Matendo 8

1 Naye Sauli alikuwepo pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano.

Kanisa Lateswa Na Kutawanyika

Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Uyahudi na Samaria.

2 Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwombolezea sana.

3 Lakini kwa habari ya Sauli alikuwa analiharibu kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanawake na wanaume na kuwatia gerezani.

Filipo Ahubiri Injili Samaria

4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda.

5 Filipo akatelemkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo.

6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema.

7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa.

8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

Simoni, Mchawi

9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu,

10 watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ”

11 Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake.

12 Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa wanaume na wanawake.

13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

14 Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko.

15 Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu,

16 kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu.

17 Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu.

18 Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akawapa fedha

19 akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.”

20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!

21 Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.

22 Kwa hiyo tubia huu uovu wako na umwombe Mungu, ili yamkini, aweze kusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako.

23 Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”

24 Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lo lote lisinitukie.”

25 Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri injili katika vijiji vingi vya Samaria.

Filipo Na Towashi Wa Kushi

26 Basi Malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.”

27 Hivyo akaondoka na kwenda. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu,

28 naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya.

29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”

30 Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?”

31 Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.

32 Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la maandiko:

“Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni,

kama mwana-kondoo anyamazavyo

mbele yake yeye amkataye manyoya,

hivyo hakukifungua kinywa chake.

33 Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake.

Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake?

Kwa maana maisha yake yameondolewa

kutoka duniani.”

34 Yule towashi akamwuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena kwa habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?”

35 Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la maandiko akamweleza habari njema za Yesu.

36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamwambia Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” (

37 Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu).”

38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakatelemka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza.

39 Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi.

40 Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/8-ddd1887ef7f7e0da01d9e0e8212f9867.mp3?version_id=1627—

Matendo 9

Kuongoka Kwa Sauli

1 Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,

2 naye akamwomba Kuhani Mkuu ampe barua ya kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu ye yote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu.

3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote.

4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.”

6 “Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

7 Watu wale waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza.

8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu cho chote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski.

9 Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa cho chote.

10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba,

12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

13 Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu.

14 Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”

15 Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli.

16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”

17 Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.”

18 Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

19 Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.

Sauli Ahubiri Dameski

20 Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu”

21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wamefungwa mbele ya viongozi wa makuhani?”

22 Sauli akazidi kuwa uhodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo.

23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakafanya shauri kumwua Sauli.

24 Lakini shauri lao likajulikana kwa Sauli. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, mchana na usiku ili wapate kumwua.

25 Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.

Sauli Huko Yerusalemu

26 Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi.

27 Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski.

28 Kwa hiyo Sauli akakaa nao akishirikiana nao na akihubiri waziwazi kwa jina la Yesu kila mahali huko Yerusalemu.

29 Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumwua.

30 Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.

31 Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka.

Kuponywa Kwa Ainea

32 Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida.

33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani.

34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka.

35 Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

Petro Amfufua Dorkasi

36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.

37 Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani.

38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”

39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.

40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi.

41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai.

42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.

43 Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/9-f0376cd5f626fa04c4abfbcb2a6ca5fc.mp3?version_id=1627—

Matendo 10

Kornelio Amwita Petro

1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia.

2 Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima.

3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”

4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”

Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro.

6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”

7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia.

8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.

Maono Ya Petro

9 Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ghorofani kuomba.

10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walipokuwa wakiandaa akalala usingizi mzito sana.

11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa kwa ncha zake nne.

12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao na ndege wa angani.

13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

14 Petro akajibu, “La Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu cho chote kilicho najisi.”

15 Ile sauti ikasema naye tena mara ya pili, “Usikiite najisi kitu cho chote alichokitakasa Bwana.”

16 Jambo hili likatukia mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

17 Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango.

18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

19 Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta.

20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”

21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na kamanda Kornelio ambaye ni mtu mwema anayemcha Mungu na kusifiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika wa Mungu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.”

23 Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, akifuatana na baadhi ya ndugu kutoka Yafa.

Petro Nyumbani Mwa Kornelio

24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu.

25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima.

26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”

27 Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika.

28 Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu ye yote kuwa najisi au asiye safi.

29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lo lote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”

30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu mwenye nguo za kumetameta akasimama mbele yangu,

31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako zimekumbukwa mbele za Mungu.

32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’

33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

Hotuba Ya Petro

34 Ndipo Petro akafumbua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo,

35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.

36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote.

37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji:

38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za Shetani, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamwua kwa kumtundika msalabani.

40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu.

41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyetiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.

43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

Watu Mataifa Wapokea Roho Mtakatifu

44 Wakati Petro akiwa anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe.

45 Wale wa tohara walioamini waliokuwa wamekuja pamoja na Petro walishangaa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu Mataifa.

