye Eleazari mwana wa Aroni akafariki akazikwa huko Gibeathi, ambapo alikuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOS/24-60870f2732749295a19fb15578d5f092.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 1

Amri Ya Kuondoka Mlima Horebu

1 Haya ni maneno Mose aliyoyasema kwa Israeli yote jangwani mashariki ya Yordani, ambayo iko katika Araba, inayokabiliana na Sufu kati ya Parani na Tofeli, Labani, Hazerothi na Dizahabu.

2 (Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya Mlima Seiri mpaka Kadesh-Barnea.)

3 Katika mwaka wa arobaini, siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, Mose aliwatangazia Waisraeli yale yoteBwanaaliyomwamuru kuwahusu.

4 Hii ilikuwa baada ya kumshinda Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, na pia huko Edrei alikuwa amemshinda Ogu mfalme wa Bashani, ambaye alitawala huko Ashtarothi.

5 Huko mashariki ya Yordani katika nchi ya Moabu, Mose alianza kuielezea sheria hii, akisema:

6 BwanaMungu wetu alisema nasi huko Horebu, “Mmekaa vya kutosha katika mlima huu.

7 Vunjeni kambi, msonge mbele kuelekea katika nchi ya vilima ya Waamori; nendeni kwa watu wote ambao ni majirani wa Araba, katika milima, upande wa magharibi chini ya vilima, katika Negebu na kandokando ya pwani, mpaka nchi ya Wakanaani hadi Lebanoni, na kufika mto mkubwa Eufrati.

8 Tazama, nimewapa ninyi nchi hii. Ingieni mkaimiliki nchi ambayoBwanaaliapa kuwa angaliwapa baba zenu, Abrahamu, Isaki na Yakobo, pamoja na vizazi vyao baada yao.”

Uteuzi Wa Viongozi

9 Wakati ule niliwaambia, “Ninyi mmekuwa mzigo mzito sana kwangu kuwachukua peke yangu.

10 BwanaMungu wenu ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani.

11 NayeBwana, Mungu wa baba zenu na awaongeze mara elfu na kuwabariki kama alivyoahidi!

12 Lakini mimi nitawezaje kubeba matatizo yenu, na mizigo yenu, na magomvi yenu peke yangu?

13 Chagueni baadhi ya watu wenye hekima, wenye ufahamu na wanaoheshimika kutoka katika kila kabila lenu, nami nitawaweka juu yenu.”

14 Mlinijibu, “Shauri ulilolitoa ni zuri.”

15 Kwa hiyo niliwachukua wanaume viongozi wa makabila yenu, wenye hekima na wanaoheshimika, nami nikawateua wawe na mamlaka juu yenu kama majemadari wa maelfu, wa mamia, wa hamsini, na wa makumi, na kama maafisa wa makabila.

16 Nami wakati ule nikawaagiza waamuzi wenu: Sikilizeni magomvi kati ya ndugu zenu na mwamue kwa haki, hata kama shauri ni kati ya ndugu wa Kiisraeli, au kati ya mmoja wa ndugu wa Kiisraeli na mgeni.

17 Msionyeshe upendeleo katika maamuzi; wasikilizeni wote sawasawa, wadogo kwa wakubwa. Msimwogope mtu ye yote, kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Mniletee mimi shauri lo lote lililo gumu sana kwenu, nami nitalisikiliza.

18 Nami wakati ule niliwaambia kila kitu ambacho mngefanya.

Wapelelezi Wanatumwa

19 Kisha, kamaBwanaMungu wetu alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea.

20 Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayoBwanaMungu wetu anatupa.

21 Tazama,BwanaMungu wenu amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kamaBwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”

22 Ndipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”

23 Wazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila.

24 Waliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza.

25 Wakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayoBwanaMungu wetu anatupa.”

Uasi Dhidi Ya Bwana

26 Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri yaBwanaMungu wenu.

27 Mkanung’unika ndani ya mahema yenu na kusema, “Bwanaanatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza.

28 Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”

29 Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope.

30 BwanaMungu wenu anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa,

31 na pia huko jangwani. Huko mliona jinsiBwanaMungu wenu alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea mpaka mkafika mahali hapa.”

32 Pamoja na hili, hamkumtegemeaBwanaMungu wenu,

33 ambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonyesha njia mtakayoiendea.

34 WakatiBwanaaliposikia lile mlilosema, alikasirika, akaapa, akasema:

35 “Hakuna mtu wa kizazi hiki kiovu atakayeona nchi nzuri niliyoapa kuwapa baba zenu,

36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune. Yeye ataiona, nami nitampa yeye na wazao wake nchi aliyoikanyaga kwa miguu, kwa sababu alimfuataBwanakwa moyo wote.”

