Danieli 4

Ndoto Ya Nebukadneza Ya Mti

1 Mfalme Nebukadneza,

Kwa kabila za watu, mataifa na watu wa kila lugha, wanaoishi katika ulimwengu wote:

Amani na mafanikio yawe kwenu!

2 Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara ya miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia.

3 Tazama jinsi ishara zake zilivyo kuu,

jinsi maajabu yake

yalivyo na nguvu!

Ufalme wake ni ufalme wa milele;

enzi yake hudumu

kutoka kizazi hadi kizazi.

4 Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiwa ninaishi kwa raha na hali yakufanikiwa.

5 Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita akilini mwangu vilinitisha.

6 Hivyo nikaagiza kwamba watu wote wenye hekima wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu.

7 Walipokuja waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria.

8 Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.)

9 Nilisema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa Roho ya Miungu Mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie.

10 Haya ndiyo maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana.

11 Mti ule ulikua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga, ulionekana mpaka miisho ya dunia.

12 Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.

13 “Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, mbele yangu alikuwepo mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni.

14 Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yaondoeni majani na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake na ndege wakimbie kutoka katika matawi yake.

15 Lakini acheni kisiki chake na mizizi, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni.

“ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia.

16 Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu na apewe akili ya mnyama, mpaka nyakati saba zipite juu yake.

17 “ ‘Uamuzi huu umetangazwa na walinzi, hukumu hii imetangazwa na watakatifu, ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme zote za wanadamu, naye humpa ye yote amtakaye na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’

18 “Hii ndiyo niliyopata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe waweza, kwa sababu Roho ya Miungu Mitakatifu imo ndani yako.”

Danieli Anafasiri Ndoto

19 Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa kitambo, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.”

Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingehusu adui zako na maana yake iwahusu watesi wako!

20 Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikigusa anga na kuonekana duniani kote,

21 ukiwa na majani yakupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani,

22 Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu, ukuu wako umekua mpaka kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea mpaka miisho ya dunia.

23 “Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni na kusema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na kwa shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama-pori mpaka nyakati saba zipite juu yake.’

24 “Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme:

25 Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori, utakula manyasi kama ng’ombe na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza ye yote amtakaye.

26 Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejezwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo zitawalazo.

27 Kwa hiyo, Ee mfalme, uwe radhi kupokea shauri langu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako uwe na huruma kwa walioonewa. Hivyo itawezekana baada ya hayo mafanikio yako yakaendelea.”

Ndoto Inatimia

28 Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza.

29 Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli,

30 alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”

31 Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya kifalme yameondolewa kutoka kwako.

32 Utafukuzwa mbali na wanadamu ukaishi pamoja na wanyama pori, utakula manyasi kama ng’ombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza ye yote amtakaye.”

33 Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege.

34 Mwisho wa huo wakati, mimi Nebukadneza, niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele.

Utawala wake ni utawala wa milele;

ufalme wake hudumu

kutoka kizazi na kizazi.

35 Mataifa yote ya dunia

yanahesabiwa kuwa si kitu.

Hufanya kama atakavyo

kwa majeshi ya mbinguni

na kwa mataifa ya dunia.

Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake

au kumwambia,

“Umefanya nini wewe?”

36 Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, heshima yangu na fahari yangu nikarudishiwa kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni.

37 Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/4-97fc40d46c29909901fa2fb18214e3b0.mp3?version_id=1627—

Danieli 5

Maandishi Ukutani

1 Mfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kwa ajili ya maelfu ya wakuu wake na akanywa mvinyo pamoja nao.

2 Wakati Belshaza alipokuwa akinywa mvinyo wake, aliamuru viletwe vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekaluni huko Yerusalemu, ili mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake waweze kuvinywea.

3 Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka katika Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea.

4 Walipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu, ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe.

5 Ghafula vidole vya kitanga cha mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika.

6 Uso wa mfalme ukageuka rangi naye aliogopa sana kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.

7 Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waganga waletwe, naye akawaambia hawa wenye hekima wa Babeli, “Ye yote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake, atavikwa nguo za zambarau na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.”

8 Ndipo watu wote wa mfalme wenye hekima wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake.

9 Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.

