Hosea 8

Israeli Kuvuna Kisulisuli

1 “Wekeni tarumbeta midomoni mwenu!

Tai yuko juu ya nyumba yaBwana

kwa sababu watu wamevunja Agano langu,

wameasi dhidi ya sheria yangu.

2 Israeli ananililia,

‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’

3 Lakini Israeli amekataa lile lililo jema,

adui atamfuatia.

4 Wanaweka Wafalme bila idhini yangu,

wamechagua wakuu bila kibali changu.

Kwa fedha zao na dhahabu

wamejitengenezea sanamu kwa ajili

ya maangamizi yao wenyewe.

5 Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama!

Hasira yangu inawaka dhidi yao.

Watakuwa najisi mpaka lini?

6 Zimetoka katika Israeli!

Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu.

Atavunjwa vipande vipande,

yule ndama wa Samaria.

7 “Wanapanda upepo

na kuvuna upepo wa kisulisuli.

Bua halina suke,

halitatoa unga.

Kama lingetoa nafaka,

wageni wangeila yote.

8 Israeli amemezwa;

sasa yupo miongoni mwa mataifa

kama kitu kisicho na thamani.

9 Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru

kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake.

Efraimu amejiuza mwenyewe

kwa wapenzi.

10 Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa,

sasa nitawakusanya pamoja.

Wataanza kudhoofika chini ya uonevu

wa mfalme mwenye nguvu.

11 “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi

kwa ajili ya sadaka za dhambi,

hizi zimekuwa madhabahu

za kufanyia dhambi.

12 Nimeandika kwa ajili yao mambo mengi

kuhusu sheria yangu,

lakini wameziangalia

kama kitu cha kigeni.

13 Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi

nao wanakula hiyo nyama,

lakiniBwanahapendezwi nao.

Sasa ataukumbuka uovu wao

na kuadhibu dhambi zao:

Watarudi Misri.

14 Israeli amemsahau Muumba wake

na kujenga majumba ya kifalme,

Yuda amejengea miji mingi ngome.

Lakini nitatuma moto kwenye miji yao

utakaoteketeza ngome zao.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/8-1765a550030a08f098e3f8b63100e9f7.mp3?version_id=1627—

Hosea 9

Adhabu Kwa Israeli

1 Usifurahie, Ee Israeli;

usishangilie kama mataifa mengine.

Kwa kuwa hukuwa

mwaminifu kwa Mungu wako;

umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu

ya kupuria nafaka.

2 Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai

havitalisha watu,

divai mpya itawapungukia.

3 Hawataishi katika nchi yaBwana,

Efraimu atarudi Misri

na atakula chakula

kilicho najisi huko Ashuru.

4 HawatammiminiaBwanasadaka ya divai

wala dhabihu zao hazitampendeza.

Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao

kama mkate wa waombolezaji;

nao wote wailao watakuwa najisi.

Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe;

kisije katika Hekalu laBwana.

5 Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamuriwa,

katika siku za sikukuu zaBwana?

6 Hata ikiwa wataokoka maangamizi,

Misri atawakusanya,

# nayo Memfisiitawazika.

Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma,

nayo miiba itafunika mahema yao.

7 Siku za adhabu zinakuja,

siku za malipo zimewadia.

Israeli na afahamu hili.

Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana

na uadui wenu ni mkubwa sana,

nabii anadhaniwa ni mpumbavu,

mtu aliyeongozwa na Mungu

anaonekana mwenda wazimu.

8 Nabii, pamoja na Mungu wangu,

ndiye mlinzi juu ya Efraimu,

hata hivyo mitego inamngojea

katika mapito yake yote,

na uadui katika nyumba ya Mungu wake.

9 Wamezama sana katika rushwa,

kama katika siku za Gibea.

Mungu atakumbuka uovu wao

na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.

10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama

kupata zabibu jangwani;

nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona

matunda ya kwanza katika mtini.

Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu

kwa ile sanamu ya aibu,

nao wakawa najisi

kama kitu kile walichokipenda.

11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege:

hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba,

hakuna kutunga mimba.

12 Hata wakilea watoto,

nitamwua kila mmoja.

