Mathayo 19

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

1 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ng’ambo ya Mto Yordani.

2 Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.

3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu wakamwuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yo yote?”

4 Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mtu mume na mtu mke.

5 Naye akasema, ‘Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’

6 Hivyo si wawili tena, bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo kile alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

7 Wakamwuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

8 Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo.

9 Mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

10 Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

11 Yesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu

12 Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine wamefanywa matowashi na wanadamu, na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.

14 Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”

15 Naye akaweka mikono yake juu yao, akaondoka huko.

Kijana Tajiri

16 Mtu mmoja akamjia Yesu na kumwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema ila Mmoja tu, ndiye Mungu: Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

18 Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?”

Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo,

19 waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

20 Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”

21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Hatari Za Utajiri

23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, amin nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni.

24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote yanawezekana.”

27 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata, tutapata nini basi?”

28 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, wakati Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake cha utukufu cha enzi, ninyi mliomfuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.

29 Kila mmoja aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo na ataurithi uzima wa milele.

30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/19-044f95bd7456d6ffbb6211b35e77dea2.mp3?version_id=1627—

Mathayo 20

Mfano Wa Wafanyakazi Katika Shamba La Mizabibu

1 “Kwa maana Ufalme wa Mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri ili kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu.

2 Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinarimoja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.

3 “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi.

4 Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa cho chote kilicho haki yenu.’

5 Kwa hiyo wakaenda.

“Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo.

6 Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’

7 “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna ye yote aliyetuajiri.’

“Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’

8 “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’

9 “Wale vibarua walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakaja na kila mmoja wao akapokea dinari moja.

10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja.

11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba,

12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’

13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja?

14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe.

15 Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’

16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

Yesu Atabiri Tena Kuhusu Kifo Chake

17 Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua kando wale wanafunzi wake kumi na wawili na kuwaambia,

18 “Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, naye Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watamhukumu kifo

19 na kumtia mikononi mwa watu Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulibisha msalabani, naye siku ya tatu atafufuka!”

Ombi La Mama Yake Yakobo Na Yohana

20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akiwa amepiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie upendeleo.

21 Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wape wanangu hawa, mmoja aketi upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”

22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloomba. Je, ninyi mnaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?”

Wakajibu, “Tunaweza.”

23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto, si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao kwa ajili yao zimeandaliwa na Baba yangu.”

24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili.

25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wasiomjua Mungu huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao.

26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,

27 Naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu ni lazima awe mtumwa wenu,

28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

Yesu Awaponya Vipofu Wawili

29 Wakati Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata.

30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, uturehemu!”

31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, uturehemu.”

32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”

34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/20-8627c7391fad704dd0cc028465326b41.mp3?version_id=1627—

Mathayo 21

Yesu Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe

1 Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili,

2 akiwaambia, “Ingieni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtakuta punda amefungwa na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee.

3 Kama mtu ye yote akiwasemesha lo lote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”

4 Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:

5 “Mwambieni Binti Sayuni,

‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,

ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,

juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”

6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza.

7 Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda na Yesu akaketi juu yake.

8 Umati mkubwa wa watu wakatandika nguo zao barabarani na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti wakayatandika barabarani.

9 Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema,

# “HosanaMwana wa Daudi!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Hosana juu mbinguni!”

10 Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”

11 Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”

Yesu Atakasa Hekalu

12 Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni, akazipindua meza za watu waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.

13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.”

14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya.

15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi”, walikasirika.

16 Wakamwuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”

Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,

“ ‘Kutoka katika vinywa vya watoto wachanga

na wale wanaonyonya

umeamuru sifa kamili?’ ”

17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.

Mtini Wanyauka

18 Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa.

19 Akauona mtini kando ya barabara, akaukaribia lakini hakupata tunda lo lote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe na usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.

20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili wakashangaa, wakamwuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”

21 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ nalo litafanyika.

22 Lo lote mtakaloomba katika kusali, mkiamini, mtapokea.”

Wahoji Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

23 Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani, naye ni nani aliyekupa mamlaka hayo?”

24 Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, mimi nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.

25 Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

Wakaanza kuhojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’

26 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’, tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.”

27 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.”

Ndipo akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

Mfano Wa Wana Wawili

28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda’, baadaye akabadili mawazo yake akaenda.

30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vile vile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda baba,’ lakini hakwenda.

31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”

Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”

Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu.

32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.”

Mfano Wa Wapangaji Waovu

33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka akasafiri kwenda nchi nyingine.

