Hesabu 15

Sadaka Za Nyongeza

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,

3 nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka katika makundi ya ng’ombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendezaBwana, ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,

4 ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele zaBwanasadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efaya unga laini uliochanganywa na robo ya hiniya mafuta.

5 Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.

6 “ ‘Pamoja na kondoo dume andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi za efaza unga laini uliochanganywa na theluthi mojaya hini ya mafuta,

7 na theluthi moja ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendezaBwana.

8 “ ‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwaBwana,

9 leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efauliochanganywa na nusu ya hiniya mafuta.

10 Pia utaleta nusu ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendezaBwana.

11 Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.

12 Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.

13 “ ‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendezaBwana.

14 Kwa vizazi vijavyo, wakati wo wote mgeni au mtu mwingine ye yote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendezaBwana, ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.

15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hii ni amri ya kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele zaBwana:

16 Sheria hizo hizo na masharti hayo hayo, yatawahusu ninyi na mgeni aishiye miongoni mwenu.’ ”

17 Bwanaakamwambia Mose,

18 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka

19 nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kama sadaka kwaBwana.

20 Toeni andazi kutoka katika malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka katika sakafu ya kupuria nafaka.

21 Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwaBwanakutoka katika malimbuko ya unga wenu.

Sadaka Kwa Ajili Ya Dhambi Isiyo Ya Makusudi

22 “ ‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazoBwanaalimpa Mose,

23 amri yo yote yaBwanakwenu kupitia Mose, tangu siku ileBwanaalipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;

24 ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendezaBwana, pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

25 Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Kiisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemleteaBwanakwa ajili ya kosa lao sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi.

26 Jumuiya yote ya Kiisraeli pamoja na wageni waishio miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.

27 “ ‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi mke wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

28 Kuhani atafanya upatanisho mbele zaBwanakwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, wakati upatanisho utakapokuwa umefanyika kwa ajili yake, atasamehewa.

29 Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe mzawa ama mgeni.

30 “ ‘Lakini ye yote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuruBwana, naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.

31 Kwa sababu amelidharau neno laBwanana kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima kwa hakika akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’ ”

Mvunja Sabato Auawe

32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.

33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Mose, Aroni na kusanyiko lote,

34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.

35 NdipoBwanaakamwambia Mose, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima limpige mawe nje ya kambi.”

36 Hivyo kusanyiko likamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kamaBwanaalivyomwamuru Mose.

Vifundo Kwenye Mavazi

37 Bwanaakamwambia Mose,

38 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.

39 Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote zaBwana, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.

40 Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.

41 Mimi NdimiBwanaMungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi NdimiBwanaMungu wenu.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/15-0376ac97d713814f2a543c9e91896b18.mp3?version_id=1627—

Hesabu 16

Kora, Dathani Na Abiramu

1 Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Palethi, wakachukua baadhi ya watu,

2 wakainuka dhidi ya Mose. Pamoja nao walikuwapo wanaume wa Kiisraeli 250, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko.

3 Wakaja kama kikundi kuwapinga Mose na Aroni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili lote ni takatifu, kila mmoja wao, nayeBwanayu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko laBwana?”

4 Mose aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi.

5 Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “AsubuhiBwanaataonyesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye.

6 Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo,

7 kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele zaBwana. Mtu ambayeBwanaatamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”

8 Pia Mose akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni.

9 Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka katika kusanyiko lote la Kiisraeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani yaBwana, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia?

10 Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye, lakini sasa unajaribu kupata na ukuhani pia.

11 Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume chaBwana. Aroni ni nani kwamba ninyi mnung’unike dhidi yake?”

12 Kisha Mose akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji!

13 Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi itiririkayo maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu?

14 Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupa urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayang’oa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”

15 Ndipo Mose akakasirika sana na kumwambiaBwana, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua cho chote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”

16 Mose akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele zaBwana, yaani wewe na hao wenzako, pamoja na Aroni.

17 Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani yake, vyetezo 250 kwa jumla na kuleta mbele zaBwana. Pia wewe na Aroni mtaleta vyetezo vyenu.”

18 Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani yake, na kusimama pamoja na Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania.

