1 Wakorintho 10

Onyo Kutoka Historia Ya Waisraeli

1 Zaidi ya hayo ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari.

2 Wote wakabatizwa kuwa wa Mose ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari.

3 Wote walikula chakula kile cha roho,

4 na wote wakanywa kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka katika ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Kristo.

5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani.

6 Basi mambo haya yalitokea kama mfano ili kutuonya tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya.

7 Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu walikaa chini wakala na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya karamu za kipagani.”

8 Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu 23,000 kwa siku moja.

9 Wala tusimjaribu Bwana, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka.

10 Msinung’unike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na mharabu.

11 Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia.

12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke.

13 Hakuna jaribu lo lote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu ambaye hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

Karamu Za Sanamu Na Meza Ya Bwana

14 Kwa hiyo wapenzi wangu, zikimbieni ibada za sanamu.

15 Nasema nanyi kama na watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo.

16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

17 (Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja).

18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni?

19 Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yo yote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yo yote?

20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani.

21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?

Fanyeni Yote Kwa Utukufu Wa Mungu

23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga.

24 Mtu ye yote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

25 Kuleni cho chote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lo lote kwa ajili ya dhamiri.

26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri.

28 Lakini kama mtu ye yote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri.

29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?

30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

31 Basi, lo lote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

32 Msiwe kikwazo kwa mtu ye yote, kwa Wayahudi au kwa Wayunani, au kwa Kanisa la Mungu,

33 kama mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali mema kwa ajili ya faida ya wengi, ili waweze kuokolewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/10-bb7318c28718f7ef5a84c831700bca42.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 11

1 Niigeni mimi, kama nami ninavyomwiga Kristo.

Utaratibu Katika Kuabudu

2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.

3 Lakini napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu.

4 Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake.

5 Lakini kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele.

6 Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake.

7 Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume.

8 Kwa maana mwanaume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume.

9 Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume.

10 Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka iliyo juu yake.

11 Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke.

12 Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu.

13 Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake?

14 Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu?

15 Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake. Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika.

16 Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.

Matumizi Mabaya Ya Meza Ya Bwana

17 Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara.

18 Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo.

19 Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu.

20 Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula,

21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine, huyu hukaa njaa na mwingine analewa.

22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule alipotolewa, alitwaa mkate,

24 naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema “Huu ndio mwili wangu, ambao ni kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

25 Vivi hivi baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni Agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu.”

26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo.

Kushiriki Meza Ya Bwana Isivyostahili

27 Kwa hiyo, mtu ye yote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana.

28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe.

29 Kwa maana mtu ye yote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, anajiletea hukumu juu yake mwenyewe.

30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa.

31 Lakini kama tungejipambanua wenyewe tusingehukumiwa.

32 Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadabishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.

33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane.

34 Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani kwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa.

Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/11-e5e321c4cd2f16120d34a29a1424eeb3.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 12

Karama Za Rohoni

1 Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu.

2 Mnajua kwamba mlipokuwa hamumjui Mungu, mlishawishika na kupotoshwa na sanamu zisizonena.

3 Kwa hiyo nataka mfahamu ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu.

4 Basi kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule.

5 Pia kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule.

6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.

7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote.

8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.

9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya.

10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, kwa mwingine tafsiri za lugha.

11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo mwenyewe.

Mwili Mmoja, Wenye Viungo Vingi

12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo.

13 Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi.

15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili.

16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si la mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili.

17 Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi?

18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda.

19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?

20 Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.

21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!”

22 Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana.

23 Navyo vile viungo vya mwili tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee.

24 Wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa,

25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake.

26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

27 Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni kiungo.

28 Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za masaidiano, karama za maongozi, aina mbalimbali za lugha.

29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanafanya miujiza?

30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri?

31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu.

Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/12-b56b4a66b53963686ec5264cc7a9bbdf.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 13

Karama Ya Upendo

1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo.

2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu.

3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno. Upendo hauna kiburi.

5 Haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya.

6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli.

7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.

9 Kwa maana tunafahamu kwa sehemu na tunatoa unabii kwa sehemu.

10 Lakini ukamilifu utakapokuja, yale yasiyo kamili yatatoweka.

11 Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto.

12 Kwa maana sasa tunaona taswira kama ya kwenye kioo, lakini wakati huo tutaona wazi. Sasa nafahamu kwa sehemu, wakati huo nitafahamu kikamilifu, kama vile mimi ninavyofahamika kikamilifu.