37 Kwa sababu yenuBwanapia alinikasirikia mimi, akasema, “Hutaingia hiyo nchi pia.

38 Lakini msaidizi wako, Yoshua mwana wa Nuni, ataiingia. Mtie moyo, kwa sababu atawaongoza Waisraeli kuirithi hiyo nchi.

39 Wale watoto ambao mliwasema wangelichukuliwa mateka, yaani watoto wenu ambao bado hawajui jema na baya, wataingia katika nchi. Nitawapa hiyo nchi, nao wataimiliki.

40 Bali ninyi geukeni, mwondoke kuelekea jangwani kwa kufuata njia ya Bahari ya Shamu.”

41 Ndipo mkanijibu, “TumemtendaBwanadhambi. Tutakwenda kupigana, kamaBwanaMungu wetu alivyotuamuru.” Hivyo kila mmoja wenu akachukua silaha zake, huku mkifikiri kuwa ni rahisi kukwea katika nchi ya vilima.

42 LakiniBwanaaliniambia, “Waambie, ‘Msipande kupigana, kwa sababu sitakuwa pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu.’ ”

43 Hivyo niliwaambia, lakini hamkutaka kusikia. Mliasi dhidi ya amri yaBwana, na katika kiburi chenu mlienda katika nchi ya vilima.

44 Waamori ambao waliishi katika vilima hivyo waliinuka dhidi yenu, wakawafukuza kama kundi la nyuki wakiwapiga njia yote ya Seiri mpaka Horma.

45 Mlirudi na kulia mbele zaBwana, lakini Mungu hakusikiliza kilio chenu, wala hakuwajali.

46 Hivyo mlikaa Kadeshi kwa siku nyingi, kwa muda ule wote mliokaa huko.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/1-95cf3f132e5a72c718bff1cef53be6f6.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 2

Kutangatanga Jangwani

1 Kisha tukageuka nyuma na kusafiri kuelekea jangwani kwa njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kamaBwanaalivyonielekeza. Kwa muda mrefu tulitembea kuzunguka vilima katika nchi ya Seiri.

2 KishaBwanaakaniambia,

3 “Umetembea kuzunguka hii nchi ya vilima kwa muda wa kutosha; sasa geukia kaskazini.

4 Wape watu maagizo haya: ‘Mko karibu kupita katikati ya nchi ya ndugu zako ambao ni wazao wa Esau, ambao wanaishi Seiri. Watawaogopa, lakini mwe waangalifu.

5 Msiwachokoze kwa vita kwa maana sitawapa ninyi sehemu yo yote ya nchi yao, hata sehemu ya kutosha kuweka wayo wenu juu yake. Nimempa Esau nchi ya vilima ya Seiri kama yake mwenyewe.

6 Mtawalipa fedha kwa chakula mtakachokula na maji mtakayokunywa.’ ”

7 BwanaMungu wenu amewabariki kwa kazi yote ya mikono yenu. Amewalinda katika safari yenu katikati ya jangwa hili kubwa. Kwa miaka hii arobainiBwanaMungu wenu amekuwa pamoja nanyi, na hamkupungukiwa na kitu cho chote.

8 Basi tulipita kwa ndugu zetu wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri. Tuligeuka kutoka njia ya Araba ambayo inatokea Elathi na Esion-Geberi, tukasafiri kufuata njia ya jangwa la Moabu.

9 KishaBwanaakaniambia, “Usiwasumbue Wamoabu kwa vita, kwa kuwa sitawapa sehemu yo yote ya nchi yao. Nimetoa nchi ya Ari kwa wazao wa Loti kama milki yao.”

10 (Waemi walikuwa wakiishi huko hapo zamani, watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki.

11 Kama walivyokuwa Waanaki, hao pia walikuwa kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi.

12 Wahori waliishi Seiri, lakini wazao wa Esau waliwafukuza. Waliwaangamiza Wahori na kukaa mahali pao, kama Waisraeli walivyofanya katika nchi ambayoBwanaaliwapa kama milki yao.)

13 Bwanaakasema, “Sasa ondokeni mvuke Bonde la Zeredi.” Hivyo tukavuka bonde.

14 Miaka thelathini na minane ilipita tangu wakati tulipoondoka Kadesh-Barnea mpaka tulipovuka Bonde la Zeredi. Kwa wakati huo kile kizazi chote cha wanaume kuanzia wale wawezao kwenda vitani kilikuwa kimekufa, kamaBwanaalivyokuwa amewaapia.

