Isaya 17

Neno Dhidi Ya Dameski

1 Neno kuhusu Dameski: “Tazama, Dameski haitakuwa tena mji

bali itakuwa lundo la magofu.

2 Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa makundi ya kondoo na mbuzi,

ambayo yatalala huko,

bila ye yote wa kuyaogopesha.

3 Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu,

nao uweza wa kifalme kutoka Dameski;

mabaki ya Aramu yatakuwa

kama utukufu wa Waisraeli,”

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

4 “Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia,

unene wa mwili wake utadhoofika.

5 Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka

na kuvuna nafaka kwa mikono yake,

kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke ya nafaka

katika Bonde la Warefai.

6 Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki,

kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa,

kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi ya kileleni,

nne au tano katika matawi yazaayo sana,”

asemaBwana, Mungu wa Israeli.

7 Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao

na kuelekeza macho yao kwa huyo Aliye Mtakatifu wa Israeli.

8 Hawataziangalia tena madhabahu,

kazi za mikono yao,

# nao hawatathamini nguzo za Ashera

na madhabahu za kufukizia uvumba

zilizofanywa kwa mikono yao.

9 Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.

10 Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu,

hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu.

Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana

na kuotesha mizabibu ya kigeni,

11 hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote

na asubuhi ile ile unayoipanda,

unaifanya ichipue,

hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu

katika siku ile ya ugonjwa

na maumivu yasiyoponyeka.

12 Lo! Ghadhabu ya mataifa mengi,

wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka!

Lo! Makelele ya mataifa

wanavuma kama ngurumo za maji mengi!

13 Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo

za maji yanayofanya mawimbi,

wakati anapoyakemea yanakimbia mbali,

yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima,

kama jani livingirishwapo na dhoruba.

14 Wakati wa jioni, hofu ya ghafula!

Kabla ya asubuhi, wametoweka!

Hili ndilo fungu la wale wanaotupora,

fungu la wale wanaotunyang’anya mali zetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/17-04b51c536a0dc3a1618bb7b3188095e8.mp3?version_id=1627—

Isaya 18

Unabii Dhidi Ya Kushi

1 Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa,

kwenye mito ya Kushi,

2 iwapelekayo wajumbe wake

kwa njia ya bahari

# kwa mashua za mafunjojuu ya maji.

Nendeni, wajumbe wepesi,

kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,

kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,

taifa gomvi lenye lugha ngeni,

ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.

3 Enyi mataifa yote ya ulimwengu,

ninyi mnaoishi duniani

wakati bendera itakapoinuliwa milimani,

mtaiona,

nayo tarumbeta itakapolia,

mtaisikia.

4 Hili ndiloBwanaaliloniambia:

“Nitatulia kimya na kutazama

kutoka maskani yangu,

kama joto linalometameta katika mwanga wa jua,

kama wingu la umande

katika joto la wakati wa mavuno.”

5 Kwa maana, kabla ya mavuno,

wakati wa kuchanua ukishapita

na maua yakawa zabibu zinazoiva,

atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi,

naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.

6 Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani

na wanyama pori,

ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi,

nao wanyama pori wakati wote wa masika.

7 Wakati huo matoleo yataletwa kwaBwanaMwenye Nguvu Zote

kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,

kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,

kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni,

ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito,

matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina laBwanaMwenye Nguvu Zote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/18-57ad4b41e9dfa662f5ab0789c6356fd2.mp3?version_id=1627—

Isaya 19

Unabii Kuhusu Misri

1 Neno kuhusu Misri:

Tazama,Bwanaamepanda juu ya wingu

liendalo kwa haraka naye anakuja Misri.

Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake,

nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.

2 “Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri,

ndugu atapigana dhidi ya ndugu,

jirani dhidi ya jirani,

mji dhidi ya mji,

ufalme dhidi ya ufalme.

3 Wamisri watakufa moyo,

na nitaifanya mipango yao kuwa batili,

watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa,

kwa wapiga ramli

na kwa wale waongeao na mizimu.

4 Nitawatia Wamisri

mikononi mwa bwana mkatili

na mfalme mkali atatawala juu yao,”

asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote.

5 Maji ya mito yatakauka,

chini ya mto kutakauka kwa jua.

6 Mifereji itanuka;

vijito vya Misri vitapungua

na kukauka.

Mafunjo na nyasi vitanyauka,

7 pia mimea iliyoko kandokando ya Mto Nile,

kwenye mdomo wa mto unapomwaga maji baharini.

Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Nile litakauka,

litapeperushwa na kutoweka kabisa.

