Kutoka 32

Ndama Ya Dhahabu

1 Watu walipoona kuwa Mose amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimkusanyikia Aroni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui jambo lililompata.”

2 Aroni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu na binti zenu wamevaa, mkaniletee.”

3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Aroni.

4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akavifanyiza kwa kusubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, Ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”

5 Aroni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwaBwana.”

6 Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.

7 KishaBwanaakamwambia Mose, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka.

8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kuyeyusha yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, Ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”

9 Bwanaakamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu.

10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”

11 Lakini Mose akamsihiBwanaMungu wake, akasema, “EeBwana, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu?

12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako.

13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ”

14 KishaBwanaakawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.

15 Mose akageuka, akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma.

16 Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.

17 Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Mose, “Kuna sauti ya vita kambini.”

18 Mose akajibu:

“Si sauti ya ushindi,

wala si sauti ya kushindwa;

ni sauti ya kuimba ninayosikia.”

19 Mose alipoikaribia kambi na kuona ile ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima.

20 Kisha akaichukua ile ndama waliyokuwa wameitengeneza na kuichoma kwenye moto, kisha akaisaga kuwa unga, akainyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.

21 Mose akamwambia Aroni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”

22 Aroni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu.

23 Wao waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatufahamu yaliyompata.’

24 Kwa hiyo nikawaambia, ‘Ye yote aliye na kito cho chote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”

25 Mose akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Aroni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao.

26 Kwa hiyo Mose akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Ye yote aliye upande waBwana, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.

27 Ndipo alipowaambia, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ”

28 Walawi wakafanya kama Mose alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao 3,000.

29 Kisha Mose akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwaBwana, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”

30 Siku iliyofuata Mose akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwaBwana, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”

31 Hivyo Mose akarudi kwaBwanana kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu.

32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kwenye kitabu ulichoandika.”

33 Bwanaakamjibu Mose, “Ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kwenye kitabu changu.

34 Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”

35 NdipoBwanaakawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya kwa ndama yule ambaye alitengenezwa na Aroni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/32-9c2805473ce6b5eed5f11431bc48c748.mp3?version_id=1627—

Kutoka 33

Amri Ya Kuondoka Sinai

1 KishaBwanaakamwambia Mose, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande mpaka nchi niliyomwahidi Abrahamu, Isaki na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’

2 Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

3 Pandeni mwende katika nchi itiririkayo maziwa na asali. Lakini mimi sitakwenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.”

4 Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yo yote.

5 Kwa kuwaBwanaalikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ”

6 Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima wa Horebu.

Hema La Kukutania

7 Basi Mose alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kulisimika nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania.” Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwaBwana, angelikwenda katika Hema la Kukutania nje ya kambi.

8 Wakati wo wote Mose alipokwenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Mose mpaka aingie kwenye Hema.

9 Kila mara Mose alipoingia ndani ya hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mungu akizungumza na Mose.

10 Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake.

11 Bwanaangezungumza na Mose uso kwa uso, kama vile mtu azungumzavyo na rafiki yake. Kisha Mose angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka mle Hemani.

Mose Na Utukufu Wa Bwana

12 Mose akamwambiaBwana, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’

13 Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.”

14 Bwanaakajibu, “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”

15 Kisha Mose akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa.

16 Mtu ye yote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipokwenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”

17 Bwanaakamwambia Mose, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.”

18 Kisha Mose akasema, “Basi nionyeshe utukufu wako.”

19 NdipoBwanaakasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu,Bwana, mbele ya uso wako. Nitakuwa na rehema kwake yeye nimrehemuye, pia nitakuwa na huruma kwake yeye nimhurumiaye.”

20 Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu ye yote awezaye kuniona akaishi.”

21 KishaBwanaakasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba.

22 Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba na kukufunika kwa mkono wangu mpaka nitakapokwisha kupita.

23 Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/33-e6cc9ea400bc61d52ad6d5ff52e892b6.mp3?version_id=1627—

Kutoka 34

Vibao Vipya Vya Mawe

1 Bwanaakamwambia Mose, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitaandika juu yake maneno yale yaliyokuwa kwenye vile vibao vya kwanza, ulivyovivunja.

