Maombolezo 4

1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng’ao wake,

dhahabu iliyo safi imekuwa haing’ai!

Vito vya thamani vimetawanywa

kwenye mwanzo wa kila barabara.

2 Jinsi wana wa Sayuni wenye thamani,

ambao mwanzo uzito wa thamani yao

ulikuwa wa dhahabu,

sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,

kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3 Hata mbweha hutoa matiti yao

kunyonyesha watoto wao,

lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma

kama mbuni katika jangwa.

4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga

umegandamana na kaakaa la kinywa chake,

watoto huomba mkate,

lakini hakuna ye yote awapaye.

5 Wale waliokula vyakula vya kifahari

ni maskini barabarani.

Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau

sasa wanalala kwenye malundo ya majivu.

6 Adhabu ya watu wangu

ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,

ambayo ilipinduliwa ghafula

bila kuwepo mkono wa kumsaidia.

7 Wakuu wao walikuwa wameng’aa kuliko theluji

na weupe kuliko maziwa,

miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,

kuonekana kwao kama yakuti samawi.

8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;

hawatambulikani barabarani.

Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,

imekuwa mikavu kama fimbo.

9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora

kuliko wale waliokufa kwa njaa;

waliteseka kwa njaa, walitokomea

kwa ajili ya kukosa chakula

kutoka shambani.

10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma

walipika watoto wao wenyewe,

ambao walikuwa chakula chao

wakati watu wangu walipoangamizwa.

11 Bwanaametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;

ameimwaga hasira yake kali.

Amewasha moto katika Sayuni

ambao umeteketeza misingi yake.

12 Wafalme wa dunia hawakuamini,

wala hapakuwepo mtu ye yote wa duniani,

kwamba adui na watesi wangeweza kuingia

kwenye malango ya Yerusalemu.

13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,

na maovu ya makuhani wake,

ambao walimwaga pamoja naye

damu ya wenye haki.

14 Sasa wanapapasa papasa barabarani

kama watu ambao ni vipofu.

Wamenajisiwa kabisa kwa damu

kwamba hakuna ye yote

anayethubutu kugusa mavazi yao.

15 Watu waliwapigia kelele wakisema, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!

Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”

Walipokimbia na kutangatanga huko na huko,

watu miongoni mwa mataifa walisema,

“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”

16 Bwanamwenyewe amewatawanya;

hawaangalii tena.

Makuhani hawaonyeshwi heshima,

wazee hawakubaliki.

17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,

kwa kutazamia bure msaada;

tuliangalia kutoka minara yetu

kwa taifa lile lisiloweza kutuokoa.

18 Watu walitunyemelea katika kila hatua

kwa hiyo hatukuweza kutembea

katika barabara zetu.

Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,

kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.

19 Waliotufuatia walikuwa wepesi

kuliko tai katika anga;

walitusaka juu milimani

na kutuvizia jangwani.

20 Mpakwa mafuta waBwana, pumzi ya uhai wetu hasa,

alinaswa katika mitego yao.

Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake

tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.

21 Shangilia na ufurahi, Ee Binti Edomu,

wewe ambaye unaishi katika nchi ya Usi.

Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,

Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.

22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,

hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.

Lakini, Ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako

na atafunua uovu wako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LAM/4-933953c0cd481067c2446f7585721e18.mp3?version_id=1627—

Maombolezo 5

1 Kumbuka, EeBwana, yaliyotupata,

tazama, nawe uione aibu yetu.

2 Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,

na nyumba zetu kwa wageni.

3 Tumekuwa yatima wasio na baba,

mama zetu wamekuwa kama wajane.

4 Ni lazima kununua maji tunayokunywa,

kuni zetu zinaweza kupatikana tu kwa kununua.

5 Wale ambao wanatufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,

tumechoka na hakuna pumziko.

6 Tumejitolea kwa Misri na Ashuru

tupate chakula cha kutosha.

7 Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,

na sisi tunachukua adhabu yao.

8 Watumwa wanatutawala

na hakuna ye yote wa kutuweka huru kutoka katika mikono yao.

9 Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu

kwa sababu ya upanga jangwani.

10 Ngozi yetu ina joto kama jiko la kuokea,

kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa.

11 Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,

na mabikira katika miji ya Yuda.

12 Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,

wazee hawapewi heshima.

13 Vijana wanaume wanataabika kwenye mawe ya kusagia,

wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.

14 Wazee wameondoka toka lango la mji,

vijana wa kiume wameacha kuimba kwa vinanda vyao.

15 Furaha imeondoka katika mioyo yetu,

kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.

16 Taji imeanguka kutoka kichwani petu.

Ole wetu, kwa maana tumetenda Dhambi!

17 Kwa sababu ya hiyo mioyo yetu inazimia,

kwa sababu ya mambo haya macho yetu yamefifia,

18 kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa,

mbweha huzungukazunguka juu yake.

19 Wewe, EeBwanatawala milele,

kiti chako cha enzi chadumu kutoka kizazi mpaka kizazi.

20 Kwa nini watusahau siku zote?

Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?