8 Wavuvi watalia na kuomboleza,

wale wote watupao ndoano katika Mto Nile,

watadhoofika kwa majonzi.

9 Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa,

wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.

10 Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa,

nao vibarua wataugua moyoni.

11 Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa,

washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga.

Unawezaje kumwambia Farao,

“Mimi ni mmojawapo wa watu wenye hekima,

mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?

12 Wako wapi sasa watu wako wenye hekima?

Wao wakuonyeshe na kukufahamisha

ni niniBwanaMwenye Nguvu Zote

amepanga dhidi ya Misri.

13 Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu,

# viongozi wa Memfisiwamedanganyika,

walio mawe ya pembe ya taifa lake

wameipotosha Misri.

14 Bwanaamewamwagia

roho ya kizunguzungu;

wanaifanya Misri iyumbeyumbe

katika yale yote inayoyafanya,

kama vile mlevi ayumbayumbavyo

katika kutapika kwake.

15 Misri haiwezi kufanya kitu cho chote,

cha kichwa wala cha mkia,

cha tawi la mtende wala cha unyasi.

16 Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono waBwanaMwenye Nguvu Zote anaoinua dhidi yao.

17 Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambachoBwanaMwenye Nguvu Zote anapanga dhidi yao.

18 Katika siku hiyo miji mitano ya Misri itazungumza lugha ya Kanaani na kuapa kumtiiBwanaMwenye Nguvu Zote. Mji mmojawapo utaitwa Mji wa Uharibifu.

19 Katika siku hiyo patakuwepo madhabahu yaBwanakatikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwaBwanakwenye mpaka wa Misri.

20 Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili yaBwanaMwenye Nguvu Zote katika nchi ya Misri. WatakapomliliaBwanakwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea Mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.

21 HivyoBwanaatajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubaliBwana. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekeaBwananadhiri na kuzitimiza.

22 Bwanaataipiga Misri kwa tauni, atawapiga na kuwaponya. WatamgeukiaBwana, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.

23 Katika siku hiyo kutakuwepo na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru watakwenda Misri na Wamisri watakwenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.

24 Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia.

25 BwanaMwenye Nguvu Zote atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu na kwa Israeli urithi wangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/19-7e69346dd835d2fc7178455831747681.mp3?version_id=1627—

Isaya 20

Unabii Dhidi Ya Misri Na Kushi

1 Katika mwaka ule ambao jemadari mkuu, alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja mpaka Ashdodi akaushambulia na kuuteka,

2 wakati uleBwanaalisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua nguo ya gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo akatembea huko na huko uchi na bila viatu.

3 KishaBwanaakasema, “Kama vile mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi,

4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri na watu wa uhamisho wa Kushi uchi na bila viatu, vijana na wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri.

5 Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika.

6 Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa ajili ya msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/20-877f55b7e4e46243d495a2c18c32868d.mp3?version_id=1627—

Isaya 21

Unabii Dhidi Ya Babeli

1 Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari:

Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,

mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,

kutoka katika nchi inayotisha.

2 Nimeonyeshwa maono ya kutisha:

Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.

Elamu, shambulia Umedi!

Izunguke kwa jeshi!

Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.

3 Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu,

maumivu makali ya ghafula yamenishika,

kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa,

nimeduwazwa na lile ninalolisikia,

nimeshangazwa na lile ninaloliona.

4 Moyo wangu unababaika,

woga unanifanya nitetemeke,

gizagiza la jioni nililolitamani sana,

limekuwa hofu kuu kwangu.

5 Wanaandaa meza,

wanatandaza mazulia,

wanakula, wanakunywa!

Amkeni, enyi maafisa,

zitieni ngao mafuta!

6 Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi,

na mtake atoe taarifa ya kile anachokiona.

7 Anapoona magari ya vita

pamoja na kundi la farasi,

wapanda punda au wapanda ngamia,

na awe macho, awe macho kikamilifu.”

8 Naye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu,

ninasimama katika mnara wa ulinzi,

kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.

9 Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita

pamoja na kundi la farasi.

Naye akajibu:

‘Babeli ameanguka,

ameanguka!

Vinyago vyote vya miungu yake

vimelala chini vikiwa vimevunjwavunjwa!’ ”

10 Ee watu wangu, mliopondwapondwa kwenye sakafu ya kupuria,

ninawaambia kile nilichokisikia

kutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote,

kutoka kwa Mungu wa Israeli.

Unabii Dhidi Ya Edomu

11 Neno kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,

“Mlinzi, ni muda gani uliobaki kupambazuke?

Mlinzi, usiku utaisha lini?”

12 Mlinzi akajibu,

“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.

