Warumi 14

Msiwahukumu Wengine

1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake.

2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu.

3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali.

4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.

5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.

6 Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Bwana. Naye alaye nyama hula kwa Bwana, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Bwana na humshukuru Mungu.

7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe.

8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana.

9 Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani, waliokufa na walio hai.

10 Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu.

11 Kwa kuwa imeandikwa:

“ ‘Kama niishivyo,’ asema Bwana,

‘kila goti litapigwa mbele zangu,

na kila ulimi utamkiri Mungu.’ ”

12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

Usimfanye Ndugu Yako Ajikwae

13 Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana: Badala yake mtu asiweke kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya mwingine.

14 Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu cho chote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi.

15 Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.

16 Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu.

17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

18 Kwa sababu mtu ye yote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.

20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu cho chote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae.

21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lo lote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.

22 Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya.

23 Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, asile hicho kitu, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa cho chote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/14-9f0688f7d0e4128d08a0ad65b0b5a4f4.mp3?version_id=1627—

Warumi 15

Usijipendeze Mwenyewe, Bali Wapendeze Wengine

1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.

2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani.

3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”

4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu,

6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Injili Sawa Kwa Wayahudi Na Kwa Watu Mataifa

7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.

8 Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani,

9 pia ili watu Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa:

“Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu Mataifa;

nitaliimbia sifa jina lako.”

10 Tena yasema,

“Enyi watu Mataifa, furahini

pamoja na watu wa Mungu.”

11 Tena,

“Mhimidini Bwana, ninyi watu wote Mataifa,

na kumwimbia sifa, enyi mataifa yote.”

12 Tena Isaya anasema,

“Shina la Yese litachipuka,

yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa,

watu Mataifa watamtumaini.”

13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Paulo Mhudumu Wa Watu Mataifa

14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, ufahamu wote, tena mnaweza kufudishana ninyi kwa ninyi.

15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa,

16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu.

18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu cho chote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya,

19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.

20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.

21 Lakini kama ilivyoandikwa:

“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,

nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”

22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.

Paulo Apanga Kwenda Rumi

23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi.

24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo.

25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko.

26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu.

27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.

28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania.

29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.

30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu.

31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu,

32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi.

33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/15-6d1ac9c8fb537f5de196c0e8410e19ea.mp3?version_id=1627—

Warumi 16

Salamu Kwa Watu Binafsi

1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea.

2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wo wote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.

3 Wasalimuni Prisilana Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu.

4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu Mataifa.

5 Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao.

Msalimuni rafiki yangu Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.

6 Msalimuni Maria, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.

7 Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walimjua Kristo kabla yangu.

8 Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana.

9 Msalimuni Urbano, mtenda kazi mwenzetu katika Kristo, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.

10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Kristo.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.

11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkisi walio katika Bwana.

12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana.

13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.

14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.

15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.

16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.

Maelekezo Ya Mwisho

17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza.

18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.

20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

Neema ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi. Amen.

21 Timotheo, mtenda kazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.

22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana.

23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kanisa lote, anawasalimu.

Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu pia wanawasalimu.

24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amen.

Maneno Ya Mwisho Ya Kumsifu Mungu

25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya ninyi imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale.

26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii

27 Mungu aliye pekee, mwenye hekima, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo utukufu una yeye milele na milele! Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/16-1c31ad45264650f46d6ec3d62bf50cff.mp3?version_id=1627—

Matendo 1

Ahadi Ya Roho Mtakatifu

1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo,

2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maelekezo kwa njia Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.

3 Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu.

4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke humu Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake.

5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku hizi chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Kupaa Kwa Yesu Kwenda Mbinguni

6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamwuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”

7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.

8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao,

11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”

Mathiya Achaguliwa Badala Ya Yuda

12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabatokutoka mjini.

13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelotena Yuda mwana wa Yakobo.

14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwapo wanawake kadha wa kadha na Maria mama yake Yesu pamoja na ndugu zake Yesu.

15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema,

16 “Ndugu zangu, ilibidi maandiko yatimie yale ambayo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu.

17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”

18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje.

19 Kila mtu huko Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).

20 “Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi,

“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa

wala asiwepo mtu atakayekaa humo,’

na,

“ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake.’

21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu,

22 kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”

23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya.

