Kutoka 12

Pasaka

1 Bwanaakamwambia Mose na Aroni katika nchi ya Misri,

2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu.

3 Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba.

4 Ikiwa nyumba yo yote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu.

5 Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasio kuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi.

6 Tunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.

7 Ndipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao.

8 Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu.

9 Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani.

10 Msibakize nyama yo yote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto.

11 Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka yaBwana.

12 “Usiku uo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumwua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimiBwana.

13 Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

14 “Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu; mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwaBwana, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu.

15 Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana ye yote atakayekula cho chote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka katika Israeli.

16 Katika siku ya kwanza mwe na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.

17 “Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu.

18 Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja.

19 Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yo yote katika nyumba zenu. Ye yote alaye cho chote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka katika jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa.

20 Msile cho chote kilichotiwa chachu. Po pote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”

21 Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.

22 Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu ye yote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi.

23 Bwanaapitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.

24 “Shikeni maagizo haya kuwa kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu.

25 Mtakapoingia katika nchiBwanaatakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii.

26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’

27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwaBwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu.

28 Waisraeli wakafanya kama vileBwanaalivyomwagiza Mose na Aroni.

29 Ilipofika usiku wa manane,Bwanaakawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia.

30 Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.

Kutoka

31 Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni katika watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabuduBwanakama mlivyoomba.

32 Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ng’ombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”

33 Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”

34 Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao.

35 Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo.

36 BasiBwanaalikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.

37 Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto.

38 Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ng’ombe.

39 Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.

40 Waisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430.

41 Ilikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vyaBwanavilipokuwa vimeondoka Misri.

42 Kwa sababuBwanaaliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, katika usiku huu Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimuBwanakatika vizazi vijavyo.

Masharti Kwa Ajili Ya Pasaka

43 Bwanaakamwambia Mose na Aroni, “Haya ndiyo masharti kwa ajili ya Pasaka:

“Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka.

44 Mtumwa ye yote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri,

45 lakini kibarua ye yote au msafiri haruhusiwi kula.

46 “Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yo yote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wo wote.

47 Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka yaBwanani lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume ye yote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila.

49 Sheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

50 Waisraeli wote walifanya kama vileBwanaalivyomwagiza Mose na Aroni.

51 Siku ile ileBwanaakawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/12-461c48e88df7e68ba51136f2ea0fa276.mp3?version_id=1627—

Kutoka 13

Kuwekwa Wakfu Kwa Wazaliwa Wa Kwanza

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Niwekeeni wakfu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kila mtoto wa kwanza aliye kifungua tumbo miongoni mwa Waisraeli ni mali yangu, akiwa wa mwanadamu au wa mnyama.”

3 Ndipo Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii, siku ambayo mlitoka katika nchi ya Misri, katika nchi ya utumwa, kwa sababuBwanaaliwatoa humo kwa mkono wenye nguvu. Msile cho chote kilichotiwa chachu.

4 Leo, katika mwezi wa Abibu, mnatoka.

5 Bwanaatakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi aliyowaapia baba zako kukupa, nchi itiririkayo maziwa na asali, utaiadhimisha sikukuu hii katika mwezi huu:

6 Kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu na katika siku ya saba utamfanyiaBwanasikukuu.

7 Kwa muda wa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu, pasionekane kitu cho chote kilicho na chachu miongoni mwako, wala chachu yo yote isionekane po pote ndani ya mipaka yako.

8 Siku ile utamwambia mwanao, ‘Nafanya hivi kwa sababu ya jambo ambaloBwanaalinitendea nilipotoka katika nchi ya Misri.’

9 Adhimisho hili, litakuwa kama alama kwenye mkono wako na ukumbusho katika paji lako la uso, kwamba sheria yaBwanainapaswa iwe kinywani mwako. Kwa kuwaBwanaalikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.

10 Ni lazima uishike amri hii kwa wakati uliopangwa mwaka baada ya mwaka.

11 “Baada yaBwanakukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako,

12 inakupasa kumtoleaBwanamzaliwa wa kwanza wa kila tumbo. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali yaBwana.

13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hukumkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.

14 “Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvuBwanaalitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.

15 Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka,Bwanaaliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwaBwanamzaliwa wa kwanza wa kiume, wa kila tumbo na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’

16 Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwambaBwanaalikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”

Nguzo Ya Wingu Na Moto

17 Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitiayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.”

18 Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka katika nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.

19 Mose akachukua mifupa ya Yosefu kwa sababu Yosefu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwiichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.”

20 Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa.