34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wakulima waliopangishwa ili kukusanya matunda yake.

35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamwua mwingine na yule wa tatu wakampiga mawe.

36 Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vile vile.

37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakaambiana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njoni na tumwue ili tuchukue urithi wake.’

39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua.

40 “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba, atakapokuja atawafanyia nini hao wakulima?”

41 Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”

42 Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika maandiko kwamba:

“ ‘Lile jiwe walilolikataa waashi

limekuwa jiwe kuu la pembeni;

Bwana ndiye aliyefanya jambo hili,

nalo ni la ajabu machoni petu’?

43 “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake.

44 Yeye aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagika kabisa.”

45 Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao.

46 Wakatafuta njia ya kumkamata lakini wakaogopa ule umati wa watu kwa kuwa wao walimwona Yesu kuwa ni nabii.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/21-94b4bf26981afcc1542db382281bca73.mp3?version_id=1627—

Mathayo 22

Mfano Wa Karamu Ya Arusi

1 Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia,

2 “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi.

3 Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.

4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba karamu iko tayari kwa ajili yenu, nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono. Karibuni.’

5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao, huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake.

6 Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake wakawatenda vibaya na kuwaua.

7 Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.

8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja.

9 Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni ye yote mtakayemwona’

10 Wale watumishi wakaenda barabarani wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.

11 “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi.

12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.

13 “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

14 “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”

Kulipa Kodi Kwa Kaisari

15 Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake.

16 Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode, wakisema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuonyesha tofauti kwa mtu wala upendeleo.

17 Tuambie basi, wewe unaonaje? Ni halali kulipa kodi kwa Kaisari au la?”

18 Lakini Yesu akijua makusudi yao mabaya akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega?

19 Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari.

20 Naye akawauliza, “Sura hii na maandishi haya ni vya nani?”

21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

22 Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.

Ndoa Na Ufufuo

23 Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumwuliza swali, wakisema,

24 “Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’

25 Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane.

26 Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili na wa tatu, hadi wote saba.

27 Hatimaye, yule mwanamke naye akafa.

28 Sasa basi, siku ile ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”

29 Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui maandiko wala uweza wa Mungu.

30 Wakati wa ufufuo watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa Mungu mbinguni.

31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia kwamba,

32 ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’ Yeye si Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai.”

33 Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.

Amri Kuu Kuliko Zote

34 Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja.

35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamwuliza swali ili kumjaribu, akisema,

36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Torati iliyo kuu kuliko zote?”

37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’

38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’

40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Torati na manabii.”

Swali Kuhusu Mwana Wa Daudi

41 Wakati Mafarisayo wakiwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza,

42 “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?”

Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”

43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,

44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

“Keti mkono wangu wa kuume,

hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako.” ’

45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?”

46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumwuliza tena maswali.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/22-063a3a05227d54be53d9d86d7df7f2cc.mp3?version_id=1627—

Mathayo 23

Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria Na Mafarisayo

1 Kisha Yesu akauambia ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake:

2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose,

3 hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri.

4 Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.

5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hufanya vikasha vya ngozi vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao,

6 wanapenda kukaa viti vya sehemu za heshima karamuni na vile viti maalum sana katika masinagogi,

7 hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’

8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu.

9 Nanyi msimwite mtu ye yote ‘Baba,’ hapa duniani kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni.

10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo.

11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.

12 Kwa kuwa ye yote anayejikweza atashushwa na ye yote anayejinyenyekeza atakwezwa.

13 “Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [

14 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo adhabu yenu itakuwa kubwa zaidi.]

15 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja ageuke na kuwafuata ninyi, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi!

16 “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu, lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’

17 Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi, ile dhahabu au lile Hekalu ambalo ndilo linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?

18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu, lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’

19 Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi, ile sadaka, au ile madhabahu ambayo ndiyo inayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu?

20 Kwa hiyo, mtu aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake.

21 Naye mtu aapaye kwa Hekalu, huapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake.

22 Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.

23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani, haki, huruma na uaminifu. Haya imewapasa kuyafanya bila kusahau hayo mengine.

24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!

25 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha nje ya kikombe na kisahani, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi.

26 Enyi Mafarisayo vipofu! Safisheni kwanza ndani ya kikombe na kisahani, ndipo nje patakuwa safi.

27 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu.

28 Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

29 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki.

30 Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’

31 Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii.

32 Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!

33 “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu?