19 Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu waBwanaukatokea kwa kusanyiko lote.

20 Bwanaakamwambia Mose na Aroni,

21 “Jitengeni kutoka kwenye kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

22 Lakini Mose na Aroni wakaanguka kufudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”

23 NdipoBwanaakamwambia Mose,

24 “Liambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”

25 Mose akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye.

26 Mose akalionya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu cho chote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.”

27 Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.

28 Ndipo Mose akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwaBwanaamenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu.

29 Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basiBwanahakunituma mimi.

30 Lakini ikiwaBwanaataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburiniwakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharauBwana.”

31 Mara Mose alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka,

32 nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali zao zote.

33 Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka katika kusanyiko.

34 Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”

35 Moto ukaja kutoka kwaBwana, ukawateketeza wale watu 250 waliokuwa wakifukiza uvumba.

36 Bwanaakamwambia Mose,

37 “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu,

38 vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele zaBwanana vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”

39 Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu,

40 kama vileBwanaalivyomwelekeza kupitia Mose. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Aroni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele zaBwana, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.

41 Siku iliyofuata jumuiya yote ya Kiisraeli wakanung’unika dhidi ya Mose na Aroni, wakisema, “Mmewaua watu waBwana.”

42 Lakini wakati kusanyiko lilipokusanyika kupingana na Mose na Aroni, nalo likageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu waBwanaukatokea.

43 Ndipo Mose na Aroni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania,

44 nayeBwanaakamwambia Mose,

45 “Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka chini kifudifudi.

46 Kisha Mose akamwambia Aroni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani yake, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwaBwana, na tauni imeanza.”

47 Hivyo Aroni akafanya kama Mose alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Aroni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao.

48 Aroni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma.

49 Lakini walikufa watu 14,700 kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora.

50 Ndipo Aroni akamrudia Mose kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/16-25a319c4b0ffc78f9cdba0660a14b15b.mp3?version_id=1627—

Hesabu 17

Kuchipuka Kwa Fimbo Ya Aroni

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa kabila za baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake.

3 Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Aroni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao.

4 Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe.

5 Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung’uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”

6 Hivyo Mose akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Aroni ikiwa miongoni mwa hizo.

7 Mose akaziweka hizo fimbo mbele zaBwanandani ya Hema la Ushuhuda.

8 Siku iliyofuata Mose aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Aroni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi.

9 Ndipo Mose akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele zaBwana. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.

10 Bwanaakamwambia Mose, “Rudisha fimbo ya Aroni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung’uniko yao dhidi yangu, ili kwamba wasife.”

11 Mose akafanya sawasawa kamaBwanaalivyomwamuru.

12 Waisraeli wakamwambia Mose, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea!

13 Ye yote akaribiaye Maskani yaBwanaatakufa. Je, sisi sote tutakufa?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/17-c6ca6c7397bf70c33aa11c7392aaf9de.mp3?version_id=1627—

Hesabu 18

Wajibu Wa Makuhani Na Walawi

1 Bwanaakamwambia Aroni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani.

2 Walete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda.

3 Watawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa.

4 Watajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine ye yote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo.

5 “Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili kwamba ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena.

6 Mimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwaBwanaili kufanya kazi katika Hema la Kukutania.

7 Lakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine ye yote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.”

Sadaka Kwa Ajili Ya Makuhani Na Walawi

8 KishaBwanaakamwambia Aroni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kama sehemu yenu na fungu lenu la kawaida.

9 Mtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka katika matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka au za dhambi au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao.

10 Myale kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume atayala. Ni lazima myaheshimu kama takatifu.

11 “Hiki pia ni chako: cho chote kilichotengwa kutoka kwenye matoleo yote ya sadaka za kupunga za Waisraeli. Ninakupa wewe haya, wana na binti zako kama sehemu yenu ya kawaida. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ni safi kwa taratibu za ibada anaweza kuyala.

12 “Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote na divai mpya iliyo bora kuliko zote wanayompaBwanakama malimbuko katika mavuno yao.

13 Malimbuko yote ya nchi ambayo wanamleteaBwanayatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani kwako ambaye ni safi kwa taratibu za Ibada anaweza kula.