15 Mkono waBwanauliwakabili hadi alipowaangamiza wote huko kambini.

16 Ikawa baada ya mtu wa mwisho kuanzia wale wawezao kwenda vitani kufa,

17 Bwanaakaniambia,

18 “Leo utapita katika nchi ya Moabu huko Ari.

19 Utakapokuja kwa Waamori, msiwasumbue wala kuwachokoza kwa vita, kwa kuwa sitawapa ardhi yo yote iliyo ya Waamori kuwa milki yenu. Nimeitoa kama milki ya wazao wa Loti.”

20 (Hiyo pia ilidhaniwa kuwa nchi ya Warefai waliokuwa wakiishi huko, lakini Waamoni waliwaita Wazamzumi.

21 Walikuwa watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki.Bwanaakawaangamiza kutoka mbele ya Waamoni, ambao waliwafukuza na kukaa mahali pao.

22 Bwanaalikuwa amefanya vivyo hivyo kwa wazao wa Esau, ambao waliishi Seiri, wakati alipowaangamiza Wahori watoke mbele yao. Waliwafukuza na wao wakaishi mahali pao mpaka leo.

23 Nao Waavi ambao waliishi katika vijiji mpaka Gaza, Wakaftori waliokuja kutoka Kaftori waliwaangamiza na kukaa mahali pao.)

Kushindwa Kwa Sihoni Mfalme Wa Heshboni

24 “Ondoka sasa na uvuke Bonde la Arnoni. Tazama, nimemweka mikononi mwako Sihoni Mwamori, mfalme wa Heshboni na nchi yake. Anza kuimiliki nchi hiyo na umwingize katika vita.

25 Siku hii ya leo nitaanza kuwatia hofu na woga mataifa yote chini ya mbingu wawaogope ninyi. Watakaposikia taarifa zenu, watatetemeka na kufadhaika kwa sababu yenu.”

26 Kutoka jangwa la Kedemothi nilituma wajumbe wenye maneno ya amani kwa Sihoni mfalme wa Heshboni kusema,

27 “Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapita katika barabara kuu, hatutageuka kuume wala kushoto.

28 Tuuzie chakula tule na maji tunywe kwa thamani yake katika fedha. Turuhusu tu tupite kwa miguu,

29 kama wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri na Wamoabu ambao wanaishi Ari walivyotufanyia, mpaka tuvuke Yordani kuingia nchi ambayoBwanaMungu wetu anatupatia.”

30 Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni alikataa kuturuhusu kupita. Kwa kuwaBwanaMungu wako alikuwa ameifanya roho yake kuwa ngumu na moyo wake kuwa mkaidi ili amweke kwenye mikono yenu, kama alivyofanya sasa.

31 Bwanaakaniambia, “Tazama, nimeanza kuwapa Mfalme Sihoni na nchi yake kwako. Sasa anzeni kuishinda na kuimiliki nchi yake.”

32 Wakati Sihoni pamoja na jeshi lake lote walipokuja kukutana nasi katika vita huko Yahazi,

33 BwanaMungu wetu alimweka mikononi mwetu, nasi tukamwangamiza pamoja na wanawe na jeshi lake lote.

34 Kwa wakati ule tuliteka miji yake yote na kuiangamiza kabisa: wanaume, wanawake na watoto. Hatukubakiza mtu hata mmoja.

35 Lakini mifugo na nyara tulizoziteka kutoka ile miji tulijichukulia wenyewe.

36 Kutoka Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kutoka mji ulio ndani ya bonde, hata mpaka Gileadi, hapakuwa na mji hata mmoja uliokuwa na nguvu kutushinda.BwanaMungu wetu alitupa yote.

37 Lakini kulingana na amri yaBwanaMungu wetu, hamkujiingiza katika nchi yo yote ya Waamori, wala katika sehemu yo yote iliyo kandokando ya Mto Yaboki, wala katika miji iliyoko katika vilima.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/2-7217c097714db04be04239e6cd0d37ae.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 3

Kushindwa Kwa Ogu Mfalme Wa Bashani

1 Kisha tukageuka tukakwea kufuata barabara iliyoelekea Bashani, Ogu mfalme wa Bashani akaondoka na jeshi lake lote kupigana na sisi huko Edrei.

2 Bwanaakaniambia, “Usimwogope kwa kuwa nimekwisha mkabidhi mikononi mwako pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Umfanyie sawasawa na ulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”

3 HivyoBwanaMungu wetu pia akamweka Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote mikononi mwetu. Tuliwaangamiza wote, hakubakia hata mmoja.

