Yohana 20

Kufufuka Kwa Yesu

1 Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio.

2 Hivyo akaja kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda akikimbia na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini na hatujui walikomweka!”

3 Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini.

4 Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.

5 Alipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani vilivyokuwa sanda mle ndani, lakini hakuingia.

6 Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini

7 na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda.

8 Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini,

9 (kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa yale maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu).

10 Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.

Yesu Anamtokea Maria Magdalene

11 Lakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini,

12 naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.

13 Wakamwuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”

Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.”

14 Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.

15 Yesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”

Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”

16 Yesu akamwita, “Maria!”

Ndipo Maria akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (Maana yake Mwalimu).

17 Yesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”

18 Kwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba amemweleza mambo hayo yote.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wake

19 Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walipokuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi, Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.”

20 Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.

21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.”

22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu.

23 Mkimwondolea mtu ye yote dhambi zake, zitaondolewa na ye yote mtakayemfungia dhambi zake, zitafungiwa.”

Yesu Anamtokea Tomasi

24 Lakini Tomasi, aliyeitwa Didimasi, yaani, Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja.

25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”

Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”

26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomasi alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.”

27 Kisha akamwambia Tomasi, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”

28 Tomasi akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

29 Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

Kusudi La Kitabu Hiki

30 Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki.

31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/20-fd05da40f495a12b16d9c0fa3b169ac3.mp3?version_id=1627—

Yohana 21

Yesu Awatokea Wanafunzi Saba

1 Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia. Yeye alijionyesha kwao hivi:

2 Simoni Petro, Tomasi aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja.

3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata cho chote.

4 Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.

5 Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wo wote?”

Wakamjibu, “La.”

6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.

7 Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini.

8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200.

9 Walipofika pwani, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.

10 Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”

11 Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika.

12 Yesu akawaambia, “Njoni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana.

13 Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki.

14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake tangu afufuke kutoka kwa wafu.

Yesu Amwuliza Petro Kama Anampenda

15 Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”

Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”

16 Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”

Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”

17 Kwa mara ya tatu Yesu akamwuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”

Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimwuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.

18 Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.”

19 Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”

20 Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”)

21 Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamwuliza Yesu, “Bwana na huyu je?”

22 Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!”

23 Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”

24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.

25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/21-b0021db52803958ee319b2013164a268.mp3?version_id=1627—

Luka 1

1 Kwa kuwa, watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotukia katikati yetu,

2 kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale ambao walikuwa mashahidi walioona na watumishi wa Bwana,

3 mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo ewe mtukufu Theofilo,

4 ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.

Kuzaliwa Kwa Yohana Mbatizaji Kwatabiriwa

5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni.

6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama.

7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.

8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu,

9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba.

10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.

11 Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria.

12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana akajawa na hofu.

13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana.

14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.

15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji cho chote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.

16 Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao.

17 Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki na kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”

18 Zekaria akamwuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”

19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema.

20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”

21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni.

22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.

23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake.

24 Baada ya muda si mrefu Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.

25 Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”

Kuzaliwa Kwa Yesu Kwatabiriwa

26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti,

27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria.

28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”

29 Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?”

30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu.

31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume na utamwita jina lake Yesu.

32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake.

33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34 Maria akamwuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli, kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.

36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa.

37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akamwacha.

Maria Aenda Kumtembelea Elizabeti

39 Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi.

40 Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti.

41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu,

42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa.

43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?

44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha.

45 Amebarikiwa yeye aliye amini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”

Wimbo Wa Maria Wa Sifa

46 Naye Maria akasema:

“Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

47 nayo roho yangu inamfurahia

Mungu Mwokozi wangu,

48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

unyonge wa mtumishi wake,

hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita mbarikiwa,

49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu

amenitendea mambo ya ajabu,

jina lake ni takatifu.

50 Rehema zake huwaendea wale wamchao,

kutoka kizazi hadi kizazi.

51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake;

amewatawanya wale wenye kiburi

ndani ya mioyo yao.

52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi,

lakini amewainua wanyenyekevu.

53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri

bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.

54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli,

kwa kumbuka ahadi yake ya kumrehemu

55 Abrahamu na uzao wake milele,

kama alivyowaahidi baba zetu.”

