Luka 19

Zakayo Mtoza Ushuru

1 Yesu akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji.

2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo.

3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Yesu ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo.

4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu, kwa sababu angeipitia njia ile.

5 Yesu alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!”

6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa.

7 Watu wote walioona, wakaanza kunung’unika wakisema, “Amekwenda kuwa mgeni wa ‘mtu mwenye dhambi.’ ”

8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu ye yote kitu cho chote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”

9 Ndipo Yesu akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu kwa sababu, huyu naye, ni mwana wa Abrahamu.

10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

Mfano Wa Fedha

11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Yesu akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa Ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa iyo hiyo.

12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa, alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi.

13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi mpaka nitakaporudi.’

14 “Lakini raia wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’

15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.

16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia nimepata faida mara kumi zaidi.’

17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’

18 “Wa pili naye akaja, akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’

19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’

20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa.

21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’

22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda,

23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba ili nitakaporudi, nichukue iliyo yangu na riba yake?’

24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyang’anyeni fungu lake la fedha mkampe yule mwenye kumi.’

25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona tayari anayo mafungu kumi?’

26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba, kila aliye na kitu, ataongezewa, naye yule asiyetumia alicho nacho atanyang’anywa hata kile alicho nacho,

27 lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao, waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Ushindi

28 Baada ya Yesu kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu.

29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye Mlima uitwao wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili akawaambia,

30 “Nendeni katika kijiji kile kilicho mbele yenu, mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda ambaye hajapandwa na mtu bado, akiwa amefungwa hapo. Mfungueni, mumlete hapa.

31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”

32 Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia.

33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”

34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”

35 Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake.

36 Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza nguo zao barabarani.

37 Alipokaribia mahali yanapoanzia matelemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:

38 “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana!”

“Amani mbinguni na Utukufu huko juu sana.”

39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwemo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”

40 Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”

Yesu Anaulilia Mji Wa Yerusalemu

41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia,

42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako.

43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani.

44 Watakuponda chini, wewe na watoto walioko ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”

Yesu Atakasa Hekaluni

45 Ndipo akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo.

46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala, lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.’ ”

47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumwua.

48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/19-09a2322e78ac839a7cf7b0ebfc17ee02.mp3?version_id=1627—

Luka 20

Wahoji Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

1 Siku moja, Yesu alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri habari njema, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, pamoja na wazee wakamjia.

2 Wakamwuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?”

3 Akawajibu, “Nami nitawauliza swali.

4 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

5 Wakasemezana wao kwa wao wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’

6 Lakini tukisema, ‘ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yohana alikuwa nabii.”

7 Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.”

8 Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.”

Mfano Wa Wapangaji Waovu

9 Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba lake la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu.

10 Wakati wa mavuno akamtuma mtumishi wake kwa hao wakulima aliowakodishia ili wampatie sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima waliokodisha wakampiga na kumfukuza mikono mitupu.

11 Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza.

12 Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba.

13 “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’

14 “Lakini wale wakulima waliokodisha shamba walipomwona wakasemezana wao kwa wao na kusema, ‘Huyu ndiye mrithi, basi na tumwue ili urithi uwe wetu.’

15 Kwa hiyo wakamtoa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua.”

“Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wakulima hawa waliokodisha shamba?

16 Atakuja na kuwaua hao wapangaji na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.”

Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!”

17 Lakini Yesu akawakazia macho akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa:

“ ‘Jiwe lile walilolikataa waashi,

limekuwa jiwe kuu la pembeni?’

18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande na ye yote litakayemwangukia litamsagasaga awe unga.”

19 Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja kwa sababu walifahamu kwamba ametoa mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu.

Kumlipa Kaisari Kodi

20 Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa waaminifu ili wapate kumtega kwa maneno asemayo ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala.

21 Hivyo wale wapelelezi wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu kwa kufuata ukweli.

22 Je, ni halali sisi kumlipa Kaisari kodi au la?”

23 Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia, “Kwa nini ninyi mnanijaribu?

24 Nionyesheni dinari. Je, picha hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni ya nani?”

25 Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.”

Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari na Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

26 Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya.

Ufufuo Na Ndoa

27 Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumwuliza,

28 “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kuacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.

29 Basi walikuwepo ndugu saba, wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto.

30 Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto.

31 Naye wa tatu pia, vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke na wote wakafa pasipo kupata mtoto.

32 Mwishowe, huyo mwanamke mjane naye akafa.

33 Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani? Maana aliolewa na ndugu wote saba.”

34 Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa.

35 Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi.

36 Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo.

37 Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Bwana ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo.’

38 Yeye Mungu si Mungu wa wafu bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.”

39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umesema sawasawa kabisa!”

40 Baada ya hayo hakuna mtu aliyethubutu kumwuliza maswali zaidi.

Kristo Ni Mwana Wa Nani?

41 Kisha Yesu akawaambia, “Imekuwaje basi wao husema Kristoni Mwana wa Daudi?

42 Daudi mwenyewe anasema katika Kitabu cha Zaburi:

“ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:

“Keti mkono wangu wa kuume

43 hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako.” ’

44 Ikiwa Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ basi atakuwaje mwanawe?”

Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria

45 Wakati watu wote walipokuwa wanamsikiliza, Yesu akawaambia wanafunzi wake,

46 “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa majoho marefu na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hukaa kwenye viti maalum katika masinagogi na kukaa kwenye sehemu za wageni wa heshima katika karamu.

47 Wanakula nyumba za wajane, na ili waonekane mbele ya watu, husali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/20-d94b2f01534cb7d715a2ff876ca7d905.mp3?version_id=1627—

Luka 21

Sadaka Ya Mjane

1 Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu.

2 Akamwona pia mwanamke mmoja mjane maskini, akiweka humo sarafu mbili za shaba.

3 Yesu akasema, “Amin, amin nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo sadaka kubwa zaidi kuliko wengine wote.

4 Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kwa Mungu kutokana na wingi wa mali zao, lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo kwa ajili ya maisha yake.”

Dalili Za Siku Za Mwisho

5 Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia,

6 “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalosalia juu ya jiwe jingine, kila moja litabomolewa.”

7 Wakamwuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani zitaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?”

8 Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai kwamba, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.

9 Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”

10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine.

11 Kutakuwa na matetemeko ya ardhi katika sehemu mbalimbali, njaa kali na magonjwa ya kuambukiza. Kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

Mateso

12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kufungwa magerezani, nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu.

13 Hii itawapa nafasi ya kushuhudia.

14 Lakini msiwe na wasiwasi kwamba mtasema nini kabla ya mashtaka.

15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.

16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na baadhi yenu watawaua.

17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu.

18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia.

19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

Kuharibiwa Kwa Yerusalemu Kwatabiriwa

20 “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia.

21 Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo na wale walioko mashambani wasiingie mjini.

22 Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na watakaokuwa wananyonyesha katika siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu

24 Wataanguka kwa makali ya upanga, wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote, nao Yerusalemu utakanyagwa na watu Mataifa hadi muda wa hao watu Mataifa utimie.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari.

26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za vitu vya angani zitatikisika.

27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu.

28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”

29 Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote.

30 Unapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia.

31 Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yakitukia, mwajua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.

32 “Amin, amin nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yatimie.

33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

Siku Ya Mwisho Itakuja Ghafula

34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo.

35 Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote.

36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”

37 Kila siku Yesu alikuwa akifundisha Hekaluni na jioni ilipofika, alikwenda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha.

38 Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/21-df74781f7dde849609baea43d528cfa5.mp3?version_id=1627—

Luka 22

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

1 Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia.

2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu.

3 Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili.

4 Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu kuzungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu.

5 Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha.

6 Naye akakubali, akaanza kutafuta wasaa mzuri wa kumsaliti Yesu kwao wakati ambapo hakuna umati wa watu.

Maandalizi Ya Pasaka

7 Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa.

8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”

9 Wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi Pasaka?”

10 Yesu akawaambia, “Sikilizeni, mtakapokuwa mmeingia mjini, mtakutana na mwanaume mmoja aliyebeba mtungi wa maji, mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia,

11 nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza, kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’

12 Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, ambacho kina samani zote kikiwa kimepambwa vizuri. Tuandalieni humo.”