4 Wakati huo tuliteka miji yake yote. Hakuna mji hata mmoja kati ya ile sitini ambao hatukuuteka, yaani eneo lote la Argobu, utawala wa Mfalme Ogu katika Bashani.

5 Miji yote hii ilijengewa ngome zenye kuta ndefu zenye malango na makomeo, pia kulikuwako na vijiji vingi ambavyo havikujengewa kuta.

6 Tuliwaangamiza kabisa, kama tulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Heshboni, tukiangamiza kila mji, yaani wanaume, wanawake na watoto.

7 Lakini wanyama wote wa kufuga pamoja na nyara kutoka kwenye miji yao tulichukua vikawa vyetu.

8 Hivyo kwa wakati huo tukachukua kutoka kwa wafalme hawa wawili wa Waamori nchi ya mashariki ya Jordani, kutoka Bonde la Arnoni mpaka kufika kwenye Mlima Hermoni.

9 (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri.)

10 Tuliteka miji yote kwenye uwanda wa juu, Gileadi yote, Bashani yote mpaka kufika Saleka na Edrei, miji ya utawala wa Ogu huko Bashani.

11 (Mfalme Ogu ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa mabaki ya Warefai. Kitanda chake kilikuwa cha chuma chenye urefu wa dhiraa tisana upana wa dhiraa nne. Mpaka sasa kinaweza kuonekana katika mji wa Waamori wa Raba.)

Mgawanyo Wa Nchi Mashariki Ya Yordani

12 Katika nchi tuliyoiteka wakati ule, niliwapa kabila la Reubeni na Gadi eneo lililoko kaskazini la Aroeri kando ya Bonde la Arnoni, na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake.

13 Kisha nusu ya kabila la Manase niliwapa sehemu ya Gileadi iliyobaki pamoja na Bashani yote, ambayo ilikuwa utawala wa Ogu. (Eneo lote la Argobu katika Bashani lilikuwa linajulikana kama nchi ya Warefai.

14 Yairi, mzao wa kabila la Manase, alichukuwa eneo lote la nchi ya Argobu hadi kufikia mpaka wa Wageshuri na Wamaaka, ukaitwa kwa jina lake; kwa hiyo mpaka leo hii Bashani inaitwa Hawath-Yairi.)

15 Nikampa Makiri nchi ya Gileadi.

16 Lakini niliwapa Wareubeni na Wagadi eneo kuanzia Gileadi hadi Bonde la Arnoni (katikati ya bonde ulikuwa ndio mpaka), kuelekea mpaka Mto Yaboki, ambao ndio mpaka wa Waamoni.

17 Kwa upande wa magharibi mpaka wao ulikuwa Yordani katika Araba, toka ziwa Galilaya hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), kwenye mitelemko ya Pisga upande wa mashariki.

18 Wakati huo nilikuamuru: “BwanaMungu wako amekupa nchi hii uimiliki. Lakini ni lazima wanaume wenu wote wenye uwezo, wakiwa wamejiandaa tayari kwa vita, wavuke ng’ambo ya pili wakiwatangulia ndugu zako Waisraeli.

19 Lakini wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu (kwani najua mnayo mifugo mingi) wanaweza kukaa katika miji niliyowapa,

20 mpaka hapoBwanaatakapowapa ndugu zenu kupumzika kama alivyowapa ninyi, wao pia wamiliki ile nchi ambayoBwanaMungu wenu anawapa, ng’ambo ya Yordani. Baada ya hapo, kila mmoja wenu anaweza kurudi kwenye milki niliyowapa.”

Mose Akataliwa Kuvuka Yordani

21 Wakati huo nilimwamuru Yoshua, “Umejionea kwa macho yako mwenyewe yale yote ambayoBwanaMungu wenu amewafanyia wafalme hawa wawili.Bwanaatazifanyia falme zote huko mnakokwenda vivyo hivyo.

22 Msiwaogope,BwanaMungu wenu atapigana kwa ajili yenu.”

23 Wakati huo nilimsihiBwana:

24 “EeBwanaMwenyezi, umemwonyesha mtumishi wako ukuu wako na mkono wako wenye uweza. Kwa kuwa ni mungu yupi aliyeko mbinguni au duniani anayeweza kufanya kazi na matendo makuu kama ufanyayo wewe?

25 Acha niende nikaione hiyo nchi nzuri ng’ambo ya Yordani, ile nchi nzuri ya vilima na Lebanoni.”

26 Lakini kwa sababu yenuBwanaalinikasirikia na hakutaka kunisikiliza.Bwanaaliniambia, “Hilo latosha; usiseme nami jambo hili tena.