56 Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa Kwa Yohana Mbatizaji

57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume.

58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.

59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake.

60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”

61 Wakamwambia, “Hakuna mtu ye yote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”

62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani.

63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.”

64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.

65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote.

66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Unabii Wa Zekaria

67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:

68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

69 Naye ametusimamishia pembeya wokovu

katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii

wake watakatifu tangu zamani,

71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu

na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:

72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu

na kukumbuka Agano lake takatifu,

73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:

74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,

tupate kumtumikia yeye pasipo hofu

75 katika utakatifu na haki mbele zake,

siku zetu zote.

76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;

kwa kuwa utamtangulia Bwana

na kuandaa njia kwa ajili yake,

77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu

utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,

78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,

nuru itokayo juu itatuzukia

79 ili kuwaangazia wale waishio gizani

na katika uvuli wa mauti,

kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”

80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/1-4ae61a593e9d6eee3074c0979e0e0c47.mp3?version_id=1627—

Luka 2

Kuzaliwa Kwa Yesu

1 Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Kirumi.

2 (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alipokuwa mtawala wa Shamu).

3 Kila mtu alikwenda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.

4 Hivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi.

5 Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito.

6 Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia,

7 naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.

Wachungaji Na Malaika

8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku.

9 Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawang’aria kotekote, wakaingiwa na hofu.

10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote.

11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye KristoBwana.

12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ng’ombe.”

13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni

na duniani iwe amani

kwa watu aliowaridhia.”

15 Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao wakisema, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”

16 Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ng’ombe.

17 Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyu mtoto.

18 Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo.

19 Lakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari.

20 Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.

21 Hata zilipotimia siku nane, ulikuwa ndio wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilokuwa amepewa na malaika kabla hajatungwa mimba.

Yesu Apelekwa Hekaluni

22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria, kwa mujibu wa Sheria ya Mose, Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana,

23 (kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”),

24 pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa, katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.”

25 Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.

26 Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristowa Bwana.

27 Simeoni akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria,

28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:

29 “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,

sasa wamruhusu mtumishi wako

aende zake kwa amani.

30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,

31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,

32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu Mataifa

na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”

33 Naye Yosefu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto.

34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake,

35 ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike na upanga utauchoma moyo wako.”

36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke mzee sana, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana, naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa.

37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba.

38 Wakati uo huo, Ana alikuja akaanza kusifu akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

39 Yosefu na Maria walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya.

40 Naye mtoto Yesu akakua na kuongezeka nguvu akiwa amejaa hekima na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Kijana Yesu Hekaluni

41 Kila mwaka Yosefu na Maria mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

42 Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.

43 Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yosefu na Maria mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua.

44 Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa zao na marafiki.

45 Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta.

46 Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa Sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.

47 Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa na majibu aliyoyatoa.

48 Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamwuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”

49 Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”

50 Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.

51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtii kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.

52 Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/2-be043f2bc18fbf40da595955667bbfae.mp3?version_id=1627—

Luka 3

Yohana Mbatizaji Aanza Kuhubiri

1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti na Lisania akiwa mfalme wa Abilene,

2 Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, ndipo neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko nyikani.

3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Sauti ya mtu aliaye nyikani,

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyosheni mapito yake,

5 kila bonde litajazwa,

kila mlima na kilima kitasawazishwa.

Njia zilizopinda zitanyooshwa,

zilizoparuza zitasawazishwa.

6 Nao watu wote watauona

wokovu wa Mungu.’ ”

7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Enyi uzao wa nyoka! Ni nani aliyewaonya mwikimbie ghadhabu ijayo?

8 Zaeni matunda yafananayo na toba yenu. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa ninyi ni uzao wa Abrahamu. Kwa maana nawaambia, Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya.

9 Hata sasa shoka limekwisha wekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

10 Ule umati wa watu ukamwuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”

11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamwuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”

13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”

14 Askari nao wakamwuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”

Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”

15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo.

16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi ambaye sistahili hata kufungua kamba ya viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwahubiri watu Habari Njema.