13 Wakaenda, wakakuta kila kitu kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Kwa hiyo wakaandaa Pasaka.

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

14 Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wanafunzi wake.

15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu.

16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”

17 Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote.

18 Kwa maana, nawaambia kwamba, tangu sasa sitakunywa tena divai hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

20 Vivyo hivyo baada ya kula, akachukua kile kikombe akasema, “Kikombe hiki ni Agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.

21 Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami.

22 Mwana wa Adamu anakwenda zake kama ilivyokusudiwa, lakini ole wake mtu huyo atakayemsaliti.”

23 Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni nani miongoni mwetu anayeweza kufanya jambo hilo?

Mabishano Kuhusu Ukuu

24 Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani anayeonekana kuwa mkuu wa wote miongoni mwao.

25 Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wakuu wasiomjua Mungu huwatawala watu wao kwa nguvu na wenye mamlaka juu yao huitwa ‘Wafadhili.’

26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye.

27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumiaye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumiaye.

28 Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu.

29 Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi,

30 ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”

Yesu Atabiri Kuwa Petro Atamkana

31 Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano.

32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”

33 Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

34 Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku huu wa leo, utanikana mara tatu kwamba hunijui Mimi.”

Mfuko, Mkoba Na Upanga

35 Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu cho chote?”

Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu cho chote.”

36 Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja.

37 Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wahalifu’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”

38 Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.”

Akawajibu, “Inatosha.”

Yesu Aomba Kwenye Mlima Wa Mizeituni

39 Yesu akatoka akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata.

40 Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni msije mkaangukia majaribuni.”

41 Akajitenga nao, kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba,

42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki, lakini si kama mimi nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”

43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.

44 Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.

45 Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni.

46 Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni mwombe ili msiangukie majaribuni.”

Yesu Akamatwa

47 Wakati Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja, ukiongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu.

48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”

49 Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”

50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.

51 Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.

52 Kisha Yesu akawaambia viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuwa wamekuja, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba Mimi ni mnyang’anyi?

53 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”

Petro Amkana Yesu

54 Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua wakaenda naye mpaka nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali.

55 Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao.

56 Mtumishi mmoja wa kike, kwa kusaidiwa na mwanga wa moto, akamwona Petro ameketi pale. Akamwangalia kwa uangalifu na kusema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Yesu!”

57 Lakini Petro akakana akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”

58 Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”

59 Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Yesu, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”

60 Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati uo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika.

61 Naye Bwana akageuka akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka yale maneno ambayo Bwana alimwambia, “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.”

62 Akatoka nje, akalia sana.

Walinzi Wamdhihaki Yesu Na Kumpiga

63 Wale watu waliokuwa wanamlinda Yesu wakaanza kumdhihaki na kumpiga.

64 Wakamfunga kitambaa machoni na kumwuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?”

65 Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.

Yesu Apelekwa Mbele Ya Baraza

66 Kulipopambazuka baraza la wazee wa watu, yaani viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, wakakutana pamoja, naye Yesu akaletwa mbele yao.

67 Wakamwambia, “Kama wewe ndiye Kristo, tuambie.”

Yesu akawajibu, “Hata nikiwaambia hamtaamini.

68 Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu.

69 Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”

70 Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu?”

Yeye akawajibu, “Ninyi mmesema kwamba Mimi ndiye.”

71 Kisha wakasema, “Kwani tunahitaji ushahidi gani zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/22-eb51a908c8dd078c98a9329d6c522151.mp3?version_id=1627—

Luka 23

Yesu Apelekwa Kwa Pilato

1 Kisha umati wote wa watu wakainuka na kumpeleka Yesu kwa Pilato.

2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Kristo, mfalme.”

3 Basi Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe wasema.”

4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwapo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”

5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”

Yesu Apelekwa Kwa Herode

6 Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?”

7 Alipofahamu kwamba Yesu alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.

8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha.

9 Herode akamwuliza maswali mengi, lakini Yesu hakumjibu lo lote.

10 Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana.

