Yohana 10

Mchungaji Mwema

1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwivi na mnyang’anyi.

2 Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo.

3 Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi.

4 Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake.

5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”

6 Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.

7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo.

8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi, lakini kondoo hawakuwasikia.

9 Mimi ndimi lango, ye yote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho.

10 Mwivi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

12 Mtu wa kuajiriwa ambaye kondoo si mali yake, amwonapo mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo na mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya.

13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua.

15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.

16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.

17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.

18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

19 Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika.

20 Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”

21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu mwenye pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”

Yesu Akataliwa Na Wayahudi

22 Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu,nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi.

23 Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni.

24 Wayahudi wakamkusanyikia wakamwuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristotuambie waziwazi.”

25 Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia.

26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu.

27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata,

28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka katika mikono yangu.

29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.

30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”

31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo,

32 lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”

33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”

34 Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Torati ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ndinyi miungu?’

35 Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka.

36 Je, mwawezaje kusema kwamba, yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru kwa sababu nilisema ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’

37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini,

38 lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.”

39 Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.

40 Akaenda tena ng’ambo ya Mto Yordani mpaka mahali pale ambapo Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko.

41 Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya mwujiza wo wote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.”

42 Nao wengi wakamwamini Yesu huko.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/10-845ea275b8972be20231aad1f117d70a.mp3?version_id=1627—

Yohana 11

Kifo Cha Lazaro

1 Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake.

2 Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.

3 Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”

4 Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.”

5 Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao,

6 baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.

7 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya na turudi Uyahudi.”

8 Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”

9 Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu.

10 Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”

11 Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini nakwenda kumwamsha.”

12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.”

13 Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.

14 Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa.

15 Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”

16 Tomasi aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”

Yesu Ndiye Ufufuo Na Uzima

17 Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekwisha kuwako kaburini siku nne.

18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili,

19 Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao.

20 Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.

21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.

22 Lakini sasa ninajua kuwa cho chote utakachomwomba Mungu, atakupa.”

23 Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”

24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”

25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi

26 na ye yote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

Yesu Alia

28 Baada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.”

29 Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Yesu.

30 Yesu alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha.

31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.

32 Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa, alipiga magoti miguuni Pake na kusema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.”

33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana.

34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”

Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”

35 Yesu akalia machozi.

36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”

37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”

Yesu Amfufua Lazaro

38 Yesu kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa penye ingilio lake.

39 Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.” Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema,

“Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwako kaburini siku nne.”

40 Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”

41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka penye kaburi. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia.

42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”

43 Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!”

44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake.

Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”

Shauri La Kumwua Yesu

45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Yesu aliyoyatenda wakamwamini.

46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Yesu aliyoyafanya.

47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza, wakaulizana,

“Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.

48 Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”

49 Mmoja wao, aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo akasema, “Ninyi hamjui kitu cho chote!

50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”

51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama Kuhani Mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Yesu angelikufa kwa ajili ya Wayahudi,

52 wala si kwa ajili ya Wayahudi peke yao, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja.

53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamwue Yesu.

54 Kwa hiyo Yesu akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.

55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase.

56 Watu wakawa wanamtafuta Yesu, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?

57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa ye yote atakayejua mahali Yesu aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/11-7a67e15798a3eee898d09a42984b791f.mp3?version_id=1627—

Yohana 12

Maria Ampaka Yesu Mafuta Huko Bethania

1 Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi.

2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu.

3 Kisha Maria akachukua chupa ya painti mojayenye manukato ya nardosafi ya thamani kubwa akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.

4 Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,

5 “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300na fedha hizo wakapewa maskini?”

6 Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwivi, kwani ndiye aliyekuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo.

7 Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu.

8 Maskini mnao siku zote lakini mimi hamko pamoja nami siku zote.”

Shauri La Kumwua Lazaro

9 Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua.

10 Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakafanya mpango wa kumwua Lazaro pia,

11 kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake Wayahudi wengi walikuwa wanamwendea Yesu na kumwamini.