19 Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia mke wa ndugu yake na maovu mengine aliyokuwa amefanya,

20 Herode akijumlisha haya yote, akamfunga Yohana gerezani.

Kubatizwa Kwa Bwana Yesu

21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka.

22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua na sauti ikaja kutoka mbinguni ikisema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa nawe sana.”

Ukoo Wa Bwana Yesu

23 Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu,

Yosefu alikuwa mwana wa Eli,

24 Eli alikuwa mwana wa Mathati,

Mathati alikuwa mwana wa Lawi,

Lawi alikuwa mwana wa Melki,

Melki alikuwa mwana wa Yanai,

Yanai alikuwa mwana wa Yosefu,

25 Yosefu alikuwa mwana wa Matathia,

Matathia alikuwa mwana wa Amosi,

Amosi alikuwa mwana wa Nahumu,

Nahumu alikuwa mwana wa Esli,

Esli alikuwa mwana wa Nagai,

26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi,

Maathi alikuwa mwana wa Matathia,

Matathia alikuwa mwana Semeini,

Semeini alikuwa mwana wa Yoseki,

Yoseki alikuwa mwana wa Yoda,

27 Yoda alikuwa mwana wa Yoanani,

Yoanani alikuwa mwana wa Resa,

Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli,

Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli,

Shealtieli alikuwa mwana wa Neri,

28 Neri alikuwa mwana wa Melki,

Melki alikuwa mwana wa Adi,

Adi alikuwa mwana wa Kosamu,

Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,

Elmadamu alikuwa mwana wa Eri,

29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua,

Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri,

Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu,

Yorimu alikuwa mwana wa Mathati,

Mathati alikuwa mwana wa Lawi,

30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni,

Simeoni alikuwa mwana wa Yuda,

Yuda alikuwa mwana wa Yosefu,

Yosefu alikuwa mwana wa Yonamu,

Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu,

Eliyakimu alikuwa mwana wa Melea,

31 Melea alikuwa mwana wa Mena,

Mena alikuwa mwana wa Matatha,

Matatha alikuwa mwana wa Nathani,

Nathani alikuwa mwana wa Daudi,

32 Daudi alikuwa mwana wa Yese,

Yese alikuwa mwana wa Obedi,

Obedi alikuwa mwana wa Boazi,

Boazi alikuwa mwana wa Salmoni,

Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni,

33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu,

Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu,

Aramu alikuwa mwana wa Hesroni,

Hesroni alikuwa mwana wa Peresi,

Peresi alikuwa mwana wa Yuda,

34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo,

Yakobo alikuwa mwana wa Isaki,

Isaki alikuwa mwana wa Abrahamu,

Abrahamu alikuwa mwana wa Tera,

Tera alikuwa mwana wa Nahori,

35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi,

Serugi alikuwa mwana wa Reu,

Reu alikuwa mwana wa Pelegi,

Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,

Eberi alikuwa mwana wa Sala,

36 Sala alikuwa mwana wa Kenani,

Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi,

Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu,

Shemu alikuwa mwana wa Noa,

Noa alikuwa mwana wa Lameki,

37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela,

Methusela alikuwa mwana wa Enoki,

Enoki alikuwa mwana wa Yaredi,

Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli,

Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani,

38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi,

Enoshi alikuwa mwana wa Sethi,

Sethi alikuwa mwana wa Adamu,

Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/3-4f24e97fdb3888418e406480ddd41e65.mp3?version_id=1627—

Luka 4

Yesu Ajaribiwa Na Shetani

1 Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi jangwani,

2 mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula cho chote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.

3 Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”

4 Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno la Mungu.’ ”

5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja.

6 Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa ye yote ninayetaka.

7 Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”

8 Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ”

9 Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu mwembamba wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa,

10 kwa maana imeandikwa:

“ ‘Atakuagizia malaika zake

ili wakulinde;

11 nao watakuchukua mikononi mwao

usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

12 Yesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

13 Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.

Mwanzo Wa Huduma Ya Galilaya

14 Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando.

15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao na kila mmoja akamsifu.

Kukataliwa Kwa Yesu

16 Yesu akaenda Nazareti, hapo alipolelewa na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome,

17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:

18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

kwa sababu amenitia mafuta

kuwaletea maskini habari njema.