Ole wao

nitakapowapiga kisogo!

13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro,

aliyeoteshwa mahali pazuri.

Lakini Efraimu wataleta

watoto wao kwa mchinjaji.”

14 Wape, EeBwana,

je, utawapa nini?

Wape matumbo ya kuharibu mimba

na matiti yaliyokauka.

15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,

niliwachukia huko.

Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,

nitawafukuza katika nyumba yangu.

Sitawapenda tena,

viongozi wao wote ni waasi.

16 Efraimu ameharibiwa,

mzizi wao umenyauka,

hawazai tunda.

Hata kama watazaa watoto,

nitawachinja watoto wao

waliotunzwa vizuri.”

17 Mungu wangu atawakataa

kwa sababu hawakumtii;

watakuwa watu wa kutangatanga

miongoni mwa mataifa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/9-cf5284957e19d6f9703ac09c90732ebf.mp3?version_id=1627—

Hosea 10

1 Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,

alijizalia matunda mwenyewe.

Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,

alijenga madhabahu zaidi;

kadiri nchi yake ilivyostawi,

alipamba mawe yake ya ibada.

2 Moyo wao ni mdanganyifu,

nao sasa lazima wachukue hatia yao.

Bwanaatabomoa madhabahu zao

na kuharibu mawe yao ya ibada.

3 Kisha watasema, “Hatuna mfalme

kwa sababu hatukumheshimuBwana.

Lakini hata kama tungelikuwa na mfalme,

angeweza kutufanyia nini?”

4 Wanaweka ahadi nyingi,

huapa viapo vya uongo

wanapofanya mapatano;

kwa hiyo mashtaka huchipuka

kama magugu ya sumu

katika shamba lililolimwa.

5 Watu wanaoishi Samaria huogopa

# kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni.

Watu wake wataiombolezea,

vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu,

wale waliokuwa wamefurahia fahari yake,

kwa sababu itaondolewa kutoka kwao

kwenda uhamishoni.

6 Itachukuliwa kwenda Ashuru

kama ushuru kwa mfalme mkuu.

Efraimu atafedheheshwa;

Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.

7 Samaria na mfalme wake wataelea

kama kijiti juu ya uso wa maji.

8 Mahali pa kuabudia sanamu pa uovupataharibiwa:

ndiyo dhambi ya Israeli.

Miiba na mibaruti itaota

na kufunika madhabahu zao.

Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!”

na vilima, “Tuangukieni!”

9 “Tangu siku za Gibea, mmetenda dhambi, Ee Israeli,

huko ndiko mlikobaki.

Je, vita havikuwapata

watenda mabaya huko Gibea?

10 Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu;

mataifa yatakusanywa dhidi yao

ili kuwaweka katika vifungo

kwa ajili ya dhambi zao mbili.

11 Efraimu ni mtamba wa ng’ombe aliyefundishwa

ambaye hupenda kupura,

hivyo nitamfunga nira

juu ya shingo yake nzuri.

Nitamwendesha Efraimu,

Yuda lazima alime,

naye Yakobo lazima avunjevunje

mabonge ya udongo.

12 Jipandieni wenyewe haki,

vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,

vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;

kwa kuwa ni wakati wa kumtafutaBwana,

mpaka atakapokuja

na kuwanyeshea juu yenu haki.

13 Lakini mmepanda uovu,

mkavuna ubaya,

mmekula tunda la udanganyifu.

Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe

na wingi wa mashujaa wenu,

14 mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako,

ili kwamba ngome zako zote zitaharibiwa:

kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita,

wakati mama pamoja na watoto wao

walipotupwa kwa nguvu ardhini.

15 Ndivyo itakavyotokea kwako, Ee Betheli,

kwa sababu uovu wako ni mkuu.

Siku ile itakapopambazuka,

mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/10-8a3954d8315f85488382196086d379dc.mp3?version_id=1627—

Hosea 11

Upendo Wa Mungu Kwa Israeli

1 “Wakati Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda,

nilimwita mwanangu kutoka Misri.

2 Lakini kadiri nilivyomwita Israeli,

ndivyo walivyokwenda mbali nami.

