Yeremia 29

Barua Kwa Watu Wa Uhamishoni

1 Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu.

2 (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekoniana malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.)

3 Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani na Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:

4 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli:

5 “Jengeni nyumba na mstarehe, pandeni bustani na mle mazao yake.

6 Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue.

7 Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. MwombeniBwanakwa ajili ya mji kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”

8 Naam, hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota.

9 Wanawatabiria ninyi uongo kwa Jina langu. Sikuwatuma,” asemaBwana.

10 Hili ndilo asemaloBwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa.

11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asemaBwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.

12 Kisha mtaniita na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza.

13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

14 Nitaonekana kwenu,” asemaBwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka katika mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa ili wachukuliwe uhamishoni,” asemaBwana.

15 Mnaweza mkasema, “Bwanaameinua manabii kwa ajili yetu huku Babeli,”

16 lakini hili ndilo asemaloBwanakuhusu mfalme aketiaye kiti cha enzi cha Daudi na watu wa kwenu wote wanaobaki katika mji huu, yaani nchi yenu, watu ambao hawakwenda pamoja nanyi uhamishoni,

17 naam, hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: “Nitatuma upanga, njaa na tauni dhidi yao nami nitawafanya kuwa kama tini dhaifu zile ambazo ni mbaya sana zisizofaa kuliwa.

18 Nitawafukuza kwa upanga, kwa njaa na kwa tauni nami nitawafanya kitu cha kuchukiza sana kwa falme zote za dunia na kuwa kitu cha laana na cha kuogofya, cha dharau na kukemewa, miongoni mwa mataifa yote nitakakowafukuzia.

19 Kwa kuwa hawakuyasikiliza maneno yangu,” asemaBwana, “maneno ambayo niliwatumia tena na tena kupitia watumishi wangu manabii. Wala ninyi watu wa uhamisho hamkusikiliza pia,” asemaBwana.

20 Kwa hiyo, sikieni neno laBwana, enyi nyote mlio uhamishoni niliowapeleka Babeli kutoka Yerusalemu.

21 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu Ahabu mwana wa Kolaya na Sedekia mwana wa Maaseya, wanaowatabiria uongo kwa Jina langu: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu hasa.

22 Kwa ajili yao, watu wote wa uhamisho kutoka Yuda walioko Babeli watatumia laana hii: ‘Bwanana akutendee kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwachoma kwa moto.’

23 Kwa kuwa wamefanya mambo maovu kabisa katika Israeli, wamezini na wake za majirani zao, tena kwa Jina langu wamesema uongo, mambo ambayo sikuwaambia kuyafanya, nami ni shahidi wa jambo hilo,” asemaBwana.

Ujumbe Kwa Shemaya

24 Mwambie Shemaya Mnehelami,

25 “Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ulituma barua kwa jina lako mwenyewe kwa watu wote wa Yerusalemu, kwa Sefania mwana wa kuhani Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Ulimwambia Sefania,

26 ‘Bwanaamekuweka wewe uwe kuhani badala ya Yehoyada uwe msimamizi wa nyumba yaBwana, utamfunga kwa mikatale na mnyororo wa shingoni mwendawazimu ye yote anayejifanya nabii.

27 Kwa nini basi hukumkemea Yeremia wa Anathothi, aliyejifanya kama nabii miongoni mwenu?

28 Ametutumia ujumbe huu huko Babeli: Mtakuwako huko muda mrefu. Kwa hiyo jengeni nyumba mkakae, pandeni mashamba na mle mazao yake.’ ”

29 Kuhani Sefania, hata hivyo, akamsomea nabii Yeremia ile barua.

30 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

31 “Tuma ujumbe huu kwa watu wote walio uhamishoni: ‘Hili ndiloBwanaasemalo kuhusu Shemaya Mnehelami: Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, hata ingawa sikumtuma, naye amewafanya kuamini uongo,

32 hili ndiloBwanaasemalo: Hakika nitamwadhibu Shemaya Mnehelami pamoja na uzao wake. Hapatakuwa na ye yote atakayebaki miongoni mwa watu hawa, wala hataona mema nitakayowatendea watu wangu, asemaBwana, kwa sababu ametangaza uasi dhidi yangu.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/29-4dcac70fef39acfd1a41fa1b2354abbd.mp3?version_id=1627—

Yeremia 30

Kurudishwa kwa Israeli

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe.

3 Siku zinakuja,’ asemaBwana, ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asemaBwana.”

4 Haya ndiyo manenoBwanaaliyoyanena kuhusu Israeli na Yuda:

5 “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Vilio vya woga vinasikika:

hofu kuu wala si amani.