14 “Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwaBwanani chenu.

15 Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwaBwanani wenu. Lakini ni lazima mumkomboe kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi.

16 Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tanoza fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.

17 “Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kama sadaka itolewayo kwa moto, harufu nzuri inayompendezaBwana.

18 Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kupungwa na paja la mguu wa kulia.

19 Cho chote kitakachotengwa kutoka katika sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtoleaBwana, ninakupa wewe, wanao na binti zako kama fungu lenu la kawaida. Ni Agano la milele la chumvi mbele zaBwanakwako na watoto wako.”

20 Bwanaakamwambia Aroni, “Hutakuwa na urithi wo wote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli.

21 “Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania.

22 Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa.

23 Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wo wote miongoni mwa Waisraeli.

24 Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwaBwanakuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuhusu wao: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ”

25 Bwanaakamwambia Mose,

26 “Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ambayo ninawapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kama sadaka kwaBwana, iwe zaka ya hiyo zaka.

27 Sadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka katika sakafu ya kupuria, au divai kutoka kwenye shinikizo la kukamulia zabibu.

28 Kwa njia hii ninyi pia mtatoa sadaka kwaBwanakutoka katika zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwenye zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu yaBwanakwa Aroni, kuhani.

29 Ni lazima mtoe kama sehemu yaBwanailiyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’

30 “Waambie Walawi: ‘Wakati mtakapotoa sehemu zilizo bora sana, itahesabiwa kwenu kama mazao ya sakafu ya kupuria nafaka, au ya shinikizo la kukamulia zabibu.

31 Ninyi na watu wa nyumbani mwenu mnaweza kula sehemu iliyobaki mahali po pote, kwani ndio ujira wenu kwa ajili ya kazi yenu katika Hema la Kukutania.

32 Kwa kutoa sehemu zake zilizo bora sana, hamtakuwa na hatia katika jambo hili; ndipo hamtatia unajisi sadaka takatifu za Waisraeli, nanyi hamtakufa.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/18-1d73cb0709c314b39800c9b6fb141162.mp3?version_id=1627—

Hesabu 19

Maji Ya Utakaso

1 Bwanaakamwambia Mose na Aroni:

2 “Hivi ndivyo sheria ambayoBwanaameagiza itakavyo: Waambie Waisraeli wakuletee mtamba mwekundu asiye na dosari wala waa na ambaye hajapata kufungwa nira.

3 Mpeni kuhani Eleazari huyo mtamba; naye atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele yake huyo kuhani.

4 Kisha kuhani Eleazari atachukua baadhi ya damu yake kwenye kidole chake na kuinyunyiza mara saba kuelekea upande wa mbele ya Hema la Kukutania.

5 Wakati akali akitazama, mtamba huyo atateketezwa: ngozi yake, nyama yake, damu na sehemu zake za ndani.

6 Kuhani atachukua kuni za mti wa mwerezi, hisopo na sufu nyekundu, na kuvitupa kwenye huyo mtamba anayeungua.

7 Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni.

8 Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi mpaka jioni.

9 “Mtu ambaye ni safi atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali ambapo ni safi nje ya kambi kwa taratibu za kiibada. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Kiisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini.

10 Mtu akusanyaye majivu ya huyo mtamba ni lazima pia afue nguo zake, kadhalika naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli na kwa wageni wanaoishi miongoni mwao.

11 “Mtu ye yote agusaye maiti ya mtu ye yote atakuwa najisi kwa siku saba.

12 Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi.

13 Mtu ye yote agusaye maiti ya mtu ye yote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani yaBwana. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake hubaki juu yake.

14 “Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Ye yote aingiaye ndani ya hema hilo na ye yote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba,

15 nacho kila chombo kisicho na mfuniko juu yake kitakuwa najisi.

16 “Mtu ye yote aliyeko nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu ye yote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.

17 “Kwa mtu aliye najisi, weka majivu ya sadaka ya utakaso wa dhambi ndani ya chombo, umimine maji safi juu yao.

