Marko 15

Yesu Mbele Ya Pilato

1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.

2 Pilato akamwuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe umesema.”

3 Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi.

4 Pilato akamwuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”

5 Lakini Yesu hakuendelea kujibu, hivyo Pilato akashangaa.

Pilato Amtoa Yesu Ili Akasulibiwe

6 Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa ye yote ambaye watu wangemtaka.

7 Wakati huo, mtu mmoja aitwaye Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wamesababisha mauaji wakati wa maasi yaliyotokea dhidi ya serikali.

8 Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.

9 Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?”

10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu.

11 Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.

12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13 Wakapiga kelele wakisema, “Msulibishe!”

14 Akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulibishe!”

15 Pilato akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba, naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulibishwe.

Maaskari Wamdhihaki Yesu

16 Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha Askari.

17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvisha kichwani.

18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!”

19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake wakamsujudia kwa kumdhihaki.

20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika zile nguo zake mwenyewe. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulibishe.

Kusulibiwa Kwa Yesu

21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, wakamlazimisha aubebe ule msalaba wa Yesu.

22 Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (ambayo, maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).

23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa.

24 Basi wakamsulibisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni nini kila mtu atakachochukua.

25 Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulibisha.

26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “MFALME WA WAYAHUDI.”

27 Pamoja naye walisulibiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto.

28 Nayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”

29 Watu waliokuwa wakipita karibu wakamtukana na kutikisa vichwa vyao kwa mzaha wakisema, “Aha! Wewe ambaye ungelibomoa Hekalu na kulijenga kwa siku tatu,

30 basi ujiokoe mwenyewe na ushuke kutoka msalabani.”

31 Vivyo hivyo viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Yeye aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe!

32 Basi huyu Kristo, huyu Mfalme wa Wayahudi, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulibiwa pamoja naye pia wakamtukana.

Kifo Cha Yesu Msalabani

33 Ilipofika saa sita, giza lilifunika nchi yote mpaka saa tisa.

34 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, “Eloi, Eloi lama Sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia maneno hayo, wakasema, “Msikieni anamwita Eliya.”

36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi, akampa Yesu ili anywe akisema, “Basi mwacheni, hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”

37 Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.

38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.

39 Basi yule jemadari, aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu, aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40 Walikuwapo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali, ambao miongoni mwao alikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome.

41 Hawa walifuatana na Yesu na kumhudumia alipokuwa Galilaya. Pia walikuwapo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.

Maziko Ya Yesu

42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizo, siku moja kabla ya Sabato,

43 Yosefu wa Arimathaya mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, ambaye yeye mwenyewe alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba huo mwili wa Yesu.

44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Akamwita yule jemadari, akamwuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa.

45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili.

46 Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili wa Yesu kutoka msalabani, akauviringishia kile kitambaa cha kitani na akamweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akalivingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi.

47 Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/15-8b3030d05e7a7da3feacc077e16b91ce.mp3?version_id=1627—

Marko 16

Kufufuka Kwa Yesu

1 Sabato ilipomalizika, Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.

2 Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua walikwenda kaburini.

3 Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka kwenye ingilio la kaburi?”

4 Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi.

5 Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.

6 Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza.

7 Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba ‘Anawatangulia kwenda Galilaya, huko ndiko mtakakomwona, kama alivyowaambia.’ ”

8 Hivyo wakatoka wakakimbia kutoka mle kaburini, kwani hofu kuu na mshangao ulikuwa umewapata, nao hawakumwambia mtu ye yote neno lo lote.

Yesu Anamtokea Maria Magdalene

9 Yesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Maria Magdalene, yule ambaye alikuwa amemtoa pepo wachafu saba.

10 Maria akaenda akawaambia wale waliokuwa wakifuatana na Yesu, ambao walikuwa wanaomboleza na kulia.

11 Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wawili

12 Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine.

13 Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.

Yesu Awaagiza Wale Wanafunzi Kumi Na Mmoja

14 Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi wake kumi na mmoja, walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutokuamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa sababu hawakuwasadiki wale waliomwona baada ya kufufuka.

15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

16 Ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini ye yote asiyeamini atahukumiwa.