21 Uturudishe kwako mwenyewe, EeBwana,

ili tupate kurudi;

zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,

22 labda uwe umetukataa kabisa

na umetukasirikia pasipo kipimo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LAM/5-39cf2feb8cdceb81c0778397c80b0acc.mp3?version_id=1627—

Yeremia 1

1 Maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani katika mji wa Anathothi katika nchi ya Benyamini.

2 Neno laBwanalilimjia katika mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda,

3 pia wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, mpaka mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na moja wa kutawala kwake Sedekia mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati watu wa Yerusalemu walipopelekwa kwenda uhamishoni.

Wito Wa Yeremia

4 Neno laBwanalilinijia, kusema,

5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;

kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;

nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

6 Nami nikasema, “Aa,BwanaMwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”

7 LakiniBwanaakaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utakwenda po pote nitakapokutuma na kunena lo lote nitakalokuagiza.

8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asemaBwana.

9 KishaBwanaakaunyosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.

10 Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kung’oa na kubomoa, ili kuharibu na kuangamiza, ili kujenga na kupanda.”

11 Neno laBwanalikanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?”

Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.”

12 Bwanaakaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.”

13 Neno laBwanalikanijia tena, “Unaona nini?”

Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka kikiwa kimeinama mdomo wake kuelekea upande wa kaskazini.”

14 Bwanaakaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote waishio katika nchi.

15 Nitawaita watu wote wa falme za kaskazini,” asemaBwana.

“Wafalme wao watakuja na kuweka viti vyao vya enzi

katika maingilio ya malango ya Yerusalemu,

watakuja dhidi ya kuta zake zote zinazouzunguka

na dhidi ya miji yote ya Yuda.

16 Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu

kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi,

kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine

na kuabudu kile ambacho mikono yao imekitengeneza.

17 “Jiandae! Simama nawe useme cho chote nitakachokuamuru. Usiwaogope, la sivyo nitakufanya uwaogope wao.

18 Leo nimekufanya mji wenye ngome, nguzo ya chuma na ukuta wa shaba ili kusimama dhidi ya nchi yote: dhidi ya wafalme wa Yuda, maafisa wake, makuhani wake na watu wa nchi hiyo.

19 Watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa kuwa niko pamoja nawe nami nitakuokoa,” asemaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/1-95955986344391729205a4da72b0ed63.mp3?version_id=1627—

Yeremia 2

Israeli Amwacha Mungu

1 Neno laBwanalilinijia kusema,

2 “Nenda ukahubiri masikioni mwa watu wa Yerusalemu:

“ ‘Nakumbuka moyo wako wa uchaji katika ujana wako,

jinsi ulivyonipenda kama bibi arusi

na kunifuata katika jangwa lile lote,

katika nchi isiyopandwa mbegu.

3 Israeli alikuwa mtakatifu kwaBwana,

malimbuko ya kwanza ya mavuno yake;

wote waliowaangamiza walihesabiwa kuwa na hatia,

nayo maafa yaliwakumba,’ ”

asemaBwana.

4 Sikia neno laBwana, Ee nyumba ya Yakobo,

nanyi nyote jamaa za nyumba ya Israeli.

5 Hivi ndivyo asemavyoBwana:

“Je, baba zenu waliona kosa gani kwangu,

hata wakatangatanga mbali nami hivyo?

Walifuata sanamu zisizofaa,

nao wenyewe wakawa hawafai.

6 Hawakuuliza, ‘Yuko wapiBwana,

aliyetupandisha kutoka Misri

na kutuongoza kupitia katika nyika kame,

kupitia katika nchi ya majangwa na mabonde,

nchi ya ukame na giza,

nchi ambayo hakuna mtu asafiriye ndani yake

wala hakuna mtu aishiye humo?’

7 Niliwaleta katika nchi yenye wingi wa vitu

mpate kula matunda yake

na utajiri wa mazao yake.

Lakini mkaja na kuinajisi nchi yangu

na kuufanya urithi wangu chukizo.

8 Makuhani hawakuuliza,

‘Yuko wapiBwana?’

Wale wanaoshughulikia sheria hawakunijua mimi;

viongozi waliasi dhidi yangu.

Manabii walitabiri kwa jina la Baali,

wakifuata sanamu zisizofaa.

9 “Kwa hiyo naleta tena mashtaka dhidi yako,”

asemaBwana.

“Nami nitaleta mashtaka dhidi ya watoto wa watoto wako.

10 Vuka, nenda ng’ambo mpaka pwani ya Kitimunawe uangalie,

tuma watu waende Kedari na wachunguze kwa makini,

uone kama kumekuwapo kitu kama hiki.

11 Je, taifa limebadili miungu yake wakati wo wote?

(Hata ingawa hao si miungu kamwe.)

Lakini watu wangu wamebadili Utukufu wao

kwa sanamu zisizofaa kitu.

12 Shangaeni katika hili, Ee mbingu,

nanyi tetemekeni kwa hofu kuu,”

asemaBwana.

13 “Watu wangu wametenda dhambi mbili:

Wameniacha mimi,

niliye chemchemi ya maji yaliyo hai,

nao wamejichimbia visima vyao wenyewe,

visima vilivyobomoka visivyoweza kuhifadhi maji.

14 Je, Israeli ni mtumishi, yaani mtumwa kwa kuzaliwa?

Kwa nini basi amekuwa mateka?