Amenituma kuwatangazia wafungwa

kufunguliwa kwao

na vipofu kupata kuona tena,

kuwaweka huru wanaoonewa

19 na kutangaza mwaka wa Bwana

uliokubalika.”

20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.

21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo maandiko haya yametimia mkiwa mnasikia.”

22 Wote waliokuwako wakamsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”

23 Yesu akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii, ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ”

24 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika kwenye mji wake mwenyewe.

25 Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Eliya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima.

26 Hata hivyo Eliya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.

27 Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Elisha, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.”

28 Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana.

29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima mahali ambapo mji huo ulikuwa umejengwa, ili wamtupe chini kutoka kwenye mtelemko mkali.

30 Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya huo umati wa watu akaenda zake.

Yesu Atoa Pepo Mchafu

31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.

32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.

33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, akapiga kelele kwa nguvu akisema,

34 “Tuache! Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”

35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza na umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha chini yule mtu mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.

36 Watu wote wakashangaa wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Kwa mamlaka na nguvu, anawaamuru pepo wachafu, nao wanatoka!”

37 Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.

Yesu Awaponya Wengi

38 Yesu akatoka kwenye sinagogi akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mkwewe Simoni ana homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie.

39 Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile akaanza kuwahudumia.

40 Jua lilipokuwa linatua, watu wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali wakawaleta kwa Yesu, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, akawaponya.

41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ni Kristo.

42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke.

43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”

44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/4-74d9ef592c42d3263c1c569544d928cf.mp3?version_id=1627—

Luka 5

Kuitwa Kwa Wanafunzi Wa Kwanza

1 Siku moja Yesu alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu,

2 akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao.

3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka pwani. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua cho chote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

6 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika.

7 Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.

8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu, mimi ni mtu mwenye dhambi!”

9 Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata,

10 vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani, Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo walishangazwa pia.

Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”

11 Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.

Yesu Amtakasa Mtu Mwenye Ukoma

12 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Yesu, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi na kumsihi akisema, “Bwana, ukitaka waweza kunitakasa.”

13 Yesu akanyosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka, takasika!” Naye mara ukoma ukapona.

14 Yesu akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu ye yote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe dhabihu alizoagiza Mose ili kuwa ushuhuda kwao.”

15 Lakini habari zake Yesu zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wo wote, makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.

16 Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.

Yesu Amponya Mtu Mwenye Kupooza

17 Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa.

18 Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu.

19 Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya vigae, wakapata nafasi ya kumtelemsha yule mgonjwa kwa mkeka wake katikati ya ule umati pale pale mbele ya Yesu.

20 Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”

21 Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya makufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

22 Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza haya mioyoni mwenu?

23 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia huyu, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, uende?’

24 Lakini ili mpate kujua ya kuwa Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi,” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, Simama, chukua mkeka wako uende nyumbani kwako.”

25 Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu.

26 Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”

Yesu Amwita Lawi

27 Baada ya haya Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kukusanyia kodi, akamwambia, “Nifuate.”

28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.

29 Kisha Lawi akamfanyia Yesu karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao.

30 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria ambao walikuwa wa madhehebu yao wakawalalamikia wanafunzi wa Yesu, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”

31 Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa.

32 Sikuja kuwaita wenye haki bali wenye dhambi wapate kutubu.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

33 Wakamwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

34 Yesu akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati akiwa pamoja nao?

35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, ndipo watakapofunga.”

36 Yesu akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo kuukuu. Akifanya hivyo atakuwa amechana nguo mpya na kile kiraka hakitaendana na ile nguo kuukuu.

37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itapasua hivyo viriba nayo yote itamwagika.

38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya.

39 Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/5-6c2cb629135db07e54ef56e942dbd4a5.mp3?version_id=1627—

Luka 6

Bwana Wa Sabato

1 Ikawa siku moja ya Sabato Yesu alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake.

2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo ambayo ni kinyume na sheria siku ya Sabato?”

3 Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamkusoma jinsi alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walipokuwa na njaa?

4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua ile mikate mitakatifu ambayo huliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake wakala!”

5 Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

6 Ikawa siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia ndani ya sinagogi akawa anafundisha, huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.

7 Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, hivyo wakawa wanamwangalia kwa karibu ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato.

