Luka 9

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

1 Yesu akiisha kuwaita wale kumi na wawili pamoja, aliwapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote,

2 kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

3 Akawaagiza akisema, “Msichukue cho chote safarini, wala fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala msichukue kanzu ya ziada.

4 Katika nyumba yo yote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.

5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kung’uteni mavumbi miguuni mwenu kuwa ushuhuda dhidi yao.”

6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

7 Basi Herode mtawala wa Galilaya akasikia habari za yote yaliyotendeka, naye akafadhaika kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuka.

8 Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine wakasema kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.

9 Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani basi huyu ambaye ninasikia habari zake kuhusu mambo kama haya?” Akatamani sana kumwona.

Yesu Awalisha Watu 5,000

10 Wale mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida.

11 Lakini umati wa watu ulipofahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakamjia Yesu na kumwambia, “Uage umati huu wa watu uondoke ili uweze kwenda kwenye vijiji vya karibu na sehemu za jirani, ili kupata chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”

13 Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wao wakasema, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, labda tuende tukanunue chakula cha kuwatosha watu wote hawa.”

14 Kwa kuwa walikuwako wanaume wapatao 5,000.

Yesu akawaambia wanafunzi wake, “waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.”

15 Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.

16 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega, kisha akawapa wanafunzi wake waugawie ule umati wa watu.

17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyobaki, vikajaa vikapu kumi na viwili.

Petro Amkiri Bwana Yesu Kuwa Ndiye Kristo

18 Wakati mmoja, Yesu alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

19 Wakamjibu, “Wengine husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na wengine husema, wewe ni mmoja wa nabii wa kale aliyefufuka kutoka kwa wafu.”

20 Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

# Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristowa Mungu.”

21 Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote jambo hilo.

22 Yesu akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, naye atauawa na siku ya tatu atafufuka.”

23 Kisha akawaambia wote, “Ye yote anayetaka kunifuata ni lazima ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake kila siku na anifuate.

24 Kwa maana ye yote atakayekuyaponya maisha yake atayapoteza, lakini ye yote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.

25 Je, itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?

26 Kama mtu ye yote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea aibu mtu huyo atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu.

27 Amin, amin nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti mpaka watakapouona Ufalme wa Mungu.”

Bwana Yesu Abadilika Sura

28 Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana akaenda nao mlimani kuomba.

29 Alipokuwa akiomba, mwonekano wa sura yake ukabadilika, mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi.

30 Ghafula wakawaona watu wawili, Mose na Eliya wakizungumza naye.

31 Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu.

32 Petro na wenzake waliokuwa wamelala usingizi mzito walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.

33 Mose na Eliya, walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho.

34 Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu.

35 Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa niliyemchagua, msikilizeni yeye.”

36 Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu ye yote yale waliyokuwa wameyaona.

Kuponywa Kwa Kijana Mwenye Pepo Mchafu

37 Kesho yake, waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu.

38 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akapiga kelele, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, ndiye mtoto wangu wa pekee.

39 Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige kelele, kisha humwangusha na kumtia kifafa akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana na hamwachi ila mara chache.

40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

41 Yesu akajibu akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Mlete mwanao hapa.”

42 Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, akamrudisha kwa baba yake.

43 Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, yeye akawaambia wanafunzi wake:

44 “Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.”

45 Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumwuliza maana yake.

Ni Nani Atakayekuwa Mkubwa Kuliko Wote

46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote.

47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake.

48 Kisha akawaambia, “Ye yote atakayemkaribisha mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, atakuwa amenikaribisha mimi na ye yote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma, kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

49 Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

50 Yesu akasema, “Msimzuie, kwa sababu ye yote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”

Yesu Akataliwa Samaria

51 Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu.

52 Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu,

53 lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anakwenda zake Yerusalemu.

54 Wanafunzi wake, yaani, Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema: “Bwana, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?”

55 Yesu akageuka na kuwakemea,

56 nao wakaenda kijiji kingine.

Gharama Ya Kumfuata Yesu

57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata ko kote uendako.”