11 Herode na maaskari wake wakamdhihaki Yesu na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato.

12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki, kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.

Yesu Ahukumiwa Kifo

13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu,

14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wo wote wa mashtaka yenu dhidi yake.

15 Wala Herode hakumwona na kosa lo lote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lo lote linalostahili kifo.

16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.”

17 (Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu).

18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!”

19 (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini na kwa ajili ya mauaji).

20 Pilato akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena.

21 Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulibishe! Msulibishe!”

22 Kwa mara ya tatu Pilato akawaambia, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yo yote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kisha nitamwachia.”

23 Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu wakidai kwamba Yesu asulibiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.

24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.

25 Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Yesu mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.

Kusulibiwa Kwa Yesu

26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anatoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu.

27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea.

28 Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu.

29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’

30 Ndipo

“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni”

na vilima, “Tufunikeni!” ’

31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”

32 Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulibiwe.

33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulibisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto.

34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”

36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki, wakamletea siki ili anywe.

37 Nao wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha ya Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe ili utuokoe na sisi.”

40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo?

41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lo lote.”

42 Kisha akasema, “Bwana Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”

Kifo Cha Yesu

44 Ilikuwa kama saa sita mchana, kukawa na giza katika nchi yote mpaka saa tisa,

45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.

46 Yesu akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.

47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”

48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.

49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.

Maziko Ya Yesu

50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Barazala Wayahudi,

51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.

52 Yosefu alikwenda kwa Pilato akaomba apewe mwili wa Yesu.

53 Akaushusha kutoka msalabani, akauzungushia kitani safi na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo lilikuwa halijazikiwa mtu mwingine ye yote.

54 Ilikuwa siku ya maandalio, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.

55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya, wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa.

56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/23-503ccfcc7c852a47541324d3f78d4958.mp3?version_id=1627—

Luka 24

Kufufuka Kwa Yesu

1 Mnamo siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa na kwenda kaburini.

2 Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka kwenye kaburi,

3 lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu.

4 Walipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayong’aa kama umeme wa radi, wakasimama karibu nao.

5 Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu?

6 Hayuko hapa, amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba:

7 ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi, waovu, asulibiwe na siku ya tatu afufuke.’ ”

8 Ndipo wakayakumbuka maneno ya Yesu.

9 Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote.

10 Basi hawa walikuwa Maria Magdalene, Yoana na Maria mama yake Yakobo, pamoja na wengine waliofuatana nao.

11 Lakini wale waliosikia hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi.

12 Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbilia kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.

Njiani Kwenda Emau

13 Ikawa siku iyo hiyo, wanafunzi wawili wa Yesu walikuwa njiani wakienda kijiji cha Emau, yapata maili sabakutoka Yerusalemu.

14 Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia.

15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akaja akatembea pamoja nao,

16 lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.

17 Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?”

Wakasimama, nyuso zao zikionyesha huzuni.

18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamwuliza, “Je, wewe ndiye peke yako mgeni huku Yerusalemu ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?”

19 Akawauliza, “Mambo gani?”

Wakamjibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote.

20 Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulibisha.

21 Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye angeliikomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee.

22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri,

23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai.

24 Kisha baadhi ya wenzetu walikwenda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.”

25 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii!

26 Je, haikumpasa Kristokuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?”

27 Naye akianzia na Mose na manabii wote, akawafafanulia jinsi maandiko yalivyosema kumhusu yeye.

28 Nao wakakaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Yesu akawa kama anaendelea mbele.

29 Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao.

30 Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia.

31 Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena.

32 Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwakawaka kwa furaha ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?”

33 Wakaondoka mara, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika

34 wakisema, “Ni kweli Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni.”

35 Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Yesu alipoumega mkate.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wake

36 Wakati walipokuwa bado wanazungumza hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.”

37 Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka.

38 Lakini Yesu akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu?

39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa. Niguseni mwone, kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa navyo.”

40 Aliposema haya, akawaonyesha mikono na miguu yake.

41 Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula cho chote hapa?”

42 Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa,

43 naye akakichukua na kukila mbele yao.

44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Torati ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”

45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko.

46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.