46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

Ndipo Petro akasema,

47 “Je, kuna mtu ye yote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.”

48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/10-c8896942f2c2eda43f616429c090084c.mp3?version_id=1627—

Matendo 11

Petro Aeleza Alivyotumwa Kwa Watu Mataifa

1 Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu Mataifa nao wamepokea neno la Mungu.

2 Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu,

3 wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”

4 Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema,

5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia.

6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani.

7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia ‘Petro, ondoka uchinje ule.’

8 “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu cho chote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu cho chote Mungu alichokitakasa.’

10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa.

12 Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio.

13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro.

14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo.

16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’

17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

Kanisa Huko Antiokia

19 Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu ye yote isipokuwa Wayahudi.

20 Lakini baadhi yao walikuwapo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakimhubiri Bwana Yesu.

21 Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.

22 Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia.

23 Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote.

24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana.

25 Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli,

26 naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.

27 Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia.

28 Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio.

29 Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo wake alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi.

30 Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/11-87727ee766d3dfd4f4440eb53c560032.mp3?version_id=1627—

Matendo 12

Yakobo Auawa, Petro Atiwa Gerezani

1 Ilikuwa wakati kama huu Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya watu wa kanisa.

2 Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga.

3 Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata pia Petro. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu.

4 Baada ya kumkamata alimtia gerezani, chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka.

5 Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii.

6 Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza.

7 Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

8 Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.”

9 Petro alitoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono.

10 Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.

11 Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yo yote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka katika makucha ya Herode Agripa na kutoka katika matazamio yote ya Wayahudi.”

12 Mara Petro alipotambua hili alikwenda nyumbani kwa Maria, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi.

13 Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mtumishi wa kike jina lake Roda, akaja kumfungulia.

14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua na kuwaeleza kwamba, “Petro yuko langoni!”

15 Wakamwambia yule mtumishi wa kike, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.”

16 Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana.

17 Yeye akawaashiria kwa mkono wake wanyamaze kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Naye akaongeza kusema, “Waelezeni Yakobo na ndugu wengine habari hizi.” Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine.

18 Kulipokucha kukawa na fadhaa kubwa miongoni mwa wale maaskari kuhusu yaliyomtukia Petro.

19 Baada ya Herode kuamuru atafutwe kila mahali na bila kumpata, aliwahoji wale askari walinzi kisha akatoa amri wauawe. Basi Herode Agripa akatoka Uyahudi akaenda Kaisaria, akakaa huko kwa muda.

Kifo Cha Herode Agripa

20 Basi Herode Agripa alikuwa amekasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Hivyo watu wa miji hiyo miwili wakaungana pamoja wakatafuta kukutana naye. Wakiisha kuungwa mkono na Blasto, mtumishi maalum wa Mfalme Herode Agripa aliyeaminika, wakaomba mapatano ya amani maana nchi zao zilitegemea nchi ya huyo mfalme kwa mahitaji yao ya chakula.

21 Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu.

22 Watu waliokuwa wamekusanyika wakapiga kelele, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.”

23 Ghafula, kwa kuwa Herode Agripa hakumpa Mungu utukufu, malaika akampiga, akaliwa na chango akafa.

24 Lakini neno la Mungu likaendelea mbele na kuenea, nao wengi wakaambatana nalo.

25 Barnaba na Sauli walipomaliza ile huduma yao iliyowapeleka, wakarudi Yerusalemu wakiwa pamoja na Yohana aitwaye Marko.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/12-5762c9302133399f9cb12c8a53be000f.mp3?version_id=1627—

Matendo 13

SAFARI YA KWANZA YA PAULO YA KITUME (13:1–14:28)

Barnaba Na Sauli Wanatumwa

1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Luko Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa na Sauli.

2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.”

3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao.

Barnaba Na Sauli Waenda Kipro

4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro.

5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.

6 Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar Yesu.

7 Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa, Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu.

8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani.

9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho yule Elima mchawi,

10 kamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka?

11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”

Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huko na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia.

12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

Paulo Na Barnaba Huko Antiokia Ya Pisidia

13 Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perge huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko akarejea Yerusalemu.

14 Kutoka Perge wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi wakaketi.

15 Baada ya kusomwa Torati na vitabu vya manabii, viongozi wa lile sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwasaidia watu hawa, tafadhali lisemeni.”

16 Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu.

17 Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile.

18 Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani.

19 Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao.

20 Haya yote yalichukua kama muda wa miaka 450.

“Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi mpaka wakati wa nabii Samweli.

21 Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini.

22 Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Ambaye pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’

23 “Kutoka katika uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Yesu, kama alivyoahidi.