15 Simba wamenguruma;

wamemngurumia.

Wameifanya nchi yake kuwa ukiwa;

miji yake imeteketezwa nayo imeachwa haina watu.

16 Pia watu wa Memfisina Tahpanhesi

wamevunja taji ya kichwa chako.

17 Je, hukujiletea hili wewe mwenyewe

kwa kumwachaBwana, Mungu wako

alipowaongoza njiani?

18 Sasa kwa nini uende Misri

kunywa maji kutoka katika Shihori?

Nawe kwa nini kwenda Ashuru

kunywa maji yatokayo katika Mto Eufrati?

19 Uovu wako utakuadhibu;

kurudi nyuma kwako kutakukemea.

Basi kumbuka, utambue

jinsi lilivyo ovu na chungu kwako

unapomwachaBwanaMungu wako

na kutokuwa na hofu yangu,”

asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote.

20 “Zamani nilivunja nira yako

na kukatilia mbali vifungo vyako;

ukasema, ‘Sitakutumikia’!

Naam kweli, kwenye kila kilima kirefu

na chini ya kila mti uliotanda matawi yake

ulijilaza kama kahaba.

21 Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana,

mkamilifu na wa mbegu nzuri.

Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami,

ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu?

22 Hata ujisafishe kwa magadi

na kutumia sabuni nyingi,

bado doa la hatia yako liko mbele zangu,”

asemaBwanaMwenyezi.

23 “Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi,

sijawafuata Mabaali’?

Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni;

fikiri uliyoyafanya.

Wewe ni ngamia jike mwenye mbio

ukikimbia hapa na pale,

24 punda-mwitu aliyezoea jangwa,

anayenusa upepo, katika tamaa yake kubwa:

akiwa katika wakati wake wa kuhitaji mbegu

ni nani awezae kumzuia?

Madume yo yote yanayomfuatilia

hayana haja ya kujichosha;

wakati wa kupandwa kwake watampata tu.

25 Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu

na koo lako liwe limekauka.

Lakini ulisema, ‘Haina maana!

Ninaipenda miungu ya kigeni,

nami ni lazima niifuatie.’

26 “Kama vile mwizi aaibikavyo wakati amekamatwa,

hivyo ndivyo na nyumba ya Israeli inavyoaibishwa,

wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao,

makuhani wao na manabii wao.

27 Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’

tena wanaliambia jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’

Wamenipa visogo vyao

wala hawakunigeuzia nyuso zao;

lakini wakiwa katika taabu, wanasema,

‘Njoo utuokoe!’

28 Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea?

Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa

wakati mnapokuwa katika taabu!

Kwa maana mna miungu mingi

kama mlivyo na miji, Ee Yuda.

29 “Kwa nini mnaleta mashtaka dhidi yangu?

Ninyi nyote mmeniasi,”

asemaBwana.

30 “Ni bure tu nimeadhibu watu wako,

wala hukujirekebisha.

Upanga wako umewala manabii wako

kama simba mwenye njaa.

31 “Enyi wa kizazi hiki, kumbukeni neno laBwana:

“Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli

au nchi ya giza kuu?

Kwa nini watu wangu wanasema, ‘Sisi tuko huru kuzurura,

hatutarudi kwako tena’?

32 Je, mwanamwali husahau vitu vyake vilivyofanyizwa kwa vito,

bibi arusi husahau mapambo yake ya arusi?

Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

tena kwa siku zisizo na hesabu.

33 Je, wewe ni fundi kiasi gani katika kufuatia mapenzi!

Hata wale wanawake wabaya kuliko wote

wanaweza kujifunza kutokana na njia zako.

34 Katika nguo zako watu huona

damu ya uhai ya maskini wasio na hatia,

ingawa hukuwakamata wakivunja nyumba.

Lakini pamoja na haya yote

35 unasema, ‘Sina hatia;

Mungu hajanikasirikia.’

Lakini nitakuhukumu kwa sababu unasema,

‘Mimi sijatenda dhambi.’

36 Kwa nini unatangatanga sana,

kubadili njia zako?

Utakatishwa tamaa na Misri

kama ulivyokatishwa na Ashuru.

37 Pia utaondoka mahali hapo

ukiwa umeweka mikono kichwani,

kwa kuwaBwanaamewakataa wale unaowatumainia;

hutasaidika kwa kupitia wao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/2-25231161dca39d00a279a7a85285a98f.mp3?version_id=1627—

Yeremia 3

Israeli Asiye Mwaminifu

1 “Kama mtu akimpa talaka mkewe,

naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine,

je, huyo mume aweza kumrudia tena?

Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa?

Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi:

je, sasa utanirudia tena?”

asemaBwana.

2 “Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone.

Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe?

Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi,

ukakaa kama yeye ahamahamaye jangwani.

Umeinajisi nchi

kwa ukahaba wako na uovu wako.

3 Kwa hiyo mvua imezuiliwa,

wala mvua za vuli hazikunyesha.

Hata hivyo, una uso wa shaba kama wa kahaba;

unakataa kutahayari kwa aibu.

4 Je, wewe hujaniita hivi punde tu:

‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,

5 je, utakasirika siku zote?

Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’

Hivi ndivyo unavyozungumza,

lakini unafanya maovu yote uwezayo.”