27 Kwea juu ya kilele cha Pisga uangalie magharibi, kaskazini, kusini na mashariki. Iangalie hiyo nchi kwa macho yako, kwa vile wewe hutavuka Yordani.

28 Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na umtie nguvu, kwa kuwa yeye atawaongoza watu hawa hadi ng’ambo na kuwarithisha nchi utakayoiona.”

29 Kwa hiyo tulikaa kwenye bonde karibu na Beth-Peori.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/3-4bb1beab748da21a6f301a0d7d9f9f21.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 4

Waamriwa Utii

1 Sikia sasa, Ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayoBwana, Mungu wa baba zako anawapa.

2 Usiongeze wala usipunguze cho chote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo yaBwanaMungu wenu ambayo nawapa.

3 Mliona kwa macho yenu wenyewe kileBwanaalichokifanya kule Baal-Peori.BwanaMungu wenu aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori,

4 lakini ninyi nyote mlioshikamana naBwanakwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai mpaka leo.

5 Tazama, nimewafundisha amri na sheria kamaBwanaMungu wangu alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki.

6 Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonyesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.”

7 Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kamaBwanaMungu wetu alivyo karibu nasi wakati wo wote tunapomwomba?

8 Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?

9 Mwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.

10 Kumbuka siku uliyosimama mbele zaBwanaMungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”

11 Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto mpaka mbinguni juu, pamoja na mawingu meusi na giza nene.

12 NdipoBwanaalipozungumza nanyi kutoka katika moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu.

13 Aliwatangazia Agano lake na Amri Kumi, ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe.

14 NayeBwanaalinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.

Kuabudu Sanamu Kwakatazwa

15 Hamkuona umbo la aina yo yote siku ambayoBwanaalizungumza na ninyi kule Horebu kutoka kwenye moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana,

16 ili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lo lote kama la mwanaume au mwanamke,

17 au kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege ye yote arukaye angani,

18 au kama kiumbe kitambaacho juu ya ardhi au samaki ye yote aliye ndani ya maji.

19 Na utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vile ambavyoBwanaMungu wenu alivyogawia mataifa yote chini ya mbingu.

20 Lakini kwenu ninyi,Bwanaamewatoa kutoka kwenye tanuru ya kuyeyushia chuma, katika Misri kuwa watu wa urithi wake kama mlivyo sasa.

21 Bwanaalinikasirikia kwa sababu yenu na akaapa kwamba sitavuka Yordani kuingia katika nchi nzuriBwanaMungu wenu anayowapa kuwa urithi wenu.

22 Nitakufa katika nchi hii; sitavuka Yordani, lakini ninyi ni karibu mvuke mkaimiliki ile nchi nzuri.

23 Jihadharini msilisahau Agano laBwanaMungu wenu lile alilofanya nanyi; msijitengenezee sanamu katika umbo la kitu cho chote ambachoBwanaMungu wenu amewakataza.

24 Kwa kuwaBwanaMungu wenu ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.

25 Baada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena kama mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yo yote, mkifanya maovu machoni paBwanaMungu wenu na kumfanya awe na hasira,

26 ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka katika nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa.

27 Bwanaatawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayoBwanaatawafukuzia.

28 Huko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa.

29 Lakini kama mtamtafutaBwanaMungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wenu wote na kwa roho yote.

30 Wakati mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudiaBwanaMungu wenu na kumtii.

31 Kwa maanaBwanaMungu wenu ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau Agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.

Bwana Ndiye Mungu

32 Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomwumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu mpaka mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa?

33 Je, kuna watu wengine wo wote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi?

34 Je, kuna mungu ye yote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu yakutisha, kama yale ambayoBwanaMungu wenu aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?

35 Mlionyeshwa mambo haya ili mpate kujua kuwaBwanandiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye.

36 Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonyesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kwenye ule moto.

37 Kwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu,

38 aliwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo.

39 Kubalini na mweke moyoni leo kuwaBwanandiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine.

40 Mshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi awapayoBwanaMungu wenu siku zote.

Miji Ya Makimbilio

41 Kisha Mose akatenga miji mitatu mashariki ya Yordani,

42 ambayo mtu ye yote aliyemwua mtu angeweza kukimbilia ikiwa amemwua jirani yake bila kukusudia na bila kuwa na chuki naye siku zilizopita. Angeweza kukimbilia katika mmojawapo ya miji hii na kuokoa maisha yake.