24 Kabla ya kuja kwa Yesu, Yohana alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli.

25 Yohana alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La hasha, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’

26 “Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.

27 Kwa sababu wakaao Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua wala kuelewa maneno ya manabii yasomwayo kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye.

28 Ijapokuwa hawakupata sababu yo yote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe.

29 Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini.

30 Lakini Mungu alimfufua kutoka katika wafu.

31 Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.

32 “Nasi tunawaletea habari njema kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu

33 sasa ameyatimiza kwetu sisi watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:

“ ‘Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa.’

34 Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya:

“ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika

nilizomwahidi Daudi.’

35 Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi,

“ ‘Hutamwacha Mtakatifu wako aone uharibifu.’

36 “Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa pamoja na baba zake na mwili wake ukaoza.

37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.

38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu.

39 Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose.

40 Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:

41 “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka,

mkastaajabu, mkaangamie,

kwa maana nitatenda jambo wakati wenu

ambalo hamtasadiki,

hata kama mtu akiwaambia.’ ”

42 Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato nyingine inayofuata.

43 Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.

44 Sabato iliyofuata karibu watu wote wa mji ule walikuja kusikiliza neno la Mungu.

45 Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu na kunena maneno ya kashfa kuhusu yale Paulo aliyokuwa akisema.

46 Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu Mataifa.

47 Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:

“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu Mataifa,

ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”

48 Watu Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49 Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote.

50 Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka kwenye eneo lao.

51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakung’uta mavumbi kutoka kwenye miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio.

52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/13-6396e13b7cf5190488969c575fd12493.mp3?version_id=1627—

Matendo 14

Paulo Na Barnaba Huko Ikonio

1 Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama kawaida yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu Mataifa wakaamini.

2 Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini, wakawachochea watu Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya wale walioamini.

3 Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.

4 Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume.

5 Watu Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe.

6 Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo.

7 Huko wakaendelea kuhubiri habari njema.

Paulo Na Barnaba Huko Listra

8 Katika mji wa Listra, alikuweko kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe.

9 Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa.

10 Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

11 Ule umati wa watu ulipoona yale yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapiga kelele kwa lugha yao ya Kilikaonia wakasema, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!”

12 Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye aliyekuwa msemaji mkuu.

13 Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye pamoja na ule umati wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.

14 Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia na kuona mambo haya waliyotaka kufanya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema,

15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na kila kitu kilicho ndani yake.

16 Zamani aliwaachia watu waishi walivyotaka.

17 Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapatia chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.”

18 Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuuzuia ule umati wa watu kuwatolea dhabihu.

19 Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa.

20 Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.

Paulo Na Barbara Warudi Antiokia Huko Syria

21 Baada ya kuhubiri habari njema katika mji huo wa Derbe na kupata wanafunzi wengi, walirudi Listra, kisha wakaenda Ikonio na Antiokia,

22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.

24 Kisha wakapitia Pisidia wakafika Pamfilia.

25 Baada ya kuhubiri neno la Mungu huko Perga, wakatelemkia Atalia.

26 Kutoka huko Atalia wakasafiri baharini kwa merikebu wakarudi mpaka Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile kazi waliokuwa wamekamilisha.

27 Walipowasili Antiokia wakaliita kanisa pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kwa kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu Mataifa.

28 Nao wakakaa huko pamoja na wanafunzi kwa muda mrefu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/14-b9f7eb01847dfe0441f2f02685350dac.mp3?version_id=1627—

Matendo 15

Baraza Huko Yerusalemu

1 Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Uyahudi, nao wakawa wanawafundisha ndugu walioamini kwamba, “Isipokuwa mmetahiriwa kufuatana na desturi aliyofundisha Mose, hamwezi kuokoka.”

2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokukubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kuingia Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee.

3 Hivyo wakasafirishwa na kanisa, wakiwa njiani wakapitia Samaria wakawaeleza jinsi watu Mataifa walivyoongoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote.

4 Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kanisa na mitume pamoja na wazee, ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya pamoja nao.

5 Ndipo baadhi ya walioamini wa madhehebu ya Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kuzitii sheria za Mose.”

6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili.

7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu Mataifa wapate kusikia ujumbe wa injili na kuamini.

8 Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi.

9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani.

10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba?

11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

12 Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu Mataifa.

13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.

14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka katika watu Mataifa kwa ajili ya Jina lake.

15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:

16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi,

nami nitajenga upya

nyumba ya Daudi iliyoanguka.

Nitajenga tena magofu yake

na kuisimamisha,

17 ili wanadamu wengine wote

wapate kumtafuta Bwana,

hata wale watu Mataifa wote

ambao wanaitwa kwa Jina langu,

asema Bwana, afanyaye mambo haya’

18 ambayo yamejulikana tangu zamani.

