Warumi 4

Abrahamu Alihesabiwa Haki Kwa Imani

1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili, yeye alipataje kujua jambo hili?

2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu.

3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili.

5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.

6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:

7 “Wamebarikiwa wale

ambao uovu wao umesamehewa

ambao dhambi zao zimefutwa.

8 Amebarikiwa mtu yule

ambaye Mungu hamhesabii dhambi zake.”

Haki Kabla Ya Tohara

9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.”

10 Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa.

11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki.

12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.

Ahadi Ya Mungu Hufahamika Kwa Imani

13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani.

14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu,

15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.

16 Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote.

17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu ambaye alimwamini, Mungu awapaye ahadi waliokufa na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

Mfano Wa Imani Ya Abrahamu

18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akakuwa Baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.”

19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara.

20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu,

21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.

22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”

23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake,

24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu.

25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuka kwa ajili yetu ili tuhesabiwe haki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/4-3ed1e86423ead7fea52c03896b553b61.mp3?version_id=1627—

Warumi 5

Matokeo Ya Kuhesabiwa Haki

1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu.

3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi,

4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo na uthabiti wa moyo huleta tumaini,

5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi.

7 Hakika, ni vigumu mtu ye yote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.

8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu kwa yeye!

10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.

11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa kupitia kwake tumepata upatanisho.

Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima

12 Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja na kupitia dhambi hii, mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi.

13 Kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria.

14 Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Mose, mauti ilitawala watu wote hata wale ambao hawakuvunja amri kama alivyofanya Adamu, ambaye alikuwa mfano wa yule atakayekuja.

15 Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, zaidi sana neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi.

16 Tena, ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.

17 Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo.

18 Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja kulileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote.

19 Kwa maana kama vile kwa kutokutii yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.

20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.

21 Ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/5-97d2d0de5438043d491142f8c5e7bc1a.mp3?version_id=1627—

Warumi 6

Kufa Na Kufufuka Pamoja Na Kristo

1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka?

2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi?

3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?

4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuka kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.

5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake.

6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulibiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi.

7 Kwa maana mtu ye yote aliyekufa amewekwa huru mbali na dhambi.

8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye.

9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, akiisha kufufuka kutoka kwa wafu, hatakufa tena, mauti haina tena mamlaka juu yake.

10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.

12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya.

13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki.

14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

Watumwa Wa Haki

15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha!

16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu ye yote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki?

17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa,

18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile kwanza mlivyokuwa mmevitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi na zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vya miili yenu vitumike kwa ajili ya haki ambayo matokeo yake ni utakatifu.

20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki.

21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti.

22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele.

23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/6-4635f90dc2f0337b75456d07f3e0de47.mp3?version_id=1627—

Warumi 7

Hatufungwi Tena Na Sheria

1 Ndugu zangu (sasa ninasema na wale wanaoijua sheria.) Je, hamjui ya kwamba sheria ina mamlaka tu juu ya mtu wakati akiwa hai?

2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka katika sheria ya ndoa.

3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.

4 Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kwa njia ya mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuka kutoka kwa wafu, ili kwamba tupate kuzaa matunda kwa Mungu.

5 Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti.

6 Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutoka katika sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa.

Sheria Na Dhambi

7 Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini, isingekuwa kwa sababu ya sheria, nisingalijua dhambi. Nisingalijua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.”

8 Lakini dhambi kwa kupata nafasi katika amri, hii ikazaa ndani yangu kila aina ya tamaa. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa.

9 Wakati fulani nilikuwa hai pasipo sheria, lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa.

10 Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti.

11 Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya na kwa kupitia hiyo amri, ikaniua.

12 Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.

13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kwa njia ya amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.

Mgongano Wa Ndani

14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi.

15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia.

16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema.

17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lo lote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda.

19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo.

20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo.

22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu.

23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.

24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/7-1de006b7f97b2238b83b57aa9020bc69.mp3?version_id=1627—

Warumi 8

Maisha Katika Roho

1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.

3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili,

4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho.

6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani.

7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.

8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu ye yote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo.

10 Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki.

11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

12 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili,

13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio watoto wa Mungu.

15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,”

16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu.

17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

Utukufu Ujao

18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu.

19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu.

20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini,

21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa uchungu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.

23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.

24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alichonacho tayari?

25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.

26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu kusikoweza kutamkwa.

27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

Tunashinda Na Zaidi Ya Kushinda

28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

Upendo Wa Mungu

31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?

32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?

33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewachagua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki.

34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, ndiye aliyefufuka kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye ndiye anayetuombea.

35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga?

36 Kama ilivyoandikwa:

“Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,

tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.

38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo,

39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/8-cc619d9fb5c32fc48007bb9fed0d1b4a.mp3?version_id=1627—

Warumi 9

Kuteuliwa Kwa Israeli Na Mungu

1 Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu.

2 Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu.

3 Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili,

4 yaani, watu wa Israeli, ambao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea sheria, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi.

5 Wao ni wa uzao wa mababa wakuu wa kwanza, ambao kutoka kwao Kristo alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen.

6 Si kwamba Neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi.

7 Wala si tu kwamba kwa sababu wamezaliwa na wazao wa Abrahamu ni watoto wake, lakini ahadi ya Mungu kwa Abrahamu ilikuwa: “Watoto wako watahesabiwa katika uzao wa Isaki.”

8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu.

9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”

10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki.

11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lo lote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama,

12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Mkubwa atamtumikia mdogo.”

13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini Esau nimemchukia.”

Mungu Hana Upendeleo

14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha!

15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

“Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

nami nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu.

17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili, ili kwamba nipate kuonyesha uweza wangu juu yako na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani pote.”

