Mathayo 9

Yesu Amponya Mtu Aliyepooza

1 Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao.

2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye kitanda. Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu, dhambi zako zimesamehewa.”

3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”

4 Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu?

5 Kwa kuwa ni lipi lililo rahisi: kusema, ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ au kusema, ‘Simama, utembee’?

6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako na uende nyumbani kwako.”

7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake.

8 Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama hii kwa wanadamu.

Kuitwa Kwa Mathayo

9 Yesu alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.

10 Wakati Yesu alipokuwa ameketi chakulani ndani ya nyumba, watoza ushuru wengi na wenye dhambi wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake.

11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu.

13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

14 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakaja na kumwuliza Yesu, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

15 Yesu akawajibu, “Je, wageni wa bwana arusi waweza kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, hapo ndipo watakapofunga.

16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo kuukuu, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo na kuchanika kwa nguo hiyo kutakuwa kubaya zaidi ya hapo mwanzo.

17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka na divai itamwagika. Navyo viriba vitaharibika, lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya na hivyo divai na viriba huwa salama.”

Mwanamke Aponywa

18 Wakati Yesu akiwa anawaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi, lakini uje uweke mkono wako juu yake naye atakuwa hai.”

19 Yesu akaondoka akafuatana naye, wanafunzi wake pia wakaandamana naye.

20 Wakati huo huo mwanamke mmoja ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu akagusa upindo wa vazi lake,

21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”

22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.

Yesu Amfufua Binti Wa Kiongozi Wa Sinagogi

23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele,

24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka.

25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka.

26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.

Yesu Awaponya Vipofu

27 Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata, wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na mnavyoamini.”

30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu ye yote asijue kuhusu jambo hili.”

31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

Yesu Amponya Mtu Bubu

32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu.

33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”

34 Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”

Watenda Kazi Ni Wachache

35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme na kuponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.

36 Alipoona makutano aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasio na mchungaji.

37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache,

38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watenda kazi katika shamba lake la mavuno.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/9-03582d35b4c2b03efe8f199af109e5fa.mp3?version_id=1627—

Mathayo 10

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

1 Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

2 Haya ndiyo majina ya hao wanafunzi kumi na wawili:

3 wa kwanza, Simoni, aitwaye Petro na Andrea nduguye, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, Filipo na Bartholomayo, Tomasi na Mathayo mtoza ushuru, Yakobo mwana wa Alfayo na Thadayo,

4 Simoni Mkananayo na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

5 Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza, “Msiende miongoni mwa watu Mataifa wala msiingie mji wo wote wa Wasamaria.

6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea.

7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’

8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.

9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu.

10 Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtenda kazi anastahili posho yake.

11 “Mji wo wote au kijiji cho chote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake mpaka mtakapoondoka.

12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani.

13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake, la sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi.

14 Kama mtu ye yote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung’uteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo.

15 Amin, amin nawaambia, miji ya Sodoma na Gomora itastahimili zaidi katika hukumu kuliko mji huo.

Mateso Yanayokuja

16 “Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.

17 “Jihadharini na wanadamu, kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao,

18 nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na mbele ya watu Mataifa.

19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikirifikiri mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo.

20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.

21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe na baba atamsaliti mtoto wake, watoto wataasi dhidi ya wazazi wao na kuwafanya wauawe.

22 Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini yeye atakayevumilia hadi mwisho ataokoka.

23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.

24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake wala mtumishi hamzidi bwana wake.

25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si zaidi sana wale wa nyumbani mwake mwenyewe!

Anayestahili Kuogopwa

26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana.

27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe na lile mnalosikia likinong’onwa, masikioni mwenu, lihubirini kwenye paa la nyumba.

28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali, mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu

29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti mbili tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka pasipo Baba yenu kujua.

30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa.

31 Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa zaidi kuliko shomoro wengi.

32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

33 Lakini ye yote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

Sikuleta Amani, Bali Upanga

34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.

35 Kwa maana nimekuja kumfitini

“ ‘mtu na babaye,

binti na mamaye,

mkwe na mama mkwe wake;

36 nao adui za mtu watakuwa

ni wale watu wa nyumbani kwake.’