47 Toba na msamaha wa dhambi utatangazwa kupitia jina lake, kuanzia Yerusalemu.

48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.

Kuahidiwa Kwa Roho Mtakatifu

49 “Tazama nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu, lakini kaeni humu Yerusalemu mpaka mtakapovikwa uwezo utokao juu.”

Kupaa Kwa Yesu Mbinguni

50 Akiisha kuwaongoza mpaka kwenye viunga vya Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki.

51 Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni.

52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu.

53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/24-7cfd6fc51db72109dcd527f3040fb377.mp3?version_id=1627—

Marko 1

Mahubiri Ya Yohana Mbatizaji

1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele yako,

yeye atakayeitengeneza njia yako”:

3 “sauti ya mtu aliaye nyikani.

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyosheni mapito yake.’ ”

4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya ondoleo la dhambi.

5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea, naye akawabatiza katika Mto Yordani, wakitubu dhambi zao.

6 Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.

7 Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake.

8 Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Ubatizo Wa Yesu

9 Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani.

10 Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua.

11 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, ambaye nimependezwa nawe.”

Majaribu Ya Yesu

12 Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani,

13 naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

Yesu Aanza Kuhubiri

14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu,

15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wanne

16 Yesu alipokuwa akitembea kandokando ya Bahari ya Galilaya alimwona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa hawa wawili walikuwa wavuvi.

17 Yesu akawaambia, “Njoni nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.”

18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata Yesu.

19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Yesu Amtoa Pepo Mchafu

21 Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia kwenye sinagogi akaanza kufundisha.

22 Watu wakashangaa sana mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria.

23 Wakati huo huo, palikuwa na mtu kwenye sinagogi lao aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu,

24 naye alikuwa akipiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Nakujua wewe ni nani, wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu!”

25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!”

26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa sana huyo mtu kwa nguvu akipiga kelele kwa sauti kubwa, kisha akamtoka.

27 Watu wote wakashangaa, hata kuulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu nao wanamtii!”

28 Sifa zake zikaanza kuenea kwa upesi katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Yesu Amponya Mama Mkwe Wa Simoni

29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea.

30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake.

31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

Yesu Aponya Wengi

32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu.

33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo.

34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme kwa sababu walimjua kuwa yeye ni nani.

Yesu Aondoka Kapernaumu Na Kwenda Galilaya

35 Mapema sana alfajiri kulipokuwa bado kungali giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha, ili kuomba.

36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta,

37 nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”

38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji vya jirani, ili niweze kuhubiri huko nako, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.”

39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

41 Yesu akiwa amejawa na huruma, akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka takasika!”

42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.

43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake

44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwa ushuhuda kwao.”

45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi isipokuwa alikaa sehemu zisizo na watu. Lakini bado watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/1-5ff4b3b32c76068a43d826c8b48a799e.mp3?version_id=1627—

Marko 2

Yesu Amponya Mtu Aliyepooza

1 Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani.

2 Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yo yote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.

3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.

4 Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia.

5 Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao,

7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

8 Mara moja Yesu akatambua kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9 Ni jambo gani lililo rahisi, kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue kitanda chako uende’?

10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anao uwezo duniani wa kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza,

11 “Nakuambia, inuka, chukua kitanda chako uende nyumbani kwako.”

12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akachukua kitanda chake akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

Yesu Amwita Lawi (Mathayo)

13 Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akaanza kuwafundisha.

14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kukusanya kodi, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.

15 Yesu alipokuwa akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi pamoja na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata.

16 Baadhi ya walimu wa sheria na Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake, “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”

17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Walio wazima hawahitaji tabibu, bali wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”

19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati bwana arusi akiwa pamoja nao? Maadamu bwana arusi yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.

20 Lakini wakati utakuja ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, siku hiyo ndipo watakapofunga.

21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kilichoshonewa kwenye nguo iliyochakaa huondoka, nayo ile nguo huchanika zaidi.

22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, kwa hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”

Bwana Wa Sabato

23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake, walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakipita wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.

24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo ambalo si halali kufanywa siku ya Sabato?”

