Yeremia 9

1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

Ningelia mchana na usiku

kwa kuuawa kwa watu wangu.

2 Laiti ningekuwa na nyumba

ya kukaa wasafiri katika jangwa,

ningewaacha watu wangu

na kwenda mbali nao,

kwa kuwa wote ni wazinzi,

kundi la watu wasio waaminifu.

3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde,

ili kurusha uongo;

wamekuwa na nguvu katika nchi

kwa ajili ya uongo,

wala si katika kweli.

Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,

hawanitambui mimi,”

asemaBwana.

4 “Jihadhari na rafiki zako;

usiwaamini ndugu zako.

Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,

na kila rafiki ni msingiziaji.

5 Rafiki humdanganya rafiki,

hakuna ye yote asemaye kweli.

Wamefundisha ndimi zao kudanganya,

wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.

6 Unakaa katikati ya udanganyifu;

katika udanganyifu wao

wanakataa kunitambua mimi,”

asemaBwana.

7 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,

kwani ni nini kingine niwezacho kufanya

kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?

8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu,

hunena kwa udanganyifu.

Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,

lakini moyoni mwake humtegea mtego.

9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”

AsemaBwana.

“Je, nisijilipizie kisasi

kwa taifa kama hili?”

10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.

Yamekuwa ukiwa na wala hakuna apitaye humo,

milio ya ng’ombe haisikiki.

Ndege wa angani wameruka

na wanyama wameondoka.

11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,

makao ya mbweha;

nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa

ili asiwepo atakayeishi humo.”

12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa naBwanaawezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?

13 Bwanaakasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu.

14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.”

15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu.

16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao hawakuwajua wala baba zao, nitawafuatia kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”

17 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,

waite wale walio na ustadi kuliko wote.

18 Nao waje upesi

kutuombolezea

mpaka macho yetu yafurike machozi

na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.

19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:

‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!

Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!

Ni lazima tuihame nchi yetu

kwa sababu nyumba zetu

zimekuwa magofu.’ ”

20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno laBwana;

fungueni masikio yenu

msikie maneno ya kinywa chake.

Wafundisheni binti zenu jinsi ya kuomboleza;

fundishaneni kila mmoja na mwenzake kuomboleza.

21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani

na imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;

imewakatilia mbali watoto katika barabara

na vijana waume kutoka katika viwanja vya miji.

22 Sema, “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Maiti za wanaume zitalala

kama mavi katika mashamba,

kama malundo ya nafaka yaliyokatwa

yalalavyo nyuma ya mvunaji,

wala hakuna anayekusanya.’ ”

23 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake

au mwenye nguvu asijisifu katika nguvu zake

au tajiri asijisifu katika utajiri wake,

24 lakini yeye ajisifuye na ajisifu kwa sababu hili:

kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

kwamba mimi ndimiBwana, nitendaye wema,

hukumu na haki duniani,

kwa kuwa napendezwa na haya,”

asemaBwana.

25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asemaBwana,

26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/9-2849268e2ce5e5921009817933f8b1bf.mp3?version_id=1627—

Yeremia 10

Mungu Na Sanamu

1 Sikieni lile ambaloBwana, anena nanyi Ee nyumba ya Israeli.

2 Hili ndilo asemaloBwana:

“Usijifunze njia za mataifa

wala usitishwe na ishara katika anga,

ingawa mataifa yanatishwa nazo.

3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,

wanakata mti kutoka msituni

na fundi anauchonga kwa patasi.

4 Wanaparemba kwa fedha na dhahabu,

wanakikaza kwa nyundo

na misumari ili kisitikisike.

5 Sanamu zao ni kama sanamu

iliyowekwa shambani kutishia ndege

kwenye shamba la matango,

nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe

kwa sababu haziwezi kutembea.

Usiziogope; haziwezi kudhuru

wala kutenda lo lote jema.”

6 Hakuna aliye kama wewe, EeBwana;

wewe ni mkuu,

jina lako ni lenye nguvu katika uweza.

7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,

Ee mfalme wa mataifa?

Hii ni stahili yako.

Miongoni mwa watu wote wenye hekima

katika mataifa na katika falme zao zote,

hakuna aliye kama wewe.

8 Wote hawana akili tena ni wapumbavu,

wanafundishwa na sanamu za miti

zisizofaa lo lote.

9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi

na dhahabu kutoka Ufazi.

Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza

huvikwa mavazi ya rangi

ya samawi na urujuani:

vyote vikiwa vimetengenezwa

na mafundi stadi.

10 LakiniBwanani Mungu wa kweli,

yeye ndiye Mungu aliye hai,

Mfalme wa milele.

Akiwa amekasirika, dunia hutetemeka,

mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.

11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka duniani na kutoka chini ya mbingu.’ ”

12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

akaufanya ulimwengu kwa hekima yake

na kwa ufahamu wake akazitandaza mbingu.

13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

huyafanya mawingu yainuke

kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua

naye huleta upepo kutoka katika ghala zake.

14 Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa,

kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.

Vinyago vyake ni madanganyo,

wala havina pumzi ndani yake.

15 Havina maana, ni vitu vya mzaha tu,

hukumu yao itakapokuja, wataangamia.

16 Yeye aliye Fungu la Yakobo si kama hivi,

kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,

pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

Maangamizi Yajayo

17 Kusanyeni mali na vitu vyenu muondoke katika nchi hii,

enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.

18 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana:

“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu

wote waishio katika nchi hii;

nitawataabisha ili waweze kutekwa.”

19 Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!

Jeraha langu ni kubwa!

Lakini nilisema,

“Kweli hii ni adhabu yangu,

nami sharti nistahimili.”

20 Hema langu limeangamizwa;

kamba zake zote zimekatwa.

Wana wangu wametekwa

na hawapo tena;

hakuna hata mmoja aliyebaki

kulisimika hema langu

wala wa kusimamisha kibanda changu.

21 Wachungaji hawana akili

wala hawamuliziBwana,

hivyo hawastawi

na kundi lao lote la kondoo

na mbuzi limetawanyika.

22 Sikilizeni! Taarifa inakuja:

ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!

Hii itafanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,

makao ya mbweha.

Maombi Ya Yeremia

23 Ninajua, EeBwana, kwamba maisha ya mwanadamu

si yake mwenyewe;

hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.

24 Unirudi, EeBwana,

lakini kwa kipimo cha haki:

si katika hasira yako,

usije ukaniangamiza.

25 Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa

yale wasiokujua wewe,

juu ya mataifa yale wasioliitia jina lako.

Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;

wamemwangamiza kabisa

na kuiharibu nchi yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/10-9deb23e784a2afef2cdc83b7e2f888c3.mp3?version_id=1627—

Yeremia 11

Agano Limevunjwa

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Sikia maneno ya Agano hili, nawe uwaambie watu wa Yuda na wale waishio katika Yerusalemu.

3 Waambie kwamba hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: ‘Amelaaniwa mtu yule ambaye hatayatii maneno ya Agano hili,

4 yaani maneno niliyowaamuru baba zenu nilipowatoa katika nchi ya Misri, kutoka tanuru la kuyeyushia vyuma.’ Nilisema, ‘Nitiini mimi na mfanye kila kitu ninachowaamuru, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

5 Kisha nitatimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi itiririkayo maziwa na asali,’ nchi ambayo mnaimiliki leo.”

Nikajibu, “Amen,Bwana.”

6 Bwanaakaniambia, “Tangaza maneno haya yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu: ‘Sikilizeni maneno ya Agano hili na kuyafuata.

7 Tangu wakati ule nilipowapandisha baba zenu kutoka Misri mpaka leo, niliwaonya tena na tena, nikisema “Nitiini mimi.”

8 Lakini hawakusikiliza wala kujali, badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Hivyo nikaleta juu yao laana zote za Agano nililokuwa nimewaamuru wao kulifuata lakini wao hawakulishika.’ ”

9 KishaBwanaakaniambia, “Kuna shauri baya linaloendelea miongoni mwa watu wa Yuda na wale wanaoishi katika Yerusalemu.

10 Wamerudia dhambi za baba zao, waliokataa kusikiliza maneno yangu. Wameifuata miungu mingine kuitumikia. Nyumba zote mbili za Israeli na Yuda zimelivunja Agano nililofanya na baba zao.

11 Kwa hivyo, hili ndilo asemaloBwana: ‘Nitaleta juu yao maafa ambayo hawawezi kuyakimbia. Hata kama wakinililia mimi sitawasikiliza.

12 Miji ya Yuda na watu wa Yerusalemu watakwenda kuililia miungu ambayo wameifukizia uvumba, lakini haitawasaidia kamwe wakati maafa yatakapowapiga.