2 Uwe tayari asubuhi, kisha upande juu ya Mlima Sinai. Uje mbele zangu kukutana nami huko juu ya mlima.

3 Mtu ye yote asije pamoja nawe, wala asionekane mtu po pote juu ya mlima, wala kondoo na mbuzi au ng’ombe wasilishe karibu mbele ya huo mlima.”

4 Kwa hiyo Mose akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, naye akapanda juu ya Mlima Sinai asubuhi na mapema, kamaBwanaalivyokuwa amemwagiza, akachukua vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake.

5 KishaBwanaakashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake,Bwana.

6 Bwanaakapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana,Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu,

7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

8 Mara Mose akasujudu na kuabudu.

9 Mose akasema, “EeBwana, kama nimepata kibali mbele zako, basiBwanauende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”

10 KishaBwanaakasema: “Tazama ninafanya Agano mbele ya watu wako wote. Mbele ya watu wako wote nitafanya maajabu ambayo hayajafanyika katika taifa lo lote katika ulimwengu wote. Watu wale mnaoishi miongoni mwao wataona jinsi ilivyo ya kushangaza ile kazi nitakayowafanyia mimiBwanawenu.

11 Tii yale ninayokuamuru leo. Tazama nawafukuza mbele yako Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

12 Uwe mwangalifu, usifanye agano na wale wanaokaa katika nchi ile unayoiendea, la sivyo watakuwa mtego katikati yako.

13 Bomoa madhabahu zao, vunja mawe yao ya kuabudia na ukatekate nguzo zao za Ashera.

14 Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwaBwana, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu.

15 “Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe nawe utakula sadaka za matambiko yao.

16 Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.

17 “Usijifanyie sanamu za kusubu.

18 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, kama nilivyokuamuru. Fanya hivi kwa wakati ulioamuriwa, katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa kuwa katika mwezi huo ndipo wewe ulipotoka Misri.

19 “Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ng’ombe au wa kondoo au mbuzi.

20 Utakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume.

“Mtu ye yote asije mbele zangu mikono mitupu.

21 “Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.

22 “Utaadhimisha Sikukuu ya Majuma kwa malimbuko ya mavuno ya ngano, na Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka.

23 Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele zaBwanaMwenyezi, Mungu wa Israeli.

24 Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu ye yote atakayeitamani nchi yako wakati unapokwenda mara tatu kila mwaka kuonana naBwanaMungu wako.

25 “Usinitolee damu ya dhabihu pamoja na kitu cho chote chenye chachu, wala usibakize dhabihu yo yote ya Sikukuu ya Pasaka mpaka asubuhi.

26 “Leta matunda ya kwanza yaliyo bora zaidi ya ardhi yako katika nyumba yaBwanaMungu wako.

“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.”

27 KishaBwanaakamwambia Mose, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya Agano na wewe pamoja na Israeli.”

28 Mose alikuwa huko pamoja naBwanakwa siku arobaini mchana na usiku bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya Agano, yaani zile Amri Kumi.

Mng’ao Wa Uso Wa Mose

29 Mose alipotelemka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa uking’aa, kwa sababu alikuwa amezungumza naBwana.

30 Aroni na Waisraeli wote walipomwona Mose, kuwa uso wake unang’aa, waliogopa kumkaribia.

31 Lakini Mose akawaita, kwa hiyo Aroni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao.

32 Baadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zoteBwanaalizompa katika Mlima wa Sinai.

33 Mose alipomaliza kuzungumza nao, akaweka utaji kwenye uso wake.

34 Lakini kila wakati Mose alipoingia mbele zaBwanakuzungumza naye, aliondoa ule utaji mpaka alipotoka nje. Naye alipotoka nje na kuwaambia Waisraeli lile ambalo ameagizwa,

35 waliona kuwa uso wake unang’aa. Kisha Mose angeliweka tena utaji juu ya uso wake mpaka alipokwenda kuzungumza naBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/34-b3222e117fa8dbf0ba215956e619cab6.mp3?version_id=1627—

Kutoka 35

Masharti Ya Sabato

1 Mose akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndiyo mambo ambayoBwanaamewaamuru ninyi mfanye:

2 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya kupumzika kwaBwana. Ye yote atakayefanya kazi yo yote siku hiyo ni lazima auawe.