58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”

Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niache kwanza nikamzike baba yangu.”

60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”

61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikaage jamaa yangu.”

62 Yesu akamwambia, “Mtu ye yote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/9-d52862eaa4c999f7c98a7cdf165e1202.mp3?version_id=1627—

Luka 10

Yesu Awatuma Wale Sabini Na Wawili

1 Baada ya hayo, Yesu akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda yeye mwenyewe.

2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, awapeleke watenda kazi katika shamba lake.

3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu.

4 Msichukue mkoba wala mfuko, wala viatu na msimsalimu mtu ye yote njiani.

5 “Mkiingia katika nyumba yo yote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’

6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake, la sivyo itawarudia.

7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtenda kazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.

8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni cho chote kiwekwacho mbele yenu,

9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’

10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:

11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakung’uta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’

12 Ninawaambia, hukumu ya Mungu katika Sodoma itavumilika zaidi kuliko ya mji ule.

Ole Wa Miji Isiyotubu

13 “Ole wako Korazini! Ole wake Bethsaida! Kwa kuwa miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika Tiro na Sidoni, ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

14 Lakini itavumilika zaidi Tiro na Sidoni katika hukumu kuliko kwenu.

15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”

16 “Yeye awasikilizaye ninyi, anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi, amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi.

19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui, wala hakuna kitu cho chote kitakachowadhuru kwa namna yo yote.

20 Basi msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Yesu Anashangilia

21 Saa ile ile, Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu akasema, “Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa sababu mambo haya umewaficha wenye hekima na wenye akili, nawe umewafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hayo ndiyo yaliyokuwa mapenzi yako.

22 “Vitu vyote vimekabidhiwa mkononi mwangu na Baba. Wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”

23 Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Yamebarikiwa macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.

24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona mnayoyaona, lakini hawakuyaona, pia kusikia mnayoyasikia, lakini hawakuyasikia.”

Mfano Wa Msamaria Mwema

25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate kurithi uzima wa milele?”

26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”

27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote, tena mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

29 Lakini yule mtaalamu wa sheria akitaka kuonyesha kuwa mwenye haki, akamwuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”

30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akitelemka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi, wakampiga, wakaondoka, wakamwacha karibu ya kufa.

31 Kwa bahati nzuri kuhani mmoja alikuwa anapitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.

32 Vivyo hivyo Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani

33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri kupitia njia hiyo alipomwona, alimhurumia,

34 akamwendea, akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake akamleta mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.

35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbiliakampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yo yote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu, wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?”

37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

Yesu Awatembelea Martha Na Maria

38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake.

39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye yeye aliketi chini miguuni mwa Yesu akisikiliza yale aliyokuwa akisema.

40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumwuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?

42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/10-f3a38dcbd98e2f9503d5ed7407c6a358.mp3?version_id=1627—

Luka 11

Yesu Afundisha Wanafunzi Wake Kuomba

1 Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tufundishe kuomba, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.”

2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni hivi:

“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

jina lako litukuzwe,

Ufalme wako uje.

3 Utupatie kila siku riziki zetu.

4 Utusamehe dhambi zetu,

kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.

Wala usitutie majaribuni,

bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu.’ ”

5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu.

6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’

7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe cho chote.’

8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.

9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni, nanyi mtafunguliwa mlango.

10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa, naye kila atafutaye hupata na kila abishaye hufunguliwa mlango.

11 “Je, kuna ye yote miongoni mwenu, ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala ya samaki?

12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge?

13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

Yesu Na Beelzebuli

14 Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa.

15 Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebubu, yule mkuu wa pepo wachafu wote.”

16 Wengine ili kumjaribu wakataka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

17 Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia, nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe huanguka.

18 Kama Shetani amegawanyika mwenyewe ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli.

19 Kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao watakuwa mahakimu wenu.

20 Lakini ikiwa ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia.

21 “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha, anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama.