18 Kisha mtu aliye safi kwa kawaida za kiibada atachukua hisopo, achovye ndani ya maji, na kunyunyizia hema na vifaa vyote pamoja na watu ambao walikuwemo. Pia ni lazima amnyunyizie mtu ye yote ambaye amegusa mfupa wa mtu aliyekufa, au kaburi, au mtu ambaye ameuawa, au mtu ambaye amekufa kifo cha kawaida.

19 Mtu ambaye ni safi ndiye atakayemnyunyizia ye yote ambaye ni najisi siku ya tatu na siku ya saba, na katika siku ya saba atamtakasa mtu huyo. Mtu ambaye ametakaswa lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, na jioni ile atakuwa safi.

20 Lakini ikiwa mtu ambaye ni najisi hakujitakasa mwenyewe, ni lazima akatiliwe mbali na jumuiya, kwa sababu ameinajisi Maskani yaBwana. Maji ya utakaso hayajanyunyizwa juu yake, naye ni najisi.

21 Hii ni sheria ya kudumu kwao.

“Mtu ye yote ambaye ananyunyiza yale maji ya utakaso lazima pia afue nguo zake, na ye yote ambaye hugusa maji ya utakaso atakuwa najisi mpaka jioni.

22 Kitu cho chote anachogusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi, na ye yote akigusaye huwa najisi mpaka jioni.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/19-0ce88076d3419b9d06406d7a26ef8714.mp3?version_id=1627—

Hesabu 20

Maji Kutoka Kwenye Mwamba

1 Katika mwezi wa kwanza jumuiya yote ya Kiisraeli ilifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa.

2 Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Mose na Aroni.

3 Watu wakagombana na Mose, na kusema, “Laiti tungelikufa wakati ndugu zetu walipoanguka na kufa mbele zaBwana!

4 Kwa nini mmeileta jumuiya yaBwanakwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu?

5 Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!”

6 Mose na Aroni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu waBwanaukawatokea.

7 Bwanaakamwambia Mose,

8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka katika huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

9 Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele zaBwanakama alivyomwagiza.

10 Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka katika mwamba huu?”

11 Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

12 LakiniBwanaakamwambia Mose na Aroni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”

13 Haya yalikuwa maji ya Meriba, mahali pale ambapo Waisraeli waligombana naBwana, naye akajionyesha mwenyewe huko kuwa mtakatifu katikati yao.

Edomu Wakatalia Israeli Kupita

14 Mose akawatuma wajumbe kutoka Kadeshi kwenda kwa mfalme wa Edomu, akisema:

“Hili ndilo ndugu yako Israeli asemalo: Wewe unafahamu juu ya taabu zote ambazo zimetupata.

15 Baba zetu walishuka Misri, nasi tumeishi huko miaka mingi. Wamisri walitutesa sisi na baba zetu,

16 lakini tulipomliliaBwana, alisikia kilio chetu na akamtuma malaika akatutoa Misri.

“Sasa tupo hapa Kadeshi, mji ulio mpakani mwa nchi yako.

17 Tafadhali turuhusu tupite katika nchi yako. Hatutapita katika shamba lo lote, wala shamba la mizabibu, au kunywa maji kutoka kwenye kisima cho chote. Tutasafiri kufuata njia kuu ya mfalme, na hatutageuka kulia wala kushoto mpaka tuwe tumeshapita nchi yako.”

18 Lakini mfalme wa Edomu akajibu:

“Hamtapita hapa; kama mkijaribu kupita, tutatoka na kuwashambulia kwa upanga.”

19 Waisraeli wakajibu:

“Sisi tutafuata njia kuu; tena ikiwa sisi au mifugo yetu tutakunywa tone la maji yenu, tutalilipia. Sisi tunataka tu kupita kwa miguu, wala si kitu kingine cho chote.”

20 Watu wa Edomu wakajibu tena:

“Hamwezi kupita hapa.”

Ndipo watu wa Edomu wakatoka dhidi ya Waisraeli, jeshi kubwa lenye nguvu.

21 Kwa kuwa Waedomu waliwakatalia Waisraeli kupita katika nchi yao, Israeli wakageuka, wakawaacha.

Kifo Cha Aroni

22 Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.