3 Msiwashe moto mahali po pote katika makazi yenu siku ya Sabato.”

Vifaa Kwa Ajili Ya Maskani Ya Mungu

4 Mose akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndiloBwanaaliloamuru:

5 Toeni kutoka katika yale mliyo nayo, sadaka kwaBwana. Kila mmoja kwa moyo wa kupenda atamleteaBwanasadaka ya dhahabu, fedha na shaba;

6 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi; singa za mbuzi;

7 ngozi za kondoo waume zilizopakwa rangi nyekundu na ngozi za mbuzi; mbao za mshita;

8 mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa, vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako pamoja na uvumba wa harufu nzuri;

9 vito vya shohamu na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani.

10 “Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kituBwanaalichoamuru:

11 Maskani pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako;

12 Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia;

13 meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonyesho;

14 kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga;

15 madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya maskani;

16 madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na kitako chake;

17 pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, pazia la ingilio la kwenye ua;

18 vigingi vya hema kwa ajili ya maskani pamoja na ua na kamba zake;

19 mavazi yaliyofumwa yavaliwayo wakati wa huduma ndani ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”

20 Ndipo jumuiya yote ya Waisraeli ilipoondoka mbele ya Mose,

21 na kila mmoja aliyependa na ambaye moyo wake ulimsukuma alikuja na kuleta sadaka kwaBwana, kwa ajili ya kazi katika Hema la Kukutania, kwa ajili ya huduma yake yote na kwa ajili ya mavazi matakatifu.

22 Wote waliokuwa na utayari, wanaume kwa wanawake, wakaja wakaleta vito vya dhahabu vya kila aina: vipini, vipuli, pete na mapambo. Wote wakatoa dhahabu zao kama sadaka ya kuinuliwa kwaBwana.

23 Kila mmoja aliyekuwa na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi, au singa za mbuzi, ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, au ngozi za mbuzi wakavileta.

24 Wale waliotoa sadaka ya fedha au shaba wakavileta kama sadaka kwaBwana, na kila aliyekuwa na mti wa mshita kwa ajili ya kazi yo yote ile akauleta.

25 Kila mwanamke aliyekuwa na ujuzi alisokota kwa mikono yake na alileta kile alichosokota, iwe ni nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, au za rangi nyekundu au kitani safi.

26 Wanawake wote waliopenda na waliokuwa na ujuzi wakasokota singa za mbuzi.

27 Viongozi wakaleta vito vya shohamu pamoja na vito vingine vya thamani kwa ajili ya kuweka kwenye kisibau na kwenye kifuko cha kifuani.

28 Wakaleta pia vikolezi na mafuta ya zeituni kwa ajili ya mwanga, kwa ajili ya mafuta ya upako na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri.

29 Waisraeli wote waume kwa wake waliokuwa wanapenda wakaleta mbele zaBwanakwa hiari yao wenyewe sadaka kwa ajili ya kazi yote yaBwanaaliyokuwa amewaagiza kuifanya kupitia kwa Mose.

Bezaleli Na Oholiabu

30 Kisha Mose akawaambia Waisraeli, “Tazameni,Bwanaamemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda,

31 naye amemjaza Roho wa Mungu, na ujuzi, uwezo na ustadi katika aina zote za ufundi,

32 ili kutengeneza michoro ya kitaalamu kwa ajili ya kazi za dhahabu, fedha na shaba,

33 kuchonga na kuyatia mawe mahali, kufanya kazi za mbao na kuhusika katika aina zote za kazi za ubunifu na ufundi.

34 Tena amemvuvia pamoja naye utaalamu huo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine.

35 Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zifanywazo na mafundi wenye kubuni, watarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi, au wafumaji; wote walikuwa mafundi na wabunifu hodari.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/35-a02786a17676a2db1f764b03be2606b1.mp3?version_id=1627—

Kutoka 36

1 Kwa hiyo Bezaleli, Oholiabu na kila mtuBwanaaliyempa ustadi na uwezo wa kujua jinsi ya kufanya kazi zote za kujenga mahali patakatifu wataifanya hiyo kazi kama vileBwanaalivyoagiza.”

2 Ndipo Mose akawaita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu mwenye ustadi ambayeBwanaalikuwa amempa uwezo na mwenye kupenda kuja na kufanya kazi.