Walitoa dhabihu kwa Mabaali

na kufukiza uvumba kwa vinyago.

3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea,

nikiwashika mikono;

lakini hawakutambua

kuwa ni mimi niliyewaponya.

4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu,

kwa vifungo vya upendo;

niliondoa nira shingoni mwao

nami nikainama kuwalisha.

5 “Je, hawatarudi Misri,

nayo Ashuru haitawatawala

kwa sababu wamekataa kutubu?

6 Panga zitametameta katika miji yao,

zitaharibu makomeo ya malango yao

na kukomesha mipango yao.

7 Watu wangu wamedhamiria kuniacha.

Hata kama wakimwita Yeye Aliye Juu Sana,

kwa vyo vyote hatawainua.

8 “Efraimu, ninawezaje kukuacha?

Ee Israeli, ninawezaje kukutoa?

Nitawezaje kukutendea kama Adma?

Nitawezaje kukufanya kama Seboimu?

Moyo wangu umegeuka ndani yangu,

huruma zangu zote zimeamshwa.

9 Sitatimiza hasira yangu kali,

wala sitageuka na kumharibu Efraimu.

Kwa kuwa mimi ndimi Mungu,

wala si mwanadamu,

Mtakatifu pekee miongoni mwenu.

Sitakuja kwa ghadhabu.

10 WatamfuataBwana;

atanguruma kama simba.

Wakati angurumapo,

watoto wake watakuja wakitetemeka

kutoka magharibi.

11 Watakuja wakitetemeka

kama ndege wakitoka Misri,

kama hua wakitoka Ashuru.

Nitawakalisha katika nyumba zao,”

asemaBwana.

Dhambi Ya Israeli

12 Efraimu amenizunguka kwa uongo,

nyumba ya Israeli kwa udanganyifu.

Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu,

hata kinyume cha yeye

aliye mwaminifu Mtakatifu Pekee.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/11-000f60637bc045ab5428ac4196071c11.mp3?version_id=1627—

Hosea 12

1 Efraimu anajilisha upepo;

hufukuzia upepo wa mashariki kutwa nzima

na kuzidisha uongo na jeuri.

Anafanya mkataba na Ashuru

na kutuma mafuta ya zeituni Misri.

2 Bwanaanalo shtaka dhidi ya Yuda,

atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake

na kumlipa kwa kadiri ya matendo yake.

3 Yakobo akiwa tumboni alishika kisigino cha kaka yake;

kama mwanadamu, alishindana na Mungu.

4 Alishindana na malaika na kumshinda;

alilia na kuomba upendeleo wake.

Alimkuta huko Betheli

na kuzungumza naye huko:

5 BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote,

Bwanandilo jina lake!

6 Lakini ni lazima urudi kwa Mungu wako;

dumisha upendo na haki,

nawe umngojee Mungu wako siku zote.

7 Mfanyabiashara hutumia vipimo vya udanganyifu;

hupenda kupunja.

8 Efraimu hujisifu akisema,

“Mimi ni tajiri sana; nimetajirika.

Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu

uovu wo wote au dhambi.”

9 “Mimi ndimiBwanaMungu wenu

niliyewaleta kutoka Misri;

nitawafanya mkae tena kwenye mahema,

kama vile katika siku

za sikukuu zenu zilizoamuriwa.

10 Niliongea na manabii, nikawapa maono mengi

na kusema mifano kupitia wao.”

11 Je, Gileadi si mwovu?

Watu wake hawafai kitu!

Je, hawatoi dhabihu za mafahali huko Gilgali?

Madhabahu zao zitakuwa

kama malundo ya mawe

katika shamba lililolimwa.

12 Yakobo alikimbilia katika nchi ya Aramu;

Israeli alitumika ili apate mke,

ili aweze kulipa kwa ajili yake alichunga kondoo.

13 Bwanaalimtumia nabii

kumpandisha Israeli kutoka Misri,

kwa njia ya nabii alimtunza.

