Matendo 28

Paulo Kisiwani Malta

1 Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta.

2 Wenyeji wa kile kisiwa wakatufanyia ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na ni baridi.

3 Paulo alikuwa amekusanya mzigo wa kuni na alipokuwa anaweka kwenye moto kwa ajili ya joto, nyoka mwenye sumu akatoka humo na kujisokotea mkononi mwake.

4 Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akining’inia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni mwuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.”

5 Lakini Paulo akamkung’utia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yo yote.

6 Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona hakuna cho chote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.

7 Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la mtu mmoja kiongozi wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio, ambaye alitupokea akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu.

8 Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaumwa homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya.

9 Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa.

10 Wakatupa heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa njia ya bahari, wakapakia melini vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji.

Paulo Anawasili Rumi

11 Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Aleksandria yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi.

12 Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu,

13 Kisha tukang’oa nanga tukafika Regio siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli.

14 Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari mpaka Rumi.

15 Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja mpaka Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo.

16 Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda.

Paulo Ahubiri Rumi Chini Ya Ulinzi

17 Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Kiyahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lo lote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi.

18 Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lo lote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo.

19 Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lo lote juu ya taifa langu.

20 Basi ili niseme nanyi, kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”

21 Wakamjibu, “Hatujapokea barua zo zote kutoka Uyahudi zinazokuhusu, wala hapana ndugu ye yote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lo lote baya juu yako.

22 Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”

23 Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Yesu kutoka katika Sheria ya Mose na kutoka Manabii.

24 Baadhi wakasadiki kwa yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini.

25 Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho Mtakatifu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu kwa kinywa cha Isaya kwamba:

26 “ ‘Nenda kwa watu hawa na useme,

“Kweli mtasikiliza lakini kamwe hamtaelewa;

kweli mtatazama, lakini hamtaona.”

27 Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu,

na masikio yao ni mazito kusikia,

nao wamefumba macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

na kusikiliza kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao

na kugeuka, nami nikawaponya.’

28 “Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu Mataifa, nao watasikiliza.”

29 Naye akiisha kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.

30 Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwenye nyumba yake mwenyewe aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote waliokwenda kumwona.

31 Akahubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri wote na bila kizuizi cho chote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/28-f02d4eb3b3f21d17fb5e2bb5aa9c1611.mp3?version_id=1627—

Yohana 1

Neno Alifanyika Mwili

1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.

2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.

3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.

4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu.

5 Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda.

6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.

7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia yeye watu wote waweze kuamini.

8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.

9 Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.

10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kwa yeye, haukumtambua.

11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea.

12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.

13 Hawa ndio waliozaliwa si kwa damu wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.

15 Yohana alishuhudia habari zake, akapiga kelele akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwako kabla yangu.’ ”

16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema.

17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo.

18 Hakuna mtu ye yote aliyemwona Mungu wakati wo wote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.

Ushuhuda Wa Yohana Mbatizaji

19 Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipotuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumwuliza, “Wewe ni nani?”

20 Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.”

21 Wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?”

Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”

“Je, wewe ni yule Nabii?”

Akajibu, “Hapana.”

22 Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”

23 Akawajibu kwa maneno ya Nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Inyosheni njia ya Bwana.’ ”

24 Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo

25 wakamwuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”

26 Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua.

27 Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”

28 Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ng’ambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.

Yesu Mwana-Kondoo Wa Mungu

29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!

30 Huyu ndiye yule niliyewaambia ya kwamba, ‘Yuaja mtu nyuma yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi kwa maana alikuwako kabla yangu.’

31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”

32 Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.

33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’

34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”

Wanafunzi Wa Kwanza Wa Yesu

35 Siku iliyofuata, Yohana alikuwako huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili.

36 Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”

37 Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu.

38 Yesu akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?”

Wakamwambia, “Rabi,” (maana yake Mwalimu), “Unaishi wapi?”

39 Yesu akawajibu, “Njoni, nanyi mtapaona!”

Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.

40 Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana aliyokuwa amesema, naye ndiye aliyemfuata Yesu.

41 Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Kristo).

42 Naye akamleta kwa Yesu.

# Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro).

Yesu Awaita Filipo Na Nathanaeli

43 Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”

44 Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro.