3 Wakapokea kutoka kwa Mose sadaka zote ambazo Waisraeli walikuwa wameleta ili kuifanya kazi ya ujenzi wa Mahali Patakatifu. Nao watu wakaendelea kuleta sadaka za hiari kila asubuhi.

4 Ikafika wakati mafundi wote wenye ujuzi waliokuwa wakiifanya kazi yote ya mahali patakatifu wakasimamisha kazi zao

5 ili kuja kumwambia Mose, “Watu wanaleta zaidi kuliko mahitaji kwa ajili ya kazi hii ambayoBwanaameagiza ifanyike.”

6 Ndipo Mose akatoa agizo, nao wakapeleka neno hili katika kambi yote: “Mtu ye yote mwanaume au mwanamke asilete tena kitu cho chote kwa ajili ya sadaka ya mahali patakatifu.” Hivyo watu wakazuiliwa kuleta zaidi,

7 kwa sababu walivyokuwa navyo tayari vilitosha na kuzidi kuifanya kazi yote.

Maskani Ya Mungu

8 Watu wote wenye ustadi miongoni mwa wafanyakazi wote wakatengeneza maskani kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, pamoja na makerubi yaliyotariziwa juu yake na fundi stadi.

9 Mapazia yote yalikuwa yamelingana: kila moja lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nanena upana wa dhiraa nne.

10 Wakayaunganisha mapazia matano pamoja, pia wakafanya hivyo hivyo kwa yale mengine matano.

11 Kisha wakatengeneza vitanzi vya buluu kwenye upindo wa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi vingine katika pazia la mwisho la kipande cha pili.

12 Wakatengeneza pia vitanzi hamsini katika pazia la kipande cha kwanza, na vitanzi vingine hamsini mwishoni mwa pazia la pili na vitanzi vyote vikaelekeana.

13 Kisha wakatengeneza vibanio hamsini vya dhahabu, na wakavitumia kufunga na kuunganisha vile vipande viwili vya pazia pamoja ili maskani ipate kuwa kitu kimoja.

14 Wakatengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya hema juu ya maskani.

15 Mapazia yote kumi na moja yalikuwa yamelingana, urefu wa dhiraa thelathinina upana wa dhiraa nne.

16 Wakaunganisha mapazia matano pamoja na yale mengine sita pamoja.

17 Kisha wakatengeneza vitanzi hamsini kwenye upindo wa pazia la mwishoni la kipande cha kwanza, na vivyo hivyo kwenye upindo wa pazia la mwishoni la kipande cha pili.

18 Wakatengeneza vibanio hamsini vya shaba ili kulikaza hema pamoja kuwa kitu kimoja.

19 Kisha wakatengeneza kifuniko cha hema kwa ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi laini za wanyama.

20 Wakatengeneza mihimili ya kusimamisha ya mti wa mshita kwa ajili ya maskani.

21 Kila mhimili ulikuwa na urefu wa dhiraa kumina upana wa dhiraa moja na nusu,

22 zikiwa na ndimi mbili kila mmoja sambamba na mwingine. Wakatengeneza mihimili yote ya maskani kwa njia hii.

23 Wakatengeneza mihimili ishirini kwa ajili ya upande wa kusini wa maskani,

24 na wakatengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuwekwa chini yake, vitako viwili kwa kila mhimili, kimoja chini ya kila ulimi.

25 Kwa upande wa kaskazini wa maskani wakatengeneza mihimili ishirini

26 na vitako arobaini vya shaba, viwili chini ya kila mhimili.

27 Wakatengeneza mihimili sita kwa ajili ya upande wa mwisho, yaani upande wa magharibi wa maskani,

28 na mihimili miwili ikatengenezwa kwa ajili ya pembe za maskani za upande wa mwisho.

29 Katika pembe hizi mbili mihimili yake ilikuwa jozi moja kuanzia chini mpaka juu, na ikaingizwa kwenye pete moja; jozi zote mbili zilikuwa za kufanana.

30 Kwa hiyo kulikuwa na mihimili minane na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila kizingiti.

31 Wakatengeneza pia mataruma kwa mti wa mshita: matano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa maskani,

32 matano kwa ajili ya yale yaliyo upande mwingine, na matano kwa ajili ya upande wa magharibi, mwisho kabisa wa maskani.