14 Lakini Efraimu amemchochea sana hasira;

Bwana wake ataleta juu yake

hatia yake ya kumwaga damu naye atamlipiza

kwa ajili ya dharau yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/12-78dc8f9269267ff93ed97af1852f50f0.mp3?version_id=1627—

Hosea 13

Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli

1 Wakati Efraimu alipozungumza, watu walitetemeka,

alikuwa ametukuzwa katika Israeli.

Lakini alikuwa na hatia ya kumwabudu Baali

naye akafa.

2 Sasa wanatenda dhambi zaidi na zaidi;

wanajitengenezea sanamu

kutokana na fedha yao,

vinyago vilivyotengenezwa kwa uhodari,

vyote kazi ya fundi stadi.

Inasemekana kuhusu hawa watu,

“Hutoa dhabihu za binadamu

na kubusu sanamu za ndama.”

3 Kwa hiyo watakuwa kama ukungu wa asubuhi,

kama umande wa alfajiri utowekao,

kama makapi yapeperushwayo

kutoka katika sakafu ya kupuria nafaka,

kama moshi utorokao kupitia dirishani.

4 “Bali mimi ndimiBwanaMungu wenu,

niliyewaleta ninyi toka Misri.

Msimkubali Mungu mwingine ila mimi,

hakuna Mwokozi isipokuwa mimi.

5 Niliwatunza huko jangwani,

katika nchi yenye joto liunguzalo.

6 Nilipowalisha, walishiba,

waliposhiba, wakajivuna,

kisha wakanisahau mimi.

7 Kwa hiyo nitakuja juu yao kama simba,

kama chui nitawavizia kando ya njia.

8 Kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake,

nitawashambulia na kurarua vifua vyenu.

Kama simba nitawala;

mnyama pori atawararua vipande vipande.

9 “Ee Israeli, Umeharibiwa,

kwa sababu wewe u kinyume nami,

kinyume na msaidizi wako.

10 Yuko wapi mfalme wako,

ili apate kukuokoa?

Wako wapi watawala wako katika miji yako yote

ambao ulisema kuwahusu,

‘Nipe mfalme na wakuu’?

11 Hivyo katika hasira yangu nilikupa mfalme

na katika ghadhabu yangu nilimwondoa.

12 Kosa la Efraimu limehifadhiwa,

dhambi zake zimewekwa katika kumbukumbu.

13 Utungu kama wa mwanamke anayejifungua mtoto humjia,

lakini yeye ni mtoto asiyekuwa na hekima;

wakati utakapowadia hatatoka

katika tumbo la mama yake.

14 “Nitawakomboa watu hawa kutoka nguvu za kaburi,

nitawakomboa kutoka mautini.

Yako wapi, Ee mauti, mateso yako?

Uko wapi, Ee kuzimu, uharibifu wako?

“Sitakuwa na huruma,

15 hata ingawa Efraimu atastawi

miongoni mwa ndugu zake.

Upepo wa mashariki kutoka kwaBwanautakuja,

ukivuma kutoka jangwani,

chemchemi yake haitatoa maji

na kisima chake kitakauka.

Ghala yake itatekwa

hazina zake zote.

16 Watu wa Samaria ni lazima wabebe hatia yao,

kwa sababu wameasi dhidi ya Mungu wao.

Wataanguka kwa upanga;

watoto wao wadogo watatupwa kwa nguvu ardhini,

wanawake wao walio na mimba watatumbuliwa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/13-4d260f4230ffca6f074e731e55a03566.mp3?version_id=1627—

Hosea 14

Toba Ya Kuleta Baraka

1 Rudi, Ee Israeli, kwaBwanaMungu wako.

Dhambi zako zimekuwa

ndilo anguko lako!

2 Chukueni maneno pamoja nanyi,

na mumrudieBwana.

Mwambieni:

“Samehe dhambi zetu zote

na utupokee kwa neema,

ili tuweze kutoa matunda yetu

kama sadaka za mafahali.

3 Ashuru hawezi kutuokoa,

hatutapanda farasi wa vita.

Kamwe hatutasema tena ‘Miungu yetu’

kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,

kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”

4 “Nitaponya ukaidi wao

na kuwapenda kwa hiari yangu,

kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.

5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli;

atachanua kama yungiyungi.