18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.

19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?”

20 Lakini, Ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ”

21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka katika bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu?

23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake,

24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu Mataifa?

Yote Yalitabiriwa Katika Maandiko

25 Kama vile Mungu asemavyo katika Hosea:

“Nitawaita ‘watu wangu’

wale ambao si watu wangu;

nami nitamwita ‘mpenzi wangu’

yeye ambaye si mpenzi wangu,”

26 tena,

“Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa,

‘Ninyi si watu wangu,’

wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ”

27 Isaya anapiga kelele kuhusu Israeli:

“Ingawa idadi ya wana wa Israeli ni wengi kama mchanga

ulioko pwani ya bahari,

ni mabaki yao tu watakaookolewa.

28 Kwa kuwa Bwana ataitekeleza

hukumu yake duniani kwa haraka

na kwa ukamilifu.”

29 Ni kama vile alivyotabiri Isaya akisema:

# “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote

asingetuachia uzao,

tungalikuwa kama Sodoma,

tungalikuwa kama Gomora.”

Kutokuamini Kwa Israeli

30 Kwa hiyo tuseme nini basi? Kwamba watu Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kwa njia ya imani.

31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kwa njia ya sheria, hawakuipata.

32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kwa njia ya imani bali kwa njia ya matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza.”

33 Kama ilivyoandikwa:

“Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza

na mwamba wa kuwaangusha,

ye yote atakayemwamini

hataaibika kamwe.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/9-2ac804dd6f26958769ce19bdf4b29bcb.mp3?version_id=1627—

Warumi 10

1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.

2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wanajuhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.

3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

Wokovu Ni Kwa Ajili Ya Wote

5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye mambo hayo ataishi kwa hayo.”

6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini)

7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.)

8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno li karibu nawe, li kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, ni lile neno la imani tunalolihubiri.

9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

11 Kama yasemavyo Maandiko, “Ye yote amwaminiye hatatahayarika.”

12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.

13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokoka.”

14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?

15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyaoandikwa, “Ni mizuri mno miguu ya hao wanaohubiri Injili ya amani na kuleta habari ya mema!”

16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”

17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo.

18 Lakini nauliza, Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:

“Sauti yao imeenea duniani kote,

nayo maneno yao yamefika

hadi miisho ya ulimwengu.”

19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema,

“Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale

ambao si taifa.

Nitawakasirisha kwa taifa la watu

wasio na ufahamu.”

20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,

“Watu wale waliokuwa hawanitafuti, wamenipata;

nimejidhihirisha kwa watu

wale waliokuwa hawaniulizii.”

21 Lakini kuhusu Israeli anasema,

“Mchana kutwa nimewanyoshea

watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/10-0864d8898873b398cc4cf456076702ae.mp3?version_id=1627—

Warumi 11

Mabaki Ya Israeli

1 Basi nauliza, je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini.

2 Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli?

3 Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?”

4 Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.”

5 Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu.

6 Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.

7 Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu,

8 kama ilivyoandikwa:

“Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo,

macho ili wasiweze kuona

na masikio ili wasiweze kusikia,

hadi leo.”

9 Naye Daudi anasema:

“Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa,

kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.

10 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,

nayo migongo yao iinamishwe daima.”

Matawi Yaliyopandikizwa

11 Hivyo nauliza tena, je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu.

12 Basi ikiwa kujikwaa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi.

13 Sasa ninasema nanyi watu Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu Mataifa, naitukuza huduma yangu

14 ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao.

15 Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa?

16 Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo.

17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka katika shina la mzeituni,

18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Kama ukijivuna, kumbuka jambo hili. Si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe.

19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.”

20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa.

21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.

22 Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali.

23 Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina.

24 Ikiwa wewe ulikatwa kutoka katika kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni!

Israeli Wote Wataokolewa

25 Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu Mataifa watakaoingia itimie.

26 Hivyo Israeli wote wataokolewa kama ilivyoandikwa:

“Mkombozi atakuja kutoka Sayuni;

ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.

27 Hili ndilo Agano langu nao

nitakapoziondoa dhambi zao.”

28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani,

29 kwa maana akishawapa watu karama haziondoi, wala wito wake.

30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao,

31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu.

32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

Wimbo Wa Shukrani

33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

wa hekima na maarifa ya Mungu!

Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

34 “Ni nani aliyeijua nia ya Bwana?

Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

35 “Au ni nani aliyempa cho chote

ili arudishiwe?”

36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

Utukufu ni wake milele! Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/11-b1d98791aabb237f65b14fb331a3ce53.mp3?version_id=1627—

Warumi 12

Maisha Mapya Katika Kristo

1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.

2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni Pake na ukamilifu.

3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja,

5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.

6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani.

7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe,

8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

Alama Za Mkristo Wa Kweli

9 Upendo lazima usiwe wa unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.

10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.

11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana.

12 Iweni na furaha katika tumaini, katika dhiki iweni na saburi, dumuni katika maombi.

13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani.

15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.

16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

17 Msimlipe mtu ye yote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote.

18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote.

19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa, asema Bwana.”

20 Badala yake:

“Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula;

akiwa na kiu, mnyweshe.

Maana ukifanya hivyo, utampalia

makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/12-9debfb689fdc0715f082d1c879de661f.mp3?version_id=1627—

Warumi 13

Kutii Mamlaka

1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu.

2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.

3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu.

4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya.

5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.

6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala.

7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.

Kupendana Kila Mmoja Na Mwingine

8 Msidaiwe kitu na mtu ye yote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza Sheria.

9 Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa Sheria.

11 Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia zaidi kuliko hapo kwanza tulipoamini.

12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru.

13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/13-a99c95b3f20bfd209712046088710c0b.mp3?version_id=1627—