13 Mnayo miungu mingi kama miji mliyo nayo, Ee Yuda, nazo madhabahu mlizozijenga za kufukizia uvumba huyo mungu wa aibu Baali ni nyingi kama barabara za Yerusalemu.’

14 “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yo yote au usinisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao.

15 “Mpenzi wangu anafanya nini hekaluni mwangu

anapofanya mashauri yake maovu na wengi?

Je, nyama iliyowekwa wakfu yaweza

kuondolea mbali adhabu yako?

Unapojiingiza katika ubaya wako,

ndipo unashangilia.”

16 Bwanaalikuita mti wa mzeituni uliostawi

ulio na matunda mazuri kwa sura.

Lakini kwa ngurumo ya mawimbi makuu

atautia moto,

nayo matawi yake yatavunjika.

17 BwanaMwenye Nguvu Zote, aliyekupanda, ametamka maafa kwa ajili yako, kwa sababu nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda mmefanya maovu na kunikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba.

Shauri Baya Dhidi Ya Yeremia

18 Kwa sababuBwanaalinifunulia hila zao mbaya, nilizifahamu, kwa kuwa wakati ule alinionyesha yale waliyokuwa wanayafanya.

19 Nilikuwa kama mwana-kondoo mpole aliyeongozwa machinjoni, mimi sikutambua kwamba walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yangu, wakisema,

“Sisi na tuuangamize mti na matunda yake;

nasi tumkatilie mbali kutoka nchi ya walio hai,

ili kwamba jina lake lisikumbukwe tena.”

20 Lakini, EeBwanaMwenye Nguvu Zote, wewe uhukumuye kwa haki,

nawe uchunguzaye moyo na akili,

mimi na nione ukiwalipiza wao kisasi,

kwa maana kwako nimeweka shauri langu.

21 “Kwa hiyo hili ndiloBwanaasemalo kuhusu watu wa Anathothi wale wanaotafuta uhai wako wakisema, ‘Usitoe unabii kwa jina laBwanala sivyo utakufa kwa mikono yetu’:

22 kwa hiyo hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu. Vijana wao waume watakufa kwa upanga, wana wao na binti zao kwa njaa.

23 Hawatasaziwa hata mabaki kwao, kwa sababu nitaleta maafa kwa watu wa Anathothi katika mwaka wa adhabu yao.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/11-b3ebb764a2340f0f013ad7dfbf8fa44a.mp3?version_id=1627—

Yeremia 12

Lalamiko La Yeremia

1 Wewe daima u mwenye haki, EeBwana,

niletapo daawa mbele yako.

Hata hivyo nitazungumza nawe kuhusu hukumu yako:

Kwa nini njia ya waovu inafanikiwa?

Kwa nini wasiowaaminifu

wote wanaishi kwa raha?

2 Umewapanda nao wameota,

wanakua na kuzaa matunda.

Daima u midomoni mwao

lakini mbali na mioyo yao.

3 Hata hivyo unanijua mimi, EeBwana;

unaniona na kuyachunguza

mawazo yangu kukuhusu wewe.

Wakokote kama kondoo wanaokwenda kuchinjwa!

Watenge kwa ajili ya siku ya kuchinjwa!

4 Je, nchi itakaa katika hali ya kuomboleza mpaka lini

na majani katika kila shamba kunyauka?

Kwa sababu wale waishio ndani yake ni waovu,

wanyama na ndege wameangamia.

Zaidi ya hayo, watu wanasema,

“Bwanahataona yatakayotupata sisi.”

Jibu La Mungu

5 “Ikiwa umeshindana mbio na watu kwa mguu

na wakakushinda,

unawezaje kushindana na farasi?

Ikiwa unajikwaa kwenye nchi ambayo ni salama,

utawezaje kwenye vichaka kando ya Yordani?

6 Ndugu zako, watu wa jamaa yako mwenyewe:

hata wao wamekusaliti;

wameinua kilio kikubwa dhidi yako.

Usiwaamini, ingawa wanazungumza

mema juu yako.

7 “Nitaiacha nyumba yangu,

nitupe urithi wangu;

nitamtia yeye nimpendaye

mikononi mwa adui zake.

8 Urithi wangu umekuwa kwangu

kama simba wa msituni.

Huningurumia mimi,

kwa hiyo ninamchukia.