37 “Ye yote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Ye yote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda Mimi, hastahili kuwa wangu.

38 Tena ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu.

39 Ayang’ang’aniaye maisha yake atayapoteza, lakini yeye atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

Watakaopokea Thawabu

40 “Mtu ye yote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi na ye yote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma.

41 Mtu ye yote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii, atapokea thawabu ya nabii na mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapokea thawabu ya mwenye haki.

42 Kama ye yote akimpa hata kikombe cha maji mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, ninawaambia, hataikosa thawabu yake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/10-378a39eeecf0e3ebe1f80b4871f8c113.mp3?version_id=1627—

Mathayo 11

Yesu Na Yohana Mbatizaji

1 Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wale wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristoalikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake

3 ili wakamwulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwarifu Yohana yale mnayosikia na kuyaona:

5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

6 Ana heri mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

7 Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Unyasi ukiyumbishwa na upepo?

8 Kama sivyo, mlitoka kwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hasha, wale wanaovaa nguo nzuri wako katika majumba ya wafalme.

9 Basi mlitoka kwenda kuona nini? Je, ni kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.

10 Huyo ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama namtuma mjumbe mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako.’

11 Amin, nawaambia, miongoni mwa watu waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu zaidi ya Yohana Mbatizaji, lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, ni mkuu kuliko Yohana.

12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, Ufalme wa Mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.

13 Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana.

14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye (Yohana) ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.

15 Yeye aliye na sikio na asikie.

16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,

17 “ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza;

tuliwaimbia nyimbo za msiba

lakini hamkuomboleza.’

18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’

19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazama, mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kwa haki ya matendo yake.”

Ole Wa Miji Isiyotubu

20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu.

21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingelifanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu tangu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

22 Lakini nawaambia, itavumilika zaidi kwa Tiro na Sidoni katika siku ya hukumu, kuliko kwenu.

23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa pande za chini sana. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwapo hadi leo.

24 Lakini nakuambia kwamba, Sodoma itastahimili zaidi katika siku ile ya hukumu kuliko wewe.”

Hakuna Amjuaye Baba Ila Mwana

25 Wakati huo Yesu alisema, “Ninakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wachanga.

26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na ye yote ambaye Mwana anapenda kumdhihirisha Baba kwake.

Yesu Awaita Waliolemewa Na Mizigo

28 “Njoni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/11-6d29c67c3f89fcc3fabb19fe8888531d.mp3?version_id=1627—

Mathayo 12

Bwana Wa Sabato

1 Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya ngano siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, wakaanza kuvunja masuke ya ngano na kuyala.

2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali siku ya Sabato.”

3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa?

4 Aliingia katika nyumba ya Mungu akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao.

5 Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia?

6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.

7 Kama mngelikuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Ninataka rehema, wala si dhabihu,’ msingeliwalaumu watu wasio na hatia,

8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Anamponya Mtu Aliyepooza Mkono

9 Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia katika sinagogi lao,

10 huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamwuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

11 Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa?

12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”

13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.

14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumwua.

Mtumishi Aliyechaguliwa Na Mungu

15 Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wote,

16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani.

17 Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:

18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,

mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

Nitaweka Roho yangu juu yake,

naye atatangaza haki kwa mataifa.

19 Hatagombana wala hatapiga kelele,

wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.

20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

utambi unaofuka moshi hatauzima,

mpaka atakapoifanya haki ishinde.

21 Katika Jina lake mataifa

wataweka tumaini lao.”

Yesu Na Beelzebuli

22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye ni kipofu na bubu, Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona.

23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”

24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”

25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja iliyogawanyika dhidi yake yenyewe haiwezi kusimama.

26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama?

27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.

28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.

30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.

31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

32 Mtu ye yote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini ye yote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

Mti Na Matunda yake

33 “Ufanye mti kuwa mzuri nayo matunda yake yatakuwa mazuri, au ufanye mti kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya, kwa maana mti hutambulikana kwa matunda yake.

34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake.

35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka katika hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake.

36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena.

37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumiwa.”