8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.

9 Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, akisema, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kutenda mema au kutenda mabaya? Kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyosha mkono wako!” Akaunyosha na mkono wake ukawa tena mzima kabisa.

11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao, ni nini watakachomtendea Yesu.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

12 Ikawa katika siku hizo Yesu alikwenda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu.

13 Kulipopambazuka akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume:

14 Simoni aliyemwita Petro, Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartolomayo,

15 Mathayo, Tomasi. Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote,

16 Yuda mwana wa Yakobo na Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Yesu Aponya Wengi

17 Akashuka pamoja nao akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni,

18 waliokuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya.

19 Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.

Baraka Na Ole

20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

“Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

kwa sababu Ufalme wa Mbinguni ni wenu.

21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

kwa sababu mtashibishwa.

Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

kwa sababu mtacheka.

22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,

watakapowatenga na kuwatukana

na kulikataa jina lenu kama neno ovu,

kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,

kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.

25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,

maana mtaona njaa.

Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,

maana mtaomboleza na kulia.

26 Ole wenu watu watakapowasifu,

kwani ndivyo baba zao walivyowasifu

manabii wa uongo.

Wapendeni Adui Zenu

27 “Lakini nawaambia wale wanaonisikia, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia.

28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya.

29 Kama mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang’anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia.

30 Mpe kila akuombaye na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.

31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.

33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo.

34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha wenye dhambi wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote.

35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na waovu.

36 Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Kuwahukumu Wengine

37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

39 Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni?

40 Mwanafunzi hamzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

41 “Mbona unatazama kibanzi kilichoko ndani ya jicho la mwenzako nawe huoni boriti iliyoko ndani ya jicho lako?

42 Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, niache nikitoe hicho kibanzi kilichoko ndani ya jicho lako’, wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyoko ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa kwanza boriti ndani ya jicho lako, ndipo utakapoweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilichoko ndani ya jicho la ndugu yako.

Mti Na Mazao Yake

43 “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri.

44 Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba wala zabibu kwenye michongoma.

45 Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo mabaya kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.

Mjenzi Mwenye Busara Na Mjenzi Mpumbavu

46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia?

47 Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda.

48 Yeye ni kama mtu anayejenga nyumba, akachimba chini sana na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yakaipiga ile nyumba lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri juu ya mwamba.

49 Lakini yeye ayasikiaye maneno yangu na asiyatende ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya mchanga bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/6-e7ebcbfbee6a8349555d7a0f68c211ea.mp3?version_id=1627—

Luka 7

Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari

1 Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu.

2 Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa.

3 Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari.

4 Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili,

5 kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.”

6 Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu.

7 Ndiyo maana sikujiona ninastahili hata kuja kwako. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.

8 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na huyu, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hili,’ yeye hufanya.”

9 Yesu aliposikia maneno haya alimshangaa sana, akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”

10 Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.

Yesu Amfufua Mwana Wa Mjane

11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye.

12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke.

13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”

14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.”

15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.

16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”

17 Habari hizi za mambo aliyofanya Yesu zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani.

Yesu Na Yohana Mbatizaji

18 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili

19 na kuwatuma kwa Bwana ili kumwuliza, “Je, wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”

20 Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Je, wewe ndiye yule ajaye au tumtazamie mwingine?’ ”

21 Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, pia akawafungua vipofu wengi macho wakaona.

22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mliyoyaona na kuyasikia. Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wahubiriwa Habari Njema.

23 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa nami.”

24 Wanafunzi wa Yohana walipoondoka, Yesu akaanza kuuambia ule umati wa watu kuhusu Yohana: “Mlipokwenda nyikani mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?

25 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya fahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya fahari na kuishi maisha ya anasa hukaa katika majumba ya kifalme.

26 Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam! Nawaambia, tena zaidi ya nabii.

27 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie,

atakayeandaa njia mbele yako.’

28 Nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na mwanamke, hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini yeye aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”

29 (Watu wote hata watoza ushuru waliposikia maneno ya Yesu, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni mwema, maana walikuwa wamebatizwa na Yohana.

30 Lakini Mafarisayo na wataalamu wa sheria walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokukubali kubatizwa na Yohana.)