Kama ungeliuliza, basi uliza;

bado na urudi tena.”

Unabii Dhidi Ya Arabia

13 Neno kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani,

Mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,

14 Leteni maji kwa wenye kiu,

ninyi mnaoishi Tema,

leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.

15 Wanaukimbia upanga,

kutoka upanga uliochomolewa alani,

kutoka upinde uliopindwa

na kutoka kwenye joto la vita.

16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho.

17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.”Bwana, Mungu wa Israeli, amesema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/21-52a2530139a33f32d01ec23aad0d1ed7.mp3?version_id=1627—

Isaya 22

Unabii Kuhusu Yerusalemu

1 Neno kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa,

kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?

2 Ewe mji uliojaa ghasia,

Ewe mji wa makelele

na karamu za sherehe!

Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,

wala hawakufa vitani.

3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,

wamekamatwa bila kutumia upinde.

Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,

mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.

4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,

niache nilie kwa uchungu.

Usijaribu kunifariji

juu ya maangamizi ya watu wangu.”

5 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, anayo siku

ya ghasia, ya kukanyaga na ya kuogofya

katika Bonde la Maono,

siku ya kuangusha kuta

na ya kupiga kelele mpaka milimani.

6 Elamu analichukua podo,

pamoja na waendesha magari ya vita na farasi,

Kiri anaifungua ngao.

7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,

nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji;

8 ulinzi wa Yuda umeondolewa.

Nawe ulitazama katika siku ile

silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni,

9 mkaona kuwa Mji wa Daudi

una matundu mengi katika ulinzi wake,

mkaweka akiba ya maji

kwenye Bwawa la Chini.

10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu

nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.

11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili

kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,

lakini hamkumtazama yule aliyelitengeneza,

au kuwa na heshima kwa yule aliyeubuni tangu zamani za kale.

12 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

aliwaita siku ile

ili kulia na kuomboleza,

kung’oa nywele zenu

na kuvaa nguo ya gunia.

13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

kuchinja ng’ombe na kuchinja kondoo,

kula nyama na kunywa mvinyo!

Mnasema, “Sisi na tule na kunywa,

kwa kuwa kesho tunakufa!”

14 BwanaMwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

15 Hili ndilo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asemalo:

“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,

ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:

16 Unafanya nini hapa na ni nani aliyekupa ruhusa

kujikatia kaburi lako mwenyewe,

ukichonga kaburi lako mahali palipo juu

na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?

17 “Jihadhari,Bwanayu karibu kukukamata kwa uthabiti

na kukutupa mbali kwa nguvu, Ewe mtu mwenye nguvu.

18 Atakuvingirisha uwe kama mpira

na kukutupa katika nchi kubwa.

Huko ndiko utakakofia,

na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,

wewe unayeifedhehesha nyumba ya bwana wako!

19 Nitakuondoa kutoka katika kazi yako,

nawe utaondoshwa kutoka katika nafasi yako.

20 “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia.

21 Nitamvika joho lako nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda.

22 Nitaweka mabegani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi, kile afunguacho hakuna awezaye kufunga na kile afungacho hakuna awezaye kufungua.

23 Nitamgongomea kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha enzi cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake.

24 Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Watoto wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25 BwanaMwenye Nguvu Zote asema, “Katika siku ile, kigingi kilichogongomewa mahali imara kitaachia njia, kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioning’inia juu yake utaanguka chini.”Bwanaamesema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/22-adb9150a718fe6572b0ba7194db44151.mp3?version_id=1627—

Isaya 23

Unabii Kuhusu Tiro

1 Neno kuhusu Tiro:

Ombolezeni, Enyi meli za Tarshishi!

Kwa kuwa Tiro imeangamizwa,

imeachwa bila nyumba wala bandari.

# Kuanzia nchi ya Kitimu

neno limewajia.

2 Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani,

pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni,

ambao mabaharia wamewatajirisha.

3 Kwenye maji makuu

nafaka za Shihori zilikuja;

mavuno ya Nile yalikuwa mapato ya Tiro,

naye akawa soko la mataifa.

4 Uaibishwe Ee Sidoni, nawe Ee ngome ya Bahari,

kwa kuwa bahari imesema,

“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa,

wala sijapata kulea wana wala kutunza mabinti.”

5 Habari ifikapo Misri,

watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.

6 Vukeni mpaka Tarshishi,

ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.

7 Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe,

mji wa zamani, zamani kabisa

ambao miguu yake imeuchukua

kufanya makao nchi za mbali sana?

8 Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro,

mji utoao mataji,

ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme

na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?