43 Miji hiyo ilikuwa: Beseri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya Wareubeni; Ramoth katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya Wagadi; nao mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya Wamanase.

Utangulizi Wa Sheria

44 Hii ndiyo sheria Mose aliyoweka mbele ya Waisraeli.

45 Haya ndiyo masharti, amri na sheria Mose aliyowapa wakati walipotoka Misri,

46 nao walikuwa katika bonde karibu na Beth-Peori mashariki ya Yordani, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, naye alishindwa na Mose na Waisraeli walipokuja toka Misri.

47 Waliimiliki nchi yake na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, wafalme hao wawili waliotawala mashariki ya Yordani.

48 Nchi hii ilienea kutoka Aroeri ukingoni mwa Bonde la Arnoni mpaka Mlima Sioni (yaani Hermoni),

49 pamoja na eneo lote la Araba mashariki ya Yordani, na kuenea mpaka Bahari ya Araba kwenye mitelemko ya Pisga.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/4-e54feee2029e3988abaff35b8a4b587e.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 5

Amri Kumi

1 Mose akawaita Israeli wote, akawaambia:

Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata.

2 BwanaMungu wetu alifanya Agano nasi katika mlima wa Horebu.

3 Si kwambaBwanaalifanya Agano na baba zetu, bali alifanya nasi, nasi sote ambao tuko hai hapa leo.

4 Bwanaalisema nanyi uso kwa uso kutoka katika moto juu ya mlima.

5 (Wakati huo nilisimama kati yaBwanana ninyi kuwatangazia neno laBwana, kwa sababu mliogopa ule moto, nanyi hamkupanda mlimani.) Naye Mungu alisema:

6 “Mimi ndimiBwanaMungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka katika nchi ya utumwa.

7 Usiwe na miungu mingine ila mimi.

8 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu cho chote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji.

9 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa maana Mimi,BwanaMungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao,

10 lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.

11 Usilitaje jina laBwanaMungu wako bure, kwa kuwaBwanahataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.

12 Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kamaBwanaMungu wako alivyokuagiza.

13 Siku sita utafanya kazi na kutenda kazi zako zote.

14 Lakini siku ya Saba ni Sabato kwaBwana, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yo yote, ikiwa ni wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au mtumishi wa kike, wala ng’ombe wako, punda wako au mnyama wako ye yote, wala mgeni aliyeko malangoni mwako, ili kwamba mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kumpumzika kama wewe.

15 Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, naBwanaMungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyoBwanaMungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.

16 Waheshimu baba yako na mama yako, kamaBwanaMungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchiBwanaMungu wako anayokupa.

17 Usiue.

18 Usizini.

19 Usiibe.

20 Usimshuhudie jirani yako uongo.

21 Usitamani mke wa jirani yako. Usitamani nyumba ya jirani yako au shamba lake, mtumishi wake wa kiume au wa kike, ng’ombe au punda wake, wala kitu cho chote cha jirani yako.”

22 Hizi ndizo amri alizozitangazaBwanakwa sauti kubwa kwa kusanyiko lenu lote huko mlimani kutoka kwenye moto, wingu na giza nene, wala hakuongeza cho chote zaidi. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, naye akanipa mimi.

23 Mliposikia sauti kutoka kwenye giza, mlima ulipokuwa ukiwaka moto, viongozi wenu wote wa makabila yenu na wazee wenu walinijia mimi.

24 Nanyi mkasema, “BwanaMungu wetu ametuonyesha utukufu na enzi yake, nasi tumesikia sauti yake kutoka kwenye moto. Leo tumeona kwamba mwanadamu anaweza kuishi hata kama Mungu akizungumza naye.

25 Lakini sasa, kwa nini tufe? Moto huu mkubwa utatuteketeza sisi na tutakufa kama tukiendelea kusikia sauti yaBwanaMungu wetu zaidi.

26 Ni mtu yupi mwenye mwili ambaye amewahi kuisikia sauti ya Mungu aliye hai akizungumza kutoka kwenye moto, kama sisi tulivyoisikia, naye akaishi?

27 Sogea karibu usikie yale yote asemayoBwanaMungu wetu. Kisha utuambie cho chote kile ambachoBwanaMungu wetu anakuambia. Tutasikiliza na kutii.”

28 Bwanaaliwasikia wakati mlipozungumza nami, naBwanaakaniambia, “Nimesikia kile hawa watu walichokuambia. Kila kitu walichokisema ni kizuri.

29 Laiti kama mioyo yao ingekuwa na mwelekeo wa kuniogopa na kuzishika amri zangu zote daima, ili kwamba wafanikiwe wao pamoja na watoto wao milele!