24 Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua

25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.”

26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/1-8e9dd28394e8feb14284adf386bc0772.mp3?version_id=1627—

Matendo 2

Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

1 Ilipowadia siku ya Pentekoste, walikuwa wote mahali pamoja.

2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi.

3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

5 Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu.

6 Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7 Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya?

8 Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa?

9 Warparthi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia,

10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi,

11 Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.”

12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”

13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa mvinyo!”

Petro Ahutubia Umati

14 Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na moja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize.

15 Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!

16 Hawa hawakulewa, ila jambo hili ni lile lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Bwana,

nitamimina Roho wangu

juu ya wote wenye mwili.

Wana wenu na binti zetu watatabiri,

vijana wenu wataona maono

na wazee wenu wataota ndoto.

18 Hata juu ya watumishi wangu

nitamwaga Roho wangu,

nao watatabiri.

19 Nami nitaonyesha maajabu mbinguni juu

na ishara duniani chini, damu,

moto na mvuke wa moshi mnene.

20 Jua litakuwa giza

na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,

kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana

iliyo tukufu.

21 Lakini ye yote atakayeliita

jina la Bwana, ataokolewa.’

22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kwa kupitia yeye, kama ninyi wenyewe mjuavyo.

23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimwua kwa kumgongomea msalabani.

24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

25 Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye:

“ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia

na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao utaishi kwa tumaini.

27 Kwa maana hutaniacha kaburini,

wala hutamwacha

aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.

28 Umenionyesha njia za uzima,

utanijaza na furaha mbele zako.’

29 “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo.

30 Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi.

31 Daudi akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.

32 Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo.

33 Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.

34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

“ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:

“Keti upande wangu wa kuume,

35 hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako.” ’

36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulibisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Ongezeko La Waamini

37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu na kwa wale wote walio mbali na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.”

41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Ushirika Wa Waamini

42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.

43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.

44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika.

45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, wakamgawia kila mtu kwa kadiri alivyokuwa anahitaji.

46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,

47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa kwa wale watu waliokuwa wakiokolewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/2-2b6fb0358cf2443c674797b766e0a22c.mp3?version_id=1627—

Matendo 3

Petro Amponya Mlemavu Kwa Jina La Yesu

1 Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri.

2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni.

3 Huyu mtu akiwaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, aliwaomba wampe sadaka.

4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.”

5 Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu wa Nazareti simama, uende.”

7 Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu.

8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu.

9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu,

10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.

Petro Anashuhudia Kuwa Yesu Anaponya

11 Yule mtu kiwete aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wanawakimbilia mpaka kwenye ukumbi wa Solomoni.

12 Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi waume wa Israeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumefanya mtu huyu kutembea?

13 Mungu wa Abrahamu na Isaki na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake.

14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule mwuaji.

15 Hivyo mkamwua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.

16 Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani ile itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.

17 “Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu.

18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristoatateswa.

19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, ili dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana.

20 Kwamba apate kumtuma Kristo, ambaye amewekwa kwa ajili yenu, yaani Yesu,

21 ambaye ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyosema kwa vinywa vya manabii wake wote watakatifu kabla ya mwanzo wa ulimwengu.

22 Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu, itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia.

23 Mtu ye yote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atakatiliwa mbali kabisa na watu wake.’

24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na wale waliofuata baada yake, wote walionena walitabiri kuhusu siku hizi.

25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Katika wewe, jamaa zote za duniani watabarikiwa.’

26 Mungu alipomfufua Yesu Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka katika njia yake mbaya.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/3-0f84bfa9e771c51cdc8bf1d043ce71fb.mp3?version_id=1627—

Matendo 4

Petro Na Yohana Mbele Ya Baraza

1 Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masudakayo wakawajia wakiwa

2 wamekasirika sana kwa sababu hao mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba katika Yesu kuna ufufuo wa wafu.

3 Wakawakamata Petro na Yohana na kuwatia gerezani mpaka kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni.

4 Lakini wengi wale waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume 5,000.

5 Siku ya pili yake viongozi wa Kiyahudi, wazee na waandishi wa sheria wakakusanyika Yerusalemu,

6 walikuwepo Kuhani Mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda na wengi wa jamaa ya Kuhani Mkuu.