Wito Kwa Ajili Ya Toba

6 Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia,Bwanaaliniambia, “Umeona kile ambacho Israeli asiyemwaminifu alichofanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko.

7 Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia lakini hakurudi, naye dada yake Yuda asiye mwaminifu aliona hili.

8 Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake asiyemwaminifu hakuogopa, pia alitoka na kufanya uzinzi.

9 Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake aliinajisi nchi kwa kuzini na jiwe na mti.

10 Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake ambaye si mwaminifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asemaBwana.

11 Bwanaakaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda aliye mdanganyifu.

12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:

“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asemaBwana,

‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,

kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asemaBwana,

‘Sitashika hasira yangu milele.

13 Ungama dhambi zako tu:

kwamba umemwasiBwanaMungu wako,

umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni

chini ya kila mti unaotanda,

nawe hukunitii mimi,’ ”

asemaBwana.

14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asemaBwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.

15 Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu.

16 Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena ‘Sanduku la Agano laBwana,’ ” asemaBwana. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine.

17 Wakati huo, watapaita Yerusalemu kiti cha enzi chaBwana, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina laBwana. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu.

18 Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini kwenda kwenye nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.

19 “Mimi mwenyewe nilisema,

“ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana

na kuwapa nchi nzuri,

urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lo lote.’

Nilidhani mngeniita ‘Baba’

na kwamba msingegeuka, mkaacha kunifuata.

20 Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe,

vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu pia, Ee nyumba ya Israeli,”

asemaBwana.

21 Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame,

kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli,

kwa sababu wamepotoka katika njia zao

na wamemsahauBwanaMungu wao.

22 “Rudini, enyi watu msio waaminifu,

nami nitawaponya ukengeufu wenu.”

“Naam, tutakujia

kwa maana wewe niBwanaMungu wetu.

23 Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima

na milimani ni udanganyifu;

hakika katikaBwana, Mungu wetu,

uko wokovu wa Israeli.

24 Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala

matunda ya kazi za baba zetu:

makundi yao ya kondoo na mbuzi, pamoja na ng’ombe,

wana wao na binti zao.

25 Sisi na tulale chini katika aibu yetu,

fedheha yetu na itufunike.

Tumetenda dhambi dhidi yaBwanaMungu wetu,

sisi na mababa zetu;

tangu ujana wetu hadi leo

hatukumtiiBwanaMungu wetu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/3-917b6ea650bc5f87169f2d50b31289b1.mp3?version_id=1627—

Yeremia 4

1 “Ikiwa utataka kurudi, Ee Israeli,

nirudie mimi,”

asemaBwana.

“Ikiwa utataka kuachilia mbali na macho yangu

sanamu zako za kuchukiza

na usiendelee kutangatanga,

2 ikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa,

‘Kwa hakika kama vileBwanaaishivyo,’

ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye

na katika yeye watajitukuza.”

3 Hili ndilo asemaloBwanakwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu:

“Vunjeni mabonge ya udongo

kwenye mashamba yenu yasiyolimwa

wala msipande katikati ya miiba.

4 Jitahirini katikaBwana,

tahirini mioyo yenu,

enyi wanaume wa Yuda

na watu wa Yerusalemu,

la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu

na kuwaka kama moto

kwa sababu ya uovu mliotenda,

ikiwaka pasipo wa kuizima.

Maafa Kutoka Kaskazini

5 “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu na kusema:

‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’

Piga kelele na kusema:

‘Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie katika miji yenye maboma!’

6 Onyesheni ishara ili kwenda Sayuni!

Kimbilieni kwenye usalama pasipo kuchelewa!

Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini,

yaani maangamizi ya kutisha.”

7 Simba ametoka nje ya pango lake,

mharabu wa mataifa amejipanga.

Ametoka mahali pake

ili kuja kuangamiza nchi yenu.

Miji yenu itakuwa magofu

pasipo mtu wa kuishi humo.

8 Hivyo vaeni nguo za magunia,

ombolezeni na kulia kwa huzuni,

kwa kuwa hasira kali yaBwana

haijaondolewa kwetu.

9 “Katika siku ile,” asemaBwana

“mfalme na maafisa watakata tamaa,

makuhani watafadhaika,

na manabii watashangazwa mno.”

10 Ndipo niliposema, “Aa,BwanaMwenyezi, umewadanganyaje kabisa watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kwenye makoo yetu!”

11 Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame katika jangwa unavuma kuelekea watu wangu, lakini sio kupepeta au kutakasa,

12 upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”

13 Tazama! Anakuja kama mawingu,

magari yake yanakuja

kama upepo wa kisulisuli,

farasi wake ni wenye mbio kuliko tai.

Ole wetu! Tunaangamia!

14 Ee Yerusalemu, uusafishe uovu

kutoka moyoni mwako na uokolewe.

Utaendelea kuficha mawazo mapotovu

mpaka lini?

15 Sauti inatangaza kutoka Dani,

ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.

16 “Waambie mataifa jambo hili,

piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu:

‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali,

likipiga kelele ya vita dhidi ya miji ya Yuda.

17 Wamemzunguka kama watu walindao shamba,

kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ”

asemaBwana.