23 Kwenye Mlima Hori, karibu na mpaka wa Edomu,Bwanaakamwambia Mose na Aroni,

24 “Aroni atakusanywa pamoja na watu wake. Hataingia katika nchi ninayowapa Waisraeli, kwa sababu ninyi wawili mliasi dhidi ya agizo langu kwenye maji ya Meriba.

25 Watwae Aroni na Eleazari mwanawe, na uwapandishe juu katika Mlima wa Hori.

26 Mvue Aroni mavazi yake, na umvike Eleazari mwanawe, kwa maana Aroni atakusanywa pamoja na watu wake; atakufa huko.”

27 Mose akafanya kamaBwanaalivyomwagiza: Wakapanda Mlima Hori mbele ya macho ya jumuiya yote ya Kiisraeli.

28 Mose akamvua Aroni mavazi yake na kumvika mwanawe Eleazari mavazi hayo. Naye Aroni akafia pale juu ya mlima. Kisha Mose na Eleazari wakatelemka kutoka mlimani.

29 Jumuiya yote ilipofahamu kwamba Aroni amekufa, jamaa yote ya Kiisraeli wakamwambolezea kwa siku thelathini.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/20-ce16522e521585315953f4a810315509.mp3?version_id=1627—

Hesabu 21

Nchi Ya Aradi Yaangamizwa

1 Mfalme wa Kikanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao.

2 Ndipo Israeli akaweka nadhiri hii kwaBwana: “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.”

3 Bwanaakasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma.

Nyoka Wa Shaba

4 Waisraeli wakasafiri kutoka mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu,kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani,

5 wakamnung’unikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”

6 NdipoBwanaakapeleka nyoka wenye sumu katikati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa.

7 Watu wakamjia Mose na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi yaBwanana dhidi yako. MwombeBwanaili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Mose akawaombea hao watu.

8 Bwanaakamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.”

9 Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu ye yote alipoumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.

Safari Kwenda Moabu

10 Waisraeli waliendelea na safari yao na wakapiga kambi huko Obothi.

11 Kisha wakaondoka Obothi na kupiga kambi huko Iye-Abarimu, katika jangwa linalotazamana na Moabu kuelekea maawio ya jua.

12 Kutoka hapo waliendelea mbele wakapiga kambi kwenye Bonde la Zeredi.

13 Wakasafiri kutoka hapo na kupiga kambi kando ya Mto Arnoni, ambao uko katika jangwa lililoenea hadi nchi ya Waamori. Arnoni ni mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.

14 Ndiyo sababu Kitabu cha Vita vyaBwanakinasema:

“…Mji wa Wahebu nchini Seifa na mabonde

ya Arnoni,

15 na mitelemko ya mabonde

inayofika hadi mji wa Ari

na huelekea mpakani mwa Moabu.”

16 Kutoka hapo waliendelea mbele hadi kisima cha Beeri; kwenye kisima ambachoBwanaalimwambia Mose, “Wakusanye watu pamoja nami nitawapa maji.”

17 Kisha Israeli akaimba wimbo huu:

“Bubujika, Ee kisima!

Imba kuhusu maji,

18 kuhusu kisima ambacho kilichimbwa na wakuu,

ambacho watu mashuhuri walikifukua,

watu mashuhuri wakiwa na fimbo za utawala na bakora.”

Kisha wakatoka jangwani kwenda Matana,

19 kutoka Matana wakafika Nahalieli, kutoka Nahalieli wakafika Bamothi,

20 na kutoka Bamothi wakafika kwenye bonde lililoko Moabu, mahali ambapo kilele cha Pisga kinatazamana na nyika.

Kushindwa Kwa Sihoni Na Ogu

21 Israeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:

22 “Uturuhusu tupite katika nchi yako. Hatutageuka kando kwenda katika mashamba au mashamba ya mizabibu, ama kunywa maji kutoka kisima cho chote. Tutasafiri kwenye njia kuu ya mfalme hata tutakapokuwa tumekwisha kupita katika nchi yako.”

23 Lakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Wakati alipofika huko Yahasa, akapigana na Israeli.

24 Hata hivyo, Israeli alimshinda kwa upanga na kuiteka ardhi yake kutoka Arnoni mpaka Yaboki, lakini ni hadi kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta.

