Isaya 7

Ishara Ya Imanueli

1 Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramuna Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.

2 Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo moyo wa Ahazi na ya watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.

3 NdipoBwanaakamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi.

4 Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia.

5 Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema,

6 “Tuishambulie Yuda, naam na tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.”

7 LakiniBwanaMwenyezi asema hivi:

“ ‘Jambo hili halitatendeka,

halitatokea,

8 kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,

na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.

Katika muda wa miaka sitini na mitano

Efraimu atakuwa ameharibiwa

kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.

9 Kichwa cha Efraimu ni Samaria,

na kichwa cha Samaria

ni mwana wa Remalia peke yake.

Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,

hamtaimarika kamwe.’ ”

10 Bwanaakasema na Ahazi tena,

11 “MwombeBwana, Mungu wako ishara, kama ni kwenye vina virefu sana au ni kwenye vimo virefu sana.”

12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribuBwana.”

13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, Ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia?

14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.

15 Atakula jibini na asali hapo atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua lililo jema.

16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa ubaya na kuchagua lililo jema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.

17 Bwanaataleta juu yako, juu ya watu wako na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18 Katika siku ileBwanaatawapigia filimbi mainzi kutoka kwenye vijito vya mbali vya Misri na nyuki kutoka nchi ya Ashuru.

19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye mitelemko na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba na kwenye mashimo yote ya maji.

20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ng’ambo ya Mtoyaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako, malaika ya miguu yako na kuziondoa ndevu zako pia.

21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai ndama mmoja na kondoo wawili.

22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali.

23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu.

24 Watu watakwenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba.

25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtakwenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba, patakuwa mahali ambapo ng’ombe wataachiwa huru na kondoo kukimbia-kimbia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/7-788558f4b6838b26743b6aa0c4b84b55.mp3?version_id=1627—

Isaya 8

Ashuru, Chombo Cha Bwana

1 Bwanaakaniambia, “Chukua gombo kubwa uandike juu yake kwa kalamu ya kawaida. Maher-Shalal-Hash-Bazi.

2 Nami nitawaita kuhani Uria na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”

3 Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba akazaa mwana. KishaBwanaakaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.

4 Kabla mtoto hajaweza kusema, ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”

5 Bwanaakasema nami tena:

6 “Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yatiririkayo taratibu

wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia,

7 kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao

# mafuriko makubwa ya Mto,

mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.

Yatafurika juu ya mifereji yake yote,

yatamwagikia juu ya kingo zake zote

8 na kufika hadi Yuda, ukizunguka kwa kasi juu yake,

yakipita kutoka upande huu

mpaka upande mwingine yakifika hadi shingoni.

Mabawa yake yaliyokunjuliwa

yatafunika upana wa nchi yako,

# Ee Imanueli!”

9 Inueni kilio cha vita, enyi mataifa

na mkavunjwevunjwe!

Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

10 Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;

fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,

# kwa maana Mungu yu pamoja nasi.

Mwogope Mungu

11 Bwanaalisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:

12 “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,

usiogope kile wanachokiogopa,

wala usikihofu.

13 BwanaMwenye Nguvu Zote ndiye peke yake

ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,

ndiye peke yake utakayemwogopa,

ndiye peke yake utakayemhofu,

14 naye atakuwa mahali patakatifu;

lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa

jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa

na mwamba wa kuwaangusha.

Kwa watu wa Yerusalemu atakuwa

mtego na tanzi.

15 Wengi wao watajikwaa;

wataanguka na kuvunjika,

watategwa na kunaswa.”

16 Funga ushuhuda na

kutia muhuri sheria

miongoni mwa wanafunzi wangu.

17 NitamngojeaBwana,

ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.

Nitaliweka tumaini langu kwake.

18 Nipo hapa pamoja na watoto ambaoBwanaamenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.

19 Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunong’ona na kunung’unika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?

20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.

21 Wakiwa na dhiki na njaa, watazunguka katika nchi yote, watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.

22 Kisha wataangalia duniani na kuona dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/8-6787976f18db72f78a8c589a8c126486.mp3?version_id=1627—

Isaya 9

Kwa Ajili Yetu Mtoto Amezaliwa

1 Hata hivyo, hapatakuwepo huzuni zaidi kwa wale waliokuwa katika dhiki. Wakati uliopita aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataiheshimu Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, kando ya Yordani:

2 Watu wanaotembea katika giza

wameona nuru kuu,

wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti,

nuru imewazukia.