10 Malkiaaliposikia sauti za mfalme na wakuu wake alikuja akaingia katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele. Usishtuke! Usibadilike rangi kiasi hicho!

11 Yuko mtu katika ufalme wako ambaye ana Roho ya Miungu Mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, yaani nasema mfalme baba yako, alimtuma kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi.

12 Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”

13 Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Uyahudi?

14 Nimesikia kwamba Roho ya Miungu iko ndani yako na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee.

15 Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia.

16 Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.”

17 Ndipo Danieli akamjibu mfalme, “Waweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine ye yote zawadi zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa ajili ya mfalme na kumwambia maana yake.

18 “Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari.

19 Kwa sababu ya nafasi ya juu aliyompa baba yako, kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua, wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai, wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha, aliotaka kuwashusha, aliwashusha.

20 Lakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwenye kiti chake cha utawala cha kifalme na kuvuliwa utukufu wake.

21 Akafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu, akala majani kama ng’ombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, mpaka alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala juu ya falme za wanadamu na kwamba humtawaza juu yao ye yote amtakaye.

22 “Lakini wewe mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote.

23 Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha, ya dhahabu, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe, miungu ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.

24 Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.

25 “Haya ndiyo maneno yaliyoandikwa:

MENE, MENE, TEKELI NA PERESI

26 “Hii ndiyo maana ya maneno haya:

Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.

27 Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua.

28 Peresi: Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.”

29 Ndipo kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.

30 Usiku ule ule Belshaza, mfalme wa Babeli akauawa,

31 naye Dario Mmedi akashika ufalme akiwa na miaka sitini na miwili.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/5-a7f0df05244ac226fbe9d69f6a2c2047.mp3?version_id=1627—

Danieli 6

Danieli Katika Tundu La Simba

1 Ilimpendeza Dario kuteua wakuu 120 kutawala katika ufalme wake wote,

2 pamoja na wasimamizi watatu juu yao, ambao mmoja wao alikuwa Danieli. Wakuu walitoa hesabu kwa hao wasimamizi ili mfalme asipate hasara.

3 Basi Danieli alijidhihirisha mwenyewe, miongoni mwa wasimamizi na wakuu kwa sifa zake za kipekee hata mfalme akapanga kumweka juu ya ufalme wote.

4 Kwa hili, wakuu na wasimamizi wakajaribu kutafuta sababu za kumshitaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu na wala hakupatikana na upotovu wala uzembe.

5 Mwishoni watu hawa walisema, “Kamwe hatutapata msingi kwa ajili ya mashtaka dhidi ya mtu huyu Danieli isipokuwa kile kinachohusiana na sheria ya Mungu wake.”

6 Basi wasimamizi na wakuu wakaingia kwa mfalme kama kikundi wakasema, “Ee Mfalme Dario, uishi milele!

7 Wasimamizi wa kifalme, wasaidizi, wakuu, washauri na watawala wote wamekubaliana kwamba mfalme atoe sheria na kukazia amri kuwa ye yote atakayemwomba Mungu ye yote au mwanadamu katika muda huu wa siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, Ee mfalme, atatupwa ndani ya tundu la simba.

8 Sasa, Ee mfalme, toa amri na uiandike ili kwamba isiweze kubadilishwa, kwa kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.”

9 Hivyo Mfalme Dario akaiweka amri hiyo katika maandishi.

10 Ikawa Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Mara tatu kwa siku akapiga magoti na kuomba, akimshukuru Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya mwanzoni.

11 Ndipo watu hawa wakamwendea kama kikundi na kumkuta Danieli anaomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada.

12 Basi wakaenda kwa mfalme na kusema naye kuhusu amri ya kifalme: “Je, hukutangaza amri kwamba kwa muda huu wa siku thelathini zijazo mtu ye yote ambaye atamwomba mungu au mwanadamu ye yote isipokuwa wewe, Ee mfalme, angetupwa ndani ya tundu la simba?”

Mfalme akajibu, “Amri ndivyo ilivyo, kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kutanguka.”

13 Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa watu wa uhamisho kutoka Yuda hakuheshimu, Ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Angalia anaomba mara tatu kwa siku.”

14 Wakati mfalme aliposikia hili, akahuzunishwa mno, akakusudia kumwokoa Danieli, naye akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua.