18 “Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe

yameleta haya juu yako.

Hii ndiyo adhabu yako.

Tazama jinsi ilivyo chungu!

Tazama jinsi inavyochoma moyo!”

19 Ee mtima wangu, mtima wangu!

Ninagaagaa kwa maumivu.

Ee maumivu makuu ya moyo wangu!

Moyo wangu umefadhaika ndani yangu,

siwezi kunyamaza.

Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta,

nimesikia kelele ya vita.

20 Maafa baada ya maafa,

nchi yote imekuwa magofu.

Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa,

makazi yangu kwa muda mfupi.

21 Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita

na kusikia sauti za tarumbeta?

22 “Watu wangu ni wapumbavu,

hawanijui mimi.

Ni watoto wasio na akili,

hawana ufahamu.

Ni hodari kutenda mabaya,

hawajui kutenda yaliyo mema.”

23 Niliitazama dunia,

nayo haikuwa na umbo tena ni tupu;

niliziangalia mbingu,

mianga ilikuwa imetoweka.

24 Niliitazama milima,

nayo ilikuwa ikitetemeka,

vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.

25 Nilitazama, wala watu hawakuwepo;

kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.

26 Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri

imekuwa jangwa,

miji yake yote ilikuwa magofu mbele zaBwana,

mbele ya hasira yake kali.

27 Hivi ndivyoBwanaasemavyo:

“Nchi yote itaharibiwa,

ingawa sitaiangamiza kabisa.

28 Kwa hiyo dunia itaomboleza

na mbingu zilizo juu zitakuwa giza,

kwa sababu nimesema nami sitakuwa na huruma,

nimeamua na wala sitageuka.”

29 Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde

kila mji unakimbia.

Baadhi wanakimbilia vichakani,

baadhi wanapanda juu ya miamba.

Miji yote imeachwa,

hakuna aishiye ndani yake.

30 Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa?

Kwa nini unajivika vazi jekundu

na kuvaa vito vya dhahabu?

Kwa nini unapaka macho yako rangi?

Unajipamba bure.

Wapenzi wako wanakudharau,

wanautafuta uhai wako.

31 Nasikia kilio kama cha mwanamke

aliye katika utungu wa kuzaa,

kilio cha uchungu kama cha anayemzaa

mtoto wake wa kwanza:

kilio cha Binti Sayuni akitapatapa ili aweze kupumua,

akiinua mikono yake, akisema,

“Ole wangu! Ninazimia;

maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/4-d6b16d9a29c1139a2216bc13a082d78a.mp3?version_id=1627—

Yeremia 5

Hakuna Hata Mmoja Aliye Mkamilifu

1 “Pandeni na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu,

tazameni pande zote na mkumbuke,

tafuteni katika viwanja vyake.

Kama mtaweza kumpata hata mtu mmoja tu

atendaye kwa uaminifu na kutafuta kweli,

nitausamehe mji huu.

2 Ingawa wanasema, ‘Kwa hakika kamaBwanaaishivyo,’

bado wanaapa kwa uongo.”

3 EeBwana, je, macho yako hayaitafuti kweli?

Uliwapiga, lakini hawakusikia maumivu,

uliwapondaponda lakini walikataa marudi.

Walifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko jiwe

nao walikataa kutubu.

4 Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu;

wao ni wapumbavu,

kwa maana hawaijui njia yaBwana,

sheria ya Mungu wao.

5 Kwa hiyo nitakwenda kwa viongozi

na kuzungumza nao,

hakika wao wanaijua njia yaBwana,

sheria ya Mungu wao.”

Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira

na kuvivunja vifungo.

6 Kwa hiyo simba kutoka mwituni atawashambulia,

mbwa mwitu kutoka jangwani atawaangamiza,

chui atawavizia karibu na miji yao

kumrarua vipande vipande ye yote

atakayethubutu kutoka nje,

kwa maana maasi yao ni makubwa

na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.

7 “Kwa nini niwasamehe?

Watoto wenu wameniacha

na kuapa kwa miungu ambayo si miungu.

Niliwapatia mahitaji yao yote,

lakini bado wamefanya uzinzi

na kusongana katika nyumba za makahaba.

8 Wamelishwa vizuri, kama farasi waume wenye tamaa nyingi,

kila mmoja akimlilia

mke wa mwanaume mwingine.

9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”

asemaBwana.

“Je, nisijilipizie kisasi

juu ya taifa kama hili?

10 “Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu,

lakini msiangamize kabisa.

Pogoeni matawi yake,

kwa kuwa watu hawa sio waBwana.

11 Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda

wamekuwa si waaminifu kwangu kamwe,”

asemaBwana.

12 Wamedanganya kuhusuBwana,

wamesema, “Yeye hatafanya jambo lo lote!

Hakuna dhara litakalotupata;

kamwe hatutaona upanga wala njaa.

13 Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao,

kwa hiyo hayo wayasemayo

na yatendeke kwao.”

14 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote:

“Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya,

nitayafanya maneno yangu

vinywani mwenu kuwa moto

na watu hawa wawe kuni

zinazoliwa na huo moto.

15 Ee nyumba ya Israeli,” asemaBwana,

“Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako,

taifa la kale na linaloendelea kudumu,

taifa ambalo lugha yao huijui,

wala msemo wao huwezi kuuelewa.