45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Torati na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”

46 Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu cho chote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”

47 Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli, hana hila ndani yake.”

48 Nathanaeli akamwuliza, “Umenifahamuje?”

Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”

49 Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”

50 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.”

51 Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/1-b4b3d60a567ee2edcc99685110897b63.mp3?version_id=1627—

Yohana 2

Arusi Huko Kana

1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwako huko.

2 Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia.

3 Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.”

4 Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.”

5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lo lote atakalowaambia, fanyeni.”

6 Basi ilikuwapo huko mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi, kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.

7 Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.

8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.”

Hivyo wakachota, wakampelekea.

9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando

10 akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

11 Huu, ndio uliokuwa mwujiza wa kwanza Yesu aliofanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini.

Yesu Atakasa Hekalu

12 Baada ya hayo, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu wakakaa huko siku chache.

13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Yesu alipanda kwenda Yerusalemu.

14 Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa na wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha.

15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao.

16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”

17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”

18 Ndipo Wayahudi wakamwuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”

19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”

20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?”

21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake.

22 Baada ya kufufuka kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.

23 Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakamwamini.

24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote.

25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu ye yote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/2-48bc4dbf98cb12b7d01420aee1805e03.mp3?version_id=1627—

Yohana 3

Nikodemo Amwendea Yesu Usiku

1 Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudilililotawala.

2 Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”

3 Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, mtu hawezi kuuona Ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili.”

4 Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”

5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu ye yote anayeweza kuingia katika Ufalme wa Mungu isipokuwa amezaliwa kwa maji na kwa Roho.

6 Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho.

7 Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili.’

8 Upepo huvuma po pote upendapo. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”

9 Nikodemo akamwuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?”

10 Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya?

11 Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu.

12 Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni?

13 Hakuna mtu ye yote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.

14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu.

15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kwa yeye ulimwengu upate kuokolewa.

18 Ye yote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu.

19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu.

20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe.

21 Lakini wale watendao yaliyo mema huja kwenye nuru, kusudi ionekane wazi kwamba matendo yao yametendeka katika Mungu.”

Ushuhuda Wa Yohana Mbatizaji Kuhusu Yesu

22 Baada ya haya, Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika nchi ya Uyahudi, nao wakakaa huko kwa muda na kubatiza.

23 Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni karibu na Salimu kwa sababu huko kulikuwa na maji tele. Watu wazima wakamjia huko ili kubatizwa.

24 (Hii ilikuwa kabla Yohana hajatiwa gerezani).

25 Mashindano yakazuka kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja kuhusu suala la desturi ya kunawa.

26 Wakamwendea Yohana wakamwambia, “Rabi, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng’ambo ya pili ya Mto Yordani, yule uliyeshuhudia habari zake, sasa anabatiza na kila mtu anamwendea!”

27 Yohana akawajibu, “Hakuna mtu ye yote awezaye kupata kitu cho chote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni.

28 Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, ila nimetumwa nimtangulie.’

29 Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika.

30 Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”

Yeye Aliyetoka Mbinguni

31 “Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, yeye aliye wa duniani ni wa dunia, naye huzungumza mambo ya duniani. Yeye aliyekuja kutoka mbinguni, yu juu ya yote.

32 Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna ye yote anayekubali ushuhuda wake.

33 Lakini ye yote anayekubali huo ushuhuda anathibitisha kwamba, Mungu ni kweli.

34 Yeye aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, kwa kuwa Mungu humtoa Roho pasipo kipimo.

35 Baba anampenda Mwana, naye ametia vitu vyote mikononi mwake.

36 Ye yote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/3-e2eb68c0f31cd4c1f24f18e327e4c8b9.mp3?version_id=1627—

Yohana 4

Yesu Azungumza Na Mwanamke Msamaria

1 Mafarisayo wakasikia kwamba Yesu alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yohana,

2 ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake.

3 Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya.

4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria.

5 Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yosefu.

6 Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.

7 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.”

8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)

9 Yule mwanamke akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.

10 Yesu akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”

11 Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi?

12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”

13 Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki, ataona kiu tena.

14 Lakini ye yote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.”

15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”

16 Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”

17 Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”

Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume.

18 Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako!”

19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii.