15 Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.”

16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!”

17 Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mdomo wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili kwamba hali ya Danieli isiweze kubadilishwa.

18 Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme na usiku kucha hakula chakula wala kutumia viburudisho alivyoletewa. Wala hakuweza kulala.

19 Mapema alfajiri mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba.

20 Wakati alipokaribia lile tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya uchungu, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je, Mungu wako unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa na simba hawa?”

21 Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele!

22 Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lo lote baya mbele yako, Ee mfalme.”

23 Mfalme akafurahi mno naye akatoa amri Danieli atolewe kwenye lile tundu. Danieli alipotolewa katika lile tundu, hakukutwa na jeraha lo lote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.

24 Kwa amri ya mfalme wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote.

25 Kisha Mfalme Dario akawaandikia kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha katika nchi yote:

“Ninyi na mstawi sana!

26 “Natoa amri hii kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli.

“Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai

naye hudumu milele,

ufalme wake hautaangamizwa,

nao utawala wake

kamwe hauna mwisho.

27 Huponya na kuokoa:

hufanya ishara na maajabu

mbinguni na duniani.

Amemponya Danieli

kutoka katika nguvu za simba.”

28 Hivyo Danieli akastawi wakati wa utawala wa Dario na utawala wa Koreshi, Mwajemi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/6-c84b04333cdcea92f852fabb510d572f.mp3?version_id=1627—

Danieli 7

Ndoto Ya Danieli Ya Wanyama Wanne

1 Katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita katika akili yake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.

2 Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, mbele yangu kulikuwepo na upepo kutoka pande nne za mbinguni zikivuruga bahari kuu.

3 Wanyama wakubwa wanne, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka baharini.

4 “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikatazama mpaka mabawa yake yalipong’olewa naye akainuliwa katika nchi akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.

5 “Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, ambaye alionekana kama dubu. Upande wake mmoja ulikuwa umeinuka, alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama mpaka ushibe!’

6 “Baada ya huyo, nilitazama, mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama yale ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.

7 “Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma, akapondaponda na kuangamiza wahanga wake na kukanyaga chini ya nyayo zake cho chote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.

8 “Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, ikajitokeza miongoni mwa zile kumi, pembe tatu za mwanzoni ziling’olewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu na mdomo ulionena kwa majivuno.

9 “Nilipokuwa ninaendelea kutazama,

“viti vya enzi vikawekwa,

naye Mzee wa Siku akaketi.

Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji,

nywele za kichwa chake

zilikuwa nyeupe kama sufu.

Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto,

nayo magurudumu yake yote

yalikuwa yanawaka moto.

10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka,

ukipita mbele yake.

Maelfu elfu wakamhudumia,

kumi elfu mara kumi elfu

wakasimama mbele zake.

Mahakama ikakaa ili kuhukumu

na vitabu vikafunguliwa.

11 “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipochinjwa na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto unaowaka.

12 (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda fulani.)

13 “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku na akaongozwa mbele zake.

14 Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu, watu, kabila zote za mataifa na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.

Tafsiri Ya Ndoto

15 “Mimi, Danieli, nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya akili zangu yalinisumbua.

16 Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale na kumwuliza maana halisi ya haya yote.

“Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi:

17 ‘Hao wanyama wakubwa wanne ni falme nne zitakazoinuka duniani.

18 Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele, naam, milele na milele.’

19 “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote tena wa kutisha mwenye meno ya chuma na makucha ya shaba, mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake na kukanyaga cho chote kilichosalia.

20 Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno.

21 Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda,

22 mpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipomiliki ufalme.

23 “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda.

24 Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu.

25 Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili sikukuu zao takatifu pamoja na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.

26 “ ‘Lakini ndipo mahakama itakapokaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele.

27 Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’

28 “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo kuwa siri moyoni mwangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/7-847ea7340d3f75e394764eb4baad7b7c.mp3?version_id=1627—

Danieli 8

Maono Ya Danieli Ya Kondoo Dume Na Beberu

1 Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake Mfalme Belshaza, mimi Danieli, nilipata maono, baada ya maono ambayo yalikuwa yamenitokea.