16 Podo zao ni kama kaburi lililo wazi,

wote ni mashujaa hodari wa vita.

17 Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu,

wataangamiza wana wenu na mabinti zenu;

wataangamiza makundi yenu

ya kondoo na mbuzi, na ya ng’ombe,

wataangamiza mizabibu yenu na mitini yenu.

Kwa upanga wataangamiza

miji yenye maboma mliyoitumainia.

18 “Hata hivyo katika siku hizo, sitakuangamiza kabisa,” asemaBwana.

19 “Nao watu watakapouliza, ‘Kwa niniBwana, Mungu wetu ametufanyia mambo haya yote?’ Utawaambia, ‘Kama vile mlivyoniacha mimi na kutumikia miungu migeni katika nchi yenu wenyewe, ndivyo sasa mtakavyowatumikia wageni katika nchi ambayo si yenu.’

20 “Itangazie nyumba ya Yakobo hili

na ulipigie mbiu katika Yuda:

21 Sikieni hili, enyi wapumbavu na watu msio na akili,

mlio na macho lakini hamwoni,

mlio na masikio lakini hamsikii:

22 Je, haiwapasi kuniogopa mimi?” asemaBwana.

“Je, haiwapasi kutetemeka mbele zangu?

Niliufanya mchanga kuwa mpaka wa bahari,

kizuizi cha milele ambacho haiwezi kupita.

Mawimbi yanaweza kuumuka, lakini hayawezi kuupita;

yanaweza kunguruma, lakini hayawezi kuuvuka.

23 Lakini watu hawa wana mioyo ya ukaidi na ya uasi,

wamegeukia mbali na kwenda zao.

24 Wao hawaambiani wenyewe,

‘Sisi na tumwogopeBwanaMungu wetu,

anayetupatia mvua za masika na za vuli

kwa majira yake,

anayetuhakikishia majuma ya mavuno

kwa utaratibu.’

25 Matendo yenu mabaya yamezuia haya yote,

dhambi zenu zimewafanya msipate mema.

26 “Miongoni mwa watu wangu wamo walio waovu

wanaovizia kama watu wanaotega ndege

na kama wale wanaoweka mitego

kuwakamata watu.

27 Kama vitundu vilivyojaa ndege,

nyumba zao zimejaa udanganyifu;

wamekuwa matajiri na wenye nguvu,

28 wamenenepa na kunawiri.

Matendo yao maovu hayana kikomo;

hawatetei mashauri ya yatima

wapate kushinda,

hawatetei haki za maskini.

29 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”

asemaBwana.

“Je, nisijilipizie kisasi

juu ya taifa kama hili?

30 “Jambo la kutisha na kushtusha

limetokea katika nchi hii:

31 Manabii wanatabiri uongo,

makuhani wanatawala

kwa mamlaka yao wenyewe,

nao watu wangu wanapenda hivyo.

Lakini mtafanya nini mwisho wake?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/5-db89a177e08909e60b4f558336801058.mp3?version_id=1627—

Yeremia 6

Yerusalemu Imezingirwa Na Jeshi

1 “Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini!

Kimbieni kutoka Yerusalemu!

Pigeni tarumbeta katika Tekoa!

Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu!

Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini

na uharibifu wa kutisha.

2 Nitamwangamiza Binti Sayuni,

aliye mzuri sana na mororo.

3 Wachungaji pamoja na makundi yao ya kondoo

na mbuzi watakuja dhidi yake;

watapiga mahema yao kumzunguka,

kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”

4 “Jiandaeni kwa vita dhidi yake!

Inukeni na tumshambulie mchana!

Lakini, ole wetu, mchana unaisha

na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.

5 Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku

na kuharibu ngome zake!”

6 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Kateni miti mjenge boma

kuzunguka Yerusalemu.

Mji huu ni lazima uadhibiwe,

umejazwa na uonevu.

7 Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake,

ndivyo anavyomwaga uovu wake.

Ukatili na maangamizi yasikika ndani yake,

ugonjwa wake na majeraha yake

viko mbele yangu daima.

8 Pokea onyo, Ee Yerusalemu,

la sivyo nitageukia mbali nawe

na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa

asiweze mtu kuishi ndani yake.”

9 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli

kwa uangalifu kama kwenye mzabibu;

pitisha mkono wako kwenye matawi tena,

kama yeye avunaye zabibu.”

10 Niseme na nani na kumpa onyo?

Ni nani atakayenisikiliza mimi?

# Masikio yao yameziba

kwa hiyo hawawezi kusikia.

Neno laBwanani chukizo kwao,

hawalifurahii.

11 Lakini nimejaa ghadhabu yaBwana,

nami siwezi kuizuia.

“Wamwagie watoto walioko barabarani,

na juu ya vijana waume

waliokusanyika pamoja;

mume na mke watakumbwa kwa pamoja ndani yake,

hata nao wazee waliolemewa na miaka.

12 Nyumba zao watapewa watu wengine,

pamoja na mashamba yao na wake zao,

nitakapounyosha mkono wangu

dhidi ya wale waishio katika nchi,”

asemaBwana.