33 Wakatengeneza taruma la katikati, likapenya katikati ya mihimili kutoka upande mmoja hadi mwingine.

34 Wakaifunika hiyo mihimili kwa dhahabu, na wakatengeneza pete za dhahabu za kushikilia hayo mataruma. Pia wakayafunika yale mataruma kwa dhahabu.

35 Wakatengeneza mapazia kwa nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kwa kitani iliyosokotwa vizuri, yakiwa yametariziwa makerubi na fundi stadi.

36 Wakatengeneza nguzo nne za mti wa mshita kwa ajili yake na kuzifunika kwa dhahabu. Wakatengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili yake na kusubu vitako vinne vya fedha.

37 Kwa ajili ya ingilio la hema wakatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi;

38 pia wakatengeneza nguzo tano zenye kulabu. Wakafunika ncha za juu za hizo nguzo kwa dhahabu pamoja na tepe zake, pia wakatengeneza vitako vyake vitano vya shaba.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/36-9e192d50f4046c5515d0a65539f7002c.mp3?version_id=1627—

Kutoka 37

Sanduku La Agano

1 Bezaleli akatengeneza Sanduku kwa mbao za mshita: urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja na nusu.

2 Akalifunika kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulizungushia ukingo wa dhahabu.

3 Akasubu pete nne za dhahabu na kuzifungia kwenye miguu yake minne, pete mbili kwa upande mmoja na nyingine mbili upande mwingine.

4 Kisha akatengeneza mipiko kwa mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.

5 Akaiingiza ile mipiko ndani ya zile pete kwenye pande za Sanduku ili kulibeba.

6 Akatengeneza kifuniko cha upatanisho kwa dhahabu safi: urefu wake dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.

7 Kisha akatengeneza makerubi mawili kwenye miisho ya kile kifuniko kutokana na dhahabu iliyofuliwa.

8 Akaweka kerubi moja mwisho huu na kerubi la pili mwisho mwingine; akayafanya kuwa kitu kimoja na hicho kifuniko.

9 Mabawa ya makerubi yalikuwa yaliyokunjuliwa kuelekea juu, yakitilia kifuniko uvuli. Makerubi yalielekeana, yakitazama kuelekea kifuniko.

Meza

10 Akatengeneza meza ya mbao za mshita urefu wake dhiraa mbili, upana wake dhiraa mojana kimo chake dhiraa moja na nusu.

11 Kisha akaifunika kwa dhahabu safi na kuitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka.

12 Pia akatengeneza upapi wenye upana wa nyanda nnekuizunguka ile meza na kuuweka ukingo wa dhahabu juu yake.

13 Akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili ya ile meza na kuzifungia kwenye pembe zake nne, pale penye miguu minne ya meza.

14 Pete hizo ziliwekwa karibu na ile duara ya upapi ili kuishikilia ile mipiko iliyotumika kuibebea hiyo meza.

15 Mipiko hiyo ya kubebea meza ilitengenezwa kwa mti wa mshita, na ilikuwa imefunikwa kwa dhahabu.

16 Vyombo vyote vya mezani vilitengenezwa kwa dhahabu safi; yaani, sahani zake, masinia, mabakuli na magudulia kwa ajili ya kumiminia sadaka za kinywaji.

Kinara Cha Taa

17 Akatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi iliyofuliwa vizuri, kitako chake na ufito, vikombe vyake vilivyofanana na ua, matovu na maua vilikuwa vya kitu kimoja.

18 Matawi sita yalijitokeza kwenye pande za kile kinara cha taa, matatu upande mmoja na matatu upande mwingine.

19 Vikombe vyenye muundo wa maua ya mlozi vikiwa na matovu na maua kwenye tawi moja, vitatu vilikuwa kwenye tawi lililofuata na yanayofanana na matawi yote sita yalitokeza kwenye kile kinara cha taa.

20 Juu ya kinara kulikuwepo na vikombe vinne vyenye muundo kama maua ya mlozi, vikiwa na matovu yake na maua yake.

21 Tovu moja lilikuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyojitokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani, jumla matawi sita.