Kama mwerezi wa Lebanoni

atashusha mizizi yake chini;

6 matawi yake yatatanda.

Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,

harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.

7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake.

Atastawi kama nafaka.

Atachanua kama mzabibu,

nao umaarufu wake utakuwa

kama divai itokayo Lebanoni.

8 Ee Efraimu, utasema, ‘Mimi nina shughuli gani tena na sanamu?’

Nitamjibu na kumtunza.

Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;

kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”

9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.

Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.

Njia zaBwanani adili;

wenye haki huenda katika njia hizo,

lakini waasi watajikwaa ndani yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HOS/14-521fc4943468d9e6135356aa63b8d720.mp3?version_id=1627—

Danieli 1

Mafunzo Ya Danieli Huko Babeli

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi.

2 Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza pamoja na baadhi ya vyombo kutoka katika Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari naye akaviweka katika nyumba ya hazina ya mungu wake.

3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa jumba lake la kifalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya kifalme na kutoka watu mashuhuri,

4 vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha ujuzi katika kila elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo.

5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka katika meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.

6 Miongoni mwa hawa vijana baadhi walikuwa kutoka Yuda: Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria.

7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya, Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki na Azaria akamwita Abednego.

8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha kifalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa kwa ajili ya kutokujinajisi kwa njia hii.

9 Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli,

10 lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu ni mbaya kuliko za vijana rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”

11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria,

12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe cho chote ila nafaka na mboga za majanitule na maji ya kunywa.

13 Ndipo ulinganishe kuonekana kwetu na vijana wanaokula chakula cha kifalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.”

14 Basi akakubali jambo hili akawajaribu kwa siku kumi.

15 Mwisho wa zile siku kumi walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko ye yote kati ya wale vijana waliokula chakula cha kifalme.

16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.

17 Mungu akawapa hawa vijana waume wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza.

19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyekuwa amelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme.

20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.

21 Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Mfalme Koreshi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/1-4ee83ff26b72d26874b0f661463536f0.mp3?version_id=1627—

Danieli 2

Ndoto Ya Nebukadneza

1 Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto, akili yake ikasumbuka na hakuweza kulala.

2 Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme,

3 akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua nami nataka nijue maana yake.”

4 Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”

5 Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti, ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi.

6 Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.”

7 Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.”

8 Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kuvuta muda, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti:

9 Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwa ajili yenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.”

10 Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vile vile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu ye yote.

11 Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna ye yote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.”

12 Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli.

13 Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue.

14 Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara.

15 Akamwuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo.

16 Katika jambo hili, Danieli akamwendea mfalme akamwomba ampe muda, ili aweze kumfasiria ile ndoto.

17 Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Meshaki na Azaria jambo hilo.

18 Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbingu kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.

19 Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni,

20 na akasema:

“Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele,

hekima na uweza ni vyake.

21 Yeye hubadili nyakati na majira,

huwaweka wafalme na kuwaondoa.

Huwapa hekima wenye hekima

na maarifa wenye ufahamu.

22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika,

anajua yale yaliyo gizani,

nuru hukaa kwake.

23 Ninakushukuru na kukuhimidi,

Ee Mungu wa baba zangu:

Umenipa hekima na uwezo,

umenijulisha kile tulichokuomba,

umetujulisha kujua ndoto ya mfalme.”

Danieli Aifasiri Ndoto

24 Ndipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.”

25 Arioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme ndoto yake inamaanisha nini.”

26 Mfalme akamwuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”

27 Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza,

28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita akilini mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:

29 “Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonyesha ni kitu gani kitakachotokea.

30 Kwangu mimi, siri hii imefunuliwa kwangu, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ni ili wewe, Ee mfalme, upate kujua tafsiri na ili uweze kuelewa kile kilichopita akilini mwako.

31 “Ee mfalme, ulitazama na mbele yako ilisimama sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu inayong’aa inayotisha kwa kuonekana kwake.

32 Kichwa cha ile sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha, tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba,

33 miguu yake ilikuwa ya chuma, kwa sehemu nyayo zake zilikuwa chuma na sehemu nyingine zilikuwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa.