20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”

21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu.

22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi.

23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta.

24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Kristo) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”

26 Yesu akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye Masiya.”

27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?”

28 Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu,

29 “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Masiya?”

30 Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Yesu.

31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau cho chote.”

32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”

33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?”

34 Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.

35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa!

36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunae wafurahi pamoja.

37 Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa.

38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”

Wasamaria Wengi Waamini

39 Wasamaria wengi kutoka katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila jambo nililotenda.”

40 Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili.

41 Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.

42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”

Yesu Amponya Mwana Wa Afisa

43 Baada ya zile siku mbili, Yesu aliondoka kwenda Galilaya.

44 (Basi Yesu mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.)

45 Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria kwenye hiyo Sikukuu.

46 Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwako na mtu mmoja afisa wa kifalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu.

47 Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.

48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”

49 Yule afisa wa kifalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”

50 Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.”

Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake.

51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima.

52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”

53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye, pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Yesu alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/4-ca8e5d8065bfaa90e861d096aad2eeac.mp3?version_id=1627—

Yohana 5

Yesu Amponya Mtu Penye Bwawa La Bethzatha

1 Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu.

2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano.

3 Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingojea maji yatibuliwe

4 [kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji na yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wo wote aliokuwa nao].

5 Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane.

6 Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwako hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”

7 Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”

8 Yesu akamwambia, “Simama, chukua mkeka wako na uende.”

9 Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea.

Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.

10 Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, ni kinyume cha sheria wewe kubeba mkeka wako.”

11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”

12 Wakamwuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”

13 Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Yesu alikuwa amejiondoa katika ule umati wa watu uliokuwa hapo.

14 Baadaye Yesu akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.”

15 Yule mtu akaenda, akawaambia wale Wayahudi kuwa ni Yesu aliyemponya.

Uzima Kupitia Mwana

16 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato.

17 Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”

18 Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumwua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.

Mamlaka Ya Mwana Wa Mungu

19 Yesu akawaambia, “Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lo lote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lo lote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo.

20 Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa.

21 Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda.

22 Wala Baba hamhukumu mtu ye yote, lakini hukumu yote amempa Mwana,

23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Ye yote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.

24 “Amin, amin ninawaambia, ye yote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani.

25 Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai.

26 Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake.

27 Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.

28 “Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake.

29 Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.

Shuhuda Kuhusu Yesu

30 “Mimi siwezi kufanya jambo lo lote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.

31 “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli.

32 Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.

33 “Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli.

34 Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa.

35 Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.

36 “Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye aliyenituma.

37 Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake,

38 wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye.

39 Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi.

40 Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.

41 “Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu.

42 Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu.

43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea.

44 Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu?

45 “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu.

46 Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu.

47 Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/5-f2235d43704bde9a9f758459df78b5df.mp3?version_id=1627—

Yohana 6

Yesu Alisha Watu 5,000

1 Baada ya haya, Yesu alikwenda ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia.

2 Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa.

3 Kisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake.

4 Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

5 Yesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?”

6 Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

7 Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili, hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa kila mtu apate kidogo.”

8 Mmoja wa wanafunzi wake, aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia,

9 “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati wote huu?”

10 Yesu akasema, “waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi, palikuwa na wanaume 5,000.

11 Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wamekaa kwa kiasi walichohitaji. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12 Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee cho chote.”

13 Hivyo wakavikusanya wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vilivyobaki vya ile mikate mitano na samaki wale wawili wadogo.

14 Baada ya watu kuona mwujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!”

15 Yesu akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walitelemka kwenda baharini.

17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao.

18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.

19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, wakaogopa sana.

20 Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope.”

21 Ndipo kwa furaha wakamkaribisha kwenye mashua, na mara wakafika walikokuwa wanakwenda.

Watu Wanamtafuta Yesu

22 Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng’ambo ya pili waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Yesu hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao.

23 Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kumshukuru Mungu.

24 Mara wale watu wakatambua kwamba Yesu hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Yesu.

Yesu Ni Mkate Wa Uzima

25 Walipomkuta Yesu ng’ambo ya bahari wakamwuliza, “Rabi, umefika lini huku?”

26 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.