22 Matovu na matawi vyote vilikuwa kitu kimoja na kinara cha taa, kikiwa kimefuliwa kwa dhahabu safi.

23 Akatengeneza taa zake saba, mikasi ya kusawazishia tambi pamoja na masinia ya dhahabu safi.

24 Akatengeneza kinara hicho cha taa pamoja na vifaa vyake vyote kutoka kwenye talantamoja ya dhahabu safi.

Madhabahu Ya Kufukizia Uvumba

25 Akatengeneza madhabahu ya kufukiza uvumba kwa mbao za mshita. Ilikuwa ya mraba, urefu wake dhiraa moja, upana wake dhiraa moja, na kimo chake dhiraa mbili: pembe zake zilikuwa za kitu kimoja nayo.

26 Sehemu ya juu ya meza pande zake zote pamoja na zile pembe zilifunikwa kwa dhahabu safi, pia akazitengenezea ukingo wa dhahabu kuizunguka.

27 Akatengeneza pete mbili za dhahabu chini ya huo ukingo, mbili kila upande, ili zishikilie ile mipiko iliyobebea hiyo madhabahu.

28 Akatengeneza mipiko kwa miti ya mshita na kuifunika kwa dhahabu.

29 Pia akatengeneza mafuta matakatifu ya upako na uvumba safi, wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/37-a9b1ff555c8c0e0dfb95e7ce17ab450c.mp3?version_id=1627—

Kutoka 38

Madhabahu Ya Sadaka Ya Kuteketezwa

1 Akatengeneza madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa mbao za mti wa mshita, kimo chake dhiraa tatu;nayo ilikuwa mraba, urefu wake dhiraa tano na upana wa dhiraa tano.

2 Akatengeneza upembe kwenye kila pembe katika hizo pembe nne, ili kwamba zile pembe na madhabahu ziwe zimeungana, akafunika madhabahu kwa shaba.

3 Akatengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, nyuma za nyama na sufuria za kuchukulia moto.

4 Akatengeneza wavu wa shaba, uwe chini ya ukingo wa madhabahu ili kwamba ufikie nusu ya kimo cha madhabahu.

5 Akasubu pete za shaba za kushikilia ile mipiko kwa ajili ya pembe nne za huo wavu wa shaba.

6 Akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuifunika kwa shaba.

7 Akaingiza ile mipiko kwenye zile pete, ili hiyo mipiko iwe upande huu na upande huu wa madhabahu kwa ajili ya kuibeba. Akaitengeneza madhabahu yenye uvungu ndani yake akitumia mbao.

Sinia La Kunawia

8 Akatengeneza sinia la shaba na kitako chake cha shaba kutokana na vioo vya shaba vilivyotolewa na wanawake waliohudumu penye ingilio la Hema la Kukutania.

Ua Wa Kukutania

9 Kisha akatengeneza ua ambao upande wa kusini ulikuwa na urefu wa dhiraa 100na ulikuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri,

10 wenye nguzo ishirini na vitako ishirini vya shaba, pia zilikuwa na kulabu za fedha na tepe za fedha juu yake.

11 Upande wa kaskazini ulikuwa pia na urefu wa dhiraa mia moja, na ulikuwa na wenye nguzo ishirini na vitako ishirini vya shaba, pamoja na kulabu za fedha na tepe za fedha juu yake.

12 Upande wa mwisho wa magharibi ulikuwa na upana wa dhiraa hamsinina ulikuwa na mapazia, pamoja na nguzo kumi na vitako kumi, pamoja na kulabu za fedha na tepe za fedha juu yake.

13 Upande wa mwisho wa mashariki linakotokea jua, pia kulikuwa na upana wa dhiraa hamsini.

14 Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tanoyalikuwa upande mmoja wa ingilio pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu,

15 mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mwingine wa ingilio kuelekea kwenye ua, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.

16 Mapazia yote yaliyozunguka ua yalikuwa ya kitani iliyosokotwa vizuri.

17 Vitako vya nguzo vilikuwa vya shaba. Kulabu na tepe juu ya nguzo zilikuwa za fedha, ncha zake zilifunikwa kwa fedha, kwa hiyo nguzo yote ya ua ilikuwa na tepe za fedha.