30 “Nenda uwaambie warudi kwenye mahema yao.

31 Lakini wewe baki hapa pamoja nami ili niweze kukupa maagizo yote, amri na sheria ambazo utawafundisha wazifuate katika nchi ninayokwenda kuwapa waimiliki.”

32 Hivyo iweni waangalifu kuyafanya yaleBwanaMungu wenu aliyowaagiza; msigeuke upande wa kuume wala wa kushoto.

33 Fuateni yale yote ambayoBwanaMungu wenu aliwaagiza, ili mpate kuishi, kustawi na kuziongeza siku zenu katika nchi mtakayoimiliki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/5-334568423215b2ac8113821ad2320506.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 6

Mpende Bwana Mungu Wako

1 Haya ndiyo maagizo, amri na sheria ambazoBwanaMungu wenu aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki,

2 ili kwamba ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamcheBwanaMungu wenu siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu.

3 Sikia, Ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi itiririkayo maziwa na asali, kamaBwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.

4 Sikia, Ee Israeli:BwanaMungu wako, niBwanammoja.

5 MpendeBwanaMungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote.

6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako.

7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.

8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako.

9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

10 WakatiBwanaMungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga,

11 nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba,

12 jihadhari usije ukamwachaBwana, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka katika nchi ya utumwa.

13 UtamchaBwanaMungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake.

14 Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka;

15 kwa kuwaBwanaMungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka katika uso wa nchi.

16 UsimjaribuBwanaMungu wako kama ulivyofanya huko Masa.

17 Utayashika maagizo yaBwanaMungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa.

18 Fanya lililo haki na jema mbele zaBwana, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayoBwanaaliahidi kwa kiapo kwa baba zako,

19 kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kamaBwanaalivyosema.

20 Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazoBwanaMungu wako alikuagiza wewe?”

21 Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakiniBwanaalitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu.

22 Bwanaakapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote.

23 Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupa nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo.

24 Bwanaakatuagiza tutii amri hizi zote na kumchaBwanaMungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo.

25 Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele zaBwanaMungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/6-bc5311edec2b518759d98228f23fe746.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 7

Kuyafukuza Mataifa

1 BwanaMungu wako akuletapo katika nchi unayoiingia ili kuimiliki na awafukuzapo mbele yako mataifa mengi, yaani, Wahiti, Wagirgashi, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, mataifa saba makubwa tena yenye nguvu kuliko wewe,

2 piaBwanaMungu wako atakapowatia mkononi mwako na ukawashinda, basi ni lazima uwaangamize wote kabisa. Usifanye agano nao, usiwahurumie.

3 Usioane nao. Usimtoe binti yako kuolewa na mwanawe, au kumchukua binti yake aolewe na mwanao.

4 Kwa maana watamgeuza mwanao aache kunifuata, ili aitumikia miungu mingine, nayo hasira yaBwanaitawaka dhidi yako, naye atakuangamiza ghafula.

5 Hili ndilo utakalowafanyia: Vunja madhabahu zao, yabomoe mawe yao yaliyowekwa wakfu, katakata nguzo zao za Ashera na kuchoma sanamu zao kwa moto.

6 Kwa kuwa wewe ni taifa takatifu kwaBwanaMungu wako.BwanaMungu wako amekuchagua wewe kutoka katika mataifa yote juu ya uso wa dunia kuwa watu wake, hazina yake ya thamani.

7 Bwanahakuweka upendo wake juu yenu na kuwachagua kwa sababu mlikuwa wengi mno kuliko watu wengine, kwa maana ninyi ndio mliokuwa wachache sana kuliko mataifa yote.

8 Lakini ni kwa sababuBwanaaliwapenda ninyi na kutunza kiapo alichowaapia babu zenu kwamba atawatoa ninyi kwa mkono wenye nguvu na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa, kutoka nguvu za Farao mfalme wa Misri.

9 Basi ujue kwambaBwanaMungu wako ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayetunza Agano la upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaompenda na kuzishika amri zake.

10 Lakini

kwa wale wanaomchukia

atawalipiza kwenye nyuso zao

kwa maangamizi;

hatachelewa kuwalipiza kwenye nyuso zao

wale wamchukiao.

11 Kwa hiyo, iweni waangalifu kufuata maagizo, amri na sheria ninazowapa leo.

12 Kama mkizingatia sheria hizi na kuzifuata kwa uangalifu, basiBwanaMungu wenu atatunza Agano lake la upendo nanyi, kama alivyowaapia baba zenu.