3 Umelikuza taifa,

na kuzidisha furaha yao,

wanafurahia mbele zako,

kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno,

kama watu wafurahivyo

wagawanyapo nyara.

4 Kama katika siku ya kushindwa kwa Wamidiani,

umevunja nira ile iliyowalemea,

gongo mabegani mwao na

fimbo yake yeye aliyewaonea.

5 Kila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani

na kila vazi lililovingirishwa katika damu

litawekwa kwa ajili ya kuchomwa,

vitakuwa kuni za kuwasha moto.

6 Kwa maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,

tumepewa mtoto mwanamume,

nao utawala utakuwa mabegani mwake.

Naye ataitwa

Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani

hakutakuwa na mwisho.

Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi

na juu ya ufalme wake,

akiuthibitisha na kuutegemeza

kwa haki na kwa adili,

tangu wakati huo na hata milele.

Wivu waBwanaMwenye Nguvu Zote

utatimiza haya.

Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli

8 Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo,

utamwangukia Israeli.

9 Watu wote watajua hili:

Efraimu na wakazi wa Samaria,

wanaosema kwa kiburi

na majivuno ya mioyo,

10 “Matofali yameanguka chini,

lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa,

mitini imeangushwa,

lakini tutapanda mierezi badala yake.”

11 LakiniBwanaamemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao

na kuchochea watesi wao.

12 Waashuru kutoka upande wa mashariki

na Wafilisti kutoka upande wa magharibi

wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

13 Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga,

wala hawajamtafutaBwanaMwenye Nguvu Zote.

14 Kwa hiyoBwanaatakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia,

tawi la mtende na unyasi katika siku moja.

15 Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa,

nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.

16 Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha,

nao wale wanaoongozwa wamepotoka.

17 Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana,

wala hatawahurumia yatima na wajane,

kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu nao ni waovu,

kila kinywa kinanena upotovu.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

18 Hakika uovu huwaka kama moto;

huteketeza michongoma na miiba,

huwasha moto vichaka vya msituni,

hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi.

19 Kwa hasira yaBwanaMwenye Nguvu Zote

nchi itachomwa kwa moto,

nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto,

hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake.

20 Upande wa kuume watakuwa wakitafuna,

lakini bado wataona njaa;

upande wa kushoto watakuwa wakila,

lakini hawatashiba.

Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya mtoto wake mwenyewe:

21 Manase atamla Efraimu,

naye Efraimu atamla Manase;

kwa pamoja watakuwa kinyume na Yuda.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/9-6adfeab4b4b730c340c8e2b1ad422194.mp3?version_id=1627—

Isaya 10

1 Ole wao wawekao sheria zisizo za haki,

kwa wale watoao amri za kuonea,

2 kuwanyima maskini haki zao

na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa,

kuwafanya wajane mawindo yao

na kuwanyang’anya yatima.

3 Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu,

wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali?

Mtamkimbilia nani awape msaada?

Mtaacha wapi mali zenu?

4 Hakutasalia kitu cho chote

isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka

au kuanguka miongoni mwa waliouawa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

Hukumu Ya Mungu Juu Ya Ashuru

5 “Ole wa Waashuru, fimbo ya hasira yangu,

ambaye mkononi mwake

iko rungu ya ghadhabu yangu!

6 Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu,

ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha,

kukamata mateka na kunyakua nyara,

pia kuwakanyaga chini

kama matope ya barabarani.

7 Lakini hili silo analokusudia,

hili silo alilonalo akilini;

kusudi lake ni kuangamiza,

kuyakomesha mataifa mengi.

8 Maana asema, ‘Je, wafalme wote

si majemadari wangu?

9 Je, Kalno hakutenda kama Karkemishi?

Hamathi si kama Arpadi,

nayo Samaria si kama Dameski?

10 Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu,

falme ambazo vinyago vyao

vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:

11 je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake

kama nilivyoshughulikia

Samaria na vinyago vyake?’ ”

12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”

13 Kwa kuwa anasema:

“ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,

kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.

Niliondoa mipaka ya mataifa,

niliteka nyara hazina zao,

kama yeye aliye shujaa

niliwatiisha wafalme wao.