18 Pazia la kwenye ingilio la ua lilikuwa la kitani lililosokotwa vizuri la rangi ya buluu, ya zambarau, na nyekundu, kazi ya mtarizi. Pazia hilo lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini kama yale ya kwenye ua, kwenda juu kwake lilikuwa dhiraa tano,

19 pakiwa na nguzo nne na vitako vinne vya shaba. Kulabu zake na tepe zake zilikuwa za fedha, ncha zake zilikuwa zimefunikwa kwa fedha.

20 Vigingi vyote vya maskani vilivyozunguka ua vilikuwa vya shaba.

Vifaa Vilivyotumika

21 Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani, maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Mose, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni.

22 (Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kituBwanaalichomwamuru Mose,

23 akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.)

24 Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta 29 na shekeli 730, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.

25 Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli 1,775, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.

26 Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume 603,550.

27 Talanta hizo 100 za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na mapazia, vitako mia moja kwa talanta mia, yaani, talanta moja kwa kila kitako.

28 Akatumia zile shekeli hizo 1,775 kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo na kutengeneza vitanzi vyake.

29 Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta 70 na shekeli 2,400

30 Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote,

31 vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya Maskani pamoja na ule ua uliozunguka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/38-dbb1618944e3e8a66b40d4b03a202922.mp3?version_id=1627—

Kutoka 39

Mavazi Ya Kikuhani

1 Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Aroni mavazi matakatifu, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Kisibau

2 Akatengeneza kisibau kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.

3 Akafua kwa nyundo vipande vyembamba vya dhahabu na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kufuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi.

4 Akatengeneza vile vipande vya begani kwa ajili ya kisibau, vilivyokuwa vimeshikizwa kwenye pembe zake mbili, ili kiweze kufungwa.

5 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho, ulikuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao ulitengenezwa kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

6 Akatengeneza vito vya shohamu, vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa kama muhuri vikiwa na majina ya wana wa Israeli.

7 Kisha akavifungia kwenye vipande vya begani vya kisibau kuwa mawe ya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Kifuko Cha Kifuani

8 Akatengeneza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kisibau: kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, ya buluu, ya zambarau, nyekundu na za kitani iliyosokotwa vizuri.

9 Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri mojana upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili.

10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, yakuti manjano na zabarajadi;

11 safu ya pili ilikuwa ya almasi, yakuti samawi na zumaridi;

12 safu ya tatu ilikuwa ya yakintho, akiki nyekundu na amethisto;

13 katika safu ya nne ilikuwa ya krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo viliwekwa kwenye vijalizo vya dhahabu.

14 Palikuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kikiwa na jina mojawapo la wana wa Israeli; kila kito kilichorwa kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.

15 Kwa kile kifuko cha kifuani akakitengenezea mikufu ya dhahabu safi, mfano wa kamba.

16 Akaitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.

17 Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,

18 zile ncha nyingine za mikufu kwenye vile vijalizo viwili, akazishikamanisha na vile vipande vya begani vya kile kisibau kwa mbele.

19 Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzishikamanisha kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani kwenye ukingo wa ndani karibu na kisibau.

20 Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzishikamanisha upande wa chini wa vipande vya begani mbele ya kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau.

21 Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kisibau kwa kamba ya buluu, wakiiunganisha na mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisije kikasogea kutoka kwenye kile kisibau, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Mavazi Mengine Ya Kikuhani

22 Akatengeneza joho la kisibau lote la rangi ya buluu, kazi ya mfumaji.

23 Joho hilo lilikuwa na nafasi ya shingo yenye ukosi na utepe ulishonewa kwa kuizunguka nafasi hiyo ili lisichanike.

24 Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho.

25 Kisha akatengeneza njuga za dhahabu safi na kuzishikamanisha kuzunguka pindo kati ya makomamanga.

26 Njuga hizo na makomamanga vilipitana kwa kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

27 Pia akamtengenezea Aroni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji,

28 kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani na nguo za ndani za kitani zilizosokotwa vizuri.

29 Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, kazi ya mtarizi, kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

30 Kisha akatengeneza bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake kama mchoro juu ya muhuri: MTAKATIFU KWABwana.

31 Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kulishikamanisha na kile kilemba kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

Mose Akagua Maskani Ya Mungu

32 Kwa hiyo kazi yote ya maskani, Hema la Kukutania ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa kama vileBwanaalivyomwagiza Mose.