31 Yesu akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini?

32 Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao wakisema:

“ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza,

tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,

lakini hamkulia.’

33 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuwa hali mkate wala hanywi divai, ninyi mkasema, ‘Ana pepo mchafu,’

34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Mtazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’

35 Nayo hekima imethibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”

Yesu Apakwa Mafuta Na Mwanamke Mwenye Dhambi

36 Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani.

37 Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marmar yenye manukato.

38 Yule mwanamke akiwa amesimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake akaibusu na kuimiminia manukato.

39 Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”

40 Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.”

Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”

41 “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500na mwingine dinari hamsini.

42 Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?”

43 Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.”

Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”

44 Kisha akamgeukia yule mwanamke akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake na kunifuta kwa nywele zake.

45 Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia.

46 Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato.

47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako simesamehewa.”

49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

50 Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/7-e68891695445d36e3d157be85994235a.mp3?version_id=1627—

Luka 8

Mfano Wa Mpanzi

1 Baada ya haya Yesu alikwenda akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,

2 pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba,

3 Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode, Susana na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

4 Wakati umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka mji hadi mji, akawaambia mfano huu:

5 “Mpanzi alitoka kwenda kusia mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, zikakanyagwakanyagwa na ndege wa angani wakazila.

6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.

7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, ile miiba ikakua pamoja nazo na kusonga hiyo mimea ikafa.

8 Mbegu nyingine zilianguka penye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia zaidi ya mbegu alizopanda.”

Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti akasema, “Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

9 Wanafunzi wake wakamwuliza maana ya mfano huu.

10 Naye akasema, “Ninyi mmejaliwa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,

“ ‘ingawa wanaona, wasione;

ingawa wanasikia, wasielewe.’

11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.

12 Zile zilizoanguka kando ya njia, ni wale ambao husikia neno na ibilisi huja na kuliondoa kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.

13 Zile za kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa kitambo kidogo, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.

14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.

15 Lakini zile mbegu kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu na wa utii, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

Mfano Wa Taa

16 “Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga.

17 Kwa maana hakuna jambo lo lote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lo lote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.

18 Kwa hiyo, iweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana ye yote aliye na kitu atazidishiwa na ye yote asiye nacho, hata kile anachodhani anacho atanyang’anywa.”

Mama Yake Yesu Na Ndugu Zake

19 Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.

20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”

21 Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

Yesu Atuliza Dhoruba

22 Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Twendeni tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa.”

23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.

24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakipiga kelele, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!”

Yeye akaamka akaukemea ule upepo na yale mawimbi, vikakoma, pakawa shwari.

25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”

Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni mtu wa namna gani ambaye anaamuru hata upepo na maji navyo vikamtii?”

Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo Mchafu

26 Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, ambayo iko upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya,

27 Yesu aliposhuka katika mashua na kukanyaga pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali makaburini.

28 Alipomwona Yesu alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”

29 Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.

30 Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?”

# Akamjibu, “Legioni,”kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda Shimoni.

32 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo karibu wakilisha kandokando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.

33 Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemkia gengeni likatumbukia ziwani na kuzama.

34 Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.

35 Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa sana.

36 Wale walioona mambo hayo wakawaeleza wenzao jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.

37 Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua akaondoka zake.

38 Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Yesu afuatane naye, lakini Yesu akamuaga, akamwambia:

39 “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu Yesu aliyomtendea.

Msichana Afufuliwa Na Mwanamke Aponywa

40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea.

41 Kisha mtu mmoja jina lake Yairo, kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake,

42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.

Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.

43 Katika umati huo alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna ye yote aliyeweza kumponya.

44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma na kugusa upindo wa vazi la Yesu, mara kutokwa damu kwake kukakoma.

45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”

Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”

46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”

47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu, akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara.

48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”

50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope, amini tu, naye binti yako atapona.”

51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu ye yote aingie ndani pamoja naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, baba na mama wa yule binti.

52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa ila amelala.”

53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa.

54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!”

55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara. Akaamuru apewe kitu cho chote cha kula.

56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote juu ya yale yaliyotukia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/8-229bb434a8336977af1bb3901b8b96f4.mp3?version_id=1627—