17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wale waaminio: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu, watasema kwa lugha mpya,

18 watashika nyoka kwa mikono yao na hata wakinywa kitu cho chote cha kuua, hakitawadhuru kamwe, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

Yesu Apaa Kwenda Mbinguni

19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu.

20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/16-1fcaa663285642a5a150865e9c93dd78.mp3?version_id=1627—

Mathayo 1

Kumbukumbu Za Ukoo Wa Yesu Kristo

1 Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:

2 Abrahamu akamzaa Isaki,

Isaki akamzaa Yakobo,

Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake,

3 Yuda akamzaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari,

Peresi akamzaa Hesroni,

Hesroni akamzaa Aramu,

4 Aramu akamzaa Aminadabu,

Aminadabu akamzaa Nashoni,

Nashoni akamzaa Salmoni,

5 Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu,

Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu,

Obedi akamzaa Yese,

6 Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme.

Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.

7 Solomoni akamzaa Rehoboamu,

Rehoboamu akamzaa Abiya,

Abiya akamzaa Asa,

8 Asa akamzaa Yehoshafati,

# Yehoshafati akamzaa Yoramu,

Yoramu akamzaa Uzia,

9 Uzia akamzaa Yothamu,

Yothamu akamzaa Ahazi,

Ahazi akamzaa Hezekia,

10 Hezekia akamzaa Manase,

Manase akamzaa Amoni,

Amoni akamzaa Yosia,

11 wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.

12 Baada ya uhamisho wa Babeli:

Yekonia alimzaa Shealtieli,

Shealtieli akamzaa Zerubabeli,

13 Zerubabeli akamzaa Abiudi,

Abiudi akamzaa Eliakimu,

Eliyakimu akamzaa Azori,

14 Azori akamzaa Zadoki,

Zadoki akamzaa Akimu,

Akimu akamzaa Eliudi,

15 Eliudi akamzaa Eleazari,

Eleazari akamzaa Matani,

Matani akamzaa Yakobo,

16 naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

17 Hivyo, kulikuwapo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.

Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo

18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”

22 Haya yote yametukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema:

23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.

25 Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/1-9229e9c077322285084c45783ed18d7a.mp3?version_id=1627—

Mathayo 2

Wataalamu Wa Nyota Wafika Kumwona Mtoto Yesu

1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu

2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”

3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu.

4 Herode akawaita pamoja makuhani wakuu na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristoangezaliwa.

5 Nao wakamwambia, “Katika Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:

6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,

wewe si mdogo miongoni

mwa watawala wa Yuda,

kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala

atakayekuwa mchungaji

wa watu wangu Israeli.’ ”

7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilipoonekana.

8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mumwonapo, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”

9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto.

10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno.

11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.

12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.

Yosefu, Maria Na Mtoto Yesu Wakimbilia Misri

13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri

15 ambako walikaa mpaka Herode alipokufa. Hili lilikuwa, ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema, “Kutoka Misri nilimwita mwanangu.”

16 Herode alipong’amua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota.

17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.

18 “Sauti ilisikika huko Rama,

kilio cha huzuni na maombolezo makuu,

Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,

akikataa kufarijiwa,

kwa sababu hawako tena.”

Kurudi Kutoka Misri

19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri

20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”

21 Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli.

22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya,

23 akaenda akaishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia lile neno lililonenwa na manabii, “Ataitwa Mnazarayo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/2-839b069cf9b58f149c63b36e2cf15c0e.mp3?version_id=1627—

Mathayo 3

Yohana Mbatizaji Atayarisha Njia

1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika Nyika ya Uyahudi, akisema,

2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni u karibu.”

3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema,

“Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,

‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,

yanyosheni mapito yake.’ ”

4 Basi Yohana alivaa vazi lililotengenezwa kwa singa za ngamia akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake, chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.

5 Watu walimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.

6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?

8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba.

9 Wala msidhani mnaweza kusemezana, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya.

10 Hata sasa shoka limekwisha kuwekwa tayari kwenye mizizi ya mti. Kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwaRoho Mtakatifu na kwa moto.

12 Chombo chake cha kupuria kiko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, akiikusanya ngano yake ghalani na kuyachoma makapi kwa moto usiozimika.”

Yesu Abatizwa

13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize.

14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikamfungukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake.