21 Wakati wa mchanaBwanaaliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku.

22 Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/13-bcb99f8610e594b7b0b18e7efa259fd8.mp3?version_id=1627—

Kutoka 14

Kuvuka Bahari Ya Shamu

1 NdipoBwanaakamwambia Mose,

2 “Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni.

3 Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’

4 Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimiBwana.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.

5 Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!”

6 Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake.

7 Akachukua magari bora mia sita, pamoja na magari mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote.

8 Bwanaakaufanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri.

9 Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.

10 Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamliliaBwana.

11 Wakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuweko makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri?

12 Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”

13 Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovuBwanaatakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena.

14 Bwanaatawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”

15 NdipoBwanaakamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.

16 Inua fimbo yako na unyoshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini.

17 Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake.

18 Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimiBwananitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”

19 Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma,

20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.

21 Ndipo Mose akanyosha mkono wake juu ya bahari, nayeBwanaakayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika,

22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

23 Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi.

24 Karibia mapambazuko,Bwanaakaliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha.

25 Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli!Bwanaanawapigania dhidi ya Misri.”

Wafuatiaji Wazama

26 NdipoBwanaakamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.”

27 Mose akanyosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakiniBwanaakawasukumia ndani ya bahari.

28 Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.

29 Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

30 Siku ileBwanaakawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa.

31 Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwaBwanaaliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopaBwanana wakaweka tumaini lao kwake na kwa Mose mtumishi wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/14-dee8855e49f0992cf88254d4bb835d84.mp3?version_id=1627—

Kutoka 15

Wimbo Wa Mose Na Miriamu

1 Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbiaBwanawimbo huu:

“NitamwimbiaBwana,

kwa kuwa ametukuzwa sana.

Farasi na mpanda farasi

amewatosa baharini.

2 Bwanani nguvu zangu na wimbo wangu;

amekuwa wokovu wangu.

Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,

Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

3 Bwanani shujaa wa vita;

Bwanandilo jina lake.

4 Magari ya vita ya Farao na jeshi lake

amewatosa baharini.

Maafisa wa Farao walio bora sana

wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.

5 Maji yenye kina yamewafunika,

wamezama mpaka vilindini kama jiwe.

6 “Mkono wako wa kuume, EeBwana

ulitukuka kwa uweza.

Mkono wako wa kuume, EeBwana,

ukamponda adui.

7 Katika ukuu wa utukufu wako,

ukawaangusha chini wale waliokupinga.

Uliachia hasira yako kali,

ikawateketeza kama kapi.

8 Kwa pumzi ya pua zako

maji yalijilundika.

Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,

vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

9 “Adui alijivuna,

‘Nitawafuatia, nitawapata.

Nitagawanya nyara;

nitajishibisha kwa wao.

Nitafuta upanga wangu

na mkono wangu utawaangamiza.’

10 Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,

bahari ikawafunika.

Wakazama kama risasi

kwenye maji makuu.

11 “Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, EeBwana?

Ni nani kama Wewe:

uliyetukuka katika utakatifu,

utishaye katika utukufu,

ukitenda maajabu?

12 Uliunyosha mkono wako wa kuume

na nchi ikawameza.

13 “Katika upendo wako usiokoma utawaongoza

watu uliowakomboa.

Katika nguvu zako utawaongoza

mpaka makao yako matakatifu.

14 Mataifa watasikia na kutetemeka,

uchungu utawakamata watu wa Ufilisti.

15 Wakuu wa Edomu wataogopa,

viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,

watu wa Kanaani watayeyuka,

16 vitisho na hofu vitawaangukia.

Kwa nguvu ya mkono wako

watatulia kama jiwe,

mpaka watu wako waishe kupita, EeBwana,

mpaka watu uliowanunua wapite.

17 Utawaingiza na kuwapandikiza

juu ya mlima wa urithi wako:

hapo mahali, EeBwana, ulipopafanya kuwa makao yako,

mahali patakatifu, EeBwana, ulipopajenga kwa mikono yako.

18 Bwanaatatawala

milele na milele.”

19 Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini,Bwanaaliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini wana wa Israeli walipita baharini mahali pakavu.

20 Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza.

21 Miriamu akawaimbia:

“MwimbieniBwana,

kwa maana ametukuka sana.

Farasi na mpanda farasi

amewatosa baharini.”

Maji Ya Mara Na Elimu

22 Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji.

23 Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara.)

24 Kwa hiyo watu wakamnung’unikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?”

25 Ndipo Mose akamliliaBwana, nayeBwanaakamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.

HukoBwanaakawapa amri na sheria na huko akawajaribu.

26 Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti yaBwanaMungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wo wote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimiBwana, niwaponyaye.”

