Matendo 18

Paulo Huko Korintho

1 Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho.

2 Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona,

3 naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao.

4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao akijitahidi kuwavuta Wayahudi na Wayunani.

5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo.

6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakung’uta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu Mataifa.”

7 Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa jirani na Sinagogi.

8 Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana pamoja na wote wa nyumbani mwake, nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo wakaamini na kubatizwa.

9 Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze,

10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu ye yote atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa kuna wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.”

11 Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akifundisha neno la Mungu miongoni mwao.

12 Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani.

13 Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”

14 Mara Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza.

15 Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.”

16 Akawafukuza kutoka mahakamani.

17 Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali hata mojawapo ya mambo haya.

Paulo Arudi Antiokia

18 Baada ya kukaa huko Korintho kwa muda, Paulo akaagana na wale ndugu walioamini akasafiri kwa njia ya bahari kwenda Shamu akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri.

19 Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye mwenyewe akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi.

20 Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali.

21 Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa njia ya bahari kutoka Efeso.

22 Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kulisalimu kanisa, kisha akaenda Antiokia.

23 Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda kutoka sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.

Huduma Ya Apolo Huko Efeso Na Korintho

24 Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Aleksandria. Yeye alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kunena, pia alikuwa hodari katika maandiko.

25 Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana.

26 Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi, Lakini Prisila na Akila walipomsikia walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo wakampa barua ya kumtambulisha kwa ndugu wa huko. Alipofika huko aliwasaidia sana wale watu ambao kwa neema ya Mungu walikuwa wameamini,

28 kwa maana kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/18-569898ba70fe739ab78724de15b5fd0f.mp3?version_id=1627—

Matendo 19

Paulo Huko Efeso

1 Wakati Apolo akiwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,

2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”

3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”

4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.”

5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Yesu.

6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.

7 Idadi yao ilikuwa wapata wanaume kumi na wawili.

8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akawa na majadiliano ya kuwafanya watu waamini mambo yanayohusu Ufalme wa Mungu.

9 Lakini baadhi yao kwa ukaidi walipokataa kuamini na kukashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu, Paulo aliachana nao, akawachukua wanafunzi na kuhojiana nao kila siku katika darasa la mtu mmoja aitwaye Tirano.

10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.

Wana Wa Skewa Wajaribu Kutoa Pepo Mchafu

11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo,

12 kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao na pepo wachafu wakawatoka.

13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu juu ya wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”

14 Palikuwa na wana saba wa mtu mmoja Myahudi jina lake Skewa, aliyekuwa kiongozi wa makuhani, ambao walikuwa wanafanya hivyo.

15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”

16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.

18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.

19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakam 50,000za fedha.

20 Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

Ghasia Huko Efeso

21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”

22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.

23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana.

24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,

25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii?

26 Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu.

27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”

28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhabika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”

29 Mara mji wote ukajaa ghasia, wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja.

30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati wa watu lakini wanafunzi hawakumruhusu.

31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.

32 Baadhi ya watu walikuwa wakilia hivi na wengine vile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.

33 Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.

34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”

35 Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?

36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lo lote kwa haraka.

37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.

38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu ye yote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.

39 Lakini kama kuna jambo jingine lo lote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.

40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”

41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/19-91ace03528c5a213e2d2c189f40ab9df.mp3?version_id=1627—

Matendo 20

Paulo Apita Makedonia Na Uyunani

1 Baada ya kumalizika kwa zile ghasia, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia.

2 Alipopita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo, ndipo hatimaye akawasili Uyunani,

3 ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Alipokuwa anakaribia kuanza safari kwa njia ya bahari kwenda Shamu, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yake, aliamua kurudi kwa kupitia njia ya Makedonia.

4 Paulo alikuwa amefuatana na Sopatro mwana wa Piro, Mberoya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike na Gayo, mtu wa Derbe, Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka sehemu ya Asia.

5 Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa.

6 Lakini sisi tukasafiri kwa njia ya bahari kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.

Eutiko Afufuliwa Huko Troa

7 Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane.

8 Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi.

9 Kijana mmoja jina lake Eutiko, aliyekuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akiendelea kuhubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa.

10 Paulo akashuka chini, akajitupa juu ya yule kijana na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.”

11 Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka.

12 Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.