2 Katika maono yangu mimi nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu, katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai.

3 Nikatazama juu, hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine lakini iliendelea kukua baadaye.

4 Nikamtazama yule kondoo alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama ye yote aliyeweza kusimama dhidi yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka katika nguvu zake. Alifanya kama atakavyo naye akawa mkuu.

5 Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa sana katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi.

6 Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto na kumshambulia kwa hasira nyingi.

7 Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akimpiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu, hivyo akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka katika nguvu za huyo beberu.

8 Yule beberu akawa mkubwa sana lakini kwenye kilele cha nguvu zake ile pembe yake ndefu ilivunjika na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.

9 Kutoka katika mojawapo ya zile pembe nne ambao ulianza ukiwa mdogo ukaongezeka nguvu kuelekea kusini na kuelekea mashariki na kuelekea Nchi ya Kupendeza.

10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani na kukanyaga juu yake.

11 Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi, ikamwondolea dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini.

12 Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mikononi mwake. Ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.

13 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie, yaani maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”

14 Akaniambia, “Itachukua siku 2,300, ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”

Tafsiri Ya Maono

15 Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja anayefanana na mwanadamu.

16 Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka mto Ulai ikiita, “Gabrieli, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”

17 Alipokuwa akikaribia pale mahali nilipokuwa nimesimama, niliogopa nikaanguka kifudifudi, akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”

18 Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kuniinua nikasimama kwa miguu yangu.

19 Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye katika wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa.

20 Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi.

21 Yule beberu mwenye nywele nyingi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.

22 Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka katika taifa lake lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ule uliovunjika.

23 “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, wakati waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali na stadi wa hila.

24 Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha na atafanikiwa kwa cho chote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu.

25 Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora. Wakati wajisikiapo kuwa wako salama, atawaangamiza wengi na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.

26 “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu wakati mrefu ujao.”

27 Mimi Danieli, nilikuwa nimechoka sana na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka nikaenda kwenye shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono, nami sikuweza kuyaelewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/8-7ab1f0e88e5d23ecf67ff878f3c00bcf.mp3?version_id=1627—

Danieli 9

Maombi Ya Danieli

1 Katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Dario mwana wa Ahusuero (mzaliwa wa Umedi) ambaye alifanywa mtawala juu ya ufalme wa Babeli,

2 katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, mimi Danieli, nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno laBwanaalilopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini.

3 Kwa hiyo nikamgeukiaBwanaMungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, kuvaa nguo ya gunia na kujipaka majivu.

4 NikamwombaBwanaMungu wangu na kutubu:

“Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika Agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake,

5 tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi, tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako.

6 Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu na watu wote wa nchi.

7 “Bwana, wewe ni mwenye haki, lakini siku hii ya leo tumefunikwa na aibu, wanaume wa Yuda na watu wa Yerusalemu nayo Israeli yote, wote walio karibu na walio mbali, katika nchi zote ulikotutawanya kwa sababu ya sisi kukosa uaminifu kwako.

8 EeBwana, sisi na wafalme wetu, wakuu wetu na baba zetu tumefunikwa na aibu kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.

9 BwanaMungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake,

10 hatukumtiiBwanaMungu wetu wala kuzishika sheria alizotupa kupitia kwa watumishi wake manabii.

11 Israeli yote imekosea sheria yako na kugeuka mbali, nao wamekataa kukutii.

“Kwa hiyo laana na viapo vya hukumu vilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, mtumishi wa Mungu, vimemiminwa juu yetu, kwa sababu tumefanya dhambi dhidi yako.

12 Umetimiza maneno uliyosema dhidi yetu na dhidi ya watawala wetu kwa kuleta maafa makubwa juu yetu. Chini ya mbingu yote kamwe hapajatendeka kitu kama kile kilichotendeka katika Yerusalemu.

13 Kama vile ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, misiba hii yote imekuja juu yetu, lakini hatujaomba fadhili kwaBwanaMungu wetu kwa kugeuka kutoka katika dhambi zetu na kuwa wasikivu katika kweli yake.

14 Bwanahakusita kuleta maafa juu yetu, kwa maanaBwanaMungu wetu ni mwenye haki katika kila afanyalo, lakini hata hivyo hatujamtii.