33 Ndipo wakaleta maskani kwa Mose: hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake;

34 kifuniko cha ngozi za kondoo waume kilichotiwa rangi nyekundu, kifuniko cha ngozi laini za wanyama, pazia la kufunikia;

35 Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema,

36 meza pamoja na vyombo vyake vyote na mikate ya Wonyesho;

37 kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa;

38 madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri na pazia la ingilio la hema;

39 madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote, sinia, na kishikilio chake;

40 mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na mapazia kwa ajili ya ingilio la kwenye ua; kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua; vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani, Hema la Kukutania;

41 na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa kwa kuhudumia mahali patakatifu, mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanapohudumu katika kazi ya ukuhani.

42 Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vileBwanaalivyokuwa amemwagiza Mose.

43 Mose akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa kama vileBwanaalivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Mose akawabariki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/39-9b32e7b9076812dcc57e7df68337f72f.mp3?version_id=1627—

Kutoka 40

Kusimika Maskani Ya Mungu

1 KishaBwanaakamwambia Mose:

2 “Simika Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.

3 Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake.

4 Kisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake.

5 Weka ile madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la Maskani ya Mungu.

6 “Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania;

7 weka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake.

8 Fanyiza ua kuzunguka maskani na uweke pazia penye ingilio la ua.

9 “Chukua mafuta ya upako, ipake Maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani mwake, nayo itakuwa takatifu.

10 Kisha ipake mafuta hiyo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo itakuwa takatifu sana.

11 Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.

12 “Mlete Aroni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji.

13 Kisha mvike Aroni yale mavazi matakatifu, umtie mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia katikati ya ukuhani.

14 Walete wanawe na uwavike makoti.

15 Kisha watie mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kutiwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.”

16 Mose akafanya kila kitu sawa kama vileBwanaalivyomwagiza.

17 Kwa hiyo Maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili.

18 Mose aliposimika Maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo.

19 Kisha akalitandaza hema juu ya Maskani ya Mungu na kuifunika hema, kamaBwanaalivyomwagiza.

20 Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake.

21 Kisha akalileta Sanduku ndani ya Maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kamaBwanaalivyomwagiza.

22 Mose akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini ya Maskani ya Mungu nje ya pazia

23 na kupanga mikate juu yake mbele zaBwana, kamaBwanaalivyomwagiza.

24 Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa Maskani ya Mungu

25 na kuziweka taa mbele zaBwana, kamaBwanaalivyomwagiza.

26 Mose akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia

27 na kufukiza uvumba wenye harufu nzuri, kamaBwanaalivyomwagiza.

28 Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la Maskani ya Mungu.

29 Akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la Maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kamaBwanaalivyomwagiza.

30 Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia,

31 Naye Mose, Aroni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao.

32 Wakanawa kila wakati walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu kamaBwanaalivyomwagiza Mose.

33 Kisha Mose akafanya ua kuizunguka Maskani ya Mungu na madhabahu, pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Mose akaikamilisha kazi.

Utukufu Wa Bwana

34 Ndipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu waBwanaukaijaza Maskani ya Mungu.

35 Mose hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu waBwanaukaijaza Maskani ya Mungu.

36 Katika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya Maskani ya Mungu, wangeondoka;

37 lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, mpaka siku lilipoinuka.

38 Kwa hiyo wingu laBwanalilikuwa juu ya maskani mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/40-c0d5b1796a5e3393606813bda0dd8e7c.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 1

Siku Sita Za Uumbaji Na Sabato

1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.

2 Wakati huu Dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu, giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji.

3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.

4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza.

5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.”

7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi na akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo.

8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.

9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo.

10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.

11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo.

12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema.

13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.

14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe mchana na usiku, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka,

15 nayo iwe ndiyo mianga kwenye nafasi ya anga itoe nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo.

16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota.

17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia,

18 itawale mchana na usiku, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.”

21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini, kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mkaongezeke mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.”

23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.

24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo.

25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wafugwao kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

27 Kwa hiyo Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

kwa mfano wa Mungu alimuumba;

mwanaume na mwanamke aliwaumba.

28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa kwa ajili ya chakula chenu,

30 cha wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi. Kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

31 Mungu akatazama vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/1-e2155c5471024fd2f1588b777b15588f.mp3?version_id=1627—