9 BwanaMwenye Nguvu Zote ndiye aliyepanga jambo hili,

ili kukishusha kiburi cha utukufu wote

na kuwanyenyekesha wale wote

ambao ni mashuhuri duniani.

10 Ee Binti Tarshishi,

pita katika nchi yako kama vile Mto Nile

kwa kuwa huna tena bandari.

11 Bwanaamenyosha mkono wake juu ya bahari

na kuzifanya falme zake zitetemeke.

Ametoa amri kuhusu Kanaani

kwamba ngome zake ziangamizwe.

12 Alisema, “Usizidi kufurahi,

Ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!

“Simama, vuka uende Kitimu;

hata huko hutapata pumziko.”

13 Tazama katika nchi ya Wakaldayo,

watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo!

Waashuri wameifanya nchi hiyo

kuwa mahali pa viumbe wa jangwani.

Wamesimamisha minara yao ya vita kuuzunguka,

wameziteka ngome zake na kuziacha tupu

na kuufanya kuwa magofu.

14 Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi;

ngome yenu imeangamizwa!

15 Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:

16 “Twaa kinubi, tembea mjini kote,

Ewe kahaba uliyesahauliwa;

piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi,

ili kwamba upate kukumbukwa.”

17 Mwishoni mwa miaka sabini,Bwanaatashughulika na Tiro. Atarudia ajira yake ya ukahaba naye atafanya biashara yake na falme zote juu ya uso wa dunia.

18 Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa ajili yaBwana; hayatahifadhiwa kwa ajili yake binafsi. Faida zake zitakwenda kwa wale wakaao mbele zaBwanakwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/23-000a34f833cc6a05893a007dcd8cc273.mp3?version_id=1627—

Isaya 24

Dunia Kuharibiwa Upesi

1 Tazama,Bwanaataifanya dunia kuwa ukiwa

na kuiharibu,

naye atauharibu uso wake

na kutawanya wakaao ndani yake:

2 ndivyo itakavyokuwa

kwa makuhani na kwa watu,

kwa bwana na kwa mtumishi,

kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike,

kwa muuzaji na kwa mnunuzi,

kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,

kwa mdaiwa na kwa mdai.

3 Dunia itaharibiwa kabisa

na kutekwa nyara kabisa.

Bwanaamesema neno hili.

4 Dunia inakauka na kunyauka,

dunia inanyong’onyea na kunyauka,

waliotukuzwa wa dunia wananyong’onyea.

5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake,

wameacha kutii sheria,

wamevunja amri na kuvunja Agano la milele.

6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,

watu wake lazima waichukue hatia yao.

Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,

nao waliosalia ni wachache sana.

7 Divai mpya inakauka

na mzabibu unanyauka,

watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.

8 Furaha ya matoazi imekoma,

kelele za wenye furaha zimekoma,

shangwe za kinubi zimenyamaza.

9 Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,

kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

10 Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,

mlango wa kila nyumba umefungwa.

11 Barabarani wanalilia kupata mvinyo,

furaha yote imegeuka kuwa majonzi,

furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.

12 Mji umeachwa katika uharibifu,

lango lake limepigwapigwa

na kuvunjwa vipande vipande.

13 Ndivyo itakavyokuwa duniani

na miongoni mwa mataifa,

kama vile wakati mzeituni upigwavyo,

au kama vile wakati masazo yabakiavyo

baada ya zabibu kuvunwa.

14 Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,

kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu waBwana.

15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeniBwanautukufu,

liadhimisheni jina laBwana, Mungu wa Israeli,

katika visiwa vya bahari.

16 Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:

“Utukufu kwa yeye Mwenye Haki.”

Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!

Ole wangu!

Watenda hila wanasaliti!

Kwa hila watenda hila wanasaliti!”

17 Hofu, shimo na mtego vinakungojea,

ewe mtu ukaaye duniani.

18 Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu

atatumbukia shimoni,

ye yote apandaye kutoka shimoni,

atanaswa kwenye mtego.

Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,

misingi ya dunia inatikisika.

19 Dunia imepasuka,

dunia imechanika,

dunia imetikiswa kabisa.

20 Dunia inapepesuka kama mlevi,

inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;

imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake

na ikianguka kamwe haitainuka tena.

21 Katika siku ileBwanaataadhibu nguvu zilizoko mbinguni juu

na wafalme walioko duniani chini.

22 Watakusanywa pamoja

kama wafungwa waliofungwa gerezani,

watafungiwa gerezani

na kujiliwa baada ya siku nyingi.