15 “Sasa, Ee Bwana Mungu wetu, ambaye uliwatoa watu wako Misri kwa mkono wenye nguvu na ambaye umejifanyia Jina linalodumu mpaka leo, tumetenda dhambi, tumefanya mabaya.

16 Ee Bwana, wewe kwa kadiri ya matendo yako ya haki, ondoa hasira yako na ghadhabu yako juu ya Yerusalemu, mji wako, mlima wako mtakatifu. Dhambi zetu na maovu ya baba zetu yameifanya Yerusalemu na watu wako kitu cha kudharauliwa kwa wale wote wanaotuzunguka.

17 “Basi Mungu wetu, sasa sikia maombi na dua ya mtumishi wako. Ee Bwana, kwa ajili yako tuangalie kwa huruma kuhusu ukiwa wa mahali pako patakatifu.

18 Ee Mungu, tega sikio na ukasikie, fumbua macho yako ukaone ukiwa wa mji ule wenye Jina lako. Hatukutolei maombi yetu kwa sababu sisi tuna haki, bali kwa sababu ya rehema zako nyingi.

19 Ee Bwana, sikiliza! Ee Bwana, samehe! Ee Bwana, sikia na ukatende! Kwa ajili yako, Ee Mungu wangu, usikawie, kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa Jina lako.”

Majuma Sabini

20 Basi, nilipokuwa bado nikinena na kuomba, nikiungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli na nikifanya maombi yangu kwaBwanaMungu wangu kwa ajili ya mlima wake mtakatifu,

21 wakati nilipokuwa bado katika maombi, Gabrieli, yule mtu niliyekuwa nimemwona katika maono hapo awali, alinijia kwa kasi karibia na wakati wa kutoa dhabihu ya jioni.

22 Akanielimisha na kuniambia, “Danieli, sasa nimekuja kukupa akili na ufahamu.

23 Mara ulipoanza kuomba, jibu lilitolewa, ambalo nimekuja kukupasha habari, kwa maana wewe unapendwa sana. Kwa hiyo, tafakari ujumbe huu na uelewe maono haya:

24 “Majuma sabini yameamuriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii pia kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu sana.

25 “Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu mpaka kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuweko majuma saba na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu.

26 Baada ya majuma sitini na mawili Mpakwa mafuta atakatiliwa mbali wala hatabakia na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea mpaka mwisho, nao ukiwa umeamriwa.

27 Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamuriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/9-3b269849c8eb26d361d0f72cb8bb3e9d.mp3?version_id=1627—

Danieli 10

Maono Ya Danieli Kuhusu Mtu

1 Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.

2 Wakati huo, mimi Danieli, nikaomboleza kwa majuma matatu.

3 Sikula chakula kizuri, nyama wala divai havikugusa midomo yangu, nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

4 Kwenye siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli,

5 nikatazama juu na mbele yangu alikuwapo mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka ufazi kiunoni mwake.

6 Mwili wake ulikuwa kama kito cha zabarijadi safi, uso wake kama umeme wa radi, macho yake kama mwali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mng’ao wa shaba iliyosuguliwa sana, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.

7 Mimi Danieli, nilikuwa ni mimi peke yangu niliyeona hayo maono, watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu wakakimbia na kujificha.

8 Kwa hiyo niliachwa peke yangu, nikikodolea macho maono hayo makubwa, sikubakiwa na nguvu, rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu.

9 Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikalala kifudifudi nikapatwa na usingizi mzito.

10 Mkono ulinigusa, ukaninyanyua, nikapiga magoti na vitanga vyangu vikiwa vimeshika chini, huku nikiwa ningali bado ninatetemeka.

11 Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa, simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliposema nami haya, nikasimama nikitetemeka.

12 Ndipo akaendelea kusema, “Danieli usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwa ajili ya kuitikia maneno yako.

13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinizuia kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi.

14 Sasa nimekuja kukueleza mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”

15 Wakati alipokuwa akinieleza haya, nilisujudu uso wangu ukiwa umeelekea chini nikawa bubu.

16 Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nimeishiwa nguvu.

17 Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia hata ninashindwa kupumua.”

18 Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu.

19 Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa, uwe na nguvu.”