9 Je, urithi wangu haukuwa

kama ndege wa mawindo wa madoadoa

ambaye ndege wengine wawindao

humzunguka na kumshambulia?

Nenda ukawakusanye pamoja wanyama wote wa mwituni;

walete ili wale.

10 Wachungaji wengi wataliharibu shamba langu la mizabibu

na kulikanyaga shamba langu;

watalifanya shamba langu zuri

kuwa jangwa la ukiwa.

11 Litafanywa kuwa jangwa,

lililokauka na kuachwa ukiwa mbele zangu;

nchi yote itafanywa jangwa

kwa sababu hakuna hata mmoja anayejali.

12 Juu ya miinuko yote ilivyo kama jangwani

mharabu atajaa

kwa maana upanga waBwanautawala,

kuanzia ncha moja ya nchi hadi nyingine;

hakuna hata mmoja atakayekuwa salama.

13 Watapanda ngano lakini watavuna miiba;

watajitaabisha lakini hawatafaidi cho chote.

Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako

kwa sababu ya hasira kali yaBwanaMungu.”

14 Hili ndilo asemaloBwana: “Kwa habari ya majirani zangu wote wabaya wanaonyang’anya urithi ambao ninawapa watu wangu Israeli, nitawang’oa kutoka katika nchi zao, nami nitaing’oa nyumba ya Yuda kutoka katikati yao.

15 Lakini baada ya kuwang’oa, nitawahurumia tena na kumrudisha kila mmoja wao kwenye urithi wake mwenyewe na kwenye nchi yake mwenyewe.

16 Ikiwa watajifunza vyema njia za watu wangu na kuapa kwa Jina langu, wakisema, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo,’ hata kama wakati fulani walifundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watakapofanywa imara katikati ya watu wangu.

17 Lakini kama taifa lo lote halitasikiliza na kutii, nitaling’oa kabisa na kuliangamiza,” asemaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/12-65b0859db929909aeaabd9cd5a5d88c2.mp3?version_id=1627—

Yeremia 13

Mkanda Wa Kitani

1 Hili ndiloBwanaaliloniambia: “Nenda ukanunue mkanda wa kitani ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.”

2 Kwa hiyo nikanunua mkanda, kamaBwanaalivyoniagiza, nikajivika kiunoni.

3 Ndipo neno laBwanalikanijia kwa mara ya pili:

4 “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Eufrati na ukaufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.”

5 Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Eufrati, kamaBwanaalivyoniamuru.

6 Baada ya siku nyingiBwanaakaniambia, “Nenda sasa Eufrati na ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.”

7 Hivyo nikaenda Eufrati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.

8 Ndipo neno laBwanalikanijia:

9 “Hili ndiloBwanaasemalo: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu.

10 Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mkanda huu ambao haufai kabisa!

11 Kwa maana kama vile mkanda ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyojifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asemaBwana, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’

Viriba Vya Mvinyo

12 “Waambie: ‘Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Kama wao wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’

13 Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo asemaloBwana: nitawajaza ulevi wote waishio katika nchi hii, pamoja na wafalme waketio juu ya kiti cha enzi cha Daudi, makuhani, manabii na wale wote waishio Yerusalemu.

14 Nitawagonganisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asemaBwana. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”

Tishio La Kutekwa

15 Sikieni na mzingatie,

msiwe na kiburi,

kwa kuwaBwanaamenena.

16 Mpeni utukufuBwanaMungu wenu,

kabla hajaleta giza,

kabla miguu yenu haijajikwaa

juu ya vilima vitakavyotiwa giza.

Mlitarajia nuru,

lakini ataifanya kuwa giza nene

na kuibadili kuwa huzuni kubwa.

17 Lakini kama hamtasikiliza,

nitalia sirini

kwa ajili ya kiburi chenu;

macho yangu yatalia kwa uchungu,

yakitiririka machozi,

kwa sababu kundi la kondoo na mbuzi laBwana

litachukuliwa mateka.

18 Mwambie mfalme na mamaye,

“Shukeni kutoka kwenye viti vyenu vya enzi,

kwa kuwa taji zenu za utukufu

zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”

19 Miji iliyoko Negebu itafungwa,

wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua.

Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni,

wakichukuliwa kabisa waende mbali.

20 Inua macho yako na uone

wale wanaokuja kutoka kaskazini.

Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa,

kondoo wale uliojivunia?

21 Utasema niniBwanaatakapowaweka juu yako

wale ulioungana nao

kama marafiki wako maalum?