17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/3-381e1740155446a1f04bd88e8865bf67.mp3?version_id=1627—

Mathayo 4

Kujaribiwa Kwa Yesu

1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kuingia nyikani ili akajaribiwe na ibilisi.

2 Baada ya kufunga siku arobaini mchana na usiku, hatimaye akaona njaa.

3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa, ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

5 Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na kumweka juu ya mnara mrefu mwembamba wa Hekalu,

6 akamwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu jitupe chini, kwa kuwa imeandikwa,

“ ‘Atakuagizia malaika zake,

nao watakuchukua mikononi mwao

ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’ ”

7 Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake,

9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako, nawe utamtumikia yeye peke yake.’ ”

11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumtumikia.

Yesu Aanza Kuhubiri

12 Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya.

13 Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na ya Naftali,

14 ili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema:

15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,

kwenye njia ya kuelekea baharini,

ng’ambo ya Yordani,

Galilaya ya watu Mataifa:

16 watu wale waliokaa gizani

wameona nuru kuu

nao wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti,

nuru imewazukia.”

17 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wake Wa Kwanza

18 Wakati Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa maana wao walikuwa wavuvi.

19 Yesu akawaambia, “Njoni, nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.”

20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo wakiziandaa nyavu zao. Yesu akawaita.

22 Nao mara wakaziacha nyavu zao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

Yesu Ahubiri Na Kuponya Wagonjwa

23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.

24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya.

25 Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ng’ambo ya Mto Yordani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/4-f9ac2dfc5a34755fd150da9a30f0b003.mp3?version_id=1627—

Mathayo 5

Sifa Za Aliyebarikiwa

1 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia.

2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

3 “Heri walio maskini wa roho,

maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

4 Heri wale wanaohuzunika,

maana hao watafarijiwa.

5 Heri walio wapole,

maana hao watairithi nchi.

6 Heri wenye njaa na kiu ya haki,

maana hao watatoshelezwa.

7 Heri wenye huruma,

maana hao watapata rehema.

8 Heri walio na moyo safi,

maana hao watamwona Mungu.

9 Heri walio wapatanishi,

maana hao wataitwa wana wa Mungu.

10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu.

12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

Chumvi Na Nuru

13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu cho chote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika.

15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba.

16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Kutimiza Sheria

17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza.

18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia.

19 Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.

20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya walimu wa sheria na Mafarisayo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Kuhusu Hasira

21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue, ye yote atakayeua atapaswa hukumu.’

22 Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’, yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako,

24 iache sadaka yako hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike, kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani.

26 Amin, nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa hadi senti ya mwisho.

Kuhusu Uzinzi

27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini’.

28 Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

29 Jicho lako la kuume likikufanya utende dhambi, ling’oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

30 Kama mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, ukate uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

Kuhusu Talaka

31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu ye yote amwachaye mkewe na ampe hati ya talaka.’

32 Lakini mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na ye yote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa azini.

Kuhusu Kuapa

33 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’

34 Lakini mimi nawaambia, Msiape kabisa, ama kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu,

35 au kwa nchi, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu, au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu.

36 Nanyi msiape kwa vichwa vyenu kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37 ‘Ndiyo,’ yenu iwe ‘Ndiyo’ na ‘Hapana’, yenu iwe ‘Hapana.’ Lo lote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

Kuhusu Kulipiza Kisasi

38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’

39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia,

40 Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua shati lako, mwachie achukue na koti pia.

41 Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili.

42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

Upendo Kwa Adui

43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’

44 Lakini mimi ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi,

45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Kama mkiwapenda wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?

47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo?

48 Kwa hiyo iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/5-287f417e0222d2926c445cc3fdde0fa2.mp3?version_id=1627—

Mathayo 6

Kuwapa Wahitaji

1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao.

3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya,

4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

Kuhusu Maombi

5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin, amin nawaambieni, wao wamekwisha kupata thawabu yao.

6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako.

7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao.

8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:

“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

Jina lako litukuzwe.

10 Ufalme wako uje.

Mapenzi yako yafanyike

hapa duniani kama huko mbinguni.

11 Utupatie leo riziki zetu

za kila siku.

12 Utusamehe deni zetu,

kama sisi nasi tulivyokwisha

kuwasamehe wadeni wetu.