22 Lakini mtu mwenye nguvu zaidi kuliko yeye amshambuliapo na kumshinda, humnyang’anya silaha zake zote alizozitegemea na kuchukua nyara.

23 “Mtu ye yote ambaye hayuko pamoja nami, yu kinyume changu na mtu ye yote asiyekusanya pamoja nami, hutapanya.

Kurudi Kwa Pepo Mchafu

24 “Pepo mchafu amtokapo mtu, huzungukazunguka sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini asipopata mahali po pote husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’

25 Arudipo na kuikuta ile nyumba imefagiliwa na kupambwa vizuri,

26 ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”

27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

Ishara Ya Yona

29 Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kufundisha akisema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ile ya Yona.

30 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi cha sasa.

31 Siku ya hukumu, Malkia wa Kusini atainuka pamoja na watu wa kizazi hiki akiwahukumu kwa sababu yeye alisafiri kutoka mbali kuja kusikiliza hekima ya Solomoni. Lakini sasa, yeye aliye mkuu kuliko Solomoni yuko hapa.

32 Siku ile ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu kwa sababu wao walitubu walipomsikia Yona akihubiri. Lakini sasa, yeye aliye mkuu kuliko Yona yuko hapa.

Taa Ya Mwili

33 “Hakuna mtu ye yote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru.

34 Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote umejaa giza.

35 Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyoko ndani yako isiwe giza.

36 Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yo yote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”

Yesu Awashutumu Mafarisayo Na Wanasheria

37 Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimkaribisha nyumbani kwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani.

38 Yule Farisayo akashangaa kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula.

39 Ndipo Bwana akamwambia, “Enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa choyo na uovu.

40 Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye aliyetengeneza na ndani pia?

41 Basi toeni sadaka vile mlivyo navyo na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.

42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kutoa matoleo hayo, wala msisahau kufanya hayo mengine.

43 “Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kuketi viti vya mbele katika masinagogi na kusalimiwa kwa heshima masokoni.

44 “Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”

45 Mtaalamu mmoja wa sheria akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Nanyi wataalamu wa sheria, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.

47 “Ole wenu, kwa sababu ninyi mnawajengea makaburi manabii waliouawa na baba zenu.

48 Hivyo ninyi ni mashahidi na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya, wao waliwaua manabii, nanyi mnawatengenezea makaburi.

49 Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’

50 Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ile ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu,

51 tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zekaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.

52 “Ole wenu ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”

53 Yesu alipoondoka huko, walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali,

54 wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/11-a66d3e7d1fd97cdc08310a982c7537ca.mp3?version_id=1627—

Luka 12

Maonyo Dhidi Ya Unafiki

1 Wakati huo, umati mkubwa wa watu kwa maelfu, walipokuwa wamekusanyika, hata wakawa wanakanyagana, Yesu akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao.

2 Hakuna jambo lo lote lililositirika ambalo halitafunuliwa au lililofichwa ambalo halitajulikana.

3 Kwa hiyo, lo lote mlilosema gizani litasikiwa nuruni na kile mlichonong’ona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.

4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili na baada ya hilo hawawezi kufanya lo lote zaidi.

5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia mwogopeni huyo!

6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao.

7 Naam, hata idadi ya nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa. Kwa hiyo msiogope, ninyi ni wa thamani kuliko mashomoro wengi.

8 “Ninawaambia kwamba, ye yote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu.

9 Lakini yeye atakayenikana mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.

10 Naye kila atakaye nena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini ye yote atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11 “Watakapowapeleka katika masinagogi mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema:

12 Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Mfano Wa Tajiri Mpumbavu

13 Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”

14 Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?”

15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana.

17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu.

19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika, ule, unywe, ufurahi.” ’

20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

Msiwe Na Wasiwasi

22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo ninawaambia, msisumbukie maisha yenu, kwamba mtakula nini, au miili yenu kwamba mtavaa nini.

23 Maisha ni zaidi ya chakula na mwili ni zaidi ya mavazi.

24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala po pote pa kuhifadhi nafaka, lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni bora kuliko ndege!