34 Kwa sababu hii tazama nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulibisha, wengine mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na wengine mtawafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine.

35 Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu.

36 Amin, nawaambia, haya yote yatakuja juu ya kizazi hiki.

Yesu Aililia Yerusalemu

37 “Ee Yerusalemu, mnaowaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwenu! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!

38 Tazama nyumba yako imeachwa tupu na ukiwa.

39 Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena mpaka siku ile mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/23-157c78699429655679f525bc292e9da9.mp3?version_id=1627—

Mathayo 24

Kubomolewa Kwa Hekalu Kwatabiriwa

1 Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu.

2 Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, amin nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, kila moja litabomolewa.”

Ishara Za Nyakati Za Mwisho

3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia mahali pasipo na watu, wakamwuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nazo ni nini dalili za kuja kwako na za mwisho wa dunia?”

4 Yesu akawajibu, “Angalieni, mtu asiwadanganye.

5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi.

6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita, angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.

7 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.

8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.

10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana.

11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi.

12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,

13 Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokoka.

14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni pote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo ule mwisho utakapokuja.

15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, asomaye na afahamu,

16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.

17 Ye yote aliyeko juu ya paa la nyumba asishuke ili kuchukua cho chote kutoka ndani ya nyumba.

18 Yeye aliye shambani na asirudi nyumbani kwenda kuchukua vazi lake.

19 Ole wa wenye mimba na wenye watoto wachanga siku hizo!

20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.

21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa, wala haitakuwako tena.

22 Kama siku hizo zisingelifupizwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeliokoka, lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupizwa.

23 Wakati huo kama mtu ye yote akiwaambia, ‘Tazama, huyu hapa ni Kristo! Au Kristo yuko kule!’ Msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo na kufanya ishara kubwa na miujiza mingi ili kuwapotosha, hata ikiwezekana wale wateule hasa.

25 Angalieni, nimetangulia kuwaambia mapema.

26 “Kwa hiyo mtu ye yote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki.

27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

28 Kwa maana po pote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

“ ‘jua litatiwa giza,

nao mwezi hautatoa nuru yake;

nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

na nguvu za anga zitatikisika.’

30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.

31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

32 “Jifunzeni kutokana na mtini. Matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchipua majani, fahamuni kwamba kiangazi kimekaribia.

33 Hata hivyo, mwonapo mambo hayo, jueni kwamba yu karibu malangoni.

34 Amin, amin nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.

35 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa

36 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna ajuaye, hata malaika mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.

37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia kwenye safina,

39 nao hawakujua lo lote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.

40 Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mwingine ataachwa.

41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, mmoja atatwaliwa, mwingine ataachwa.

42 “Kwa hiyo kesheni, kwa maana hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni hili kwamba: Kama mwenye nyumba angelijua ni wakati gani wa usiku ambao mwivi anakuja, angelikesha na asingeliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

Mfano Wa Mtumishi Mwaminifu

45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati muafaka?

46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.

47 Amin, amin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.

48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’

49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake na kula na kunywa pamoja na walevi,

50 bwana wa mtumishi huyo atakuja siku ambayo mtumishi huyo hamtazamii na saa ile ambayo haijui.

51 Atamkata huyo mtumishi vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/24-12b492eae209243b33cb8e7d8107616c.mp3?version_id=1627—

Mathayo 25

Mfano Wa Wanawali Kumi

1 “Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi.

2 Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.

3 Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba,

4 lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo.

5 Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.

6 “Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’

7 “Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao.

8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo, taa zetu zinazimika.’

9 “Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’

10 “Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari, wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.

11 “Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’

12 “Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’

13 “Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.

Mfano Wa Watumishi Watatu Walioachiwa Talanta

14 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu anayetaka kusafiri, akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao.

15 Mmoja akampa talantatano mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri.

16 Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi.

17 Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi.

18 Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake.

19 “Baada ya muda mrefu yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao.

20 Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida talanta tano zaidi.’

21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache, nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

22 “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’

23 “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu, umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache, nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

24 “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu.

25 Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’

26 “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu.

27 Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.

28 “ ‘Basi mnyang’anyeni hiyo talanta mkampe yule mwenye talanta kumi.

29 Kwa maana kila mtu mwenye kitu ataongezewa, naye atakuwa navyo tele. Lakini kwa mtu yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

30 Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

Kondoo Na Mbuzi

31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake.

32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi.

33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wake wa kushoto.

34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha,

36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha au ukiwa na kiu tukakunywesha?