7 Wakiisha kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”

8 Petro akiwa amejaa Roho Mtakatifu akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu,

9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa,

10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa uwezo wa Yesu, kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa.

11 Huyu Yesu ndiye

“ ‘lile jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,

ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’

12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna Jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Ujasiri Wa Petro Na Yohana Washangaza Watu

13 Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu.

14 Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lo lote kuwapinga.

15 Wakawaamuru watoke nje ya barazawakati wakisemezana jambo hilo wao kwa wao.

16 Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha mwujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu.

17 Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi miongoni mwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu ye yote kwa jina la Yesu.”

18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.

Imetupasa Kumtii Mungu Kuliko Wanadamu

19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko Mungu.

20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

21 Baada ya vitisho vingi, wakawaacha waende zao. Hawakuona njia yo yote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia.

22 Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa mwujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.

Maombi Ya Waamini

23 Mara Petro na Yohana walipoachiwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.

24 Watu hao waliposikia hayo, wakainua sauti zao wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mwenyezi, uliyeumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo.

25 Wewe ulisema kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:

“ ‘Mbona watu Mataifa wanaghadhibika,

na kabila za watu zinawaza ubatili?

26 Wafalme wa dunia wamejipanga

na watawala wanakusanyika pamoja

dhidi ya Bwana

# na dhidi ya Mpakwa Mafutawake.’

27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta.

28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani.

29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu.

30 Nyosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

31 Walipokwisha kuomba, mahali pale walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Walioamini Washirikiana Mali Zao

32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema cho chote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho.

33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote.

34 Wala hapakuwepo mtu ye yote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa,

35 wakaiweka miguuni pa wale mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja),

37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/4-01d250ef26d7dbdb206cc05e0e5fa862.mp3?version_id=1627—

Matendo 5

Anania Na Safira

1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja.

2 Mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.

3 Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja?

4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia.

6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.

7 Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia.

8 Petro akamwuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”

9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho Mtakatifu wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”

10 Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa, wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe.

11 Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.

Mitume Waponya Wengi

12 Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Nao wale wote walioamini walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni kwa nia moja.

13 Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu.

14 Lakini wengi walioamini idadi kubwa ya wanaume na wanawake wakaongezeka kwa Bwana.

15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao.

16 Pia watu wakakusanyika kutoka katika miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu, hao wote wakaponywa.

Mitume Washtakiwa

17 Kisha Kuhani Mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye (ambao ni wa kundi la Masadukayo), wakiwa wamejawa na wivu,

18 wakawakamata mitume na kuwatia gerezani.

19 Lakini wakati wa usiku malaika wa Bwana akaja akafungua milango ya gereza akawatoa nje akawaambia,

20 “Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”

21 Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.

Kuhani Mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani.

22 Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta wale mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari.

23 Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na maaskari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu ye yote ndani.”

24 Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu, viongozi na makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.

25 Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu wale mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.”

26 Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na maaskari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.

27 Wakiisha kuwaleta hao mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza. Kuhani Mkuu akawahoji.

28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.

30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimwua kwa kumtundika kwenye msalaba.

31 Mungu alimtukuza akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi.

32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”

33 Wale wajumbe wa baraza la wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua wale mitume.

34 Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru wale mitume watolewe nje kwa muda.

35 Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu yale mnayotaka kuwatendea watu hawa.

36 Kwa maana wakati uliopita aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda ambaye alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa na wafuasi wake wote wakatawanyika na kupotea.

37 Baada yake alitokea Yuda Mgalilaya wakati ule wa kuandikwa orodha ya watu akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye naye aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika.

38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu haitafanikiwa.

39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamtaweza kuwazuia watu hawa, badala yake mtajikuta mnapigana dhidi ya Mungu.”

40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, nao wakawaachia waende zao.

41 Wale mitume walitoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu.

42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/5-a3b11d975c0ba3630ee044039f3b29fe.mp3?version_id=1627—

Matendo 6

Saba Wachaguliwa Kuhudumia

1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku.

2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani.

3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii,

4 wakati sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.”

5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao mwongofu wa kutoka Antiokia.

6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.

7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

Kukamatwa Kwa Stefano

8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu.

9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano.

10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.

11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Mose na dhidi ya Mungu.”

Stefano Afikishwa Mbele Ya Baraza

12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Torati, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza.