25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kusumbuka anaweza kujiongeza maisha yake hata kwa saa moja?

26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafumi wala hayasokoti, lakini ninawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo.

28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani ambayo leo yapo kesho yanatupwa motoni, si zaidi sana atawavika ninyi enyi wa imani haba!

29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya.

30 Watu wasiomjua Mungu husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote. Naye Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnavihitaji.

31 Bali utafuteni Ufalme wa Mungu na vitu hivyo vyote atawapatia pia.

Utajiri Wa Mbinguni

32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme.

33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwivi hakaribii wala nondo haharibu.

34 Kwa maana hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwa pia.

Kukesha

35 “Iweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka,

36 kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka kwenye karamu ya arusi, ili ajapo na kugonga mlango waweze kumfungulia mara.

37 Heri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia.

38 Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja mnamo usiku wa manane, au karibu na mapambazuko.

39 Lakini fahamuni jambo hili kwamba: Kama mwenye nyumba angalijua ni saa ipi mwivi atakapokuja, asingaliacha nyumba yake kuvunjwa.

40 Ninyi nanyi imewapasa kuwa tayari saa zote, kwa maana Mwana wa Adamu atakuja saa ambayo hamumtarajii.”

Mtumishi Mwaminifu Na Yule Asiye Mwaminifu

41 Ndipo Petro akamwuliza, “Bwana, mfano huu unatuambia sisi peke yetu au watu wote?”

42 Yesu akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya nyumba yake yote, naye awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa?

43 Itakuwa ni furaha kwa mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.

44 Amin nawaambia, atampa mamlaka juu ya vyote alivyo navyo.

45 Lakini ikiwa yule mtumishi atawaza moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike na kula na kunywa na kulewa,

46 bwana wake yule mtumwa atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Huyo bwana wake atamkata vipande vipande na kumwekea fungu lake pamoja na wale wasio waaminifu.

47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi.

48 Lakini ye yote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa atapigwa kidogo. Ye yote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi na ye yote aliyekabidhiwa vingi kwake vitatakiwa vingi.

Sikuleta Amani Bali Mafarakano

49 “Nimekuja kuleta moto duniani, laiti kama ungekuwa tayari umewashwa!

50 Lakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu mpaka ubatizo huo ukamilike!

51 Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano.

52 Kuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili na wawili dhidi ya watatu.

53 Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, mama mkwe dhidi ya mkwewe. Naye mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”

Kutambua Majira

54 Pia Yesu akauambia ule umati wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha.

55 Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo.

56 Enyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa?

57 “Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki?

58 Uwapo njiani na adui yako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani.

59 Nawaambia, hautatoka humo hadi ulipe senti ya mwisho.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/12-40aae8bdd940f94e810371a998b38991.mp3?version_id=1627—

Luka 13

Tubu, La Sivyo Utaangamia

1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa.

2 Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo wao walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote?

3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.

4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu, mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu?

5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”

Mfano Wa Mti Usiozaa Matunda

6 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja.

7 Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’

8 “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea.

9 Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo ukate.’ ”

Yesu Amponya Mwanamke Kilema Siku Ya Sabato

10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato.

11 Wakati uo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyoka wima.

12 Yesu alipomwona, akamwita akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.”

13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.

14 Lakini mkuu wa sinagogi, akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Kwa hiyo mkuu wa sinagogi akaendelea kuuambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi, katika siku hizo, njoni mponywe, lakini si kuja kuponywa siku ya Sabato.”

15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng’ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato?

16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka katika kifungo hicho siku ya Sabato?”

17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.

Mfano Wa Punje Ya Haradali

18 Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini?

19 Umefanana na punje ya haradali ambayo ni ndogo sana, ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti na ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

20 Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini?

21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua na kuichanganya kwenye vipimo vitatuvya unga hadi wote ukawa umeumuka.”

Mlango Mwembamba

22 Yesu akapita katika miji na vijiji akifundisha wakati akisafiri kwenda Yerusalemu.

23 Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”

24 Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana, nawaambia, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza.