Je, hutapatwa na utungu kama ule wa mwanamke

aliye katika kuzaa?

22 Nawe kama ukijiuliza,

“Kwa nini haya yamenitokea?”

Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi

kwamba marinda yako yameraruliwa

na mwili wako umetendewa vibaya.

23 Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake

au chui kubadili madoadoa yake?

Vivyo hivyo nawe huwezi kufanya mema

wewe uliyezoea kutenda mabaya.

24 “Nitawatawanya kama makapi

yapeperushwayo na upepo wa jangwani.

25 Hii ndiyo kura yako,

fungu nililokuamuria,”

asemaBwana,

“kwa sababu umenisahau mimi

na kuamini miungu ya uongo.

26 Nitayafunua marinda yako mpaka juu ya uso wako

ili aibu yako ionekane:

27 uzinzi wako na kulia kwako kama farasi

kulikojaa tamaa,

ukahaba wako usio na aibu!

Nimeyaona matendo yako ya machukizo

juu ya vilima na mashambani.

Ole wako, Ee Yerusalemu!

Utaendelea kuwa najisi mpaka lini?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/13-a244425ef0b8613c409f06ffcbe12b8b.mp3?version_id=1627—

Yeremia 14

Ukame, Njaa Na Upanga

1 Hili ndilo neno laBwanakwa Yeremia kuhusu ukame:

2 “Yuda anaomboleza,

miji yake inayodhoofika;

wanaomboleza kwa ajili ya nchi,

nacho kilio kinapanda kutoka Yerusalemu.

3 Wakuu wanawatuma watumishi wao maji;

wanakwenda visimani

lakini humo hakuna maji.

Wanarudi na vyombo bila maji;

wakiwa na hofu na kukata tamaa,

wanafunika vichwa vyao.

4 Ardhi imepasuka nyufa

kwa sababu hakuna mvua katika nchi;

wakulima wana hofu

na wanafunika vichwa vyao.

5 Hata kulungu mashambani

anamwaacha mtoto wake aliyezaliwa wakati huo huo

kwa sababu hakuna majani.

6 Punda-mwitu wanasimama juu ya miinuko iliyo kame

na kutweta kama mbweha;

macho yao yanakosa nguvu za kuona

kwa ajili ya kukosa malisho.”

7 Ingawa dhambi zetu zinashuhudia juu yetu,

EeBwana, tenda jambo kwa ajili ya jina lako.

Kwa kuwa kukengeuka kwetu ni kukubwa,

nasi tumetenda dhambi dhidi yako.

8 Ee Tumaini la Israeli,

Mwokozi wake wakati wa taabu,

kwa nini unakuwa kama mgeni katika nchi,

kama msafiri anayekaa kwa usiku mmoja tu?

9 Mbona unakuwa kama mtu aliyeshtukizwa,

kama shujaa asiye na uwezo wa kuokoa?

Wewe uko katikati yetu, EeBwana,

nasi tunaitwa kwa jina lako;

usituache!

10 Hili ndiloBwanaasemalo kuhusu watu hawa:

“Wanapenda sana kutangatanga,

hawaizuii miguu yao.

HivyoBwanahawakubali;

sasa ataukumbuka uovu wao

na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.”

11 KishaBwanaakaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa.

12 Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao, hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”

13 Lakini nikasema, “Aa,BwanaMwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”

14 NdipoBwanaakaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa Jina langu. Sikuwatuma wala sikuwaweka wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.

15 Kwa hiyo, hili ndiloBwanaasemalo kuhusu manabii wanaotabiri kwa Jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na kwa njaa.

16 Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwepo ye yote wa kuwazika wao au wake zao, wana wao au binti zao. Nitawamwagia maafa wanayostahili.

17 “Nena nao neno hili:

“ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi

usiku na mchana bila kukoma;

kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu,

amepata jeraha baya,

pigo la kuangamiza.

18 Kama nikienda mashambani,

ninaona wale waliouawa kwa upanga;

kama nikienda mjini,

ninaona maangamizi ya njaa.

Nabii na kuhani kwa pamoja

wamekwenda katika nchi wasiyoijua.’ ”

19 Je, umemkataa Yuda kabisa?

Umemchukia Sayuni kabisa?

Kwa nini umetuumiza hata kwamba

hatuwezi kuponyeka?