13 “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi mkubwa kabisa,

wote wanatamani kupata faida isiyo halali;

makuhani na manabii wanafanana,

wote wanafanya udanganyifu.

14 Hufunga majeraha ya watu wangu

kama vile hawakuumia sana.

Husema, ‘Amani, amani,’

wakati hakuna amani.

15 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao

inayochukiza mno?

Hapana, hawana aibu hata kidogo;

hawajui hata kuona haya.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa nitakapowaadhibu,”

asemaBwana.

16 Hivi ndivyo asemavyoBwana:

“Simama kwenye njia panda utazame,

ulizia mapito ya zamani,

ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo,

nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita hiyo.’

17 Niliweka walinzi juu yenu na kusema,

‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’

Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’

18 Kwa hiyo sikilizeni, Enyi mataifa,

angalieni, Enyi mashahidi,

lile litakalowatokea.

19 Sikia Ee nchi:

Ninaleta maafa juu ya watu hawa,

matunda ya mipango yao,

kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu

na wameikataa sheria yangu.

20 Wanifaa nini uvumba kutoka Sheba

au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?

Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki,

dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”

21 Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyoBwana:

“Nitawawekea vikwazo mbele ya watu hawa.

Baba na wana wao watajikwaa juu yake,

majirani na marafiki wataangamia.”

22 Hivi ndivyo asemavyoBwana:

“Tazama, jeshi linakuja

kutoka nchi ya kaskazini,

taifa kubwa linaamshwa

kutoka miisho ya dunia.

23 Wamejifunga pinde na mkuki,

ni wakatili na hawana huruma.

Wanatoa sauti kama bahari inayonguruma

wanapokuwa wamepanda farasi zao,

wanakuja kama watu walioandaliwa tayari kwa vita

kukushambulia wewe, Ee Binti Sayuni.”

24 Tumesikia taarifa zao,

nayo mikono yetu imelegea.

Uchungu umetushika,

maumivu kama mwanamke

mwenye utungu wa kuzaa.

25 Usitoke kwenda mashambani

au kutembea barabarani,

kwa kuwa adui ana upanga

na kuna vitisho kila upande.

26 Enyi watu wangu, vaeni magunia

mjivingirishe kwenye majivu,

ombolezeni kwa kilio cha uchungu

kama amliliaye mwana pekee,

kwa maana ghafula

mharabu atatujia.

27 “Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma

na watu wangu kama mawe yenye madini,

ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.

28 Wote ni waasi sugu,

wakienda huko na huko kusengenya.

Wao ni shaba na chuma,

wote wanatenda kwa upotovu.

29 Mivuo inavuma kwa nguvu,

kinachoungua kwa huo moto ni risasi,

lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure;

waovu hawaondolewi.

30 Wanaitwa fedha iliyokataliwa,

kwa sababuBwanaamewakataa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/6-e49680ec34ceddf994d47cedcf5c68f0.mp3?version_id=1627—

Yeremia 7

Dini Za Uongo Hazina Maana

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Simama kwenye lango la nyumba yaBwanana huko upige mbiu ya ujumbe huu:

“ ‘Sikieni neno laBwana, enyi watu wote wa Yuda mliokuja kupitia malango haya ili kumwabuduBwana.

3 Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Tengenezeni njia zenu na matendo yenu, nami nitawaacha mkae mahali hapa.

4 Msitumainie maneno ya udanganyifu na kusema, “Hili ni Hekalu laBwana, hili ni Hekalu laBwana, Hekalu laBwana!”

5 Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu mkitendeana haki kila mmoja na mwenzake,

6 kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe,

7 ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele.

8 Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.

9 “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo na kufukiza uvumba kwa Baali na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua,

10 kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii, inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza?

11 Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! AsemaBwana.

12 “ ‘Nendeni sasa mahali pangu palipokuwa huko Shilo, mahali ambapo nilipafanya pa kwanza kuwa makao ya Jina langu, nanyi mwone lile nililopafanyia kwa ajili ya uovu wa watu wangu Israeli.

13 Mlipokuwa mnafanya yote haya, asemaBwana, nilisema nanyi tena na tena, lakini hamkusikiliza, niliwaita, lakini hamkujibu.

14 Kwa hiyo, nililolifanyia Shilo, nitalifanya sasa kwa nyumba hii iitwayo kwa Jina langu, Hekalu mnalolitumainia, mahali nilipowapa ninyi na baba zenu.

15 Nitawafukuza mbele yangu, kama nilivyowafanyia ndugu zenu, watu wa Efraimu.’

16 “Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, usinililie, usifanye maombi kwa ajili yao, wala usinisihi kwa sababu sitakusikiliza.

17 Je, huyaoni hayo wanayoyatenda katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu?

18 Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha.

19 Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asemaBwana. Je, hawajiumizi wenyewe kwa aibu yao?

20 “ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu itamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.

21 “ ‘Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe!

22 Kwa kuwa nilipowaleta baba zenu kutoka Misri na kusema nao, sikuwapa amri kuhusu sadaka za kuteketezwa na dhabihu tu,

23 lakini niliwapa amri hii nikisema: Mtanitii mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Enendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa.

24 Lakini hawakusikiliza wala kujali, badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

25 Tangu wakati ule baba zenu walipotoka Misri hadi sasa, siku baada ya siku, tena na tena nimewatumia watumishi wangu manabii.