38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au ukiwa uchi tukakuvika?

39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake.

42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha,

43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

45 “Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/25-3f21dbebbc09bdd954a711868fab6301.mp3?version_id=1627—

Mathayo 26

Shauri Baya La Kumwua Yesu

1 Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake,

2 “Mnajua kwamba baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulibiwe.”

3 Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa.

4 Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumwua.

5 Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa sikukuu, la sivyo kutakuwa na ghasia miongoni mwa watu.”

Yesu Anapakwa Mafuta Huko Bethania

6 Wakati Yesu akiwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma,

7 mwanamke mmoja alimjia akiwa na chupa ya marumaru yenye manukato ya thamani kubwa, akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

8 Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Kwa nini ubadhirifu huu wote?

9 Manukato haya yangeliuzwa kwa bei kubwa na fedha hizo wakapewa maskini.”

10 Yesu akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana.

11 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.

12 Alipomiminia haya manukato kwenye mwili amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu.

13 Ninawaambia kweli, mahali po pote habari njema itakapohubiriwa ulimwenguni mwote, jambo hili alilofanya litatajwa pia, kwa ukumbusho wake.”

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

14 Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani

15 na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha.

16 Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wasaa mzuri wa kumsaliti Yesu.

Yesu Ala Pasaka Pamoja Na Wanafunzi

17 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu wanafunzi walimjia Yesu wakamwuliza, “Unataka tuandae wapi kwa ajili yako ili kuila Pasaka?”

18 Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia, nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ”

19 Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu, alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.

20 Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale kumi na wawili.

21 Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22 Wakahuzunika sana, wakaanza kumwambia mmoja mmoja, “Je, ni mimi Bwana?”

23 Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami, ndiye atakayenisaliti.

24 Mwana wa Adamu yu aenda kama alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingelikuwa bora kwake kama asingelizaliwa!”

25 Kisha Yuda, yule aliyemsaliti akasema, “Kweli, si mimi Rabi?”

Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

26 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni, mle, huu ndio mwili wangu.”

27 Kisha akachukua kikombe, akashukuru, akawapa akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki.

28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, ile imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena kutoka katika uzao huu wa mzabibu, mpaka siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

30 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka kwenda mlima wa Mizeituni.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

31 Kisha Yesu akawaambia, “Usiku wa leo ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

“ ‘Nitampiga mchungaji,

nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’

32 Lakini baada ya mimi kufufuka, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

33 Petro akajibu “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

34 Yesu akajibu, “Amin, amin ninakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35 Lakini Petro akasema, “Hata kama itabidi kufa pamoja na wewe, kamwe sitakukana.” Nao wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Yesu Anaomba Gethsemane

36 Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda kule kuomba.”

37 Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, naye akaanza kuhuzunika na kufadhaika.

38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe.”

40 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake na kuwakuta wamelala. Akamwuliza Petro, “Je, ninyi wanaume, hamkuweza kukesha pamoja nami kwa saa moja?

41 Kesheni na muombe, msije mkaanguka majaribuni. Hakika roho iko radhi lakini mwili ni dhaifu.”

42 Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

43 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito.

44 Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

45 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu hana budi kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.

46 Inukeni, twendeni zetu! Huyu hapa yule anisalitiye!”

Yesu Akamatwa

47 Alipokuwa bado anasema, Yuda, mmojawapo wa wale Kumi na Wawili, akafika, akiwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.

48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara kwamba: “yeye nitakayembusu ndiye, mkamateni.”

49 Mara akamjia Yesu na kumsalimu, “salamu, Rabi!” Akambusu.

50 Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”

Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.

51 Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

52 Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga.

53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

54 Lakini je, maandiko yatatimiaje yale yasemayo kwamba ni lazima itokee hivi?”

55 Wakati huo Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Mmetoka na panga na marungu kuja kunikamata kama vile mimi ni mnyang’anyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata?

56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

57 Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika.

58 Lakini Petro akamfuata kwa mbali mpaka uani kwa Kuhani Mkuu. Akaingia ndani akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

59 Basi viongozi wa wazee, makuhani na baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumwua.

60 Lakini hawakupata jambo lo lote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo

61 na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62 Kisha Kuhani Mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi wa namna gani hawa watu wauletao dhidi yako?”

63 Lakini Yesu alikuwa kimya.

# Ndipo Kuhani Mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai, tuambie ikiwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”

64 Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote, tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65 Ndipo Kuhani Mkuu akararua nguo zake na kusema, “Amekufuru! Kwa nini tunahitaji ushahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru.