Kuingia Kwa Yesu Yerusalemu Kwa Ushindi

12 Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu.

13 Basi wakachukua matawi ya mitende wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema,

# “Hosana!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!”

14 Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa,

15 “Usiogope, Ewe binti Sayuni;

tazama, Mfalme wako anakuja,

amepanda mwana-punda!”

16 Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.

17 Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia.

18 Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda mwujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki.

19 Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lo lote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”

Yesu Anatabiri Kifo Chake

20 Basi palikuwapo Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu.

21 Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi, wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.”

22 Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.

23 Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.

24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi.

25 Mtu ye yote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata uzima wa milele.

26 Mtu ye yote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.

27 “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe na saa hii.’ Lakini, ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu.

28 Baba, litukuze jina lako.”

Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”

29 Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.”

30 Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu.

31 Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.

32 Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka katika nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.”

33 Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa.

34 Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka katika Torati kwamba ‘Kristoadumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu?’ Huyu ‘Mwana wa Adamu ni nani?’ ”

35 Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda.

36 Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.

Wayahudi Waendelea Kutokuamini

37 Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.

38 Hii ilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:

“Bwana, ni nani aliyesadiki ujumbe wetu

na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”

39 Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:

40 “Amewafanya vipofu

na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,

ili wasiweze kuona kwa macho yao,

wala kuelewa kwa mioyo yao,

wasije wakageuka, nami nikawaponya.”

41 Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake.

42 Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.

43 Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.

Amwaminiye Yesu Hatabaki Gizani

44 Yesu akapaza sauti akasema, “Ye yote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma.

45 Ye yote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma.

46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.

47 “Mimi simhukumu mtu ye yote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa.

48 Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.

49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema.

50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lo lote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/12-cc4dd27936139e631432e60f12efc92a.mp3?version_id=1627—

Yohana 13

Yesu Awanawisha Wanafunzi Wake Miguu

1 Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.

2 Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu.

3 Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu,

4 hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni.

5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”

7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”

8 Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”

Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”

9 Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”

10 Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.”

11 Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.

12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia?

13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo.

14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi.

15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi.

16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala anayetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma.

17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

18 “Sisemi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili maandiko yapate kutimia, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’

19 “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye.

20 Amin, amin, nawaambia, ye yote anayempokea yule niliyemtuma, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”

Yesu Anatabiri Kusalitiwa Kwake

21 Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22 Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani.

23 Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu.

24 Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi akamwambia, “Mwulize anamaanisha ni nani.”

25 Yule mwanafunzi akiwa amemwegemea Yesu akamwuliza, “Bwana tuambie ni nani?”

26 Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote.

27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.

Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.”

28 Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa ameketi nao chakulani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo.

29 Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini cho chote.

30 Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.

32 Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.

33 “Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja.

34 “Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane.

35 Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”

36 Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, unakwenda wapi?”

Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”

37 Petro akamwuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”

38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/13-2efb32d3d7034779a4734219846747aa.mp3?version_id=1627—

Yohana 14

Yesu Awatia Moyo Wanafunzi Wake

1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia.

2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Nakwenda kuwaandalia makao.

3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

Yesu Ndiye Njia Ya Kwenda Kwa Baba

5 Tomasi akamwam bia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”

6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”

8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”

9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu ye yote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba?’

10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi.

11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.

12 Amin, amin nawaambia, ye yote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba.

13 Nanyi mkiomba lo lote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana.

14 Kama mkiniomba lo lote kwa Jina langu nitalifanya.

Yesu Aahidi Roho Mtakatifu

15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele.

17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

18 Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.

19 Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.

20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu.

21 Ye yote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”

23 Yesu akamjibu, “Mtu ye yote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake.

24 Mtu ye yote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati nikiwa bado niko pamoja nanyi.

26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa nakwenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi.

29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini.

30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu,

31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile vile kama Baba alivyoniamuru.