Paulo Awaaga Wazee Wa Efeso

13 Tukaingia melini tukasafiri kwa njia ya bahari mpaka Aso ambako ndiko tungempakia Paulo, alikuwa amepanga hivyo maana alitaka kufika kwa miguu.

14 Alipotukuta huko Aso, tulimpakia melini tukasafiri wote mpaka Mitilene.

15 Kutoka huko tuliendelea kwa njia ya bahari na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo na kesho yake tukawasili Mileto.

16 Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko sehemu za Asia, kwa sababu alikuwa anatamani kama ikiwezekana kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste.

17 Paulo akiwa Mileto, akatuma ujumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye.

18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia.

19 Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi.

20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lo lote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba.

21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

22 “Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko.

23 Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja.

24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani, kazi ya kuishuhudia injili ya neema ya Mungu.

25 “Nami sasa najua ya kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu ninyi ambaye nimemhubiria Ufalme wa Mungu katika kwenda kwangu huko na huko, atakayeniona uso tena.

26 Kwa hiyo nawaambieni leo hii kwamba sina hatia ya damu ya mtu awaye yote.

27 Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.

28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.

29 Najua kwamba baada mimi kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi.

30 Hata kutoka miongoni mwenu wenyewe watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate.

31 Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya, kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

32 “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa.

33 Sikutamani fedha wala dhahabu wala nguo ya mtu ye yote.

34 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.

35 Katika kila jambo nililofanya, nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni baraka zaidi kutoa kuliko kupokea.’ ”

36 Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba.

37 Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu,

38 Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye mpaka kwenye meli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/20-9275e89002c23326abbae4e33ffa1c17.mp3?version_id=1627—

Matendo 21

SAFARI YA TATU YA PAULO YA KITUME

Paulo Aenda Yerusalemu

1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara.

2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo.

3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake.

4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba.

6 Baada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.

7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu wanafunzi wa huko tukakaa nao kwa siku moja.

8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale watu saba waliochaguliwa kule Yerusalemu, tukakaa kwake.

9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira ambao walikuwa wanatoa unabii.

10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akatelemka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo.

11 Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu Mataifa.’ ”

12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.

13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”

14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu.

16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.

Paulo Awasili Yerusalemu

17 Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha.

18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo na wazee wote wa kanisa walikuwepo.

19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu Mataifa kwa kupitia huduma yake.

20 Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kuna elfu nyingi za Wayahudi walioamini, nao wote wana bidii kwa ajili ya sheria.

21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu Mataifa kumkataa Mose na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi.

22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu.

23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri.

24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria.

25 Lakini kuhusu wale watu Mataifa walioamini tumewaandikia uamuzi wetu kwamba wajitenge na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu na damu au kula nyama ya mnyama aliyeuawa kwa kunyongwa, tena wajitenge na uasherati.”

26 Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili akatoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Paulo Akamatwa

27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu wakamkamata.

28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”

29 (Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)

30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka mle Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa.

31 Walipokuwa wakitaka kumwua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko.

32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na maaskari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.

33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani na alikuwa amefanya nini.

34 Baadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine wakisema lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi.

35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi maaskari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa.

36 Ule umati wa watu walikuwa wakifuata wakiendelea kupiga kelele wakisema, “Mwondoe huyu!”

Paulo Anajitetea

37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”

Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?

38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”

39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raia wa mji usiokuwa wa kawaida. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”

40 Akiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/21-e86edac31bc7014729c50c5db7e652b1.mp3?version_id=1627—

Matendo 22

Ushuhuda Wa Paulo Kwa Wayahudi Wa Yerusalemu

1 “Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu.”

2 Waliposikia akisema kwa lugha ya Kiebrania, wakanyamaza kimya kabisa.

Ndipo Paulo akasema,

3 “Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu, miguuni mwa Gamalieli. Nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, nikiwa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama kila mmoja wenu alivyo leo.

4 Niliwatesa watu wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata, waume kwa wake na kuwatupa gerezani.

5 Kama Kuhani Mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kuhusu mimi. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.

Paulo Aeleza Juu Ya Kuongoka Kwake

6 “Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kote kote.

7 Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli, Mbona unanitesa?’

8 “Nikajibu, ‘Wewe ni nani Bwana?’

“Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayenitesa.’