6 Ulizeni na mkaone:

Je, mwanaume aweza kuzaa watoto?

Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu

ameweka mikono yake tumboni

kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa,

kila uso umegeuka rangi kabisa?

7 Tazama jinsi ile siku itakavyokuwa ya kutisha!

Hakutakuwa na nyingine mfano wake.

Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo,

lakini ataokolewa kutoka katika hiyo.

8 “ ‘Katika siku ile,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote,

‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao

na kuvipasua vifungo vyao;

wageni hawatawafanya tena watumwa.

9 Badala yake, watamtumikiaBwana, Mungu wao

na Daudi mfalme wao,

nitakayemwinua kwa ajili yao.

10 “ ‘Hivyo usiogope, Ee Yakobo mtumishi wangu,

usifadhaike, Ee Israeli,’

asemaBwana.

‘Hakika, nitakuokoa wewe kutoka mahali pa mbali,

wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao,

Yakobo atakuwa tena na amani na usalama,

wala hakuna atakayemtia hofu.

11 Mimi niko pamoja nawe nami nitakuokoa,’

asemaBwana.

‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote

ambamo miongoni mwao nimewatawanya,

sitawaangamiza ninyi kabisa.

Nitawaadhibu, lakini kwa haki.

Sitawaacha kabisa bila adhabu.’

12 “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Kidonda chako hakina dawa,

jeraha lako haliponyeki.

13 Hakuna ye yote wa kukutetea shauri lako,

hakuna dawa ya kidonda chako,

wewe hutapona.

14 Wale walioungana nawe wote wamekusahau,

hawajali cho chote kukuhusu wewe.

Nimekupiga kama vile ambavyo adui angelifanya

na kukuadhibu kama vile ambavyo

mtu mkatili angelifanya,

kwa sababu hatia yako ni kubwa mno

na dhambi zako ni nyingi sana.

15 Kwa nini unalia kwa ajili ya jeraha lako,

yale maumivu yako yasiyoponyeka?

Kwa sababu ya uovu wako mkubwa

na dhambi zako nyingi

nimekufanyia mambo haya.

16 “ ‘Lakini watu wote wakuangamizao wataangamizwa;

adui zako wote watakwenda uhamishoni.

Wale wote wakutekao nyara watatekwa nyara;

wote wakufanyao mateka nitawafanya mateka.

17 Lakini nitakurudishia afya yako

na kuyaponya majeraha yako,’

asemaBwana,

‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa,

Sayuni ambaye hakuna ye yote anayekujali.’

18 “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Nitarudisha baraka za mahema ya Yakobo

na kuhurumia maskani yake.

Mji utajengwa tena juu ya magofu yake,

nalo jumba la kifalme litasimama

mahali pake halisi.

19 Nyimbo za kushukuru zitatoka kwao

na sauti ya furaha.

Nitaiongeza idadi yao

wala hawatapungua,

nitawapa heshima

na hawatadharauliwa.

20 Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa

siku za zamani,

nayo jumuiya yao itaimarishwa mbele yangu;

nitawaadhibu wale wote wawaoneao.

21 Mmoja wao atakuwa kiongozi wao;

mtawala wao atainuka miongoni mwao.

Nitamleta karibu nami naye atanikaribia mimi,

kwa maana ni nani yule atakayejitolea

kuwa karibu nami?’

asemaBwana.

22 ‘Kwa hiyo ninyi mtakuwa watu wangu,

nami nitakuwa Mungu wenu.’ ”

23 Tazama, tufani yaBwana

italipuka kwa ghadhabu,

upepo wa kisulisuli uendao kasi

utashuka juu ya vichwa vya waovu.

24 Hasira kali yaBwanahaitarudi nyuma

mpaka atakapotimiza

makusudi yote ya moyo wake.

Siku zijazo

mtayaelewa haya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/30-b858b21008b4995dad5e3ad2b0161b92.mp3?version_id=1627—

Yeremia 31

Kurudi Kwa Watu Wa Uhamishoni Kwa Shangwe

1 “Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli nao watakuwa watu wangu,” asemaBwana.

2 Hili ndilo asemaloBwana:

“Watu watakaopona upanga

watapata upendeleo jangwani,

nitakuja niwape Israeli pumziko.”

3 Bwanaalitutokea wakati uliopita akisema:

“Nimekupenda kwa upendo wa milele,

nimekuvuta kwa wema.

4 Nitakujenga tena nawe utajengeka upya,

Ewe Bikira Israeli.