“Haya inukeni; twendeni zetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/14-0e7ea4ae285c8489f93131c582f64b0e.mp3?version_id=1627—

Yohana 15

Yesu Mzabibu Wa Kweli

1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima.

2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi.

3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi.

4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.

5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lo lote.

6 Mtu ye yote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea.

7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo, nanyi mtatendewa.

8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu.

10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.

11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili.

12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi.

13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.

14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.

16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda na matunda yenu yapate kudumu, ili lo lote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape.

17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

Ulimwengu Wawachukia Wanafunzi

18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu.

19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia.

20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa, kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia.

21 Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma.

22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao.

23 Ye yote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu.

24 Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine ye yote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu.

25 Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Torati kwamba ‘Walinichukia pasipo sababu.’

26 “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.

27 Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/15-2e72bbe28130cd80e146593ab9082d85.mp3?version_id=1627—

Yohana 16

1 “Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkaiacha imani.

2 Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu ye yote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu.

3 Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi.

4 Lakini nimewaambia ninyi mambo haya, ili saa hiyo ikiwadia mpate kukumbuka ya kuwa nilikuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.

Kazi Ya Roho Mtakatifu

5 “Sasa mimi ninakwenda kwake yeye aliyenituma, lakini hakuna hata aniulizaye, ‘Unakwenda wapi?’

6 Kwa sababu nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni.

7 Lakini amin nawaambia, yafaa mimi niondoke kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu.

8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu.

9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi,

10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena,

11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

12 “Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa.

13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo.

14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.

15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.

16 “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”

Huzuni Itageuka Kuwa Furaha

17 Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’ Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninakwenda kwa Baba?’ ”

18 Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo?’ Hatuelewi hilo analosema.”

19 Yesu akatambua kuwa walitaka kumwuliza juu ya hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’

20 Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.

21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni.

22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye.

23 Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lo lote kwa Jina langu, yeye atawapa.

24 Mpaka sasa hamjaomba jambo lo lote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.

Amani Kwa Wanafunzi

25 “Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Saa yaja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nitawaeleza waziwazi kuhusu Baba.

26 Siku hiyo mtaomba kwa Jina langu. Wala sitawaambia kwamba nitamwomba Baba kwa ajili yenu,

27 kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.

28 Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni, sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”

29 Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo.

30 Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”

31 Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini?

32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi si peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami.

33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/16-3d4c134a7dd614ff1cca0e64928d2938.mp3?version_id=1627—

Yohana 17

Yesu Ajiombea Mwenyewe

1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

“Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.

2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa.

3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.

4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.

5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwako.

Yesu Awaombea Wanafunzi Wake

6 “Nimewajulisha jina lako wale ulionipa kutoka katika ulimwengu. Walikuwa wako, ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako.

7 Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako,

8 kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma.

9 Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako.

10 Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao.

11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.

12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa, ili Maandiko yapate kutimia.

13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao.

14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu.

15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.

16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu.

17 Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli.

18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo.

19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.

Yesu Awaombea Wote Wamwaminio

20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao

21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi.

22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja.

23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.

24 “Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.

25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma.

26 Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/17-89102c90f70bdc121aa055df6a76927c.mp3?version_id=1627—

Yohana 18

Yesu Akamatwa

1 Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.

2 Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Yesu alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara.

3 Hivyo Yuda akaja bustanini, akiongoza kikosi cha maaskari wa Kirumi na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo, wakiwa wamechukua taa, mienge na silaha.

4 Yesu akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”

5 Wao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”

Yesu akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.

6 Yesu alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!

7 Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?”

Nao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”

8 Yesu akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.”

9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”

10 Simoni Petro aliyekuwa na upanga akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa Kuhani Mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko.

11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

12 Hivyo wale maaskari wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Yesu na kumfunga.

13 Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule.

14 Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.

Petro Anamkana Yesu

15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Yesu. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Yesu.

16 Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani.

17 Yule msichana akamwuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?”

Petro akajibu, “Mimi sio.”