19 “Kwa hiyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwasumbue watu Mataifa wanaomgeukia Mungu kwa desturi zetu,

20 badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe tu na vitu vilivyotiwa unajisi na uasherati na wasile nyama za wanyama walionyongwa au kunywa damu.

21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”

Barua Kwa Watu Mataifa Waaminio

22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao wenyewe na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili ambao walikuwa viongozi miongoni mwa ndugu.

23 Wakatumwa na barua ifuatayo:

Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,

Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:

Salamu.

24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiwataabisha mawazo yenu.

25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,

26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.

27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia.

28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wo wote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima:

29 Kwamba mjiepushe na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu, kunywa damu, nyama ya wanyama walionyongwa na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya mtakuwa mmefanya vyema.

Kwaherini.

30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua.

31 Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.

32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini.

33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma.

34 [Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.]

35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi waliwafundisha na kuhubiri neno la Bwana.

SAFARI YA PILI YA PAULO YA KITUME (15:41–18:22)

Paulo Na Barnaba Wagawanyika

36 Baada ya siku kadhaa, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote ambamo tulihubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.”

37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye.

38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi nao.

39 Pakatokea kutokukubaliana kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro.

40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana.

41 Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/15-c0379c3f6e22eca653595eb16801ced6.mp3?version_id=1627—

Matendo 16

Timotheo Aungana Na Paulo Na Sila

1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani.

2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio

3 Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani.

4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa yale maamuzi yaliyokuwa yametolewa.

5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.

6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, wakiwa wamekatazwa na Roho Mtakatifu wasihubiri neno huko Asia.

7 Walipofika kwenye mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.

8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa.

9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia ukatusaidie.”

10 Baada ya Paulo kuona maono haya, mara tulijiandaa kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kwa hakika kwamba Mungu ametuita kuhubiri habari njema huko.

Kuongoka Kwa Lidia

11 Tukasafiri kwa njia ya bahari kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, kesho yake tukafika Neapoli.

12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa Makedonia sehemu walipokuwa wanakaa Warumi, nasi tukakaa kwenye mji huo kwa siku kadhaa.

13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko.

14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanya biashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.

15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumbani mwake, alitukaribisha nyumbani mwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Paulo Na Sila Watiwa Gerezani

16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusalia, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapatia mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri.

17 Huyu mtumwa wa kike alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.”

18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

19 Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji.

20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi.

21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”

22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko.

23 Baada ya kuchapwa sana wakatupwa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu,

24 kwa kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.

28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila.

30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini ili nipate kuokoka?”

31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na wa nyumbani mwako.”

32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake.

33 Wakati ule ule yule mkuu wa gereza akawachukua akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa.

34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia meza mbele yao, yeye pamoja na wa nyumbani mwake wote wakafurahi sana kwa kuwa amemwamini Mungu.

35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.”

36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni.”

37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raia wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”

38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raia wa Rumi.

39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji.

40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/16-0cec2393049e2d3d913162ac52be00c6.mp3?version_id=1627—

Matendo 17

Ghasia Huko Thesalonike

1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.

2 Kama desturi yake Paulo aliingia ndani ya sinagogi na kwa muda wa majuma matatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko

3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristoateswe na afufuke kutoka kwa wafu, akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.”

4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wengi wa wanawake mashuhuri.

5 Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu.

6 Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku nako,

7 naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.”

8 Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia.

9 Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.

Paulo Na Sila Huko Beroya

10 Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi.

11 Hawa Wayahudi wa Beroya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.

12 Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.

13 Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko nako wakishawishi watu na kuwachochea.

14 Ndipo wale ndugu wa Beroya mara moja wakamsafirisha Paulo aende zake pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.

15 Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.

Paulo Huko Athene

16 Wakati Paulo akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona kwamba mji umejaa sanamu.

17 Hivyo akahojiana kila siku na Wayahudi pamoja na wacha Mungu kwenye sinagogi na pia sokoni kwa wale waliokutana naye huko.

18 Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye elimu ya juu sana wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu.

19 Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini?

20 Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.”

21 (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya cho chote kingine isipokuwa kueleza au kusikia jambo jipya).

22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana.

23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu.

25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji cho chote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.

26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi.

27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu.

28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa Uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe iliyotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.

30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu.

31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua, kwake huyo amewahakikishia watu wote kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

32 Waliposikia habari za ufufufo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.”

33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao.

34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/17-50b13e9b92ad3a5eb08c1cdcde730e8e.mp3?version_id=1627—