Utachukua tena matari yako

na kwenda kucheza na wenye furaha.

5 Utapanda tena shamba la mizabibu

juu ya vilima vya Samaria,

wakulima watapanda

na kufurahia matunda yake.

6 Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele

juu ya vilima vya Efraimu wakisema,

‘Njoni, twendeni juu Sayuni,

kwakeBwanaMungu wetu.’ ”

7 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mwimbieni Yakobo kwa furaha,

mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa.

Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme,

‘EeBwana, okoa watu wako,

mabaki ya Israeli.’

8 Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini

na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia.

Miongoni mwao watakuwepo vipofu na viwete,

mama wajawazito na wenye utungu wa kuzaa,

umati mkubwa wa watu utarudi.

9 Watakuja wakilia;

wataomba wakati nikiwarudisha.

Nitawaongoza kando ya vijito vya maji

katika mapito yaliyo tambarare

ambapo hawatajikwaa,

kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli,

naye Efraimu ni mwanangu,

mzaliwa wangu wa kwanza.

10 “Sikieni neno laBwana, Enyi mataifa,

litangazeni katika nchi za pwani ya mbali:

‘yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya

na atalichunga kundi lake la kondoo

kama mchungaji.’

11 Kwa kuwaBwanaatamlipia fidia Yakobo

na kuwakomboa kutoka mkononi mwao

walio na nguvu kuliko wao.

12 Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni;

watashangilia ukarimu waBwana:

nafaka, divai mpya na mafuta,

wana-kondoo wachanga

na ndama wa makundi ya ng’ombe nitakaowapa.

Watakuwa kama bustani iliyonyeshewa vizuri,

wala hawatahuzunika tena.

13 Kisha wanawali watacheza na kufurahi,

vijana waume na wazee pia.

Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,

nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.

14 Nitawashibisha makuhani kwa wingi,

nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,”

asemaBwana.

15 Hili ndilo asemaloBwana:

“Sauti imesikika huko Rama,

maombolezo na kilio kikubwa,

Raheli akiwalilia watoto wake

na anakataa kufarijiwa,

kwa sababu watoto wake hawako tena.”

16 Hili ndilo asemaloBwana:

“Izuie sauti yako kulia

na macho yako yasitoe machozi,

kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,”

asemaBwana.

“Watarudi kutoka nchi ya adui.

17 Kwa hiyo kuna tumaini kwa ajili yako

katika siku zijazo,”

asemaBwana.

“Watoto wako watarudi

katika nchi yao yenyewe.

18 “Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:

‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,

nami nimekubali kutii.

Unirudishe, nami nitarudi,

kwa sababu wewe ndiweBwana, Mungu wangu.

19 Baada ya kupotea,

nilitubu;

baada ya kuelewa,

nilijipiga kifua.

Niliaibika na kuona haya

kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’

20 Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,

mtoto ninayependezwa naye?

Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,

bado ninamkumbuka.

Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,

nina huruma kubwa kwa ajili yake,”

asemaBwana.

21 “Weka alama za barabara,

weka vibao vya kuelekeza.

Zingatia vyema njia kuu,

barabara ile unayoipita.

Rudi, Ee Bikira Israeli,

rudi kwenye miji yako.

22 Utatangatanga hata lini,

Ee binti usiye mwaminifu?

Bwanaameumba kitu kipya duniani,

mwanamke atamlinda mwanaume.”

23 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘Bwanaakubariki, Ee makao ya haki, Ee mlima mtakatifu.’

24 Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao.

25 Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”

26 Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.

27 Bwanaasema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.

28 Kama vile nilivyowaangalia ili kuwang’oa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asemaBwana.

29 “Katika siku hizo watu hawatasema tena,

“ ‘Baba wamekula zabibu chachu,

nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’

30 Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; ye yote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi.

31 “Wakati unakuja,” asemaBwana,

“nitakapofanya Agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

32 Halitafanana na Agano

nililofanya na baba zao

wakati nilipowashika mkono

na kuwaongoza watoke Misri,

kwa sababu walivunja Agano langu,

ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”

asemaBwana.

33 “Hili ndilo Agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli,

baada ya wakati ule,” asemaBwana.

“Nitaweka sheria yangu ndani yao

na kuiandika katika mioyo yao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

au mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘UmjueBwanaMungu,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

kuanzia aliye mdogo kabisa kwao hata aliye mkuu sana,”

asemaBwana.

“Kwa sababu nitausamehe uovu wao

na sitazikumbuka dhambi zao tena.”