25 Israeli akaiteka miji yote ya Waamori na kuikalia, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka.

26 Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alikuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia na akawa amechukua ardhi yake yote mpaka Arnoni.

27 Ndiyo sababu watunga mashairi husema:

“Njoo Heshboni na ujengwe tena;

mji wa Sihoni na ufanywe upya.

28 “Moto uliwaka kutoka Heshboni,

mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni.

Uliteketeza Ari ya Moabu,

raia wa mahali pa Arnoni palipoinuka.

29 Ole wako, Ee Moabu!

Umeharibiwa, Enyi watu wa Kemoshi!

Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi,

na binti zake kama mateka

kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.

30 “Lakini tumewashinda;

Heshboni umeharibiwa hadi Diboni.

Tumebomoa hadi kufikia Nofa,

ulioenea hadi Medeba.”

31 Kwa hiyo Israeli akaishi katika nchi ya Waamori.

32 Baada ya Mose kutuma wapelelezi kwenda mji wa Yazeri, Waisraeli waliteka viunga vya mji huo na kuwafukuza Waamori waliokuwa wanaishi huko.

33 Kisha wakageuka na kwenda katika njia inayoelekea Bashani, naye Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote wakatoka kupigana nao huko Edrei.

34 Bwanaakamwambia Mose, “Usimwogope Ogu, kwa sababu nimeshamkabidhi mikononi mwako, pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Mtendee kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”

35 Kwa hiyo wakamwua, pamoja na wanawe na jeshi lake lote, bila ya kumwacha hata mtu mmoja hai. Nao wakaimiliki nchi yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/21-ac29d865b2cda095a76e01534208e4a5.mp3?version_id=1627—

Hesabu 22

Balaki Anamwita Balaamu

1 Kisha Waisraeli wakasafiri katika tambarare za Moabu na kupiga kambi kando ya Mto Yordani, ng’ambo ya Yeriko.

2 Basi Balaki mwana wa Sipori, aliona mambo yote yale Israeli aliyowatendea Waamori;

3 Moabu aliogopa, kwa kuwa walikuwapo watu wengi sana. Hakika, Moabu alijawa na hofu kubwa kwa sababu ya Waisraeli.

4 Wamoabu wakawaambia wazee wa Midiani, “Umati huu wa watu unakwenda kulamba kila kitu kinachotuzunguka, kama maksai alambavyo majani ya shambani.”

Kwa hiyo Balaki mwana wa Sipori, ambaye alikuwa mfalme wa Moabu wakati huo,

5 akatuma wajumbe kwenda kumwita Balaamu mwana wa Beori, ambaye alikuwa huko Pethori, karibu na Mto Eufrati, katika nchi yake ya kuzaliwa. Balaki akasema:

“Taifa limekuja kutoka Misri, nao wamefunika uso wa nchi, nao wametua karibu nami.

6 Sasa uje kuwalaani watu hawa, kwa kuwa wana nguvu sana kuliko mimi. Kisha huenda nikaweza kuwashinda na kuwatoa nje ya nchi. Kwa kuwa ninajua kwamba, wale unaowabariki wanabarikiwa na wale unaowalaani wanalaaniwa.”

7 Wazee wa Moabu na Wamidiani wakaondoka, wakiwa wamechukua ada ya uaguzi. Walipokwenda kwa Balaamu, wakamweleza kile Balaki alichokuwa amesema.

8 Balaamu akawaambia, “Mlale hapa usiku huu, nami nitawaletea jibu lileBwanaatakalonipa.” Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakakaa naye.

9 Mungu akamjia Balaamu na kumwuliza, “Watu gani hawa walio pamoja nawe?”

10 Balaamu akamwambia Mungu, “Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alinipelekea ujumbe huu:

11 ‘Taifa ambalo limekuja kutoka Misri limefunika uso wa nchi. Sasa uje unilaanie hao watu. Kisha huenda nitaweza kupigana nao na kuwafukuza.’ ”

12 LakiniBwanaakamwambia Balaamu, “Usiende pamoja nao. Hupaswi kulaani watu hao, kwa kuwa wamebarikiwa.”

13 Asubuhi iliyofuata akaamka, akawaambia wakuu wa Balaki, “Rudini katika nchi yenu, kwa kuwaBwanaamenikataza nisiende pamoja nanyi.”