27 Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/15-59e293d86eea0dfee99768ebff317802.mp3?version_id=1627—

Kutoka 16

Mana Na Kware

1 Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri.

2 Huko jangwani hiyo jumuiya yote ikamnung’unikia Mose na Aroni.

3 Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono waBwanahuko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”

4 KishaBwanaakamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu.

5 Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”

6 Kwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwambaBwanandiye aliyewatoa katika Misri,

7 kisha asubuhi mtauona utukufu waBwana, kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunung’unikie?”

8 Pia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwaBwanawakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnung’uniki dhidi yetu, bali dhidi yaBwana.”

9 Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zakeBwana, kwa maana amesikia manung’uniko yenu.’ ”

10 Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu waBwanaukitokeza katika wingu.

11 Bwanaakamwambia Mose,

12 “Nimesikia manung’uniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimiBwanaMungu wenu.’ ”

13 Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi.

14 Wakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa.

15 Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.

Mose akawaambia, “Huu ndio mkate ambaoBwanaamewapa mle.

16 Hivi ndivyoBwanaalivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishimoja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ”

17 Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu.

18 Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, pia yule aliyekusanya kidogo hakuwa na upungufu. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

19 Kisha Mose akawaambia, “Mtu ye yote asibakize cho chote mpaka asubuhi.”

20 Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia.

21 Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka.

22 Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwuarifu Mose.

23 Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagizaBwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwaBwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini cho chote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”

24 Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu.

25 Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwaBwana. Hamtapata cho chote juu ya nchi leo.

26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo cho chote.”

27 Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata cho chote.

28 NdipoBwanaakamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini?

29 Fahamuni kuwaBwanaamewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.”

30 Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.

31 Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.

32 Mose akasema, “Hivi ndivyo alivyoagizaBwana: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”

33 Kwa hiyo Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele zaBwanaili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

34 KamaBwanaalivyomwagiza Mose, hatimaye Aroni alikuja kuihifadhi ndani ya Sanduku la Ushuhuda.

35 Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana mpaka walipofika mpakani mwa Kanaani.

36 (Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.)

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/16-021c3b6793586c4779042bb2798f880c.mp3?version_id=1627—

Kutoka 17

Maji Kutoka Kwenye Mwamba

1 Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kamaBwanaalivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa.

2 Kwa hiyo wakagombana na Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”

Mose akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribuBwana?”

3 Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanung’unika dhidi ya Mose, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”

4 Kisha Mose akamliliaBwana, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”

5 Bwanaakamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Nile, nawe uende.

6 Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli.

7 Naye akapaita mahali pale Masana Meriba, kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribuBwanawakisema, “Je,Bwanayu pamoja nasi au la?”

Vita Na Waamaleki

8 Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu.

9 Mose akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”

10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Mose alivyomwagiza, nao Mose, Aroni na Huri wakapanda juu ya kilima.

11 Ikawa wakati wote Mose alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda.

12 Mikono ya Mose ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Aroni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Mose, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki imeinuliwa mpaka jua lilipozama.

13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.

14 KishaBwanaakamwambia Mose, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”

15 Mose akajenga madhabahu na kuiita, Yehova Nisi.

16 Mose akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa mpaka kwenye kiti cha enzi chaBwana.Bwanaatakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kutoka kizazi hata kizazi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/17-4b1a9844ef7ad31cc5c584330df7a670.mp3?version_id=1627—

Kutoka 18

Yethro Amtembelea Mose

1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Mose na watu wake wa Israeli, pia jinsiBwanaalivyowatoa Israeli Misri.

2 Baada ya Mose kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea

3 pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershoni, kwa kuwa Mose alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”

4 Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”

5 Yethro, baba mkwe wa Mose, pamoja na wana wawili wa Mose na mkewe, wakamjia Mose huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu.

6 Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”

7 Kwa hiyo Mose akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani.

8 Mose akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kituBwanaalichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsiBwanaalivyowaokoa.

9 Yethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuriBwanaaliyowatendea Waisraeli katika kuwaokoa na mkono wa Wamisri.

10 Akasema, “Sifa na ziwe kwaBwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri.

11 Sasa najua ya kuwaBwanani mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.”

12 Kisha Yethro, baba mkwe wa Mose, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Aroni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Mose mbele za Mungu.

Ushauri Wa Yethro

13 Siku iliyofuata, Mose akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni.

14 Baba mkwe wake alipoona yote Mose anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”

15 Mose akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu.

16 Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.”

17 Baba mkwe wa Mose akamjibu, “Unachofanya sio kizuri.

18 Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe.

19 Sasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake.

20 Uwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya.

21 Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.

22 Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe.