Ishara Ya Yona

38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona.

40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumikwa muda wa siku tatu mchana na usiku, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, mchana na usiku.

41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu, kwa maana wao walitubu katika kuhubiri kwa Yona na tazama hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.

42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki, kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

Mafundisho Kuhusu Pepo Mchafu

43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati.

44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye ile nyumba yangu nilikotoka,’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri.

45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba, wabaya zaidi kuliko yeye, nao huingia na kuishi humo. Nayo hali ya mwisho ya mtu yule huwa mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki cha uovu.”

Mama Na Ndugu zake Yesu

46 Wakati alipokuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake walisimama nje wakitaka kuongea naye.

47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama mama Yako na ndugu Zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”

48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?”

49 Akiwanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu Zangu!

50 Kwa maana ye yote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/12-ec6476471eef8b07bceca2860e22e35f.mp3?version_id=1627—

Mathayo 13

Mfano Wa Mpanzi

1 Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba akaketi kando ya bahari.

2 Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari.

3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akipanda, baadhi zikaanguka kando ya njia, ndege wakaja na kuzila.

5 Nyingine zikaanguka sehemu yenye mawe, ambapo hapana udongo mwingi. Zikaota haraka kwa sababu udongo ulikuwa hauna kina.

6 Lakini jua lilipozidi, mimea hiyo ilinyauka na kukauka kwa sababu mizizi yake haikuwa na kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka katikati ya miiba, miiba hiyo ikakua ikazisonga.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini na nyingine mara thelathini.

9 Yeye mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

Sababu Ya Kufundisha Kwa Mifano

10 Wanafunzi wake wakamwendea wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11 Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao sivyo.

12 Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele, lakini yule asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa.

13 Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano:

“Ingawa wanatazama, hawaoni,

wanasikiliza, lakini hawasikii

wala hawaelewi.

14 Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema:

“ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa,

na pia mtatazama lakini hamtaona.

15 Kwa maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito,

hawasikii kwa masikio yao,

na wamefumba macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

wakasikia kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao,

wakageuka, nami nikawaponya.’

16 Lakini heri macho yenu, kwa sababu yanaona na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia.

17 Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona, nao hawakuyaona na kusikia yale mnayosikia lakini hawakuyasikia.

Maelezo Ya Mfano Wa Mbegu

18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi:

19 Mtu ye yote anaposikia neno la Ufalme, naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake, hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia.

20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha.

21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hukaa kwa muda mfupi. Inapotokea dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno, yeye mara huchukizwa.

22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya dunia na ushawishi wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.

23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika hutoa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano Wa Magugu

24 Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

25 Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.

27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’

28 “Akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya jambo hili.’

“Wale watumishi wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’

29 “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo.

30 Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji, wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto, kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

31 Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua akaipanda shambani mwake.

32 Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hata ndege wa angani huja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

33 Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika vipimo vitatuvya unga mpaka wote ukaumuka.”

Sababu Ya Yesu Kutumia Mifano

34 Yesu alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala pasipo mfano hakuwaambia lo lote.

35 Hii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa vinywa vya manabii kusema:

“Nitakifungua kinywa changu niseme nao kwa mifano,

nitahubiri mambo yaliyofichika

tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”

Ufafanuzi Wa Mfano Wa Magugu

36 Kisha Yesu akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”

37 Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu.

38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu.

39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

40 “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia.

41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote.

42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.

43 Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

Mfano Wa Hazina Iliyofichwa Na Wa Lulu

44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanya biashara aliyekuwa akitafuta lulu safi.

46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

Mfano Wa Wavu

47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina.

48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa.

49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki.

50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

51 Yesu akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”

Wakamjibu, “Ndiyo.”

52 Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka katika ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

Yesu Akataliwa Nazareti

53 Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka.

54 Alipofika mjini kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?”

55 “Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?