14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,

ndivyo mkono wangu

ulivyochukua utajiri wa mataifa;

kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,

ndivyo nilivyokusanya nchi zote;

wala hakuna hata mmoja aliyepigapiga bawa

au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”

15 Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi

kuliko yule anayelitumia,

au msumeno kujisifu

dhidi ya yule anayeutumia?

Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye,

au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!

16 Kwa hiyo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atatuma ugonjwa wa kudhoofisha

kwa askari wake walio hodari,

katika fahari yake moto utawaka

kama mwali wa moto.

17 Nuru ya Israeli itakuwa moto,

Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto;

katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba

na michongoma yake.

18 Fahari ya misitu yake

na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa,

kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.

19 Nayo miti inayobaki katika misitu yake

itakuwa michache sana

kwamba hata mtoto mdogo

angeweza kuihesabu.

Mabaki Ya Israeli

20 Katika siku ile mabaki ya Israeli,

walionusurika wa nyumba ya Yakobo,

hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga,

lakini watamtegemea kwa kweli

BwanaAliye Mtakatifu wa Israeli.

21 Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo

watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.

22 Ingawa watu wako, Ee Israeli,

ni wengi kama mchanga kando ya bahari,

ni mabaki yao tu ndio watakaorudi.

Maangamizi yamekwisha amriwa,

ni mengi tena ni haki.

23 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atatimiza maangamizi

yaliyoamriwa juu ya nchi yote.

24 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Enyi watu wangu mkaao Sayuni,

msiwaogope Waashuru,

wanaowapiga ninyi kwa fimbo

na kuinua rungu dhidi yenu,

kama Misri ilivyofanya.

25 Bado kitambo kidogo

sana hasira yangu dhidi yenu itakoma,

na ghadhabu yangu itaelekezwa

kwenye maangamizi yao.”

26 BwanaMwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi,

kama alivyowapiga Wamidiani

katika mwamba wa Orebu,

naye atainua fimbo yake juu ya maji,

kama alivyofanya huko Misri.

27 Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa

kutoka mabegani mwenu,

na nira yao kutoka shingoni mwenu;

nira itavunjwa

kwa sababu ya kutiwa mafuta.

28 Wanaingia Ayathi,

wanapita katikati ya Migroni,

wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi.

29 Wanavuka kivukoni, nao wanasema,

“Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.”

Rama inatetemeka;

Gibea ya Sauli inakimbia.

30 Piga kelele, Ee Binti wa Galimu!

Sikiliza, Ee Laisha!

Maskini Anathothi!

31 Madmena inakimbia;

watu wa Gebimu wanajificha.

32 Siku hii ya leo watasimama Nobu;

watatikisa ngumi zao

katika Mlima wa Binti Sayuni,

katika kilima cha Yerusalemu.

33 Tazama, Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atayakata matawi kwa nguvu kuu.

Miti mirefu sana itaangushwa,

ile mirefu itashushwa chini.

34 Atakata vichaka vya msitu kwa shoka;

Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/10-534bef37fc072b5a69f674d40031757a.mp3?version_id=1627—

Isaya 11

Tawi Kutoka Kwa Yese

1 Chipukizi litatokea kutoka katika shina la Yese,

kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.

2 Roho waBwanaatakaa juu yake,

Roho wa hekima na wa ufahamu,

Roho wa shauri na uweza,

Roho wa maarifa na wa kumchaBwana

3 naye atafurahia kumchaBwana.

Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,

wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

4 bali kwa adili atahukumu wahitaji,

kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.

Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,

kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

5 Haki itakuwa mkanda wake

na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

chui atalala pamoja na mbuzi,

ndama, mwana simba na ng’ombe aliyenona wa mwaka mmoja watalisha pamoja,

naye mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja,

watoto wao watalala pamoja

na simba atakula majani makavu kama maksai.

8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo

la nyoka mwenye sumu kali,

naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

kwenye kiota cha nyoka mwenye sumu.

9 Hawatadhuru wala kuharibu

juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

kwa kuwa dunia itajawa na kumjuaBwana

kama maji yajazavyo bahari.

10 Katika siku hiyo, shina la Yese litasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa, mataifa yatamkusanyikia na mahali pake pa kupumzika patatukuka.

11 Katika siku hiyo Bwana atanyosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.

12 Atainua bendera kwa mataifa

na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni;

atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika

katika pembe nne za dunia.

13 Wivu wa Efraimu utatoweka

na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;

Efraimu hatamwonea Yuda wivu

wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.