35 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyeweka jua

liwake mchana,

yeye anayeamuru mwezi na nyota

kung’ara usiku,

yeye aichafuaye bahari

ili mawimbi yake yangurume;

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:

36 “Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”

asemaBwana,

“ndipo wazao wa Israeli watakoma

kuwa taifa mbele yangu daima.”

37 Hili ndilo asemaloBwana:

“Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika

na misingi ya dunia chini

ikaweza kuchunguzwa,

ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli

kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”

asemaBwana.

38 “Siku zinakuja,” asemaBwana, “wakati mji huu utakapojengwa kwa upya kwa ajili yangu kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.

39 Kamba ya kupimia itaanzia hapo kunyooka mpaka kwenye kilima cha Garebu na kisha kugeuka kuelekea Goa.

40 Bonde lote watupwapo maiti na majivu pia na matuta yote kutoka Bonde la Kidroni upande wa mashariki mpaka kwenye pembe ya Lango la Farasi, itakuwa takatifu kwaBwana. Kamwe mji huu hautang’olewa tena wala kubomolewa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/31-9fa262e701d74299e658fe94c13bfda7.mp3?version_id=1627—

Yeremia 32

Yeremia Anunua Shamba

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwanakatika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Mfalme Nebukadneza.

2 Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzunguka mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda.

3 Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka.

4 Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe.

5 Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi mpaka nitakapomshughulikia, asemaBwana. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ”

6 Yeremia akasema, “Neno laBwanalilinijia kusema:

7 Hanameli mwana wa Shalumu mwana wa ndugu wa baba yako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulinunua.’

8 “Kisha, kamaBwanaalivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, ujinunulie.’

“Nilijua kwamba hili lilikuwa neno laBwana.

9 Hivyo nikalinunua shamba lile huko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli nami nikampimia shekeli kumi na sabaza fedha.

10 Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi na kupima ile fedha kwenye mizani.

11 Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri,

12 nami nikampa Baruki mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi.

13 “Mbele yao, nilimpa Baruki maelezo hayo:

14 ‘Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu.

15 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’

16 “Baada ya kumkabidhi Baruki mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwombaBwana:

17 “EeBwanaMwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.

18 Huonyesha upendo kwa maelfu lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako niBwanaMwenye Nguvu Zote,

19 makusudi yako ni makuu na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake na kama yanayostahili matendo yake.

20 Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri na umeyaendeleza mpaka leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo mpaka leo.

21 Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa matisho makuu.

22 Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi ijaayo maziwa na asali.

23 Wakaingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako, hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao.

24 “Tazama jinsi ambavyo tumezungukwa na jeshi ili kuuteka mji huu. Kwa sababu ya upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo ambao wanaushambulia. Ulilosema limetokea kama vile unavyoona sasa.

25 Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, EeBwanaMwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha na jambo hilo lishuhudiwe.’ ”

26 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

27 “Mimi ndimiBwana, Mungu wa wote wenye mwili, Je, kuna jambo lo lote lililo gumu nisiloliweza?

28 Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa Wakaldayo na mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ambaye atauteka.

29 Wakaldayo ambao wanaushambulia mji huu watakuja na kuuchoma moto na kuuteketeza, pamoja na nyumba ambamo ndani yake watu wamenikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba katika mapaa na kumimina sadaka ya kinywaji kwa miungu mingine.

30 “Watu wa Israeli na wa Yuda hawakufanya kitu kingine cho chote ila uovu mbele zangu tangu ujana wao, naam, watu wa Israeli hawakufanya kitu kingine cho chote ila kunikasirisha kwa kazi ambazo mikono yao imetengeneza, asemaBwana.

31 Tangu siku ulipojengwa hadi sasa, mji huu umenikasirisha na kunighadhibisha kiasi kwamba ni lazima niuondoe machoni pangu.

32 Watu wa Israeli na wa Yuda wamenikasirisha kwa uovu wote waliofanya, wao, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu.

33 Walinigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao, ingawa niliwafundisha tena na tena, hawakupenda kusikiliza wala kuitikia marudi.

34 Waliweka miungu yao ya kuchukiza sana katika nyumba iitwayo kwa Jina langu na kuinajisi.

35 Wakajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu kwa ajili ya Baali katika Bonde la Ben-Hinomu ambapo walitoa wana wao na binti zao kafara kwa Moleki, ingawa kamwe sikuamuru, wala halikuingia akilini mwangu, kwamba watafanya chukizo kama hilo na kumfanya Yuda atende dhambi.