Alipozungumza nami, nilipata nguvu nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”

20 Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja,

21 lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/10-8372668a01e90903cab32e79de2e87c7.mp3?version_id=1627—

Danieli 11

1 Nami katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Dario, Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.)

Wafalme Wa Kusini Na Wa Kaskazini

2 “Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme watatu zaidi watatokea Uajemi, kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Wakati atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani.

3 Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, ambaye atatawala kwa nguvu nyingi na kufanya anavyopenda.

4 Baada ya kujitokeza, milki yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautakwenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizoonyesha, kwa sababu milki yake itang’olewa na kupewa wengine.

5 “Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko mfalme, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi.

6 Baada ya miaka kadha wa kadha, wataungana. Binti wa mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini huyo binti nguvu zake za ushawishi hazitadumu, vivyo hivyo na baba yake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, watoto wake na ye yote aliyemuunga mkono.

7 “Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Huyo mtu atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake, atapigana dhidi yao naye atashinda.

8 Naye ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu na kuvichukua hadi Misri kama nyara za vita. Kwa miaka kadha wa kadha atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua.

9 Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia kwa vita mfalme wa Kusini lakini atarudi nyuma hadi kwenye nchi yake mwenyewe.

10 Hata hivyo, wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.

11 “Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye ataunda jeshi kubwa, lakini litashindwa.

12 Wakati jeshi litakapokuwa limechukuliwa, mfalme wa Kusini atajawa na majivuno na atachinja maelfu mengi, hata hivyo hatabaki na ushindi.

13 Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi jingine, kubwa kuliko lile la kwanza, na baada ya miaka kadha wa kadha, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.

14 “Katika nyakati hizo wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio.

15 Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzunguka mji kwa majeshi na kuuteka mji uliozungushiwa boma. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu ya kuyazuia, naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora kuliko vingine, havitakuwa na nguvu ya kuwakabili.

16 Huyo avamiaye nchi kwa vita atafanya apendavyo, hakuna ye yote atakayeweza kusimama mbele yake. Atajiimarisha mwenyewe katika Nchi ya Kupendeza na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza.

17 Naye atafanya mipango kuja na nguvu za ufalme wake wote na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kufanya mipango ya kuuangusha ufalme ndani kwa ndani, lakini mipango haitafanikiwa wala kumsaidia.

18 Ndipo atabadili mwelekeo wake kuelekea nchi za pwani na ataziteka nyingi, lakini jemadari kutoka mahali pengine atakomesha ufidhuli wake na kurudisha ufidhuli wake juu yake.

19 Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.

20 “Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, kwa miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.

21 “Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona wako salama, naye atautwaa kwa hila.

22 Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake, jeshi pamoja na mkuu wa agano wataangamizwa.

23 Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, pamoja na watu wachache tu ataingia madarakani.

24 Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanapojiona salama, atayavamia naye atafanikisha kile ambacho baba zake wala babu zake hawakufanya. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atafanya hila ya kupindua miji yenye maboma, lakini kwa muda mfupi tu.

25 “Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya mashauri yaliyofanywa kwa hila dhidi yake.

26 Wale wanaokula kutoka kwenye ruzuku za mfalme watajaribu kumwangamiza, jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani.

27 Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamuriwa.

28 Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume na Agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano na kisha atarudi katika nchi yake.

29 “Katika wakati ulioamuriwa atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza.

30 Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atageuka nyuma na kutoa wazi hasira yake dhidi ya Agano takatifu. Atarudi na kuonyesha fadhili kwa wale waliachao Agano takatifu.

31 “Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu lisababishalo ukiwa.

32 Kwa udanganyifu atapotosha wale walionajisi Agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.

33 “Wale wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa na kufanywa mateka.

34 Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi ambao si waaminifu wataungana nao.

35 Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili kwamba waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa mpaka wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamuriwa.

Mfalme Ajikwezaye Mwenyewe

36 “Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza mwenyewe kujihesabu mwenye nguvu zaidi juu ya kila mungu naye atasema vitu ambavyo havijasikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitokee.

37 Hataonyesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu ye yote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote.

38 Badala ya kuwajali hao miungu, ataheshimu mungu wa ngome, mungu ambaye hakujulikana na baba zake, atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani na zawadi za thamani kubwa.