34 Ulipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo wa mfinyanzi na kuivunja.

35 Ndipo ile chuma, ule udongo wa mfinyanzi, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja na kuwa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.

36 “Hii ndiyo iliyokuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme.

37 Ee mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu na utukufu,

38 mikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani. Po pote waishipo amekufanya wewe kuwa mtawala juu yao wote. Wewe ndiye kile kichwa cha dhahabu.

39 “Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye, utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, utatawala juu ya dunia yote.

40 Hatimaye, kutakuweko na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu, kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote.

41 Kama vile ulivyoona kuwa kwa sehemu nyayo na vidole vilikuwa vya udongo wa mfinyanzi uliochomwa na kwa sehemu nyingine chuma, hivyo huu utakuwa ufalme uliogawanyikagawanyika, hata hivyo kutakuwa na baadhi zenye nguvu za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona chuma imechanganywa na udongo wa mfinyanzi.

42 Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na sehemu udongo wa mfinyanzi, hivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu.

43 Kama vile ulivyoona chuma kikiwa kimechanganyikana na udongo wa mfinyanzi uliochomwa, ndivyo watu watakavyokuwa mchanganyiko wala hawatabaki kuwa wameungana tena kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.

44 “Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele.

45 Hii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu vipande vipande.

“Mungu Mkuu amemwonyesha mfalme kile kitakachotokea wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.”

46 Ndipo Mfalme Nebukadneza akaanguka kifudifudi mbele ya Danieli kumpa heshima na kuagiza kwamba wamtolee Danieli sadaka na uvumba.

47 Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu na Bwana wa wafalme na mfunuaji wa siri zote, kwa maana umeweza kufunua siri hii.”

48 Ndipo mfalme akamweka Danieli kwenye nafasi ya juu na kumpa zawadi nyingi tele. Akamfanya kuwa mtawala wa jimbo lote la Babeli na kumweka kuwa mkuu wa wote wenye hekima.

49 Zaidi ya hayo, kwa ombi la Danieli mfalme akawateua Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa jimbo la Babeli, huku Danieli akibaki katika ukumbi wa kifalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/2-5f025cd69caa5915457c7a76108715d3.mp3?version_id=1627—

Danieli 3

Sanamu Ya Dhahabu Na Moto Mkali

1 Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitinina upana wake dhiraa sita, akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la nchi ya Babeli.

2 Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.

3 Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wa jimbo walikusanyika kwa ajili ya kuizindua sanamu ile ambayo mfalme alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu.

4 Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, kusema, “Enyi watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya:

5 Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima mwanguke chini na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha.

6 Mtu ye yote ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.”

7 Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda na aina zote za ala za uimbaji, watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha wakaanguka chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.

8 Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi.

9 Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele!

10 Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda, zumari na aina zote za ala za uimbaji lazima aanguke chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu,

11 na kwamba ye yote ambaye hataanguka chini na kuiabudu atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.

12 Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli: yaani, Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, Ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

13 Mfalme Nebukadneza akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme,

14 naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?

15 Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Naye ni mungu yupi atakayeweza kuwaokoa ninyi, kutoka katika mkono wangu?”

16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea wenyewe mbele zako kuhusu jambo hili,

17 ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, Ee mfalme.

18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, Ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

19 Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika juu yao. Akaagiza tanuru ichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake

20 na kuwaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu kuliko wengine wote katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa ndani ya tanuru iwakayo moto.

21 Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine.

22 Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowachukuwa Shadraki, Meshaki na Abednego.

23 Watu hawa watatu, wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana, walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto.

24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”

Washauri wakajibu, “Hakika, Ee mfalme.”

25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembea-tembea ndani ya moto, hawakufungwa na hawakudhurika, naye mtu yule wanne anaonekana kama mwana wa miungu.”

26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njoni huku!”

Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto.

27 Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa kifalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao.

28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Waliomtumaini na kutoogopa amri ya mfalme nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine ye yote isipokuwa Mungu wao.

29 Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lo lote au lugha yo yote watakaosema kitu cho chote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”

30 Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/3-655d7a63af06b510f0e85976e4d007c5.mp3?version_id=1627—