9 Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.

10 “Nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’

“Naye Bwana akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa mambo yote yakupasayo kufanya.’

11 Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mng’ao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski.

12 “Mtu mmoja Mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona, aliyeshika sana sheria zetu, na ambaye aliheshimiwa sana na Wayahudi waliokuwa wakiishi huko Dameski,

13 alisimama karibu nami akasema, ‘Ndugu Sauli, upate kuona tena!’ Saa ile ile nikapata kuona tena, nami nikaweza kumwona.

14 “Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake.

15 Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia.

16 Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’

Paulo Atumwa Kwa Watu Mataifa

17 “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula

18 nikamwona Yesu akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu mimi.’

19 “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyokwenda kwenye kila sinagogi ili kuwatia gerezani na kuwapiga wale waliokuamini.

20 Wakati damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomwua.’

21 “Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu Mataifa.’ ”

Paulo Na Jemadari Wa Kirumi

22 Ule umati wa watu wakamsikiliza Paulo mpaka aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!”

23 Wakati walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani,

24 yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba achapwe viboko na aulizwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo.

25 Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wamchape viboko, Paulo akamwambia kiongozi wa maaskari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumchapa mtu ambaye ni raia wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?”

26 Yule askari aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raia wa Rumi.”

27 Yule jemadari akaja akamwuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raia wa Rumi?”

Paulo akajibu, “Naam, hakika ndiyo.”

28 Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.”

Paulo akasema “Lakini mimi ni raia wa Rumi kwa kuzaliwa.”

29 Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka na yule jemadari akaingiwa na hofu, alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi kwa minyororo.

Paulo Apelekwa Mbele Ya Baraza

30 Kesho yake, kwa kuwa yule Jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua na kuwaagiza viongozi wa makuhani na baraza lote likutane. Kisha akamleta Paulo akamsimamisha mbele yao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/22-674ff108531bd4452dfc6ab0fd6444d0.mp3?version_id=1627—

Matendo 23

1 Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.”

2 Kwa ajili ya jambo hili Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani.

3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”

4 Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?”

5 Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa Kuhani Mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ”

6 Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.”

7 Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika.

8 (Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)

9 Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lo lote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye”

10 Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.

11 Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

Hila Za Kumwua Paulo

12 Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo.

13 Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini.

14 Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo.

15 Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mumjulishe jemadari ili amtelemshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumwua kabla hajafika hapa.”

16 Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.

17 Ndipo Paulo akamwita mmoja wa wakuu wa maaskari akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.”

18 Hivyo yule mkuu wa maaskari akampeleka yule kijana kwa jemadari akamwambia, “Paulo, yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”

19 Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumwuliza, “Unataka kuniambia nini?”

20 Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake.

21 Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.”

22 Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu ye yote kwamba umenieleza habari hizi.”

Paulo Ahamishiwa Kaisaria

23 Kisha yule jemadari akawaita wakuu wake wawili wa maaskari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki.

24 Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mumpeleke salama mpaka kwa mtawala Feliksi.”

25 Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:

26 Klaudio Lisia,

Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi:

Salamu.

27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumwua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya maaskari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi.

28 Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao.

29 Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lo lote linalostahili kifo au kifungo.

30 Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara, nikiwaagiza washtaki wake pia waeleze mbele yako mashtaka yao dhidi yake.

31 Hivyo maaskari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri.

32 Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wakati wao walirudi kwenye ngome ya maaskari.

33 Walipofika Kaisaria kumpa mtawala ile barua, walimkabidhi pia Paulo kwake.

34 Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimwuliza Paulo kwamba alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia,

35 alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/23-cc3928062fcfec48d02ebcaf63e52ec2.mp3?version_id=1627—

Matendo 24

Mbele Ya Feliksi Huko Kaisaria

1 Baada ya siku tano, Kuhani Mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala.

2 Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele.

3 Wakati wote na kila mahali, kwa namna yo yote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi.

4 Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.

5 “Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo,

6 na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu.

7 Lakini jemadari Lisia, alitujia na nguvu nyingi akamwondoa mikononi mwetu,

8 akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote yale tunayomshtaki kwayo.”

9 Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka yote haya ni kweli.

Paulo Ajitetea Mbele Ya Feliksi

10 Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha.

11 Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu.