25 Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkigonga mlango na kusema, ‘Bwana, utufungulie mlango.’

“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako.’

26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’

27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako. Ondokeni kwangu ninyi watenda maovu!’

28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapomwona Abrahamu, Isaki na Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.

29 Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu.

30 Tazama wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Aomboleza Kwa Ajili Ya Yerusalemu

31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”

32 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’

33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa, kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.

34 “Ewe Yerusalemu, Yerusalemu, wewe uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, lakini hamkutaka!

35 Tazama nyumba yenu inaachwa ukiwa, ninawaambia hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye katika jina la Bwana.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/13-e32a47fa9b8ef3d34ec26811cb21ec5d.mp3?version_id=1627—

Luka 14

Yesu Nyumbani Mwa Farisayo

1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii.

2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili.

3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?”

4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ng’ombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?”

6 Nao hawakuwa na la kusema.

Unyenyekevu Na Ukarimu

7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu:

8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe.

9 Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa.

10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote.

11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu, ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako.

13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu,

14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Mfano Wa Karamu Kuu

15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”

16 Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi.

17 Wakati wa karamu ulipofika akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ni tayari sasa.’

18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’

19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ng’ombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’

20 Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’

21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’

22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’

23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa.

24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”

Gharama Ya Kuwa Mwanafunzi

25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia,

26 “Mtu ye yote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.

27 Ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha?

29 La sivyo, akiisha kuweka msingi naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki,

30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000?

32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani.

33 Vivyo hivyo, ye yote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Chumvi Isiyofaa

34 “Chumvi ni kitu kizuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, inawezaje kurudishiwa tena ladha yake?

35 Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje.

“Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/14-852ddf10c94fcd0e935166d3470a7140.mp3?version_id=1627—

Luka 15

Mfano Wa Kondoo Aliyepotea

1 Basi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Yesu.

2 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanung’unika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”

3 Ndipo Yesu akawaambia mfano huu:

4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate?

5 Naye akiisha kumpata, kwa furaha humbeba mabegani mwake

6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, nimempata kondoo wangu aliyepotea.’

7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Mfano Wa Sarafu Iliyopotea

8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate?

9 Naye akisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’

10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

Mfano Wa Mwana Mpotevu

11 Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili.

12 Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.

13 “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa.

14 Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana cho chote.

15 Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

16 Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa cho chote.

17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa!

18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako.

19 Sistahili tena kuitwa mwanao, nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’

20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

21 “Yule mtoto akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake.

23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi.

24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

25 “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza.

26 Akamwita mmoja wa watumishi na kumwuliza, ‘Kuna nini?’

27 Akamwambia, ‘Mdogo wako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’

28 “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumbembeleza.

29 Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu.

30 Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’

31 “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako.

32 Lakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu mdogo wako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/15-e579d12e34698ff550faf587dc0db4c8.mp3?version_id=1627—

Luka 16

Mfano Wa Msimamizi Mjanja

1 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake.

2 Hivyo huyo tajiri akamwita na kumwuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’

3 “Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba.

4 Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’

5 “Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamwuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’

6 “Akajibu, ‘Galoni 800za mafuta ya mizeituni.’

“Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’

7 “Kisha akamwuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’

# “Akajibu, ‘Vipimo 1,000vya ngano.’

“Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’

8 “Yule bwana akamsifu yule msimamizi kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru.

9 Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.

10 “Ye yote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.

11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?

12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine au atamheshimu mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”

14 Mafarisayo, ambao walikuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau.

15 Yesu akawaambia, “Ninyi mnajifanya kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.

Sheria Na Ufalme Wa Mungu

16 “Torati na manabii vilitumiwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu.

17 Lakini ni rahisi zaidi mbingu na nchi kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria.

18 “Mtu ye yote ampaye mkewe talaka na kumwoa mwanamke mwingine azini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa azini.

Tajiri Na Lazaro

19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa, kila siku.

20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima.

21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kulamba vidonda vyake.

22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa.

23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake.

24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’

25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu.