13 Atawapenda ninyi na kuwabariki na kuongeza idadi yenu. Atabariki uzao wa tumbo lenu, mazao ya nchi yenu, nafaka, divai mpya na mafuta, ndama wa ng’ombe wa kundi lenu na kondoo za kundi lenu katika nchi ile aliyoapa kuwapa baba zenu.

14 Mtabarikiwa kuliko mataifa mengine yote, hakuna wanaume wala wanawake kwenu watakaokosa watoto, wala mifugo yenu haitakuwa tasa.

15 Bwanaatawakinga na kila ugonjwa. Mungu hatatia juu yenu ugonjwa wo wote mbaya mlioufahamu huko Misri, lakini atatia ugonjwa juu ya wale wote wanaokuchukia.

16 Ni lazima mwangamize watu wote ambaoBwanaMungu wenu atawatia mikononi mwenu. Msiwatazame kwa kuwahurumia na msitumikie miungu yao, kwa kuwa itakuwa mtego kwenu.

17 Mnaweza kujiuliza wenyewe “Mataifa haya ni yenye nguvu kuliko sisi. Tutawezaje kuwafukuza?”

18 Lakini msiwaogope. Kumbukeni vyema jinsiBwanaMungu wenu alivyofanya kwa Farao na kwa wote huko Misri.

19 Mliona kwa macho yenu wenyewe majaribu makubwa, ishara za miujiza na maajabu, mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, ambao kwa huoBwanaMungu wenu aliwatoa mtoke Misri.BwanaMungu wenu atawafanyia hivyo watu wote ambao mnawaogopa sasa.

20 Zaidi ya hayo,BwanaMungu wenu atatuma manyigu miongoni mwao hadi yale mabaki watakaojificha waangamie.

21 Msiingiwe na hofu kwa sababu yao, kwa kuwaBwanaMungu wenu, ambaye yupo miongoni mwenu ni mkuu naye ni Mungu wa kutisha.

22 BwanaMungu wenu atawafukuza mataifa hayo mbele yenu kidogo kidogo. Hamtaruhusiwa kuwaondoa wote kwa mara moja, la sivyo wanyama mwitu wataongezeka na kuwa karibu nanyi.

23 LakiniBwanaMungu wenu atawatia watu hao mikononi mwenu, akiwatia katika kuchanganyikiwa kukubwa mpaka wawe wameangamizwa.

24 Atawatia wafalme wao mikononi mwenu, nanyi mtayafuta majina yao chini ya mbingu. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama dhidi yenu bali mtawaangamiza.

25 Vinyago vya miungu yao mtavichoma moto. Msitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala msizichukue kwa ajili yenu, la sivyo mtakuwa mmetekwa navyo. Kwa kuwa ni chukizo kwaBwanaMungu wenu.

26 Msilete vitu vya machukizo katika nyumba zenu kwani ninyi, mtatengwa kama vitu hivyo kwa maangamizo. Ukichukie kabisa kitu hicho kwa kuwa kimetengwa kwa maangamizo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/7-fadc45cb5701ff3fb9ac1fe8a4a350b9.mp3?version_id=1627—

Kumbukumbu La Torati 8

Usimsahau Bwana

1 Uwe mwangalifu kufuata kila agizo ninalokupa wewe leo, ili mweze kuishi, kuongezeka na mweze kuingia mkamiliki nchi ambayoBwanaaliahidi kwa kiapo kwa baba zenu.

2 Kumbuka jinsiBwanaMungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la.

3 Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa chaBwana.

4 Nguo zenu hazikuchakaa wala miguu yenu haikuvimba kwa miaka hii arobaini.

5 Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyoBwanaMungu wako atawaadibisha ninyi.

6 Shikeni maagizo yaBwanaMungu wenu mtembee katika njia zake na kumheshimu.

7 Kwa kuwaBwanaMungu wenu anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima;

8 nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali;

9 nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa cho chote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima.

10 Wakati mtakapokwisha kula na kushiba, msifuniBwanaMungu wenu kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa.

11 Jihadharini msimsahauBwanaMungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo.

12 Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo,

13 na wakati makundi yenu ya ng’ombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa,

14 basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahauBwanaMungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.

15 Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu.

16 Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekesha na kuwajaribu ninyi ili mwishoni apate kuwatendea mema.

17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.”

18 Lakini kumbukeniBwanaMungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

19 Ikiwa mtamsahauBwanaMungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa.

20 Kama mataifaBwanaaliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtiiBwanaMungu wenu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DEU/8-8aca7ac071be4b88ae744c88841996b7.mp3?version_id=1627—