13 Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/13-3abe1747968f2652e7e85c1ce78adfe6.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 14

Karama Za Unabii Na Lugha

1 Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii.

2 Kwa maana mtu ye yote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu ye yote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa Roho.

3 Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji.

4 Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa.

5 Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha mpya, lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa kama kuna mtu wa kutafsiri, ili kanisa zima lipate kujengwa.

6 Sasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho?

7 Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji?

8 Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita?

9 Vivyo hivyo na ninyi, kama mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu.

10 Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana.

11 Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu.

12 Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa.

13 Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena.

14 Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda.

15 Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, lakini nitaomba kwa akili yangu pia. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia.

16 Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema?

17 Mnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki.

18 Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote.

19 Lakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka kwa akili ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha.

20 Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima.

21 Katika sheria imeandikwa kwamba:

“Kwa kupitia watu wenye lugha ngeni

na kupitia midomo ya watu wageni,

nitasema na watu hawa,

lakini hata hivyo hawatanisikiliza,”

asema Bwana.

22 Basi kunena kwa lugha mpya ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa ajili ya wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio.

23 Kwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu?

24 Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote,

25 nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

Kumwabudu Mungu Kwa Utaratibu

26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, mmoja ana wimbo, mwingine neno la mafundisho, mwingine ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine ataongea lugha mpya na mwingine atatafsiri hiyo lugha. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kujenga kanisa.

27 Kama mtu ye yote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri.

28 Lakini kama hakuna mtu ye yote wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.

29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo.

30 Kama mtu ye yote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze.

31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo.

32 Roho za manabii huwatii manabii.

33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.

Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,

34 wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo.

35 Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lo lote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.

36 Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia?

37 Kama mtu ye yote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana.

38 Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa.

39 Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha.

40 Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/14-90e04b893109a421582a23d8a32f0898.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 15

Kufufuka Kwa Kristo

1 Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama.

2 Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.

3 Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemayo Maandiko,

4 ya kuwa alizikwa na alifufuka siku ya tatu,

5 na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili.

6 Baadaye akawatokea wale ndugu waamini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala.

7 Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote.

8 Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.

9 Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu.

10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.

11 Hivyo basi, kama ilikuwa ni mimi au ni wao hili ndilo tulihubirilo na hili ndilo mliaminilo.

Ufufuo Wa Wafu

12 Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuka kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu?

13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuka.

14 Tena ikiwa Kristo hakufufuka kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili.

15 Zaidi ya hayo basi, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi.

16 Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka.

17 Tena kama Kristo hajafufuka, imani yenu ni batili, nanyi bado mko katika dhambi zenu.

18 Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea.

19 Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wengine wote duniani.

20 Lakini kweli Kristo amefufuka kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala.

21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja.

22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai.

23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza la ufufuo, kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja.

24 Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba Ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu.

25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake.

26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti.

27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa.

28 Atakapokuwa amekwisha kutiisha vitu vyote chini ya Mwana, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.

29 Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao?

30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa?

31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku.

32 Kama kwa tumaini la kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani kwa jambo hilo? Kama wafu hawafufuliwi,

“Sisi na tule na kunywa,

kwa kuwa kesho tutakufa.”

33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”

34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.

Mwili Wa Ufufuo

35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”

36 Ninyi wapumbavu! Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa.

37 Mpandapo, hampandi mwili ule unaotegemewa kuwako, bali mwapanda mbegu tupu, pengine ya ngano au ya kitu kingine.

38 Lakini Mungu huipa hiyo mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake.

39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti.

40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini uzuri wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na uzuri wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine.

41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.

42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika,

43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu,

44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.

Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia.

45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima.

46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho.

47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni.

48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni.

49 Kama vile tulivyochukua mfano wa yule mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.

50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi Ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika.

51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa

52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa.

53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa.

54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”

55 “Kuko wapi, Ewe mauti, kushinda kwako?

Uko wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”

56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria.

57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu si bure katika Bwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/15-2683f6ada298e2070e042d7ffaea2e3c.mp3?version_id=1627—

1 Wakorintho 16

Changizo Kwa Ajili Ya Watakatifu

1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo.

2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.

3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke sadaka zenu huko Yerusalemu.

4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.

Mahitaji Binafsi

5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia.

6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari zangu, po pote niendapo.

7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu, natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda.

8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste,

9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi.