14 Watawashukia katika mitelemko ya Wafilisti

hadi upande wa magharibi,

kwa pamoja watawateka watu nyara

hadi upande wa mashariki.

Watawapiga Edomu na Moabu,

na Waamoni watatawaliwa nao.

15 Bwanaatakausha

ghuba ya Bahari ya Misri;

kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake

juu ya Mto Eufrati.

Ataugawanya katika vijito saba

ili watu waweze kuuvuka

wakiwa wamevaa viatu.

16 Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake

wale waliosalia kutoka Ashuru,

kama ilivyokuwa kwa Israeli

walipopanda kutoka Misri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/11-2d0bea8c3d526964595a3f81ddac2594.mp3?version_id=1627—

Isaya 12

Kushukuru Na Kusifu

1 Katika siku ile utasema:

“Nitakusifu wewe, EeBwana.

Ingawa ulinikasirikia,

hasira yako imegeukia mbali

nawe umenifariji.

2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;

nitamtumaini wala sitaogopa.

Bwana,Bwana, ni nguvu zangu

na wimbo wangu;

amekuwa wokovu wangu.”

3 Kwa furaha mtachota maji

kutoka katika visima vya wokovu.

4 Katika siku hiyo mtasema:

“MshukuruniBwana, mliitie jina lake;

julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya,

tangazeni kuwa jina lake limetukuka.

5 MwimbieniBwana, kwa kuwa ametenda mambo makuu,

hili na lijulikane duniani kote.

6 Paza sauti uimbe kwa furaha, watu wa Sayuni,

kwa maana mkuu ni yeye

Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/12-3cb1715dd81e8f1610a2b4da0e31be68.mp3?version_id=1627—

Isaya 13

Unabii Dhidi Ya Babeli

1 Neno kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:

2 Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu,

wapazieni sauti,

wapungieni mkono waingie

katika malango ya wenye heshima.

3 Nimewaamuru watakatifu wangu;

nimewaita mashujaa wangu

waitimize hasira yangu:

wale wanaoshangilia ushindi wangu.

4 Sikilizeni kelele juu ya milima,

kama ile ya umati mkubwa wa watu!

Sikilizeni, makelele katikati ya falme,

kama mataifa yanayokusanyika pamoja!

BwanaMwenye Nguvu Zote anakusanya

jeshi kwa ajili ya vita.

5 Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,

kutoka miisho ya mbingu,

Bwanana silaha za ghadhabu yake,

kuangamiza nchi yote.

6 Ombolezeni, kwa maana siku yaBwanai karibu,

# itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.

7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,

moyo wa kila mtu utayeyuka.

8 Hofu itawakamata,

uchungu na maumivu makali yatawashika,

watajinyonganyonga kama mwanamke

aliye na utungu wa kuzaa.

Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,

nyuso zao zikiwa katika hali

ya kuwaka kama moto.

9 Tazameni, siku yaBwanainakuja,

siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

kuifanya nchi kuwa ukiwa

na kuwaangamiza wenye dhambi

waliomo ndani yake.

10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

havitatoa mwanga wake.

Jua linalochomoza litatiwa giza

na mwezi hautatoa nuru yake.

11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,

waovu kwa ajili ya dhambi zao.

Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi

Na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

12 Nitawafanya wanadamu kuwa adimu

kuliko dhahabu safi,

watakuwa wachache sana

kuliko dhahabu ya Ofiri.

13 Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,

nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake

katika ghadhabu yaBwanaMwenye Nguvu Zote,

katika siku ya hasira yake iwakayo.

14 Kama swala awindwaye,

kama kondoo wasio na mchungaji,

kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe,

kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.

15 Ye yote atakayetekwa atapasuliwa tumbo,

wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.

16 Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande

mbele ya macho yao;

nyumba zao zitatekwa

na wake zao watatendwa jeuri.

17 Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao,

ambao hawajali fedha

wala hawafurahii dhahabu.

18 Mishale yao itawaangusha vijana,

hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga

wala hawataangalia watoto kwa huruma.

19 Babeli, johari ya falme,

# utukufu wa kiburi cha Wababeli,

itaangushwa na Mungu

kama Sodoma na Gomora.

20 Hautakaliwa na watu kamwe

wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote,

hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko,

hakuna mchungaji atakayepumzisha

makundi yake ya kondoo

na mbuzi huko.