Tulitarajia amani,

lakini hakuna jema lililotujia;

tulitarajia wakati wa kupona

lakini kuna hofu kuu tu.

20 EeBwana, tunatambua uovu wetu

na kosa la baba zetu;

kweli tumetenda dhambi dhidi yako.

21 Kwa ajili ya Jina lako usituchukie kabisa;

usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka.

Kumbuka Agano lako nasi

na usilivunje.

22 Je, kuna sanamu yo yote isiyofaa kitu ya mataifa

iwezayo kuleta mvua?

Je, anga peke yake zaweza kutoa mvua?

La hasha, ni wewe peke yako,

EeBwana, Mungu wetu.

Kwa hiyo tumaini letu liko kwako,

kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/14-375eb06c0288e89ca8c54c81523aeee7.mp3?version_id=1627—

Yeremia 15

Adhabu Isiyoepukika

1 KishaBwanaakaniambia: “Hata kama Mose na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende!

2 Nao kama wakikuuliza, ‘Tuende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndiloBwanaasemalo:

“ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, wakafe;

waliowekwa kwa ajili ya upanga, kwa upanga;

waliowekwa kwa ajili ya njaa, kwa njaa:

waliowekwa kwa ajili ya kutekwa, watekwe.’ ”

3 Bwanaasema, “Nitatuma aina nne ya waharabu dhidi yao, upanga ili kuua na mbwa ili wakokote mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili kula na kuangamiza.

4 Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.

5 “Ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu?

Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?

Ni nani atakayesimama ili kuuliza

kuhusu hali yako?

6 Umenikataa mimi,” asemaBwana.

“Unazidi kukengeuka.

Hivyo nitanyosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,

siwezi kuendelea kukuonea huruma.

7 Nitawapepeta kwa uma wa kupepetea

kwenye malango ya miji katika nchi.

Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,

kwa maana hawajabadili njia zao.

8 Nitawafanya wajane wao kuwa wengi

kuliko mchanga wa bahari.

Wakati wa adhuhuri nitamleta mharabu

dhidi ya mama wa vijana wao waume;

kwa ghafula nitaleta juu yao

maumivu makuu na hofu kuu.

9 Mama mwenye watoto saba atazimia

na kupumua pumzi yake ya mwisho.

Jua lake litatua kungali bado mchana,

atatahayarika na kufedheheka.

Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga

mbele ya adui zao,”

asemaBwana.

10 Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,

mtu ambaye ulimwengu wote

unashindana na kugombana naye!

Sikukopa wala sikukopesha,

lakini kila mmoja ananilaani.

11 Bwanaakasema,

“Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,

hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada

nyakati za maafa na nyakati za dhiki.

12 “Je, mtu aweza kuvunja chuma,

chuma kitokacho kaskazini na shaba?

13 Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,

bila gharama,

kwa sababu ya dhambi zako zote

katika nchi yako yote.

14 Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako

katika nchi usiyoijua,

kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa

utakaowaka juu yako daima.”

15 Wewe unajua, EeBwana,

unikumbuke na unitunze mimi.

Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.

Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;

kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.

16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;

yakawa shangwe yangu

na furaha ya moyo wangu,

kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,

EeBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote.

17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,

wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;

niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako

ulikuwa juu yangu

na wewe ulikuwa umenijaza hasira.

18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi

na jeraha langu ni la kuhuzunisha

wala haliponyeki?

Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,

kama chemchemi iliyokauka?

19 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwana:

“Kama ukitubu, nitakurejeza

ili uweze kunitumikia;

kama ukinena maneno yenye maana,

wala si ya upuzi,

utakuwa mnenaji wangu.

Watu hawa ndio watakaokugeukia,

wala si wewe utakayewageukia wao.

20 Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,

ngome ya ukuta wa shaba;

watapigana nawe

lakini hawatakushinda,

kwa maana mimi niko pamoja nawe

kukuponya na kukuokoa,”

asemaBwana.

21 “Nitakuokoa kutoka katika mikono ya waovu,

na kukukomboa kutoka katika makucha ya watu wakatili.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/15-4548a78186f4e02936d325653f06a3bb.mp3?version_id=1627—

Yeremia 16

Siku Ya Maafa

1 Kisha neno laBwanalikanijia:

2 “Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.”

3 Kwa maana hilo ndilo asemaloBwanakuhusu wana na binti wazaliwao katika nchi hii na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao na wale wanaume ambao ni baba zao:

4 “Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa lakini watakuwa kama mavi yaliyosambaa juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa, nazo maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na cha wanyama wa nchi.”