25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walipokuwa na njaa na uhitaji wa chakula?

26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu wakati Abiathari akiwa Kuhani Mkuu, akaila ile Mikate Mitakatifu, ambayo ilikuwa hairuhusiwi mtu ye yote kuila isipokuwa makuhani, naye akawapa wenzake.”

27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.

28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/2-133c114d435642dbff0d57776d3d79a6.mp3?version_id=1627—

Marko 3

Yesu Amponya Mtu Mwenye Mkono Uliopooza

1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi na huko palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza.

2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.

3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele.”

4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kufanya jema au baya, kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukapona kabisa!

6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, mara wakaanza kufanya shauri la kumwua Yesu wakiwa na kundi la wafuasi wa Herode.

Umati Wa Watu Wamfuata Yesu

7 Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata.

8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, Ng’ambo ya Yordani pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni.

9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.

10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.

11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.

14 Akawachagua kumi na wawili ambao pia aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye na kuwatuma kwenda kuhubiri

15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro),

17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo),

18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomasi, Yakobo, mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo na

19 Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Yesu Na Beelzebuli

20 Ndipo Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.

21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22 Walimu wa sheria waliotelemka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu, anatoa pepo wachafu.”

23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?

24 Kama ufalme ukigawanyika wenyewe kwa wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.

25 Nayo nyumba kama ikigawanyika yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe akiwa amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.

27 Hakuna mtu ye yote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu, ndipo awezapo kuteka nyara.

28 Amin, amin nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa.

29 Lakini ye yote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama Na Ndugu Zake Yesu

31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita.

32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama zangu na ndugu zangu.

35 Mtu ye yote anayetenda mapenzi ya Mungu huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/3-69d5e075b3d87913941228fcda2cdb33.mp3?version_id=1627—

Marko 4

Mfano Wa Mpanzi

1 Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umemkusanyikia na kumzunguka ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ilimbidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo.

2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:

3 “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka kando ya njia, ndege wakaja na wakazila.

5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba,

6 jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake ilikuwa haina kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, miiba hiyo ikakua ikaisonga hiyo mimea hivyo haikutoa mazao.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja thelathini, nyingine sitini na nyingine mia moja.”

9 Kisha Yesu akasema, “Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

Sababu Za Mifano

10 Alipokuwa peke yake, wale waliokuwepo pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili, wakamwuliza kuhusu mifano yake.

11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu, lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano

12 ili,

“ ‘daima waone lakini wasitambue,

daima wasikie lakini wasielewe;

wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine?

14 Yule mpanzi hupanda neno.

15 Hawa ndio wale walio kando ya njia, ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao.

16 Nazo hizi ni zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, wanapolisikia neno, mara hulipokea kwa furaha.

17 Basi kwa kuwa hawana mizizi, hudumu kwa muda mfupi tu, kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, wao mara huiacha imani.

18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno,

19 lakini masumbufu ya maisha haya, udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae.

20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kutoa mazao: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mara mia moja ya ile iliyopandwa.”

Mfano Wa Taa

21 Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake?

22 Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lo lote la siri ambalo halitaletwa nuruni.

23 Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

24 Naye akawaambia, “Iweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo mnachotumia kuwapimia wengine, ndicho kitakachotumika kuwapimia ninyi, hata na zaidi.

25 Kwa maana aliye na kitu ataongezewa na yeye asiye na kitu hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Mfano Wa Mbegu Inayoota

26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani.

27 Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo.

28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke.

29 Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia maana mavuno yamekuwa tayari.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

30 Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza?

31 Uko kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini.

32 Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani kujenga viota kwenye matawi yake.”

33 Kwa mifano mingine mingi kama hii Yesu alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa.

34 Hakusema nao neno lo lote pasipo mifano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Yesu Atuliza Dhoruba

35 Siku hiyo, ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke na twende mpaka ng’ambo.”

36 Wakiuacha ule umati wa watu nyuma, wakamchukua vile vile kama alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye.

37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji.

38 Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/4-74f4defb3384b67a4beb90520b4a556b.mp3?version_id=1627—