66 Uamuzi wenu ni nini?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67 Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine walimpiga makofi

68 na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Petro Amkana Bwana Yesu

69 Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

70 Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

71 Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwapo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

72 Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

73 Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana ile namna yako ya kusema ni kama yao.”

74 Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

Papo hapo jogoo akawika.

75 Ndipo Petro akakumbuka lile neno alilokuwa amesema Yesu, “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Akaenda nje, akalia sana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/26-b8d260ee828f3c6962137190d2856308.mp3?version_id=1627—

Mathayo 27

Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato

1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumwua.

2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala.

Yuda Ajinyonga

3 Yuda, ambaye ndiye aliyekuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.

4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6 Wale makuhani wakuu wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.”

7 Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni.

8 Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo.

9 Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli,

10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Yesu Mbele Ya Pilato

11 Wakati Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamwuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.

13 Ndipo Pilato akamwuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”

14 Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja atakayechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.

16 Wakati huo alikuwapo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.

17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?”

18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lo lote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”

Wakajibu, “Baraba.”

22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”

Wakajibu wote, “Msulibishe!”

23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakazidi kupiga kelele, “Msulibishe.”

24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lo lote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”

25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

26 Basi akawafungulia Baraba na baada ya kumchapa Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.

Askari Wamdhihaki Yesu

27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitoriona wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.

28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha

29 wakasokota taji ya miiba wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki wakisema “salamu, mfalme wa Wayahudi!”

30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.

31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile vazi, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili kumsulibisha.

Yesu Asulibishwa

32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.

33 Wakafika mahali paitwapo Golgotha (ambayo maana yake ni, Mahali pa Fuvu la Kichwa),

34 wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe, lakini alipoionja, akakataa kuinywa.

35 Walipokwisha kumsulibisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura, [ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]

36 Kisha wakaketi, wakamchunga.

37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.

38 Wanyang’anyi wawili walisulibiwa pamoja naye, mmoja kuume kwake na mwingine kushoto kwake.

39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamvurumishia matukano huku wakitikisa vichwa vyao

40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

41 Vivyo hivyo, viongozi wa, makuhani, walimu wa sheria na wazee wakamdhihaki wakisema,

42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, tutamwamini.

43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ”

44 Hata wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

Kifo Cha Yesu

45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza lilifunika nchi yote.

46 Ilipofika saa tisa Yesu akapaza sauti akalia,“Eloi, Eloi lama Sabakthani?”Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

47 Baadhi ya wale watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia haya, wakasema “Anamwita Eliya.”

48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi akampa Yesu ili anywe.

49 Wengine wakasema, “Mwacheni na tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.

52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuka.

53 Wakatoka makaburini na baada ya Yesu kufufuka waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, wakaogopa wakasema, “Hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu!”

55 Walikuwako wanawake huko, wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulika na mahitaji yake.

56 Miongoni mwao walikuwapo Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo na Yosefu na mama yao wana wa Zebedayo.

Maziko Ya Yesu

57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathea aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.

58 Akamwendea Pilato, kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe.

59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akauviringishia nguo ya kitani safi nyeupe

60 na kuuzika kwenye kaburi lake mwenyewe jipya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mlangoni mwa kaburi, akaenda zake.

61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwapo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

Walinzi Pale Kaburini

62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato

63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu kabla hajafa alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’

64 Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuka kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.”

66 Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/27-52f4057a249835fb52788d246254f4bf.mp3?version_id=1627—

Mathayo 28

Yesu Afufuka

1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.

2 Ghafula pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni akaenda penye kaburi akalivingirisha lile jiwe na kulikalia.

3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.

4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.

5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa.

6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa.

7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtakakomwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini, wakiwa wamejawa na hofu lakini wenye furaha nyingi, wakaenda mbio ili kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo.

9 Ghafula Yesu akakutana nao, akasema, “salamu!” Wale wanawake wakamkaribia wakaishika miguu yake, wakamwabudu.

10 Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Taarifa Ya Walinzi

11 Wakati wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia.

12 Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha

13 wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’

14 Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lo lote.”

15 Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.

Yesu Awatuma Wanafunzi Wake

16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza.

17 Walipomwona, wakamwabudu, lakini baadhi yao wakaona shaka.

18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19 Kwa sababu hii, enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu,

20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.” Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/28-39505513c8105efac416b48c5e89234f.mp3?version_id=1627—