36 “Mnasema kuhusu mji huu, ‘Kwa upanga, njaa na tauni mji utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli,’ lakini hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo:

37 Hakika nitawakusanya kutoka katika nchi zote nilizowafukuzia katika hasira yangu kali na ghadhabu yangu kuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwaruhusu waishi kwa salama.

38 Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.

39 Nitawapa moyo mmoja na kutenda pamoja, ili kwamba waniche daima kwa mema yao wenyewe na kwa mema ya watoto wao baada yao.

40 Nitafanya nao Agano la milele: Kamwe sitaacha kuwatendea mema, nami nitawavuvia kunicha mimi, ili kwamba kamwe wasigeukie mbali nami.

41 Nitafurahia kuwatendea mema na kwa hakika nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na roho yangu yote.

42 “Hili ndilo asemaloBwana: Kama nilivyoleta maafa haya makubwa kwa watu hawa, ndivyo nitakavyowapa mafanikio niliyowaahidi.

43 Kwa mara nyingine tena mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo mlisema, ‘Imekuwa ukiwa, isiyofaa, isiyo na watu wala wanyama, kwa sababu imetiwa mikononi mwa Wakaldayo.’

44 Mashamba yatanunuliwa kwa fedha na hati zitatiwa sahihi, zitatiwa muhuri na kushuhudiwa katika nchi ya Benyamini katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, katika miji ya Yuda na katika miji ya nchi ya vilima, sehemu ya magharibi katika miji ya tambarare na katika Negebu, kwa sababu nitarudisha tena mafanikio yao, asemaBwana.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/32-6c94f231c5d7297db41fee6303780ebd.mp3?version_id=1627—

Yeremia 33

Ahadi Ya Kurudishwa

1 Wakati Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno laBwanalilimjia mara ya pili kusema:

2 “Hili ndiloBwanaasemalo, yeye aliyeumba dunia,Bwanaaliyeifanya na kuithibitisha,Bwanandilo jina lake:

3 ‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika usiyoyajua.’

4 Kwa maana hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba katika mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda yaliyobomolewa yatumiwe dhidi ya kule kuzungukwa na jeshi na upanga

5 katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowachinja katika hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.

6 “ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama.

7 Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka katika nchi ya kutekwa kwao na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali.

8 Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu.

9 Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia juu ya mambo yote mazuri ninayoufanyia, nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’

10 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine

11 sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi na bwana arusi na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba yaBwana, wakisema,

“ ‘ “MshukuruniBwanaMwenye Nguvu Zote,

kwa maanaBwanani mwema;

upendo wake wadumu milele.”

Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama zilivyokuwa hapo awali,’ asemaBwana.

12 “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: ‘Mahali hapa, ambapo ni ukiwa pasipo na wanadamu wala wanyama, katika miji yake, patakuwepo tena malisho kwa ajili ya wachungaji kupumzisha makundi yao ya kondoo na mbuzi.

13 Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo na mbuzi yatapita tena chini ya mkono wa yeye ayahesabuye,’ asemaBwana.

14 “ ‘Siku zinakuja,’ asemaBwana, ‘wakati nitakapotimiza ahadi yangu ya rehema niliyoifanya kwa nyumba ya Israeli na kwa nyumba ya Yuda.

15 “ ‘Katika siku hizo na wakati huo nitalifanya Tawi la haki

lichipuke kutoka ukoo wa Daudi,

naye atafanya lile lililo haki na sawa

katika nchi.

16 Katika siku hizo, Yuda ataokolewa

na Yerusalemu ataishi salama.

Hili ndilo jina atakaloitwa:

BwanaNdiye Haki Yetu.’

17 Kwa maana hili ndilo asemaloBwana: ‘Daudi kamwe hatakosa mtu wa kukalia kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli,

18 wala hata makuhani, ambao ni Walawi, kamwe hawatakosa mtu wa kusimama mbele zangu daima ili kutoa sadaka za kuteketezwa, ili kuteketeza sadaka ya nafaka na kutoa dhabihu.’ ”

19 Neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

20 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Ikiwa mtaweza kuvunja Agano langu kuhusu mchana na usiku, ili mchana na usiku visiwepo kwa nyakati zake,

21 basi Agano langu na Daudi mtumishi wangu na Agano langu na Walawi ambao ni makuhani wanaohudumu mbele zangu, linaweza kuvunjwa na Daudi hatakuwa tena na mzao wa kutawala katika kiti chake cha enzi.