21 Lakini viumbe wa jangwani watalala huko,

mbweha watajaza nyumba zake,

bundi wataishi humo

nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.

22 Fisi watalia ndani ya ngome zake,

mbweha ndani ya majumba yake

ya kifalme ya fahari.

Wakati wake umewadia,

na siku zake hazitaongezwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/13-151cf828900c0ae989de041b08c49078.mp3?version_id=1627—

Isaya 14

Yuda Kufanywa Upya

1 Bwanaatamhurumia Yakobo,

kwa mara nyingine tena atamchagua Israeli

na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe.

Wageni wataungana nao

na kujiunga na nyumba ya Yakobo.

2 Mataifa watawachukua

na kuwaleta mahali pao wenyewe.

Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi wa kiume na watumishi

wa kike katika nchi yaBwana.

Watawafanya watekaji wao kuwa mateka

na kutawala juu ya wale waliowaonea.

3 Katika sikuBwanaatakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,

4 utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli:

Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho!

Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!

5 Bwanaamevunja fimbo ya mwovu,

fimbo ya utawala ya watawala,

6 ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa

kwa mapigo yasiyo na kikomo,

nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa

kwa jeuri pasipo huruma.

7 Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani,

wanabubujika kwa kuimba.

8 Hata misonobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema,

“Basi kwa sababu umeangushwa chini,

hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”

9 Huko chini Kuzimu kote kumetaharuki

kukulaki unapokuja,

inaamsha roho za waliokufa ili kukupokea,

wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu,

inawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme,

wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.

10 Wote wataitika,

watakuambia,

“Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo;

wewe umekuwa kama sisi.”

11 Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu,

pamoja na kelele ya vinubi vyako,

mafunza yametanda chini yako

na minyoo imekufunika.

12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

Ewe nyota ya asubuhi,

mwana wa mapambazuko!

Umetupwa chini duniani,

wewe uliyepata kuangusha mataifa!

13 Ulisema moyoni mwako,

“Nitapanda juu hadi mbinguni,

nitakiinua kiti changu cha enzi

juu ya nyota za Mungu,

nitaketi nimetawazwa

juu ya mlima wa kusanyiko,

kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

14 Nitapaa juu kupita mawingu,

nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,

hadi kwenye vina vya shimo.

16 Wale wanaokuona wanakukazia macho,

wanatafakari hatima yako:

“Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia

na kufanya falme zitetemeke,

17 yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa,

aliyeipindua miji yake

na ambaye hakuwaachia

mateka wake waende nyumbani?”

18 Wafalme wote wa mataifa wamelala

kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake mwenyewe.

19 Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako

kama tawi lililokataliwa,

umefunikwa na waliouawa

pamoja na wale waliochomwa kwa upanga,

wale washukao mpaka

kwenye mawe ya shimo.

Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,

20 Hutajumuika nao kwenye mazishi,

kwa kuwa umeharibu nchi yako

na kuwaua watu wako.

Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe.

21 Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe

kwa ajili ya dhambi za baba zao,

wasije wakainuka ili kuirithi nchi

na kuijaza dunia kwa miji yao.

22 BwanaMwenye Nguvu Zote asema,

“Nitainuka dhidi yao,

nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli

pamoja na watu wake walionusurika,

watoto wake na wazao wake,”

asemaBwana.

23 “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi,

na kuwa nchi ya matope;

nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,”

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

Unabii Dhidi Ya Ashuru

24 BwanaMwenye Nguvu Zote ameapa,

“Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,

nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.

25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,

juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.

Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,

nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”

26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,

huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.

27 Kwa kuwaBwanaMwenye Nguvu Zote amekusudia,

ni nani awezaye kumzuia?

Mkono wake umenyooshwa,

ni nani awezaye kuurudisha?

Unabii Dhidi Ya Wafilisti

28 Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipokufa:

29 Msifurahi, enyi Wafilisti wote,

kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika;

kutoka katika mzizi wa huyo nyoka

atachipuka nyoka mwenye sumu kali,

uzao wake utakuwa joka lirukalo,

lenye sumu kali.

30 Maskini kuliko maskini wote watapata malisho,

nao wahitaji watalala salama.

Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa,

nayo njaa itawaua walionusurika.

31 Piga yowe, Ee lango! Bweka, Ee mji!

Yeyukeni, enyi Wafilisti wote!

Wingu la moshi linakuja toka kaskazini,

wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.