23 Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”

Kuchaguliwa Kwa Waamuzi

24 Mose akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema.

25 Akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi.

26 Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Mose, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.

27 Kisha Mose akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi katika nchi yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/18-8d053026aca932600fd4604168ebbed4.mp3?version_id=1627—

Kutoka 19

Waisraeli Kwenye Mlima Sinai

1 Mnamo mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, siku kama iyo hiyo, wakafika katika Jangwa la Sinai.

2 Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima.

3 Kisha Mose akakwea kwenda kwa Mungu, nayeBwanaakamwita kutoka kwenye ule mlima akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia watu wa Israeli:

4 ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mbawa za tai na kuwaleta kwangu.

5 Sasa kama mkinitii kikamilifu na kutunza Agano langu, basi ninyi mtakuwa mali yangu ya thamani kubwa miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu,

6 ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndiyo maneno utakayosema kwa wana wa Israeli.”

7 Kwa hiyo Mose akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayoBwanaalikuwa amemwamuru ayaseme.

8 Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kituBwanaalichokisema.” Naye Mose akarudisha majibu yao kwaBwana.

9 Bwanaakamwambia Mose, “Nitakujia katika wingu zito, ili watu wanisikie nikinena nawe na kila mara waweke tumaini lao kwako.” Kisha Mose akamwambiaBwanayale ambayo watu walikuwa wamesema.

10 NayeBwanaakamwambia Mose, “Nenda kwa watu ukawaweke wakfu leo na kesho. Waambie wafue nguo zao

11 na wawe tayari katika siku ya tatu, kwa sababu siku hiyo,Bwanaatashuka juu ya mlima Sinai machoni pa watu wote.

12 Weka mipaka kuzunguka mlima kwa ajili ya watu, uwaambie, ‘Mwe waangalifu, msije mkapanda mlimani au kuugusa. Ye yote atakayeugusa mlima hakika atauawa.

13 Hakika atapigwa mawe au kupigwa mishale; mkono wa mtu hautamgusa. Akiwa mwanadamu au mnyama, hataruhusiwa kuishi.’ Ila tu wakati baragumu itakapopigwa kwa mfululizo, ndipo watu wote watakapopanda mlimani.”

14 Baada ya Mose kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao.

15 Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume ye yote asimkaribie mwanamke.”

16 Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka.

17 Kisha Mose akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima.

18 Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababuBwanaalishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka kwenye tanuru kubwa na mlima wote ukatetemeka kwa nguvu nyingi,

19 nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Mose akazungumza na sauti yaBwanaikamjibu.

20 Bwanaakashuka juu ya mlima Sinai na akamwita Mose apande juu mlimani. Kwa hiyo Mose akapanda juu

21 naBwanaakamwambia, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwonaBwanana wengi wao wakafa.

22 Hata makuhani, watakaomkaribiaBwanani lazima wajiweke wakfu, la sivyoBwanaatawaadhibu.”

23 Mose akamwambiaBwana, “Watu hawawezi kupanda mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ”

24 Bwanaakajibu, “Shuka ukamlete Aroni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwaBwana, nisije nikawaadhibu.”

25 Basi Mose akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/19-f8dcaee78cf7a2f20a50619359ad7fe0.mp3?version_id=1627—

Kutoka 20

Amri Kumi

1 Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:

2 “Mimi ndimiBwanaMungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.

3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.

4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji.

5 Usivisujudie au kuviabudu; kwa kuwa Mimi,BwanaMungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,

6 lakini ninaonyesha upendo kwa vizazi elfu vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.

7 Usilitaje bure jina laBwanaMungu wako, kwa kuwaBwanahataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.

8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase.

9 Kwa siku sita utafanya kazi zako zote,

10 lakini siku ya saba ni Sabato kwaBwanaMungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yo yote, wewe, wala mwana wako au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.

11 Kwa kuwa kwa siku sita,Bwanaaliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyoBwanaakaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.

12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupaBwanaMungu wako.

13 Usiue.

14 Usizini.

15 Usiibe.

16 Usitoe ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yako.

17 Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wake au punda wake, wala cho chote kile alicho nacho jirani yako.”

18 Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali

19 na wakamwambia Mose, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”

20 Mose akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”

21 Watu wakabaki mbali, wakati Mose alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.

Sanamu Na Madhabahu

22 KishaBwanaakamwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni:

23 Msijifanyizie miungu yo yote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.

24 “ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo zako, mbuzi na ng’ombe zako. Po pote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki.

25 Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi.