56 Nao dada zake wote hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?”

57 Wakachukizwa naye.

Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/13-a919a5133c4e97aa62376d5cfb8e49b5.mp3?version_id=1627—

Mathayo 14

Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa

1 Wakati huo, Mfalme Herode aliyekuwa mtawala alisikia habari kuhusu sifa za Yesu,

2 akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu! Hiyo ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”

3 Herode alikuwa amemkamata Yohana akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake,

4 kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode kwamba, “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.”

5 Herode alitaka sana kumwua Yohana, lakini akaogopa watu kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.

6 Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria akamfurahisha sana Herode

7 kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti lo lote atakaloomba.

8 Yeye akiwa amefundishwa na mama yake, huyo binti akasema, “Nipatie kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”

9 Mfalme akasikitika, lakini kwa ajili ya kile kiapo alichoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake.

10 Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani.

11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake.

12 Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.

Yesu Alisha Watu Elfu Tano

13 Yesu aliposikia haya yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu, kutoka mijini.

14 Yesu alipofika kando ya bahari aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha, waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”

16 Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”

17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.”

19 Akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate, kisha akawapa wanafunzi wake hiyo mikate na hao samaki, wanafunzi wakawagawia makutano.

20 Wote wakala, wakatosheka, nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

21 Idadi ya wale watu waliokula walikuwa wanaume 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

22 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye chombo watangulie kwenda ng’ambo ya pili ya bahari, wakati yeye anawaaga wale makutano.

23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake.

24 Wakati huo kile chombo kilikuwa kimeshafika mbali kutoka nchi kavu kikisukwasukwa na mawimbi kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.

25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji.

26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi. Msiogope.”

28 Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”

29 Yesu akamwambia, “Njoo.”

Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu.

30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!”

31 Mara Yesu akanyosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”

32 Nao walipoingia ndani ya chombo, upepo ukakoma.

33 Ndipo wote waliokuwamo ndani ya kile chombo wakamwabudu Yesu wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

Yesu Awaponya Wagonjwa Genesareti

34 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti.

35 Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote

36 wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/14-fdea054a7ab78ed9f9ee0c53c4be9752.mp3?version_id=1627—

Mathayo 15

Mapokeo Ya Wazee

1 Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjia Yesu kutoka Yerusalemu na kumwuliza,

2 “Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee waliopita? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”

3 Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu?

4 Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako’ na ‘Ye yote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’

5 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ basi hana tena sababu ya kumsaidia baba yake.

6 Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu.

7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:

8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,

lakini mioyo yao iko mbali nami.

9 Kuniabudu kwao ni bure,

nayo mafundisho yao

ni maagizo ya wanadamu tu.’ ”

Vitu Vitiavyo Unajisi

10 Yesu akaita ule umati wa watu akawaambia, “Sikilizeni na muelewe:

11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”

12 Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumwuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”

13 Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litang’olewa.

14 Waacheni, wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”

15 Petro akasema, “Tuelezee maana ya huu mfano.”

16 Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu?

17 Je, hamuelewi kwamba cho chote kiingiacho kinywani huenda tumboni na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu?

18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi.

19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio.

20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi, lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

Imani Ya Mwanamke Mkanaani

21 Yesu aliondoka mahali pale akaenda sehemu za Tiro na Sidoni.

22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi jirani na sehemu hizo akaja kwake, akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi, binti yangu amepagawa na pepo mchafu na anateseka sana.”

23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”

24 Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”

25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”

26 Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

28 Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

Yesu Aponya Watu Wengi

29 Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko.

30 Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake, naye akawaponya.

31 Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.

Yesu Alisha Watu Elfu Nne

32 Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninahurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula cho chote, nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa wasije wakazimia njiani.”

33 Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”

34 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”

Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”

35 Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini.

36 Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu.

37 Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.

38 Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

39 Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia chomboni akaenda sehemu za Magadani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/15-7cf46e1d05338d4505dbd3dd3979ae42.mp3?version_id=1627—

Mathayo 16

Mafarisayo Wadai Ishara

1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

2 Akawajibu akawaambia, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu,’

3 nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati.

4 Kizazi cha waovu na cha zinaa hutafuta ishara ya majira, lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.

Chachu Ya Mafarisayo Na Masadukayo

5 Wanafunzi wake walipofika ng’ambo ya pili ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate.

6 Yesu akawaambia, “Jihadharini, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”

7 Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”

8 Yesu, akitambua mazungumzo yao, akasema, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate?

9 Je, bado tu hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na ni idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?