5 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asemaBwana.

6 “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.

7 Hakuna ye yote atakayewapa chakula ili kuwafariji wale waombolezao kwa ajili ya wale waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, hakuna ye yote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.

8 “Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu na kuketi humo ili kula na kunywa.

9 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, nazo sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’

10 “Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa niniBwanaameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi yaBwana, Mungu wetu?’

11 Basi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asemaBwana.

12 ‘Lakini ninyi mmetenda kwa uovu zaidi kuliko baba zenu. Tazama jinsi ambavyo kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya badala ya kunitii mimi.

13 Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, nako huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu huko.’

14 “Hata hivyo, siku zinakuja,” asemaBwana, “wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’

15 bali watasema, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewatoa wana wa Israeli kutoka katika nchi ya kaskazini na nchi zote ambako alikuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.

16 “Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asemaBwana, “nao watawavua. Baada ya hilo nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima na katika nyufa za miamba.

17 Macho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika.

18 Nitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”

19 EeBwana, nguvu zangu na ngome yangu,

kimbilio langu wakati wa taabu,

kwako mataifa yatakujia

kutoka miisho ya dunia na kusema,

“Baba zetu hawakuwa na cho chote zaidi ya miungu ya uongo,

sanamu zisizofaa kitu

ambazo hazikuwafaidia lo lote.

20 Je, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe?

Naam, lakini hao si miungu!”

21 “Kwa hiyo nitawafundisha:

wakati huu nitawafundisha

nguvu zangu na uwezo wangu.

Ndipo watakapojua

kuwa Jina langu ndimiBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/16-7520136cf9d9651718f03e54d7447a3e.mp3?version_id=1627—

Yeremia 17

Dhambi Ya Yuda Na Adhabu yake

1 “Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma,

imeandikwa kwa ncha ya almasi,

kwenye vibao vya mioyo yao

na kwenye pembe za madhabahu zao.

2 Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao

# na nguzo za Ashera

kandokando ya miti iliyotanda

na juu ya vilima virefu.

3 Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri

na hazina zako zote

nitazitoa ziwe nyara,

pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia miungu

kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.

4 Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza

urithi niliokupa.

Nitakufanya mtumwa wa adui zako

katika nchi usiyoijua,

kwa kuwa umeiwasha hasira yangu,

nayo itawaka milele.”

5 Hili ndilo asemaloBwana:

“Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,

ategemeaye mwenye mwili

kwa ajili ya nguvu zake,

ambaye moyo wake

umemwachaBwana.

6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;

hataona mafanikio yatakapokuja.

Ataishi katika sehemu zisizo na maji,

katika nchi ya chumvi ambapo

hakuna ye yote aishiye humo.

7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katikaBwana,

ambaye matumaini yake ni katikaBwana.

8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji

uenezao mizizi yake

karibu na kijito cha maji.

Hauogopi wakati wa joto ujapo;

majani yake ni mabichi daima.

Hauna hofu katika mwaka wa ukame

na hautaacha kuzaa matunda.”

9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,

ni mwovu kupita kiasi.

Ni nani awezaye kuujua?

10 “MimiBwanahuchunguza moyo

na kuzijaribu nia,

kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,

kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”

11 Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga,

ndivyo alivyo mtu apataye mali

kwa njia zisizo za haki.

Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha,

na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.

12 Kiti cha enzi kilichotukuzwa, kilichoinuliwa tangu mwanzo,

ndiyo sehemu yetu ya mahali patakatifu.

13 EeBwana, uliye tumaini la Israeli,

wote wakuachao wataaibika.

Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini

kwa sababu wamemwachaBwana,

chemchemi ya maji yaliyo hai.

14 Uniponye, EeBwana, nami nitaponyeka;

uniokoe nami nitaokoka,

kwa maana wewe ndiwe ninayekusifu.

15 Wao huendelea kuniambia,

“Liko wapi neno laBwana?

Sasa na litimie!”

16 Sijakukimbia na kuacha kuwa mchungaji wako;

unajua sijaitamani siku ya kukata tamaa.

Kile kipitacho midomoni mwangu

ki wazi mbele yako.

17 Usiwe kwangu kitu cha kunitia hofu kuu;

wewe ndiwe kimbilio langu katika siku ya maafa.