26 Zaidi ya hayo kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu,

28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.

29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Mose na Manabii, wawasikilize hao.’

30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’

31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na manabii, hawataweza kushawishiwa hata kama atafufuka mtu kutoka kwa wafu.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/16-e47c0cc05bb4bd5e39a7c02eec781c02.mp3?version_id=1627—

Luka 17

Yesu Afundisha Kuhusu Majaribu, Dhambi Na Imani

1 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yasababishayo watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha.

2 Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe zito la kusagia shingoni na kutoswa baharini kuliko kumfanya mmoja wa hawa wadogo atende dhambi.

3 Kwa hiyo, jilindeni.

“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe.

4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu’, msamehe.”

Imani

5 Wanafunzi wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”

6 Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng’oka ukaote baharini,’ Nao ungewatii.

Wajibu Wa Mtumishi

7 “Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula?’

8 Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa, baadaye waweza kula na kunywa?’

9 Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamuriwa?

10 Vivyo hivyo nanyi mkiisha kufanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”

Yesu Atakasa Wakoma Kumi

11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya.

12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali,

13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”

14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.

15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu.

16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.

17 Yesu akauliza, “Je, hawakuponywa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa?

18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?”

19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”

Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu

20 Yesu alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii,

21 wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”

22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona.

23 Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie.

24 Kwa maana Mwana wa Adamu katika siku yake atakuwa kama umeme wa radi, umulikao katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine.

25 Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.

26 “Kama ilivyokuwa siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu.

27 Wakati huo wa Noa watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina, gharika ikaja na kuwaangamiza wote.

28 “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga.

29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.

30 “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa.

31 Siku hiyo, mtu ye yote aliyeko kwenye dari ya nyumba yake, vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliyeko shambani asirudi nyumbani kuchukua cho chote.

32 Mkumbukeni mke wa Loti!

33 Mtu ye yote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza na ye yote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa.

34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja, mmoja atachukuliwa, mwingine ataachwa.

35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

36 Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.”

37 Kisha wakamwuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?”

Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyika.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/17-e85f1183335dd051ee2ce15c5f64859e.mp3?version_id=1627—

Luka 18

Mfano Wa Mjane Asiyekata Tamaa

1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.

2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwapo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.

3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’

4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Japokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,

5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”

6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.

7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia?

8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”

Mfano Wa Farisayo Na Mtoza Ushuru

9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiona kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine.

10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.

11 Yule Farisayo, akiwa amesimama peke yake, akasali hivi: ‘Mungu, ninakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine: Wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipiga piga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana ye yote ajikwezaye atashushwa na ye yote ajishushaye atakwezwa.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.

16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama hawa watoto.

17 Amin, nawaambia, ye yote ambaye hataupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Mtawala Tajiri

18 Mtawala mmoja akamwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna mtu ye yote aliye mwema ila Mungu peke yake.

20 Unazifahamu amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

21 Akajibu, “Amri zote hizi nimezishika tangu ujana wangu.”

22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.

24 Yesu akamtazama akasema, “Tazama ni jinsi gani ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!

25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Kama ni vigumu hivyo, ni nani basi awezaye kuokoka?”

27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu kwa Mungu yawezekana.”

28 Ndipo Petro akasema, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwanavyo tukakufuata!”

29 Yesu akajibu, “Amin nawaambia, hakuna hata mmoja aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu

30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Yesu Kwa Mara Ya Tatu Atabiri Kifo Chake

31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.

32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua.

33 Siku ya tatu atafufuka.”

34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.

Yesu Amponya Kipofu Karibu Na Yeriko

35 Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.

36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?”

37 Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”

38 Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu!”

39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, unirehemu!”

40 Yesu akasimama, akawaamuru huyo mtu aletwe kwake. Alipokaribia, Yesu akamwuliza,

41 “Unataka nikufanyie nini?”

Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”

42 Yesu akamwambia, “Basi upate kuona, imani yako imekuponya.”

43 Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/18-d1f12901b554265eb700b70f240e5a09.mp3?version_id=1627—