10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na ni idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?

11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”

12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

Petro Amkiri Yesu Kuwa Ni Mwana Wa Mungu

13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”

14 Wakamjibu, “Baadhi ya watu husema ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na bado wengine husema, ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”

15 Akawauliza, “Je, ninyi, mnasema mimi ni nani?”

16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”

17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya kuzimu hayataweza kulishinda.

19 Nitakupa funguo za Ufalme wa Mbinguni na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, lo lote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa Mbinguni.”

20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote kwamba yeye ndiye Kristo.

Yesu Anatabiri Juu Ya Kifo Chake

21 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi kwa mikono ya wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa sheria na kwamba itampasa auawe na siku ya tatu atafufuka.

22 Petro akamchukua kando akaanza kumkemea, akisema, “Mungu apishie hayo mbali! Jambo hili kamwe halitakupata!”

23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe na auchukue msalaba wake, anifuate.

25 Kwa maana ye yote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini ye yote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

26 Kwa maana itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya maisha yake?

27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/16-a89bc161473fc620baa899bc75068651.mp3?version_id=1627—

Mathayo 17

Yesu Abadilika Sura Mlimani

1 Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, na kuwaleta mpaka juu ya mlima mrefu mahali pasipo na watu.

2 Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.

3 Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.

4 Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”

5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula, wingu linalong’aa likawafunika na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye sana, msikilizeni yeye.”

6 Wale wanafunzi, waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu.

7 Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.”

8 Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine ye yote isipokuwa Yesu.

9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu ye yote maono haya mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu.”

10 Wale wanafunzi wakamwuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria wanasema kwamba lazima Eliya aje kwanza?”

11 Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza naye atatengeneza mambo yote.

12 Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.”

13 Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.

Yesu Amponya Kijana Mwenye Pepo

14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema,

15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji.

16 Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.”

17 Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi hata lini, nami nitawavumilia hadi lini? Mleteni kijana hapa kwangu.”

18 Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

19 Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakati ambapo hakuna watu, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani kama punje ndogo ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu.”

21 “Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.”

22 Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.

23 Nao watamwua na siku ya tatu atafufuka.” Wanafunzi wakahuzunika sana.

Yesu Na Petro Watoa Kodi Ya Hekalu

24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekaluwakamjia Petro na kumwuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamwuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa.

27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua, fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/17-92d7539442a4741528d3ef4c6aefd5b9.mp3?version_id=1627—

Mathayo 18

Aliye Mkuu Katika Ufalme Wa Mbinguni

1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumwuliza “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”

2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao.

3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

4 Kwa hiyo mtu ye yote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

5 “Ye yote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi.

6 Lakini kama mtu ye yote anamsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini atende dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake na kutoswa katika kilindi cha bahari.

Kujaribiwa Ili Kutenda Dhambi

7 “Ole wa ulimwengu kwa sababu ya yale mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha.

8 Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili na kutupwa katika moto wa milele.

9 Nalo jicho lako kama linakusababisha utende dhambi ling’oe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa katika moto wa jehanamu.

Mfano Wa Kondoo Aliyepotea

10 “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [

11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]

12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu anao kondoo mia moja na mmoja wao akapotea, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea?

13 Naye akisha mpata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea.

14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

Ndugu Yako Akikukosea

15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.

16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe na ushahidi wa mashahidi wawili au watatu.

17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa, naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi mtendeeni mtu huyo kama vile ambavyo mngemtendea asiyeamini.

18 “Amin, nawaambia, lo lote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni na lo lote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lo lote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.

20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

Kusamehe

21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

Mfano Wa Mtumishi Asiyesamehe

23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake.

24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta10,000, aliletwa kwake.

25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.

26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.

28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinarimia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’

29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni.

31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.

32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi.

33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’

34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe kutoka moyoni kila mmoja ndugu yake aliyemkosea.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/18-f0f6800b386bc8af0c723e32fb333ded.mp3?version_id=1627—