14 Kwa hiyo wakuu wa Maobu wakarudi kwa Balaki na kumwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”

15 Kisha Balaki akatuma wakuu wengine, wengi zaidi na wanaoheshimiwa zaidi kuliko wale wa kwanza.

16 Wakafika kwa Balaamu na kumwambia:

“Balaki mwana wa Sipori amesema hivi: Usiruhusu kitu cho chote kikuzuie kuja kwangu,

17 kwa sababu nitakulipa vizuri sana na kufanya lo lote usemalo. Njoo unilaanie watu hawa.”

18 Lakini Balaamu akawajibu, “Hata kama Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, singeweza kufanya kitu cho chote kikubwa au kidogo ili kutenda kitu nje ya agizo laBwanaMungu wangu.

19 Mlale hapa usiku huu kama wale wengine walivyofanya, nami nitatafuta ni nini kingineBwanaatakachoniambia.”

20 Usiku uleBwanaakamjia Balaamu na kumwambia, “Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita wewe, nenda nao, lakini ufanye tu lile nitakalokuambia.”

Punda Wa Balaamu

21 Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.

22 Lakini Mungu alikasirika sana alipokwenda, naye malaika waBwanaakasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

23 Wakati punda alipomwona malaika waBwanaakiwa amesimama barabarani akiwa na upanga uliofutwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani.

24 Ndipo malaika waBwanaakasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili.

25 Punda alipomwona malaika waBwana, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda.

26 Kisha malaika waBwanaakaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwepo nafasi ya kugeuka, upande wa kulia wala wa kushoto.

27 Punda alipomwona malaika waBwana, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake.

28 KishaBwanaakakifunua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?”

29 Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningelikuwa na upanga mkononi mwangu, ningelikuua sasa hivi.”

30 Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?”

Akajibu, “Hapana.”

31 KishaBwanaakafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika waBwanaamesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi.

32 Malaika waBwanaakamwuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu.

33 Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.”

34 Balaamu akamwambia malaika waBwana, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.”

35 Malaika waBwanaakamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki.

36 Balaki aliposikia kuwa Balaamu anakuja, akatoka kumlaki katika mji wa Moabu, katika mpaka wa Arnoni, ukingoni mwa nchi yake.

37 Balaki akamwambia Balaamu, “Je, sikukupelekea jumbe za haraka? Kwa nini hukuja kwangu? Hivi kweli mimi siwezi kukulipa?”

38 Balaamu akajibu, “Vema, sasa nimekuja kwako. Lakini kwani nina uwezo wa kusema tu cho chote? Ni lazima niseme tu kile ambacho Mungu ataweka kinywani mwangu.”

39 Kisha Balaamu alikwenda na Balaki mpaka Kiriath-Husothi.

40 Balaki akatoa dhabihu ya ng’ombe na kondoo; baadhi yake akampa Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye.

41 Asubuhi iliyofuata Balaki akamchukua Balaamu mpaka Bamothi Baali, na kutoka huko Balaamu akawaona baadhi ya watu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/22-94907a16a7c2116fb8da1251a306061b.mp3?version_id=1627—

Hesabu 23

Ujumbe Wa Kwanza Wa Balaamu

1 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo waume saba.”

2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

3 Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninakwenda kando. HuendaBwanaatakuja kukutana nami. Lo lote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.

4 Mungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”

5 Bwanaakaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”

6 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu.

7 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:

“Balaki amenileta kutoka Aramu,

mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki.

Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo;

njoo unishutumie Israeli.’

8 Nitawezaje kuwalaani,

hao ambao Mungu hajawalaani?

Nitawezaje kuwashutumu

hao ambao Mungu hakuwashutumu?

9 Kutoka vilele vya miamba ninawaona,

kutoka mahali palipoinuka ninawatazama.

Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao,

nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.

10 Ni nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo,

au kuhesabu robo ya Israeli?

Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki,

na mwisho wangu na uwe kama wao!”

11 Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”

12 Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kileBwanaanachoweka katika kinywa changu?”