12 Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu ye yote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine po pote mjini.

13 Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayonishtaki kwayo.

14 Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii,

15 nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wote wenye haki na wasio na haki.

16 Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.

17 “Basi, baada ya kutokuwapo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu.

18 Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yo yote.

19 Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lo lote dhidi yangu.

20 Au, watu hawa walioko hapa waseme ni uhalifu gani walioniona nao waliponisimamisha mbele ya baraza,

21 isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yako leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”

22 Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapotelemka huku, nitaamua shauri lako.”

23 Ndipo akaamuru mkuu wa maaskari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.

24 Baada ya siku kadhaa Feliksi alipokuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi, alituma aitiwe Paulo na kumsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Yesu Kristo.

25 Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.”

26 Wakati huo huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempatia rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.

27 Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/24-9dd5c19556d65bad567b4247b48b8725.mp3?version_id=1627—

Matendo 25

Paulo Mbele Ya Festo

1 Siku tatu baada ya Festo kuwasili Kaisaria kuchukua wajibu wake mpya, alipanda kwenda Yerusalemu,

2 ambako viongozi wa makuhani na viongozi wa Wayahudi walikuja mbele yake na kuleta mashtaka yao dhidi ya Paulo.

3 Wakamsihi sana Festo, kama upendeleo kwao, aamuru Paulo ahamishiwe Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wanaandaa kumvizia ili wamwue akiwa njiani.

4 Festo akawajibu, “Paulo amezuiliwa huko Kaisaria, nami mwenyewe ninakwenda huko hivi karibuni.

5 Baadhi ya viongozi wenu wafuatane nami na kutoa mashtaka dhidi ya mtu huyo huko, kama amekosa jambo lo lote.”

6 Baada ya Festo kukaa miongoni mwao kwa karibu siku nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria na siku iliyofuata akaitisha mahakama, akaketi penye kiti chake cha hukumu, akaamuru Paulo aletwe mbele yake.

7 Paulo alipotokea, wale Wayahudi waliokuwa wametelemka toka Yerusalemu wakasimama wakiwa wamemzunguka, wakileta mashtaka mengi mazito dhidi yake ambayo hawakuweza kuyathibitisha.

8 Ndipo Paulo akajitetea, akasema, “Mimi sikufanya jambo lo lote kinyume cha sheria ya Wayahudi au dhidi ya Hekalu au kinyume cha Kaisari.”

9 Festo, akitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na kukabili mashtaka mbele yangu huko?”

10 Paulo akasema, “Mimi sasa nimesimama mbele ya mahakama ya Kaisari, ambako ndiko ninakostahili kushtakiwa. Kama vile wewe mwenyewe ujuavyo vyema kabisa sijawatendea Wayahudi kosa lo lote.

11 Basi kama mimi nina hatia ya kutenda kosa lo lote linalostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama mashtaka yaliyoletwa dhidi yangu na hawa Wayahudi si kweli, hakuna ye yote aliye na haki ya kunikabidhi mikononi mwao. Naomba rufaa kwa Kaisari!”

12 Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utakwenda!”

Festo Aomba Ushauri Kwa Agripa

13 Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo.

14 Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani.

15 Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.

16 “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu ye yote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa.

17 Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe.

18 Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wo wote niliokuwa ninatarajia.

19 Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai.

20 Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimwuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya.

21 Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.”

22 Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.”

Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.”

Paulo Aletwa Mbele Ya Agripa

23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani.

24 Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi.

25 Sikuona kwamba ametenda jambo lo lote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa Mfalme, niliamua kumpeleka Rumi.

26 Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, wewe Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika.

27 Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/25-7eddf5e0f29c830d9554491e030654ca.mp3?version_id=1627—

Matendo 26

Paulo Ajitetea Mbele Ya Agripa

1 Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Unayo ruhusa kujitetea.”

Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema:

2 “Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi,

3 hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.

4 “Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu.

5 Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu niliishi nikiwa Farisayo.

6 Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo.

7 Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii mchana na usiku.

8 Kwa nini ye yote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?

9 “Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti.

10 Nami hayo ndiyo nilivyofanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono.

11 Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi jingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa.

Paulo Aeleza Kuhusu Kuongoka Kwake

12 “Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani.

13 Ilikuwa yapata adhuhuri, Ee Mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, iking’aa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao.