22 Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”

23 Neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

24 “Je, hujasikia kwamba watu hawa wanasema, ‘Bwanaamezikataa zile falme mbili alizozichagua?’ Kwa hiyo wamewadharau watu wangu na hawawaoni tena kama taifa.

25 Hili ndilo asemaloBwana: ‘Kama sijathibitisha Agano langu na mchana na usiku na kuzisimika sheria za mbingu na nchi,

26 basi nitawakataa wazao wa Yakobo na Daudi mtumishi wangu na sitachagua mmoja wa wanawe kutawala juu ya wazao wa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Kwa maana nitawarudisha kutoka kwenye nchi ya kutekwa kwao na kuwaonea huruma.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/33-2a1aedabc8ed086cc555318a1a07e42a.mp3?version_id=1627—

Yeremia 34

Onyo Kwa Sedekia

1 Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walipokuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote inayoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli, kusema: Nenda kwa Sedekia, mfalme wa Yuda na umwambie, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli naye atauteketeza kwa moto.

3 Hutaweza kuepuka mkono wake bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utakwenda Babeli.

4 “ ‘Lakini sikia ahadi yaBwana, Ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemaloBwanakukuhusu: Hutakufa kwa upanga,

5 utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, EeBwana!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asemaBwana.’ ”

6 Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu,

7 wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda ambayo bado ilikuwa imara yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa ndiyo miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.

Uhuru Kwa Watumwa

8 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwanabaada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu kutangaza uhuru kwa watumwa.

9 Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania wanawake na wanaume, hakuna mtu ye yote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa.

10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru.

11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru na kuwafanya tena watumwa.

12 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

13 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya Agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nikasema,

14 ‘Kila mwaka wa saba kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza mwenyewe kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali.

15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya Agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu.

16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi Jina langu, kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.

17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwana, hamkunitii mimi, hamkutangaza uhuru kwa ajili ya watu wa kwenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asemaBwana, ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya muwe chukizo kwa falme zote za dunia.

18 Watu waliovunja Agano langu na ambao hawakutunza masharti ya Agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili kisha kutembea kati ya vile vipande vya huyo ndama.

19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama,

20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.

21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu.

22 Nitatoa amri, asemaBwana, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, watautwaa na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na ye yote atakayeweza kuishi humo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/34-708bbfd1d2edd2547a5530ab7fbdbe21.mp3?version_id=1627—

Yeremia 35

Warekabi Wasifiwa

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwanawakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:

2 “Nenda kwa jamaa ya Warekabi na uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba yaBwanana uwape divai wanywe.”

3 Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi.

4 Nikawaleta katika nyumba yaBwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu aliyekuwa bawabu.

5 Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”

6 Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai.

7 Pia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu, kamwe msiwe na kitu cho chote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’

8 Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu, mwana wa Rekabu, alichotuamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai

9 wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao.

10 Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu.

11 Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njoni, ni lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washami.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”

12 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

13 “Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu na kuyatii maneno yangu?’ asemaBwana.

14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi.

15 Tena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya na kuyatengeneza matendo yake, msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza.

16 Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’

17 “Kwa hiyo, hili ndiloBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza, niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”

18 Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’

19 Kwa hiyo hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kumpata mtu wa kunitumikia mimi.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/35-7693612bbd58e667378b5d475304d49d.mp3?version_id=1627—

Yeremia 36

Yehoyakimu Achoma Kitabu Cha Yeremia

1 Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwaBwanakusema:

2 “Chukua kitabu na uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa.

3 Labda watu wa Yuda watakaposikia juu ya kila maafa ninayokusudia kuwapiga nayo kila mmoja wao atageuka kutoka katika njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”

4 Hivyo Yeremia akamwita Baruki mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasemaBwana, Baruki akayaandika katika kitabu.

5 Kisha Yeremia akamwambia Baruki, “Nimezuiliwa, mimi siwezi kuingia katika Hekalu laBwana.

6 Basi wewe nenda katika nyumba yaBwanasiku ya kufunga na uwasomee watu maneno yaBwanakutoka katika kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka kwenye miji yao.

7 Labda wataomba na kusihi mbele zaBwanana kila mmoja atageuka kutoka katika njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa naBwanani kubwa.”

8 Baruki mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya, katika Hekalu laBwanaalisoma maneno yaBwanakutoka katika kile kitabu.

9 Katika mwezi wa tisa, mnamo mwaka wa tano wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele zaBwanailitangazwa kwa watu wote walioko Yerusalemu na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda.

10 Kutoka katika chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruki akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu laBwanamaneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.