27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

28 Ndipo wakamwuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

29 Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

30 Hivyo wakamwuliza, “Utafanya ishara gani ya mwujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani?

31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”

32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni.

33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe.

36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini.

37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na ye yote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe.

38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.

39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho.

40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

41 Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”

42 Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yosefu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”

43 Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunung’unikiana ninyi kwa ninyi.

44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.

45 Imeandikwa katika manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Ye yote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu.

46 Hakuna mtu ye yote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba.

47 Amin, amin nawambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele.

48 Mimi ni mkate wa uzima.

49 Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa.

50 Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu ye yote akiula, hatakufa.

51 Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu ye yote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”

52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”

53 Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.

54 Mtu ye yote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56 Ye yote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake.

57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu.

58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.”

59 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.

Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu

60 Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”

61 Yesu alipojua kwamba wafuasi wake wananung’unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi?

62 Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza?

63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima.

64 Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Yesu alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti.

65 Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

66 Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.

67 Hivyo Yesu akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”

68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.

69 Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai.”

70 Ndipo Yesu akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.”

71 (Hapa alikuwa anasema juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Yesu.)

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/6-386d0a6993cf9fb91ae8e827742fab75.mp3?version_id=1627—

Yohana 7

Kutokuamini Kwa Ndugu Zake Yesu

1 Baada ya mambo haya, Yesu alikwenda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Uyahudi kwa sababu Wayahudi huko walitaka kumwua.

2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

3 Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya.

4 Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya jionyeshe kwa ulimwengu.”

5 Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.

6 Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote.

7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.

8 Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.”

9 Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.

Yesu Kwenye Sikukuu Ya Vibanda

10 Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri.

11 Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”

12 Kulikuwa na minong’ono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”

Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.”

13 Lakini hakuna mtu ye yote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.

Yesu Afundisha Kwenye Sikukuu

14 Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.

15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

16 Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma.

17 Mtu ye yote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.

18 Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake.

19 Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

20 Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

21 Yesu akawajibu, “Nimefanya mwujiza mmoja na nyote mkastaajabu.

22 Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato.

23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato?

24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Je, Yesu Ndiye Kristo?

25 Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumwua?

26 Mbona yuko hapa anazungumza hadharani na wala hawamwambii neno lo lote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo?

27 Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna ye yote atakayejua atokako.”

28 Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hamumjui.

29 Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.”

30 Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu ye yote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia.

31 Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu zaidi kuliko aliyoifanya mtu huyu?”

Walinzi Wanatumwa Kumkamata Yesu

32 Mafarisayo wakasikia watu wakinong’ona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani, wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.

33 Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.

34 Mtanitafuta, lakini hamtaniona, nami niliko, ninyi hamwezi kuja.”

35 Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?

36 Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona na huko nitakapokuwa ninyi hamwezi kuja?’ ”

Mito Ya Maji Ya Uzima

37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu ye yote anaona kiu na aje kwangu anywe.

38 Ye yote aniaminiye mimi, kama maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”

39 Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.

Mgawanyiko Miongoni Mwa Watu

40 Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”

41 Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!”

Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya?

42 Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka katika jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”

43 Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu.

44 Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

Kutokuamini Kwa Viongozi Wa Wayahudi

45 Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”

46 Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu ye yote kama yeye anenavyo.”

47 Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?

48 Je, kuna kiongozi ye yote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?

49 Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.”

50 Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, ambaye alikuwa mmoja wao akauliza,

51 “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”

52 Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!”

53 [Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/7-e91315c00867568676bdff1dec566020.mp3?version_id=1627—

Yohana 8

Mwanamke Aliyefumaniwa Akizini

1 Lakini Yesu akaenda katika Mlima wa Mizeituni.

2 Alfajiri na mapema Yesu akaja tena Hekaluni, watu wote wakakusanyika, akakaa akaanza kuwafundisha.

3 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote.

4 Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini.

5 Katika sheria, Mose alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa wewe wasemaje?”

6 Walimwuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki.

Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake.

7 Walipoendelea kumwulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu ye yote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”

8 Akainama tena na kuandika ardhini.

9 Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake.

10 Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”

11 Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.”

Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]

Yesu Nuru Ya Ulimwengu

12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu ye yote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

13 Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”

14 Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.

15 Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu ye yote.