32 Ni jibu gani litakalotolewa

kwa wajumbe wa taifa hilo?

“Bwanaameifanya imara Sayuni,

nako ndani yake watu wake walioonewa

watapata kimbilio.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/14-eae0592fce4bc6b4c99ed9ef6670f182.mp3?version_id=1627—

Isaya 15

Unabii Dhidi Ya Moabu

1 Neno kuhusu Moabu:

Ari iliyo katika Moabu imeangamizwa:

imeharibiwa kwa usiku mmoja!

Kiri iliyo katika Moabu imeangamizwa,

imeharibiwa kwa usiku mmoja!

2 Diboni anakwea hadi kwenye Hekalu lake,

mpaka mahali pake pa juu pa kuabudia miungu ili walie,

Moabu anaombolezea Nebo na Medeba.

Kila kichwa kimenyolewa

na kila ndevu zimeondolewa.

3 Wamevaa nguo za magunia barabarani,

juu ya mapaa na kwenye viwanja wote

wanaomboleza,

hulala kifudifudi kwa kulia.

4 Heshboni na Eleale wanalia,

sauti zao zinasikika hadi Yahasa.

Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu

wanapiga kelele,

nayo mioyo yao imezimia.

5 Moyo wangu unamlilia Moabu;

wakimbizi wake wanakimbilia Soari,

hadi Eglath-Shelishiya.

Wanapanda njia ya kwenda Luhithi,

wanakwenda huku wanalia;

kwenye barabara iendayo Horonaimu

wanaombolezea maangamizi yao.

6 Maji ya Nimrimu yamekauka

na majani yamenyauka;

mimea imekauka wala hakuna

kitu cho chote kibichi kilichobaki.

7 Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba

wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.

8 Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu,

kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu,

maombolezo yao hadi Beer-Elimu.

9 Maji ya Dimoni yamejaa damu,

lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni:

simba juu ya wakimbizi wa Moabu

na juu ya wale wanaobaki katika nchi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/15-f1ae431bfd5abb13adc60051601fe9a6.mp3?version_id=1627—

Isaya 16

Hali Ya Kukata Tamaa Ya Moabu

1 Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi,

Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni.

2 Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kwenye kiota chao,

ndivyo walivyo wanawake wa Moabu

kwenye vivuko vya Arnoni.

3 “Tupeni shauri,

toeni uamuzi.

Wakati wa adhuhuri,

fanyeni kivuli chenu kama usiku.

Waficheni watoro,

msisaliti wakimbizi.

4 Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi;

iweni mahali pao pa salama

ili kuepuka mharabu.”

Mtesi atafikia mwisho

na maangamizi yatakoma,

aletaye vita atatoweka kutoka katika nchi.

5 Kwa upendo kiti cha enzi kitaimarishwa,

kwa uaminifu mtu ataketi juu yake,

yeye atokaye katika nyumba ya Daudi:

yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki,

na huhimiza njia ya haki.

6 Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu,

kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu,

kiburi chake na ufidhuli wake,

lakini majivuno yake si kitu.

7 Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza,

wanaiombolezea Moabu kwa pamoja.

Wanaomboleza na kuhuzunika

kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.

8 Mashamba ya Heshboni yananyauka,

pia na mizabibu ya Sibma.

Watawala wa mataifa

wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana,

ambayo ilipata kufika Yazeri

na kuenea kuelekea jangwani.

Machipukizi yake yalienea

yakafika hadi baharini.

9 Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo,

kwa ajili ya mizabibu ya Sibma.

Ee Heshboni, Ee Eleale,

ninakulowesha kwa machozi!

Kelele za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva

na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa.

10 Furaha na shangwe zimeondolewa

kutoka katika mashamba ya matunda;

hakuna ye yote aimbaye

wala apazaye sauti

katika mashamba ya mizabibu;

hakuna ye yote akanyagaye zabibu shinikizoni,

kwa kuwa nimekomesha makelele.

11 Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi,

nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi.

12 Wakati Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu,

anajichosha mwenyewe tu;

anapokwenda mahali pake pa kuabudia miungu ili kuomba,

haitamfaidia lo lote.

13 Hili ndilo neno ambaloBwanaameshasema kuhusu Moabu.

14 Lakini sasaBwanaanasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana tena wanyonge.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/16-d91df6bdb9aa60c24594b248f5d7ef31.mp3?version_id=1627—