13 Usitutie majaribuni,

bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

[kwa kuwa Ufalme ni wako na nguvu

na utukufu, hata milele. Amen].’

14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe na ninyi pia.

15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Kuhusu Kufunga

16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu.

17 Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu

18 ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri, naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

Akiba Ya Mbinguni

19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba.

20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba.

21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

Jicho Ni Taa Ya Mwili

22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utakuwa na nuru.

23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza, hilo ni giza kuu namna gani!

Mungu Na Mali

24 “Hakuna mtu ye yote awezaye kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa ama atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau huyu mwingine. Ninyi hamwezi kumtumikia Mungu na Mali.

Msiwe Na Wasiwasi

25 “Kwa hiyo nawaambia, msiwe na wasiwasi kuhusu maisha yenu: mtakula nini au mtakunywa nini, au kuhusu miili yenu, mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi?

26 Waangalieni ndege wa angani, wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege?

27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake aweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake au kuongeza dhiraa mojakwenye kimo chake?

28 “Nanyi kwa nini kujitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi.

29 Lakini nawaambia, hata Mfalme Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa kama mojawapo ya hayo maua.

30 Lakini ikiwa Mungu anayavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba?

31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ Au ‘Tutakunywa nini?’ Au ‘Tutavaa nini?’

32 Kwa maana watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kwamba mnahitaji hayo yote.

33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa.

34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/6-9a238dbed23a3ab247ef6b09a2d9c394.mp3?version_id=1627—

Mathayo 7

Kuwahukumu Wengine

1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa.

2 Kwa maana kwa jinsi ile unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa na kwa kipimo kile utakachotoa ndicho utakachopokea.

3 “Kwa nini unatazama kibanzi kidogo kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako?

4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?’

5 Ewe mnafiki, toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe, nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yako.

6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu, wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyaga-kanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

Omba, Tafuta, Bisha

7 “Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.

8 Kwa maana kila aombaye hupewa, naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa mlango.

9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe?

10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka?

11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

12 Kwa hiyo cho chote ambacho mnataka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.

Njia Nyembamba Na Njia Pana

13 “Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo.

14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

Mti Na Tunda Lake

15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.

16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba au tini kwenye michongoma?

17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya.

18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.

19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

20 Hivyo kwa matunda yao mtawatambua.

Mwanafunzi Wa Kweli

21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’

23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

Msikiaji Na Mtendaji

24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba.

25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, lakini haikuanguka kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba.

26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga.

27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

28 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake,

29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/7-89cc956bb23cb8869ceee4ea0a9cdcbb.mp3?version_id=1627—

Mathayo 8

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata.

2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”

3 Yesu akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka, takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.

4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote. Lakini nenda, ukajionyeshe kwa kuhani na utoe sadaka aliyoamuru Mose, iwe ushuhuda kwao kwamba umepona.”

Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari

5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,

6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.

9 Kwa kuwa mimi nami niko chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu ‘Nenda,’ huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo’, huja. Nami nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ hufanya.”

10 Yesu aliposikia maneno haya, akashangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, amin nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona imani kubwa namna hii.

11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni.

12 Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa na kulia na kusaga meno.”

13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.

Yesu Aponya Wengi

14 Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa ana homa.

15 Akamgusa mkono wake na homa ikamtoka, naye akainuka na kuanza kumhudumia.

16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuponya wagonjwa wote.

17 Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:

“Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu

na alichukua magonjwa yetu.”

Gharama Ya Kumfuata Yesu

18 Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ng’ambo.

19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata po pote uendako.”

20 Naye Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo, nao ndege wa angani wana viota vyao, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”

22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, nawe waache wafu wazike wafu wao.”

Yesu Atuliza Dhoruba

23 Naye alipoingia kwenye chombo, wanafunzi wake wakamfuata.

24 Ghafula kukainuka dhoruba kali baharini hata chombo kikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi.

25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kuu.

27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

Wawili Wenye Pepo Waponywa

28 Walipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu wakitoka makaburini walikutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile.

29 Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”

30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu tuende kwenye lile kundi la nguruwe.”

32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemka mbio gengeni, likaingia baharini na kufa ndani ya maji.

33 Wale waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.

34 Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/8-e8b4ea0652e416d2e3bde5b78855b1dd.mp3?version_id=1627—