39 Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala juu ya watu wengi na atagawa nchi kwa kulipia.

40 “Katika wakati wa mwisho mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita na askari wapanda farasi na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kukumba nchi hizo kama mafuriko.

41 Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka katika mkono wake.

42 Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi, Misri haitaepuka.

43 Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na utajiri wote wa Misri, pamoja na Walibya na Wakushi kwa kujisalimisha.

44 Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu kabisa wengi.

45 Atasimika mahema yake ya kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna ye yote atakayemsaidia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/11-37c4a2e2404f6fe831f988a0934ec6db.mp3?version_id=1627—

Danieli 12

Nyakati Za Mwisho

1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.

2 Watu wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwenye aibu na kudharauliwa milele.

3 Wale wenye hekima watang’aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang’aa kama nyota milele na milele.

4 Lakini wewe Danieli, yafunge na kuyatia muhuri maneno ya kitabu hiki mpaka wakati wa mwisho. Wengi watakwenda huku na huko na maarifa yataongezeka.”

5 Ndipo mimi Danieli, nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto na mwingine ukingo wa pili wa mto.

6 Mmoja wao akasema na yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?”

7 Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.”

8 Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?”

9 Akajibu, “Danieli, enenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri mpaka wakati wa mwisho.

10 Wengi watatakaswa na kuondolewa mawaa na kuwa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu.

11 “Tangu wakati ule wa kukomeshwa dhabihu ya kila siku na kusimamishwa kwa chukizo la uharibifu kutakuweko siku 1,290.

12 Amebarikiwa mtu yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku 1,335.

13 “Kuhusu wewe, enenda zako mpaka mwisho. Utapumzika, nawe ndipo mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekwa kwa ajili yako.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/12-d698d106db79b7a2795e0f235a49d9a1.mp3?version_id=1627—

Ezekieli 1

Viumbe Hai Na Utukufu Wa Bwana

1 Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.

2 Katika siku ya tano ya mwezi, ilikuwa mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehayakini,

3 neno laBwanalilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono waBwanaulikuwa juu yake.

4 Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto.

5 Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu,

6 lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne.

7 Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa.

8 Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa,

9 nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea.

10 Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng’ombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai.

11 Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake.

12 Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Po pote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka.

13 Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi.

14 Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.

15 Nilipokuwa nikitazama vile viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe kikiwa na nyuso zake nne.

16 Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yaling’aa kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilikuwa na gurudumu jingine ndani yake.

17 Yalipokwenda yalielekea upande wo wote wa pande nne walipoelekea wale viumbe, magurudumu hayakuzunguka wakati viumbe vile vilipokwenda.

18 Kingo zake zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.

19 Vile viumbe hai vilipokwenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea na wakati hivyo viumbe hai vilipoinuka kutoka ardhini magurudumu nayo yaliinuka.

20 Mahali po pote roho alipokwenda wale viumbe nao walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja navyo, kwa sababu roho ya vile viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

21 Wakati viumbe vile viliposogea, nayo magurudumu yalisogea, viumbe viliposimama kimya, nayo pia yalisimama kimya, viumbe vilipoinuka juu ya nchi magurudumu yaliinuliwa pamoja navyo kwa kuwa roho ya hivyo viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

22 Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na lenye kutisha.

23 Chini ya hiyo nafasi mabawa yao yalitanda moja kuelekea jingine, kila mmoja alikuwa na mabawa mengine mawili yaliyofunika mwili wake.

24 Viumbe wale waliposogea nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama makelele ya jeshi. Waliposimama kimya walishusha mabawa yao.

25 Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, wakati waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa.

26 Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi kuonekana kwake chenye rangi ya yakuti samawi, na juu ya kile kiti cha enzi kulikuwa na umbo mfano wa mwanadamu.

27 Nikaona kwamba kutokana na kile nilichoona kama kiuno chake kuelekea juu alionekana kama chuma inayowaka kana kwamba imejaa moto na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto na mwanga mkali ulimzunguka.

28 Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng’ao uliomzunguka.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa utukufu waBwana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZK/1-641cb6f6c2bbe5248b2f6c79869990b7.mp3?version_id=1627—