11 Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote yaBwanakutoka kwenye kile kitabu,

12 alishuka kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote, yaani: Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania na maafisa wengine wote.

13 Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruki akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu,

14 maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruki, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruki mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake.

15 Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”

Ndipo Baruki akawasomea kile kitabu.

16 Walipoyasikia maneno haya yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruki, “Ni lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.”

17 Kisha wakamwuliza Baruki, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”

18 Baruki akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”

19 Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruki, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu ye yote asijue mahali mlipo.”

20 Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu.

21 Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu na Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme.

22 Ulikuwa mwezi wa tisa na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto.

23 Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni hadi kitabu chote kikateketea.

24 Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yo yote wala hawakuyararua mavazi yao.

25 Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu lakini hakuwasikiliza.

26 Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruki na nabii Yeremia. LakiniBwanaalikuwa amewaficha.

27 Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruki aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno laBwanalilimjia Yeremia likisema:

28 “Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto.

29 Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?”

30 Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwanakuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu ye yote atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi, maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku.

31 Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao, nitaleta juu yao na wote waishio Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”

32 Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruki mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruki akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto na maneno mengine mengi yanayofanana na hayo yaliyoongezewa humo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/36-2fda8ecc95aeb8e760099e8bb2aca80c.mp3?version_id=1627—

Yeremia 37

Yeremia Gerezani

1 Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, akatawala mahali pa Yehoyakinimwana wa Yehoyakimu.

2 Lakini si Sedekia wala watumishi wake wala watu wa nchi waliosikiliza maneno yaBwanaaliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.

3 Hata hivyo, Mfalme Sedekia, akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia wakiwa na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwaBwana, Mungu wetu.”

4 Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani.

5 Jeshi la Farao lilikuwa limetoka Misri, nao Wakaldayo ambao walikuwa wameuzunguka Yerusalemu kwa majeshi waliposikia taarifa kuhusu jeshi hilo walijiondoa Yerusalemu.

6 Ndipo neno laBwanalikamjia nabii Yeremia kusema:

7 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililotoka kuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri.

8 Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’

9 “Hili ndiloBwanaasemalo: Msijidanganye wenyewe mkifikiri kwamba, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawashambulia!

10 Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.”

11 Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao,

12 Yeremia akaanza kuondoka mjini ili kwenda kwenye nchi ya Benyamini ili akapate sehemu yake ya milki miongoni mwa watu huko.

13 Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi, ambaye jina lake lilikuwa Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, akamkamata na kusema, “Wewe unakwenda kujiunga na Wakaldayo!”

14 Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa.

15 Wakamkasirikia Yeremia, wakaruhusu apigwe na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya gereza.

16 Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu.

17 Kisha Mfalme Sedekia akatuma aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomwuliza kwa siri, “Je, kuna neno lo lote kutoka kwaBwana?”

Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”

18 Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanitia gerezani?

19 Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii?’

20 Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi nisije nikafa humo.”

21 Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku mpaka mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/37-5b5fbaef301f5b47a1a458dfc81aca3f.mp3?version_id=1627—

Yeremia 38

Yeremia Atupwa Kwenye Kisima

1 Shefatia mwana wa Matani, Gedalia mwana wa Pashuri, Yehukali mwana wa Shelemia na Pashuri mwana wa Malkiya wakasikia kile Yeremia alichokuwa akiwaambia watu wote wakati aliposema,

2 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Ye yote akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni, lakini ye yote atakayejisalimisha kwa Wakaldayo ataishi. Atakayeyatoa maisha yake kama nyara, ataishi.’

3 Tena hili ndilo asemaloBwana: ‘Mji huu kwa hakika utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babeli, ambaye atauteka.’ ”

4 Ndipo maafisa wakamwambia mfalme, “Mtu huyu imempasa kuuawa. Anawakatisha tamaa askari waliobaki katika mji huu, vivyo hivyo na watu wote pia, kwa ajili ya mambo anayowaambia. Mtu huyu hawatakii mema watu hawa bali maangamizi yao.”

5 Mfalme Sedekia akajibu, “Yeye yuko mikononi mwenu! Mfalme hawezi kufanya lo lote kuwapinga ninyi.”

6 Basi wakamchukua Yeremia na kumtia kwenye kisima cha Malkiya, mwana wa mfalme, kilichokuwa katika ua wa walinzi. Wakamtelemsha Yeremia kwa kamba ndani ya kisima, hakikuwa na maji ndani yake, ila tope tu, naye Yeremia akazama ndani ya matope.