14 Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’

15 “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’

“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayenitesa.

16 Lakini sasa inuka usimame kwa miguu yako, kwa sababu nimekutokea kwa kusudi hili, ili kukuweka utumike na kushuhudia juu ya mambo ambayo umeyaona na yale nitakayokutokea kwayo.

17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu Mataifa ambao ninakutuma kwao,

18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni na kutoka kwenye nguvu za Shetani, wamgeukie Mungu ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

19 “Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni,

20 bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Uyahudi na pia kwa watu Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao.

21 Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua.

22 Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu na hivyo nasimama hapa nikishuhudia wakubwa na wadogo, bila kusema cho chote zaidi ya yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia:

23 kwamba Kristoatateswa na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu Mataifa.”

Paulo Aeleza Juu Ya Kuhubiri Kwake

24 Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”

25 Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu.

26 Naam, Mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni.

27 Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”

28 Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe Mkristo?”

29 Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, isipokuwa minyororo hii.”

30 Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao.

31 Wakati walipokuwa wakiondoka, wakaambiana “Mtu huyu hafanyi jambo lo lote linalostahili kufa au kufungwa.”

32 Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeweza kuachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/26-1bbad31e11dbd98f2d28c3f000f8dac9.mp3?version_id=1627—

Matendo 27

Paulo Asafiri Kwa Njia Ya Bahari Kwenda Rumi

1 Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa askari mmoja jina lake Juliasi, ambaye alikuwa wa kikosi cha walinzi wa Kaisari Agusto.

2 Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike.

3 Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wampatie mahitaji yake.

4 Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.

5 Baada ya sisi kuvuka bahari iliyoko upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia.

6 Huko yule jemadari akapata meli ya Aleksandria ikielekea Italia, akatupandisha humo.

7 Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone.

8 Tukaambaa-ambaa na pwani, kwa shida tukafika sehemu moja iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea.

9 Muda mwingi ulikuwa umepotea na kusafiri baharini kulikuwa hatari kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya siku za kufunga. Hivyo Paulo akawaonya akasema,

10 “Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.”

11 Lakini badala ya yule askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli.

12 Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyoko katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.

Dhoruba Baharini

13 Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakang’oa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete.

14 Lakini baada ya muda mfupi ikavuma tufani kubwa iitwayo “Eurakilo” toka kisiwa cha Krete.

15 Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea.

16 Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu.

17 Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo.

18 Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka melini,

19 siku ya tatu kwa mikono yao wenyewe, wakatupa vyombo vya meli baharini.

20 Kulipokuwa hakuna kuonekana kwa jua wala nyota kwa siku nyingi, nayo dhoruba ikiwa inaendelea kuwa kali, hatimaye tulikata kabisa tamaa ya kuokoka.

21 Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao akasema, “Enyi watu, iliwapasa kunisikiliza na kuacha kusafiri baharini kutoka Krete, ndipo ninyi mngekuwa mmejinusuru na uharibifu huu na hasara hii.

22 Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo mkuu kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia.

23 Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ambaye ninamwabudu alisimama karibu nami,

24 naye akasema, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amewapa usalama wote wanaosafiri pamoja nawe.

25 Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia.’

26 Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”

27 Usiku wa kumi na nne, ulipofika, tulipokuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria, ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu.

28 Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini, baada ya kuendelea mbele kidogo wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano.

29 Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke.

30 Katika jaribio la kutoroka kutoka kwenye meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanakwenda kushusha nanga za omo.

31 Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na maaskari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.”

32 Hivyo basi wale maaskari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini.

33 Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula cho chote.

34 Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele mmoja kutoka kichwani mwake.”

35 Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula.

36 Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula.

37 Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu 276.

38 Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.

39 Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana.

40 Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli, kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani.

41 Lakini wakafika mahali ambapo bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni, omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa, lakini sehemu ya shetriikavunjika vipande vipande kwa kule kupiga kwa mawimbi yenye nguvu.

42 Wale maaskari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka.

43 Lakini yule jemadari akitaka kuokoa maisha ya Paulo, akawazuia maaskari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee mpaka nchi kavu.

44 Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo ikatimia kwamba wote wakaokoka na kufika nchi kavu salama.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/27-6ddbe8f3eceeaf731e970ca17e87d1c2.mp3?version_id=1627—