Ujumbe Wa Pili Wa Balaamu

13 Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.”

14 Basi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

15 Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapokwenda kuonana na Mungu kule.”

16 Bwanaakakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”

17 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamwuliza, “Je,Bwanaamesema nini?”

18 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:

“Balaki, inuka na usikilize,

nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.

19 Mungu si mtu, hata aseme uongo,

wala yeye si mwanadamu, hata ajute.

Je, anasema, kisha asitende?

Je, anaahidi, asitimize?

20 Nimepokea agizo kubariki;

amebariki, nami siwezi kubadilisha.

21 “Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo,

wala taabu katika Israeli.

Bwana, Mungu wao yu pamoja nao,

nayo sauti kuu ya Mfalme imo katikati yao.

22 Mungu aliwatoa kutoka Misri;

wao wana nguvu za nyati.

23 Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo,

wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli.

Sasa itasemwa kuhusu Yakobo

na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’

24 Taifa lainuka kama simba jike;

linajiinua kama simba

ambaye hatulii mpaka amalize kurarua mawindo yake

na kunywa damu ya mawindo yake.”

25 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”

26 Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lo lote analosemaBwana?”

Ujumbe Wa Tatu Wa Balaamu

27 Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.”

28 Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.

29 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo waume saba kwa ajili yangu.”

30 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/23-4c471dea8647356566b93305053ba025.mp3?version_id=1627—

Hesabu 24

1 Basi Balaamu alipoona imempendezaBwanakubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani.

2 Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake,

3 naye akatoa ujumbe wake:

“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,

ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;

4 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,

# ambaye huona maono kutoka kwa Mwenyezi,

ambaye huanguka kifudifudi, na ambaye macho yake yamefunguka:

5 “Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, Ee Yakobo,

maskani yako, Ee Israeli!

6 “Kama mabonde, yanaenea,

kama bustani kando ya mto,

kama miti ya udi iliyopandwa naBwana,

kama mierezi kando ya maji.

7 Maji yatatiririka kutoka katika ndoo zake;

mbegu yake itakuwa na maji tele.

“Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi;

ufalme wake utatukuka.

8 “Mungu alimleta kutoka Misri;

yeye ana nguvu kama nyati.

Anayararua mataifa yaliyo adui zake,

na kuvunja mifupa yao vipande vipande;

huwachoma kwa mishale yake.

9 Hujikunyata na kuvizia kama simba,

kama simba jike; nani anayethubutu kumwaamsha?

“Abarikiwe kila akubarikiye,

na alaaniwe kila akulaaniye!”

10 Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kulaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu.

11 Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakiniBwanaamekuzuia usizawadiwe.”

12 Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi,

13 ‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu cho chote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo laBwana, nami imenipasa kusema tu kileBwanaatakachosema’?

14 Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.”

Ujumbe Wa Nne Wa Balaamu

15 Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake:

“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,

ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;

16 ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,

ambaye ana maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana,

huona maono kutoka Mwenyezi,

ambaye huanguka kifudifudi

na ambaye macho yake yamefunguka:

17 “Namwona yeye, lakini si sasa;

namtazama yeye, lakini si karibu.

Nyota itatoka kwa Yakobo,

fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli.

Atawaponda Wamoabu vipaji vya nyuso

na mafuvu yote ya wana wa Shethi.

18 Edomu itamilikiwa,

Seiri, adui wake, itamilikiwa,

lakini Israeli atakuwa na nguvu.

19 Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo

na kuangamiza walionusurika katika mji.”

Ujumbe Wa Mwisho Wa Balaamu

20 Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake:

“Amaleki ilikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa,

lakini mwisho wake itaangamizwa milele.”

21 Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake:

“Makao yenu ni salama,

kiota chenu kiko kwenye mwamba.

22 Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa

Ashuru atakapowachukuwa mateka.”

23 Ndipo akatoa ujumbe wake:

“Lo, ni nani atakayeweza kuishi wakati Mungu atakapofanya hili?

24 Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu,

zitaitiisha Ashuru na Eberi,

lakini nao pia wataangamizwa.”

25 Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani kwake, naye Balaki akashika njia yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NUM/24-8db1943ec6fa9461e30b691addbe0457.mp3?version_id=1627—