18 Wale watumishi na maaskari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.

Kuhani Mkuu Amhoji Yesu

19 Wakati huo Kuhani Mkuu akawa anamwuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.

20 Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lo lote kwa siri.

21 Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowambia. Wao wanajua niliyosema.”

22 Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa maaskari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?”

23 Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?”

24 Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.

Petro Amkana Yesu Tena

25 Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamwuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?”

Petro akakana, akasema, “Mimi sio.”

26 Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Yesu?”

27 Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati uo huo.

Yesu Apelekwa Kwa Pilato

28 Ndipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka.

29 Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”

30 Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”

31 Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”

Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu ye yote.”

32 Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.

33 Kwa hiyo Pilato akaingia ndani akamwita Yesu, akamwuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34 Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35 Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37 Pilato akamwuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni ili niishuhudie kweli. Mtu ye yote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38 Pilato akamwuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lo lote alilotenda mtu huyu.

39 Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi?’ ”

40 Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu bali tufungulie Baraba!” Basi Baraba alikuwa mnyang’anyi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/18-df17c8d27d9301c86c53de44b3c1704a.mp3?version_id=1627—

Yohana 19

Yesu Ahukumiwa Kusulibiwa

1 Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi.

2 Askari wakasokota taji ya miiba wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau.

3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.

4 Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.”

5 Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”

6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulibishe! Msulibishe!”

Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulibishe, mimi sioni hatia juu yake.”

7 Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”

8 Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi.

9 Akaingia tena ukumbini akamwuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu.

10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulibisha?”

11 Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”

12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu ye yote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”

13 Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha.

14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.

Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”

15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulibishe!”

Pilato akawauliza, “Je, nimsulibishe mfalme wenu?”

Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”

16 Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulibishe.

Kusulibiwa Kwa Yesu

Kwa hiyo maaskari wakamchukua Yesu.

17 Yesu akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa, Fuvu la Kichwa (ambapo kwa Kiebrania ni Golgotha).

18 Hapo ndipo walipomsulibisha. Pamoja naye walisulibisha watu wengine wawili, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kuume wa Yesu.

19 Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu: “YESU WA NAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.”

20 Kwa kuwa mahali hapo aliposulibiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini.

21 Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba, mtu huyu alisema, ‘Mimi ni mfalme wa Wayahudi.’ ”

22 Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”

Mavazi Ya Yesu Yagawanywa

23 Askari walipokwisha kumsulibisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini.

24 Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani alichukue.”

Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,

“Waligawana nguo zangu

na mavazi yangu wakayapigia kura.”

Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.

25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama: Maria mama yake, Maria dada wa mamaye, yaani, mke wa Klopa na Maria Magdalene.

26 Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,”

27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.

Kifo Cha Yesu

28 Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.”

29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni.

30 Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akakata roho.

Yesu Achomwa Mkuki Ubavuni

31 Kwa kuwa ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, hasa kwa kuwa hiyo Sabato ingekuwa Sikukuu. Wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulibiwa ivunjwe ili wafe haraka miili iondolewe kwenye misalaba.

32 Kwa hiyo maaskari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulibiwa pamoja na Yesu na yule mwingine pia.

33 Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake.

34 Badala yake mmoja wa wale maaskari akamchoma mkuki ubavuni na mara pakatoka damu na maji.

35 Mtu aliyeona mambo hayo ndiye aliyetoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini.

36 Kwa maana mambo haya yalitukia ili Maandiko yapate kutimia, yale yasemayo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”

37 Tena Maandiko mengine yanasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma kwa mkuki.”

Maziko Ya Yesu

38 Baada ya mambo haya, Yosefu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Yesu, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Yesu. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.

39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Yesu usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini.

40 Wakauchukua mwili wa Yesu, wakauviringishia sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi.

41 Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulibiwa, nako ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo hajazikiwa mtu bado.

42 Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Yesu humo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/19-d9d978c170a3184398315acc39607f22.mp3?version_id=1627—