26 Lakini hawakunisikiliza wala hawakujali. Walikuwa na shingo ngumu na kufanya maovu kuliko baba zao.’

27 “Utakapowaambia haya yote, hawatakusikiliza, utakapowaita, hawatajibu.

28 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ni taifa ambalo halimtiiBwana, Mungu wao wala kukubali kurudiwa. Kweli imekufa, imetoweka midomoni mwao.

29 Nyoeni nywele zenu na kuzitupa, ombolezeni juu ya miinuko iliyo kame, kwa kuwaBwanaamekikataa na kukiacha kizazi hiki kilichomkasirisha.

Bonde La Machinjo

30 “ ‘Watu wa Yuda wamefanya maovu machoni pangu, asemaBwana. Wameziweka sanamu zao za machukizo ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu na wameitia unajisi.

31 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia sanamu pa Tofethi kwenye Bonde la Ben-Hinomu ili kuwateketeza wana wao na binti zao kwenye moto, kitu ambacho sikuamuru, wala hakikuingia akilini mwangu.

32 Kwa hiyo mjihadhari, siku zinakuja, asemaBwana, wakati watu watakapokuwa hawapaiti Tofethi au Bonde la Ben-Hinomu, lakini watapaita Bonde la Machinjo, kwa sababu watawazika wafu huko Tofethi mpaka pasiwe tena nafasi.

33 Ndipo mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo na ye yote wa kuwafukuza.

34 Nitazikomesha sauti za shangwe na furaha na sauti za bwana arusi na bibi arusi katikati ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/7-33a1b99e0bdfada4376ac4250541752a.mp3?version_id=1627—

Yeremia 8

1 “ ‘Wakati huo, asemaBwana, mifupa ya Wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, nayo mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka katika makaburi yao.

2 Itawekwa wazi juani na kwenye mwezi na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi.

3 Po pote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.’

Dhambi Na Adhabu

4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana:

“ ‘Je, watu wanapoanguka hawainuki?

Je, mtu anapopotea harudi?

5 Kwa nini basi watu hawa walipotea?

Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara?

Wanang’ang’ania udanganyifu

na wanakataa kurudi.

6 Nimewasikiliza kwa makini,

lakini hawataki kusema lililo sawa.

Hakuna anayetubia makosa yake

akisema, “Nimefanya nini?”

Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe

kama farasi anayekwenda vitani.

7 Hata korongo aliyeko angani

anayajua majira yake yaliyoamriwa,

nao njiwa, mbayuwayu na koikoi

hufuata majira yao ya kurudi.

Lakini watu wangu hawajui

Bwanaanachotaka kwao.

8 “ ‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara

kwa sababu tunayo sheria yaBwana,”

wakati ambapo kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi

imeandika kwa udanganyifu?

9 Wenye hekima wataaibika,

watafadhaika na kunaswa.

Kwa kuwa wamelikataa neno laBwana,

hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?

10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao

na mashamba yao wamiliki wengine.

Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

wana tamaa ya kupata zaidi,

manabii na makuhani vivyo hivyo,

wote wanafanya udanganyifu.

11 Wanafunga majeraha ya watu wangu

bila uangalifu.

Wanasema, “Amani, amani,”

wakati hakuna amani.

12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno?

Hapana, hawana aibu hata kidogo,

hawajui hata kuona haya.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa chini watakapoadhibiwa,

asemaBwana.

13 “ ‘Nitayaondoa mavuno yao,

asemaBwana.

Hapatakuwepo zabibu kwenye mzabibu.

Hapatakuwepo na tini kwenye mtini,

majani yake yatanyauka.

Kile nilichowapa

watanyang’anywa.’ ”

14 “Kwa nini tunaketi hapa?

Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie kwenye miji yenye maboma

na tukaangamie huko!

Kwa kuwaBwana, Mungu wetu

ametuhukumu kuangamia,

na kutupa maji yenye sumu tunywe,

kwa sababu tumemtenda dhambi.

15 Tulitegemea amani,

lakini hakuna jema lililokuja,

tulitegemea wakati wa kupona,

lakini kulikuwa hofu tu.

16 Mkoromo wa farasi za adui

umesikika kuanzia Dani,

kwa mlio wa madume yao ya farasi,

nchi yote inatetemeka.

Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo,

mji na wote waishio ndani yake.”

17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali katikati yenu,

nyoka wenye sumu ambao hawawezi kulogwa,

nao watawauma,”

asemaBwana.

18 Ee mfariji wangu katika huzuni,

moyo wangu umezimia ndani mwangu.

19 Sikia kilio cha watu wangu

kutoka nchi ya mbali:

“Je,Bwanahayuko Sayuni?

Je, mfalme wake hayuko tena huko?”

“Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao,

kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”

20 “Mavuno yamepita,

kiangazi kimekwisha,

nasi hatujaokolewa.”

21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa,

nami nimepondeka pia;

ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.

22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi?

Je, hakuna tabibu huko?

Kwa nini basi hakuna uponyaji

wa majeraha ya watu wangu?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/8-e933fd5efcea2bc05863648d23243122.mp3?version_id=1627—