18 Watesi wangu na waaibishwe,

lakini nilinde mimi nisiaibike;

wao na watiwe hofu kuu,

lakini unilinde mimi na hofu kuu.

Uwaletee siku ya maafa;

waangamize kwa maangamizi maradufu.

Kuiadhimisha Sabato

19 Hili ndiloBwanaaliloniambia: “Nenda ukasimame kwenye lango la watu, mahali ambako wafalme wa Yuda huingilia na kutokea, simama pia kwenye malango mengine yote ya Yerusalemu.

20 Waambie, ‘Sikieni neno laBwana, Enyi wafalme wa Yuda nanyi watu wote wa Yuda na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya.

21 Hili ndilo asemaloBwana: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu.

22 Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yo yote wakati wa Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu.

23 Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao na hawakutaka kusikia wala kukubali marudi.

24 Lakini mkiwa waangalifu katika kunitii, asemaBwana, nanyi msipoleta mzigo wo wote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo,

25 ndipo wafalme wakaao juu ya kiti cha enzi cha Daudi, wataingia kupitia malango ya mji huu pamoja na maafisa wao. Wao na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari na farasi, wakiandamana na watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima.

26 Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na chini ya vilima vya magharibi, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba yaBwana.

27 Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wo wote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/17-f25fcda9b39efdb8a11607a42c6053f0.mp3?version_id=1627—

Yeremia 18

Katika Nyumba Ya Mfinyanzi

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Shuka uende mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.”

3 Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake.

4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.

5 Kisha neno laBwanalikanijia kusema:

6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” AsemaBwana. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.

7 Ikiwa wakati wo wote nikitangaza kuwa taifa au ufalme utang’olewa, utaangushwa na kuangamizwa,

8 ikiwa lile taifa nililolionya litatubia uovu wake, ndipo nitakapokuwa na huruma wala sitawapiga kwa maafa niliyokuwa nimekusudia kwa ajili yao.

9 Ikiwa wakati mwingine nitatangaza kuwa taifa ama utawala ujengwe na kusimikwa,

10 ikiwa utafanya maovu mbele zangu na hukunitii, ndipo nitakapoghairi makusudio yangu mema niliyokuwa nimeyakusudia kwa ajili yake.

11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Tazama! Ninaandaa maafa kwa ajili yenu nami ninabuni mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka katika njia zenu mbaya, kila mmoja wenu, tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’

12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”

13 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwana:

“Ulizia miongoni mwa mataifa:

Ni nani alishasikia jambo kama hili?

Jambo la kutisha sana limefanywa

na Bikira Israeli.

14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka

kwenye mitelemko yake ya mawe

wakati wo wote?

Je, maji yake baridi yatokayo katika vyanzo vilivyo mbali

yaliwahi kukoma kutiririka wakati wo wote?

15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

wanafukizia uvumba sanamu zisizofaa kitu,

zilizowafanya wajikwae katika njia zao

na katika mapito ya zamani.

Zimewafanya wapite kwenye vichochoro

na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.

16 Nchi yao itaharibiwa,

itakuwa kitu cha kudharauliwa daima;

wote wapitao karibu nayo watashangaa

na kutikisa vichwa vyao.

17 Kama upepo utokao mashariki,

nitawatawanya mbele ya adui zao;

nitawapa kisogo wala sio uso,

katika siku ya maafa yao.”

18 Wakasema, “Njoni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njoni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali cho chote asemacho.”

19 Nisikilize, EeBwana,

sikia wanayosema washitaki wangu!

20 Je, mema yalipwe kwa mabaya?

Lakini wao wamenichimbia shimo.

Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako

na kunena mema kwa ajili yao

ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.

21 Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa;

uwaache wauawe kwa makali ya upanga.

Wake zao na wasiwe na watoto, na wawe wajane;

waume wao na wauawe,

nao vijana wao waume

wachinjwe kwa upanga vitani.

22 Kilio na kisikike kutoka kwenye nyumba zao

ghafula uwaletapo adui dhidi yao,

kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata

na wameitegea miguu yangu mitego.

23 Lakini unajua, EeBwana,

hila zao zote za kuniua.

Usiyasamehe makosa yao

wala usifute dhambi zao

mbele za macho yako.

Wao na waangamizwe mbele zako;

uwashughulikie wakati wa hasira yako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/18-27ca7468582c0c018208e2a71f9f5661.mp3?version_id=1627—