26 Msitumie ngazi kupandia kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/20-7933d7c9e006684b236f50dd5eeb824f.mp3?version_id=1627—

Kutoka 21

1 “Hizi ndizo sheria utakazoweka mbele ya Waisraeli:

Watumishi Wa Kiebrania

2 “Kama ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia kwa miaka sita. Lakini katika mwaka wa saba, atakuwa huru naye atakwenda zake pasipo kulipa cho chote.

3 Kama akija peke yake, atakwenda huru peke yake, lakini kama akija na mke, ataondoka pamoja naye.

4 Kama bwana wake alimpatia mke naye akamzalia wana au binti, mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wake na huyo mwanaume ataondoka peke yake.

5 “Lakini kama mtumishi akisema, ‘Ninampenda bwana wangu, mke wangu pamoja na watoto na sitaki kuwa huru,’

6 ndipo bwana wake atakapolazimika kumpeleka mbele ya waamuzi. Kisha atampeleka kwenye mlango au kizingiti na kutoboa sikio lake kwa shazia. Naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote.

7 “Kama mtu akimwuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume waachiwavyo.

8 Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumwuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu.

9 Kama akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake.

10 Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa.

11 Iwapo hatamtosheleza kwa mambo hayo matatu, huyo mke wa kwanza ataondoka na kuwa huru bila malipo yo yote ya fedha.

Majeraha Ya Mwilini

12 “Ye yote ampigaye mtu na kumwua ni lazima auawe hakika.

13 Hata hivyo, kama hakumwua kwa makusudi, lakini Mungu akaruhusu itokee hivyo, basi atakimbilia mahali nitakapomchagulia.

14 Lakini kama mtu akipanga na kumwua mwingine kwa makusudi, mwondoe katika madhabahu yangu na kumwua.

15 “Ye yote amshambuliaye baba yake au mama yake ni lazima auawe.

16 “Ye yote amtekaye nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe.

17 “Ye yote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe.

18 “Kama watu wakigombana na mmoja akimpiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa bali akaugua na kulala kitandani,

19 yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia kama mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda wake aliopoteza na awajibike mpaka apone kabisa.

20 “Kama mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na mtumwa huyo akafa papo hapo, ni lazima aadhibiwe

21 lakini ikiwa mtumwa ataamka baada ya siku moja au mbili, hataadhibiwa, kwa sababu yule mtumwa ni mali yake.

22 “Ikiwa watu wawili wanapigana na wakamwumiza mwanamke mja mzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua.

23 Lakini kukiwa na jeraha kubwa, ni lazima ulipe uhai kwa uhai,

24 jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,

25 kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, mchubuko kwa mchubuko.

26 “Ikiwa mtu atampiga mtumwa mwanaume au mwanamke kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho.

27 Kama akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino.

28 “Kama fahali akimwua mwanaume au mwanamke kwa kumpiga kwa pembe, fahali huyo ni lazima auawe kwa kupigwa mawe, na nyama yake haitaliwa. Lakini mwenye fahali huyo hatawajibika.

29 Lakini hata hivyo, ikiwa huyo fahali amekuwa na tabia ya kupiga kwa pembe, na mwenyewe ameonywa na hakutaka kumfungia naye akamwua mwanaume au mwanamke, huyo fahali ni lazima auawe kwa mawe na mwenye fahali pia auawe.

30 Lakini ikiwa malipo yatatakiwa kwake, basi anaweza kulipa kinachodaiwa ili kuukomboa uhai wake.

31 Sheria hii pia itatumika ikiwa fahali atampiga kwa pembe mwana au binti.

32 Ikiwa fahali atampiga mtumwa wa kike au wa kiume, mwenye fahali atalipa shekeli thelathiniza fedha kwa bwana mwenye mtumwa, na fahali ni lazima auawe kwa mawe.

33 “Kama mtu akiacha shimo wazi, ama akachimba shimo kisha asilifukie, na ng’ombe au punda akatumbukia ndani yake,

34 mwenye shimo ni lazima alipe hasara iliyotokea; ni lazima amlipe mwenye mnyama. Mnyama aliyekufa atakuwa wake.

35 “Kama fahali wa mtu fulani atamwumiza fahali wa mtu mwingine na akafa, watamwuza yule aliye hai na wagawane sawa fedha pamoja na mnyama aliyekufa.

36 Hata hivyo, kama ikifahamika kwamba fahali huyo alikuwa na tabia ya kupiga kwa pembe na mwenyewe hakumfunga, ni lazima mwenye fahali alipe mnyama kwa mnyama, na mnyama aliyekufa atakuwa wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/21-420047c3582a586d61248a7ca6e74c6b.mp3?version_id=1627—