23 Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;

kwa maanaBwanaMwenye Nguvu Zote atawala

juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,

tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/24-8dc01515934c24aa4e99b6094af8ed27.mp3?version_id=1627—

Isaya 25

Msifuni Bwana

1 EeBwana, wewe ni Mungu wangu,

nitakutukuza na kulisifu jina lako,

kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

umetenda mambo ya ajabu,

mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

2 Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,

mji wenye ngome kuwa magofu,

ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,

wala hautajengwa tena kamwe.

3 Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,

miji ya mataifa katili itakuheshimu wewe.

4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

hifadhi wakati wa dhoruba

na kivuli wakati wa hari.

Kwa maana pumzi ya wakatili

ni kama dhoruba ipigayo ukuta

5 na kama joto la jangwani.

Wewe wanyamazisha makelele ya wageni,

kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,

ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.

6 Juu ya mlima huuBwanaMwenye Nguvu Zote ataandaa

karamu ya vinono kwa mataifa yote,

karamu ya mvinyo wa zamani,

nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

7 Juu ya mlima huu ataharibu sitara ile ihifadhiyo mataifa yote,

kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

8 yeye atameza mauti milele katika ushindi.

BwanaMwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote,

ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

Bwanaamesema hili.

9 Katika siku ile watasema,

“Hakika huyu ndiye Mungu wetu,

tuliyemtumaini naye akatuokoa.

Huyu ndiyeBwana, tuliyemtumaini;

sisi na tushangilie

na kufurahia katika wokovu wake.”

10 Mkono waBwanautatulia juu ya mlima huu,

bali Moabu atakanyagwa chini

kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.

11 Ingawa watakunjua mikono yao katikati yake,

kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.

Mungu atashusha kiburi chao

licha ya ujanja wa mikono yao.

12 Atabomoa kuta ndefu za maboma yako

na kuziangusha chini,

atazishusha chini ardhini,

mpaka mavumbini kabisa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/25-cd29ea3c711afef4cf9519ee40cb09d5.mp3?version_id=1627—

Isaya 26

Wimbo Wa Ushindi

1 Katika siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:

Tuna mji ulio na nguvu,

Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.

2 Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,

taifa lile lishikalo imani.

3 Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye

moyo wake ni thabiti

kwa sababu anakutumaini wewe.

4 MtumainiBwanamilele,

kwa kuwaBwana,Bwana,

ni Mwamba wa milele.

5 Huwashusha wale wajikwezao,

huushusha chini mji wenye kiburi,

huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini.

6 Miguu hukanyaga chini,

miguu ya hao walioonewa,

hatua za hao maskini.

7 Mapito ya wenye haki yamenyooka,

Ewe uliye mwenye haki,

waisawazisha njia ya mtu mnyofu.

8 Naam,Bwanatukienenda katika sheria zako,

twakungojea wewe,

kulikumbuka jina lako

na sifa zako ndiyo shauku ya mioyo yetu.

9 Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,

wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.

Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,

watu wa ulimwengu hujifunza haki.

10 Ingawa neema yaonyeshwa kwa waovu,

hawajifunzi haki,

hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya

wala hawaoni utukufu waBwana.

11 EeBwana, mkono wako umeinuliwa juu,

lakini hawauoni.

Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe,

moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.

12 Bwana, unaamuru amani kwa ajili yetu,

yale yote tuliyoweza kuyakamilisha

ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.

13 EeBwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala,

lakini jina lako peke yako ndilo tunaloliheshimu.

14 Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai,

roho za waliokufa hazitarudi tena.

Uliwaadhibu na kuwaangamiza,

umefuta kumbukumbu lao lote.

15 Umeliongeza hilo taifa, EeBwana,

umeliongeza hilo taifa.

Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe,

umepanua mipaka yote ya nchi.

16 Bwana, walikujia katika taabu yao,

wewe ulipowarudi,

waliweza kuomba kwa kunong’ona kwa shida sana.

17 Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa

anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake,

ndivyo tulivyokuwa mbele zako, EeBwana.

18 Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu,

lakini tulizaa upepo.

Hatukuleta wokovu duniani,

hatujazaa watu katika ulimwengu huu.

19 Lakini wafu wenu wataishi,

miili yao itafufuka.

Ninyi mnaokaa katika mavumbi,

amkeni mkapige kelele kwa furaha.

Umande wenu ni kama umande wa asubuhi,

dunia itawazaa wafu wake.

20 Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu

na mfunge milango nyuma yenu,

jificheni kwa kitambo kidogo

mpaka ghadhabu yake ipite.

21 Tazama,Bwanaanakuja kutoka katika makao yake

ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao.

Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake,

wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/26-5e3fa261bb59ab57eddae9a43d7103c3.mp3?version_id=1627—