16 Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu, bali mimi pamoja na Baba aliyenituma.

17 Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti.

18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”

19 Ndipo wakamwuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?”

Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hamumfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”

20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia. Yesu akasema, “ ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kufika.’ ”

Yesu Atabiri Kifo Chake Mwenyewe

21 Yesu akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako ninyi hamwezi kuja.”

22 Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako Mimi ninyi hamwezi kuja’?”

23 Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini, mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.

24 Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”

25 Wakamwuliza, “Wewe ni nani?”

Naye Yesu akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo.

26 Nina mambo mengi ya kusema juu yenu na mengi ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kweli, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.”

27 Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia juu ya Baba yake wa Mbinguni.

28 Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lo lote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha.

29 Yeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’ ”

30 Wengi waliomsikia Yesu akisema maneno haya wakamwamini.

Wanafunzi Wa Kweli

31 Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.

32 Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.”

33 Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu ye yote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?”

34 Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.

35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima.

36 Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.

37 Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu.

38 Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”

Yesu Na Abrahamu

39 Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.”

Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu.

40 Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Abrahamu hakufanya jambo la namna hii.

41 Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.”

Wakamjibu, “Sisi si watoto wa haramu, tunaye Baba mmoja ndiye Mungu.”

42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.

43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho.

44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.

45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini!

46 Je, kuna ye yote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?

47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”

Maelezo Ya Yesu Kuhusu Yeye Mwenyewe

48 Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?”

49 Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau.

50 Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi.

51 Amin, amin nawaambia, mtu ye yote akilitii neno langu hataona mauti milele.”

52 Ndipo Wayahudi wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu. Ikiwa Abrahamu alikufa na vivyo hivyo manabii, nawe unasema ‘Mtu akitii neno langu hatakufa?’

53 Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa na manabii ambao nao pia walikufa? Hivi wewe unajifanya kuwa nani?”

54 Yesu akawajibu, “Kama nikijitukuza utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi.

55 Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake.

56 Baba yenu Abrahamu alishangilia kwamba angaliiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”

57 Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, wewe wasema umemwona Abrahamu?”

58 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Abrahamu hajakuwako, ‘Mimi niko.’ ”

59 Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/8-43413bfd11168f52cf7c5c4e693c8c0a.mp3?version_id=1627—

Yohana 9

Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa.

2 Wanafunzi wake wakamwuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.

4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.

5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni.

7 Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu, maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.

8 Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?”

9 Wengine wakasema, “Ndiye.”

Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.”

Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”

10 Wakamwuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”

11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”

12 Wale wakamwuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?”

Akawajibu, “Sijui.”

Mafarisayo Wachunguza Kuponywa Kwa Kipofu

13 Wakamleta kwa Mafarisayo yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali.

14 Basi siku hiyo Yesu alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato.

15 Mafarisayo nao wakaanza kumwuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”

16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”

Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.

17 Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho, wasemaje kuhusu mtu huyo?” Maana macho yako ndiyo yaliyofumbuliwa.

Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”

18 Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake.

19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”

20 Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu.

21 Lakini sisi hatujui ni kwa jinsi gani kwamba sasa anaona, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Mwulizeni, yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.”

22 Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu ye yote atakayemkiri Yesu kuwa ndiye Kristoatafukuzwa kutoka katika sinagogi.

23 Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Mwulizeni.”

24 Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”

25 Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”

26 Wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”

27 Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”

28 Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake, Sisi ni wanafunzi wa Mose.

29 Tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini kwa habari ya mtu huyu hatujui atokako.”

30 Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu!

31 Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii.

32 Tangu kuumbwa kwa ulimwengu hatujasikia kwamba mtu amemponya ye yote aliyekuwa kipofu.

33 Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lo lote.”

34 Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.

Upofu Wa Kiroho

35 Yesu aliposikia kuwa wamemfukuzia nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta akamwuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”

36 Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani ili nipate kumwamini, niambie ili nipate kumwamini.”

37 Yesu akamjibu, “Umekwisha kumwona, naye anayezungumza nawe, ndiye.”

38 Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.

39 Yesu akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona, wawe vipofu.”

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”

41 Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/9-66f2b4d1ea4ba355f2b6be6d7dae7c0a.mp3?version_id=1627—