13 Wakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Torati.

14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba huyu Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Mose.”

15 Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang’aa kama uso wa malaika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/6-41b2f4a922ddd41f6e02c2eb2b0dfef3.mp3?version_id=1627—

Matendo 7

Hotuba ya Stefano

1 Ndipo Kuhani Mkuu akamwuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”

2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani,

3 akamwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na kutoka kwa jamii yako uende katika nchi nitakayokuonyesha.’

4 “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa.

5 Mungu hakumpa urithi wo wote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto.

6 Mungu akasema naye hivi, ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kutendewa vibaya miaka 400.’

7 Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa na baadaye watatoka katika nchi hiyo na kuniabudu mahali hapa.’

8 Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu wakuu kumi na wawili.

9 “Kwa sababu wazee wetu wakuu walimwonea wivu Yosefu ndugu yao, walimwuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye.

10 Akamwokoa kutoka katika mateso yote yaliyompata, tena akampa kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimweka kuwa mtawala juu ya Misri na juu ya jumba lote la kifalme.

11 “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula.

12 Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza.

13 Walipokwenda mara ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, nao ndugu zake Yosefu wakajulishwa kwa Farao.

14 Ndipo Yosefu akatuma wamlete Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote, jumla yao walikuwa watu sabini na watano.

15 Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia.

16 Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.

17 “Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Abrahamu, watu wetu walizidi na kuongezeka sana.

18 Ndipo mfalme mwingine ambaye hakujua lo lote kuhusu Yosefu, akatawala Misri.

19 Huyu mfalme akawatendea watu wetu kwa hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.

20 “Wakati huo Mose alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani kwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu.

21 Waliposhindwa kumficha zaidi, wakamweka nje mtoni na binti Farao akamchukua akamtunza kama mtoto wake mwenyewe.

22 Mose akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.

23 “Mose alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli.

24 Aliona mmoja wao akionewa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamwua kulipiza kisasi.

25 Mose alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa.

26 Siku iliyofuata Mose aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kuumizana?’

27 “Lakini yule mtu aliyekuwa akimwonea mwenzake akamsukuma Mose kando, akamwuliza, ‘Ni nani alikuweka uwe mtawala na mwamuzi juu yetu?

28 Je, unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’

29 Mose aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.

30 “Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto.

31 Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Bwana, ikisema:

32 ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo.’ Mose alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.

33 “Ndipo Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana hapo unaposimama ni mahali patakatifu.

34 Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’

35 “Huyu ndiye Mose yule waliyemkataa wakisema, ‘Ni nani aliyekufanya uwe mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka.

36 Aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamuna katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.

37 “Huyu ndiye yule Mose aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kutoka miongoni mwa ndugu zenu.’

38 Huyu ndiye yule Mose aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.

39 “Lakini baba zetu walikataa kumtii Mose, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena.

40 Wakamwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu watakaotuongoza, kwa maana mtu huyu Mose aliyetutoa Misri hatujui yaliyompata.’

41 Huu ndio wakati walipotengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe.

42 Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii:

“ ‘Je, mlinitolea Mimi dhabihu na sadaka

kwa kipindi cha miaka arobaini kule jangwani, enyi nyumba ya Israeli?

43 La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki

na ya mungu wenu Refani,

vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu.

Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.

44 “Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani. Lilikuwa limetengenezwa kama Mungu alivyokuwa amemwelekeza Mose, kulingana na kielelezo alichoona.

45 Baba zetu wakiisha kulipokea hema kwa kupokezana wakiongozwa na Yoshua katika milki ya nchi kutoka kwa yale mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao, nalo likadumu katika nchi mpaka wakati wa Daudi,

46 ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.

47 Lakini alikuwa Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.

48 “Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:

49 “ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi,

na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.

Mtanijengea nyumba ya namna gani?

asema Bwana.

Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

50 Je, mikono yangu haikuumba vitu hivi vyote?’

51 “Ninyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zetu.

52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zetu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji.

53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”

Stefano Apigwa Mawe

54 Waliposikia haya wakaghadhabika, wakamsagia Stefano meno.

55 Lakini yeye Stefano akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, naye Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”

57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja.

58 Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.

59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu”

60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/7-7a36112779864a61cb0c06fdae778546.mp3?version_id=1627—