10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, mkaribisheni. Hakikisheni kwamba hana hofu yo yote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo.

11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia yeye pamoja na hao ndugu.

12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.

Maneno Ya Mwisho

13 Kesheni, simameni imara katika imani, iweni mashujaa na hodari.

14 Fanyeni kila kitu katika upendo.

15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi,

16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii.

17 Nilifurahi Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu hawa wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu.

18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.

Salamu Za Mwisho

19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu katika Bwana.

20 Pia ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.

21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.

22 Kama mtu ye yote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo!

23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.

24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/16-e2ab227aec3cf5c30146420196087cd7.mp3?version_id=1627—

Warumi 1

1 Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu,

2 Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika maandiko matakatifu,

3 yaani, Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi

4 na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani, Yesu Kristo Bwana wetu.

5 Kwa kupitia kwake na kwa ajili ya Jina lake, tumepokea neema na utume ili kuwaita watu miongoni mwa watu wote wasiomjua Mungu, waje kwenye utii utokanao na imani.

6 Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili mpate kuwa mali ya Kristo Yesu.

7 Kwa wote walioko Rumi wapendwao na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu: Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Maombi Na Shukrani

8 Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote.

9 Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka

10 katika maombi yangu siku zote, nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nipate kuja kwenu.

11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara,

12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.

13 Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa mpaka sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa wengine ambao ni watu Mataifa wasiomjua Mungu.

14 Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima.

15 Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.

16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia.

17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

Ghadhabu Ya Mungu Kwa Wanadamu

18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao,

19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameliweka wazi kwao.

20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, umeonekana waziwazi ukitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza.

22 Ingawa wakijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga

23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao.

25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa.

27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.

28 Nao kwa kuwa walikataa kumkubali Mungu, yeye akawaacha wafuate akili zao za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa.

29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji,

30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao,

31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili.

32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/1-ebcf1ec4d4a403ab8794ab17ae62f742.mp3?version_id=1627—

Warumi 2

Hukumu Ya Mungu

1 Kwa hiyo huna udhuru wo wote, wewe mtu uwaye yote, utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lo lote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo yayo hayo.

2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli.

3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?

4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?

5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa.

6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake.

7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele.

8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.

9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu Mataifa pia,

10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu Mataifa.

11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria.

13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki.

14 (Naam, wakati wa watu Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria.

15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea).

16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.

Wayahudi Na Torati

17 Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea Sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu,

18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria,

19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani,

20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria,

21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba?

22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu?

23 Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria?

24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu mataifa.”

25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.

26 Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa?

27 Ndipo wale ambao kimwili hawakutahiriwa lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi Wayahudi, ambao mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu lakini mwaivunja.

28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili.

29 Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani na tohara ya kweli ni jambo la rohoni, ni la kiroho, wala si la kimwili. Mtu wa namna hiyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/2-eb82c3f45578050da9c23d425b6a0629.mp3?version_id=1627—

Warumi 3

Uaminifu Wa Mungu

1 Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara?

2 Kuna faida kubwa kwa kila namna, kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa lile Neno halisi la Mungu.

3 Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu?

4 La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa:

“Ili uweze kujulikana kuwa na haki katika maneno yako,

nawe ukashinde katika hukumu.”

5 Ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.)

6 La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angehukumuje ulimwengu?

7 Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonyesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?”

8 Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja?” Wao wanastahili hukumu yao.

Wote Wametenda Dhambi

9 Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyo vyote kwamba Wayahudi na watu Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi.

10 Kama ilivyoandikwa:

“Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.

11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,

hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.

12 Wote wamegeukia mbali,

wote kwa pamoja hawafai;

hakuna atendaye mema,

naam, hata mmoja.”

13 “Makoo yao ni makaburi wazi;

kwa ndimi zao hufanya udanganyifu.”

“Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”

14 “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”

15 “Miguu yao ina haraka kumwaga damu;

16 maangamizi na taabu viko katika njia zao,

17 wala njia ya amani hawaijui.”

18 “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”

19 Basi tunajua ya kwamba cho chote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu.

20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.

Haki Kwa Njia Ya Imani

21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Torati na Manabii wanaishuhudia.

22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti,

23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu,

24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.

25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa.

26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

Umuhimu Wa Kuwa Na Imani

27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani.

28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria.

29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu Mataifa pia.

30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo.

31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/3-d80026ecca8b0cff718999723576c131.mp3?version_id=1627—