7 Lakini Ebed-Meleki, Mkushi, aliyekuwa afisa katika jumba la kifalme, akasikia kuwa walikuwa wamemtia Yeremia ndani ya kisima. Wakati mfalme alipokuwa ameketi katika lango la Benyamini,

8 Ebed-Meleki akatoka nje ya jumba la kifalme na kumwambia,

9 “Mfalme bwana wangu, watu hawa wamefanya uovu kwa yote waliomtendea nabii Yeremia. Wamemtupa ndani ya kisima, mahali ambapo atakufa kwa njaa wakati ambapo hakuna chakula po pote katika mji.”

10 Kisha mfalme akamwamuru Ebed-Meleki, Mkushi, akisema, “Chukua watu thelathini kutoka hapa pamoja nawe, mkamtoe nabii Yeremia huko kwenye kisima kabla hajafa.”

11 Basi Ebed-Meleki akawachukua watu pamoja naye wakaenda mpaka kwenye chumba kilichoko chini ya hazina ndani ya jumba la kifalme. Akachukua matambaa makukuu pamoja na nguo zilizochakaa kutoka huko na kumshushia Yeremia kwa kamba ndani ya kisima.

12 Ebed-Meleki Mkushi akamwambia Yeremia, “Weka haya matambaa makukuu na hizo nguo zilizochakaa makwapani ili kuzuia kamba.” Yeremia akafanya hivyo,

13 nao wakamvuta juu kwa kamba na kumtoa katika kisima. Yeremia akakaa katika ua wa walinzi.

Sedekia Amhoji Yeremia Tena

14 Ndipo Mfalme Sedekia akatuma wamwitie nabii Yeremia na kutaka wamlete kwake kwenye ingilio la tatu kwenye Hekalu laBwana. Mfalme akamwambia Yeremia, “Ninataka kukuuliza jambo fulani, usinifiche kitu cho chote.”

15 Yeremia akamwambia Sedekia, “Nikikupa jibu, je, hutaniua? Hata kama nikikupa shauri wewe hutanisikiliza.”

16 Lakini Mfalme Sedekia akamwapia Yeremia kiapo hiki kwa siri, akisema, “Hakika kama aishivyoBwana, ambaye ametupa pumzi, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako.”

17 Kisha Yeremia akamwambia Sedekia, “Hili ndilo asemaloBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Ikiwa utajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, maisha yako yatasalimika na mji huu hautateketezwa kwa moto, wewe na jamaa yako mtaishi.

18 Lakini ikiwa hutajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwa Wakaldayo na watauteketeza kwa moto na wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao.’ ”

19 Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Ninawaogopa Wayahudi ambao wamekimbilia kwa Wakaldayo, kwa kuwa Wakaldayo wanaweza kunitia mikononi mwao nao wakanitenda vibaya.”

20 Yeremia akajibu, “Hawatakutia mikononi mwao. MtiiBwanakwa kufanya kile ninachokuambia. Kisha utafanikiwa na maisha yako yatakuwa salama.

21 Lakini ukikataa kujisalimisha, hili ndiloBwana, alilonifunulia:

22 Wanawake wote walioachwa katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda wataletwa mbele ya maafisa wa mfalme wa Babeli. Wanawake hao watakuambia:

“ ‘Walikupotosha na kukushinda,

wale rafiki zako uliowaamini.

Miguu yako imezama matopeni;

rafiki zako wamekuacha.’

23 “Wake zako wote na watoto wataletwa na kutiwa mikononi mwa Wakaldayo. Wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao. Lakini utatekwa na mfalme wa Babeli na mji huu utateketezwa kwa moto.”

24 Kisha Sedekia akamwambia Yeremia, “Mtu ye yote na asijue juu ya haya mazungumzo, la sivyo utakufa.

25 Ikiwa maafisa watasikia kwamba nimezungumza nawe, nao wakakujia na kusema, ‘Tuambie kile ulichozungumza na mfalme na kile mfalme alichokuambia, usitufiche au sivyo tutakuua,’

26 basi waambie, ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme asinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani nisije nikafia huko.’ ”

27 Maafisa wote wakamjia Yeremia na kumwuliza, naye Yeremia akawaambia kila kitu mfalme alichomwagiza kusema. Kisha hawakusema lo lote zaidi na Yeremia kwa sababu hakuna ye yote aliyesikia mazungumzo yake na mfalme.

28 Naye Yeremia akabaki katika ua wa walinzi mpaka siku Yerusalemu ilipotekwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/38-d77bf7850fbfaa60d21dd26098288fd9.mp3?version_id=1627—